MYANMAR-Mazishi baada ya maporoko katika machimbo MYANMAR-Mazishi baada ya maporoko katika machimbo 

Myanmar:Makanisa ya Asia yashutumu vitendo vya uchu na ukiukwaji wa haki za binadamu!

Maaskofu wa Kanisa Katoliki Barani Asia wamekemea vikali uchu wa mali na uvunjifu wa haki kwa baadhi ya viongozi wa Migodi ambao kwa kutokujali kwao wamesababisha madhara makubwa katika jamii ya Myanmar ambapo tarehe 2 Julai 2020 ilisababisha kuwepo kwa maparomoko ya vifusi vya mgodi na kupelekea vifo zaidi ya 170.

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea mnamo Alhamisi ya tarehe 2 Julai, 2020 katika migodi ya Jade huko Hpakant kaskazini mwa Myanmar, ambapo vifusi vya migodi vilivyochanganyikana na tope zito la maji liliporomoka kutoka huko mlimani kuelekea ziwani na kusomba makazi ya watu maskini waliokuwa wakiishi kandokando ya milima hiyo.    Kardinali Charles Bo wa Yangon huko Myanmar na Rais wa Shirikisho la Barazala Maaskofu Barani Asia (FABC) katika kutoa salaam za rambirambi zake kwa Askofu Francisko Daw Tang wa Myitkyina, amesema, amepokea taarifa hizo kwa masikitiko makubwa. Wakiwa na mioyo iliyoghubikwa na huzuni, kutokana na taarifa za kusikitisha za vifo vya vijana vilivyotokea katika migodi ya Jade na ameeleza kuguswa kwa kwa tukio hilo lililopelekea zaidi ya watu 170 kupoteza maisha yao.

Miili ya marehemu hao ilifunikwa na vifusi hivyo ambavyo vinatokana na kuporomoka. Akiongea kwa niaba ya Maaskofu wote Baran Asia, Kardinali Bo amemnukuu Papa Francisko katika wosia wake kuhusu mwendelezo wa vita vya kudumu vya kiuchumi na kimazingira na kuliita jina la sunami kwa lengo la kuwatetea maskini ulimwenguni kote.  Aidha Kardinali Bo amebainisha changamoto zinazolikumba Bara la Asia zikiwemo uchu wa mali, kutojali, na uchochezi kutoka kwa matajiri.  Kwa mujibu wake amesema watu waliokufa ni kama vile wametolewa tambiko katika madhabahu ya uchu na kutojali makampuni yanayojirimbikizia utajiri na kuvunja haki za binadamu. Kunako Novemba 2015, tukio jingine la namna hiyo, lilitokea huko  Kachin na ambalo liliuwa zaidi ya watu 113. Lakini kwa awamu hii tukio hili limetia fora.  Takribani asilimia 90 ya madini ya Jade yanayouzwa nchi jirani yanatoka katika eneo la  Kachin. Machimbo hayo yako maeneo ya Hpakant yanayozalisha madini ya Jade kwa kiwango kukubwa ulimwenguni.  Kutokana na taarifa za utafiti wa Mashuhuda zinaonesha kuwa tangu 2014 rasilimali za madini ya Jade nchini Myanmar huchangia pato la Taifa kwa bilioni 31 za dola za kimarekani na faida kubwa inayopatikana hugawanywa na makampuni hayo yanayoongozwa na watawala wa kijeshi.

Katika kuziombea familia zilizoathirika, Kardinali Bo ameunganisha dhana ya janga la COVID 19 na janga la njaa linalowakabiri watu maskini nchini humo ambalo haliwafanyi kukaa ndani.  Kwa maana hiyo Kardinali ametoa wito  kwa watu wote kuwa tukio hilo liwe fundisho na kuwafanya watu wabadilishe mtindo wa maisha na kumgeukia Mwenyezi Mungu anayetaka rasi        mali za Myanmar kunufaisha wananchi wote wa Myanmar. Aidha Kardinali Bo amesema, ikiwa viongozi wa Makampuni hayo hawataitikia wito huo, basi majanga kama hayo yataendelea kutokea. Na baada ya siku moja Bwana Aung San Suu Kyi alitoa pia salaam za rambirambi kwa waathirika wa janga hilo na wakati huo huo akitoa hoja ya kufungua fursa mpya za ajira nchini humo.  Naye Bwana Antonio Gutteres Katibu wa Umoja wa Mataifa, alitoa rambirambi zake akieleza kwa namna wavyosikitishwa na tarifa za janga hilo ambalo wahanga wa tukio hilo ni wahamiaji na wafanyakazi wanaojitafutia riziki zao kwa kufanya vibarua.

06 July 2020, 14:16