Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linaadhimisha Siku ya SECAM kuanzia tarehe 29 Julai hadi tarehe 2 Agosti 2020: Siku za Sala, Umoja na Mshikamano. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM linaadhimisha Siku ya SECAM kuanzia tarehe 29 Julai hadi tarehe 2 Agosti 2020: Siku za Sala, Umoja na Mshikamano. 

Maadhimisho ya Siku ya SECAM: 29 Julai - 2 Agosti, 2020! Ujumbe!

Waamini wajenge utamaduni wa kukutana na Yesu katika Neno la Sakramenti zake. Toba na wongofu wa ndani, uwasaidie waamini kuambata utakatifu wa maisha tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.. Waamini wajibidiishe kufahamu Mafundisho Tanzu ya Kanisa ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu inayowajibika Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM mwaka 2019 yalipambwa na kauli mbiu “Kanisa, familia ya Mungu Barani Afrika; Sherehekea Jubilei yako! Mtangaze Kristo Yesu Mkombozi wako”. Hii ilikuwa ni nafasi muafaka ya kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Lengo kuu la Jubilei hiyo ilikuwa ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya imani kwa familia ya Mungu Barani Afrika. Huu ni wakati kwa waamini kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanashiriki: ukuhani, unabii na ufalme wa Kristo, hivyo wanaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufka kwa wafu ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

SECAM ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, uliowahamasisha Maaskofu kutoka Barani Afrika, kushikamana kwa hali na mali, ili kuweza kukoleza ari na moyo wa kimisionari, tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. SECAM ikazinduliwa rasmi tarehe 31 Julai 1969 huko Uganda kwa ushuhuda na uwepo wa Mtakatifu Paulo VI. Familia ya Mungu Barani Afrika, kila mwaka ifikapo tarehe 29 Julai inaadhimisha kilele cha Siku ya SECAM Barani Afrika, lakini kwa mwaka huu, kwa vile siku hii inaangukia kati kati ya juma, kumbe kilele cha sherehe hizi ni Jumapili tarehe 2 Agosti 2020. Hii ni siku ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani, umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa watu wa Mungu Barani Afrika. Huu ni muda wa kutafakari kwa kina na mapana mafanikio, matatizo, changamoto na matumaini ya Kanisa Barani Afrika kwa siku za usoni.

Katika kipindi cha miaka 51 iliyopita, kumekuwepo na mafanikio makubwa na changamoto katika maisha na utume wa SECAM Barani Afrika. Mwaka 2019, Kanisa Barani Afrika limeadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu maadhimisho ya Sinodi ya Kwanza ya Maaskofu Barani Afrika ilipoadhimishwa kunako mwaka 1994 chini ya uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Familia ya Mungu inayowajibika, ikawa ni nguzo msingi katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili Barani Afrika. Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kujifunga kibwebwe ili kuendelea kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kama sehemu ya mchakato wa maisha na utume wa Kanisa katika kuinjilisha, ili kweli bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Watakatifu Mashahidi wa Uganda pamoja na watakatifu na wenye heri kutoka Barani Afrika wawe ni mifano bora ya kuigwa katika kumwilisha misingi ya imani, matumaini na mapendo miongozi mwa watu wa Mungu ndani na nje ya Bara la Afrika.

Kardinali Philippe Ouédraogo kutoka Burkina Faso, ambaye ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar, SECAM, katika ujumbe wake kwa Siku ya SECAM kwa Mwaka 2020 amekazia umuhimu wa kuendeleza mchakato wa uinjilishaji wa kina Barani Afrika. Waamini wajenge utamaduni wa kukutana na Kristo Yesu katika Neno la Sakramenti za Kanisa. Toba na wongofu wa ndani, uwasaidie waamini kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha tayari kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Waamini wajibidiishe kufahamu Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu inayowajibika Barani Afrika. Ni wakati wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga na kuendeleza misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu Barani Afrika.

Wongofu na mshikamano wa shughuli za kichungaji ni kati ya changamoto ambazo waasisi wa SECAM waliwataka watu wa Mungu Barani Afrika, kuzifanyia kazi, ili kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na hivyo kuendeleza utume wa kinabii Barani Afrika! Umefika wakati kwa familia ya Mungu Barani Afrika kuhakikisha kwamba, inajitegemea kwa mahitaji yake msingi, kwa rasilimali watu, fedha na vitu. Ili kufikia hatua hii, kuna haja ya kuendelea kujizatiti katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi Barani Afrika. Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa SECAM ilijenga matumaini makubwa kwa watu wa Mungu Barani Afrika. Lakini kwa bahati mbaya, janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 limekuwa na madhara makubwa sana kwa familia ya Mungu Barani Afrika.

Taarifa ya Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis inabainisha kwamba, watu wa Mungu Barani Afrika wameathirika sana na COVID-19. Kuna uhaba mkubwa wa ukosefu wa fursa za ajira, baa la njaa na umaskini vinaendelea kuongezeka kila kukicha, mchakato wa uzalishaji na huduma vimeathirika sana. Kuna baadhi ya nchi zimeathirika sana kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Kuna nchi ambazo zimeshambuliwa na Nzige wa jangwani na hivyo mambo yote haya kuchangia katika uvunaji haba wa mazao ya chakula na biashara! Zote hizi ni changamoto zinazoendelea kuwakabili watu wa Mungu Barani Afrika. Katika shida na mahangaiko yote haya, watu wa Mungu Barani Afrika hawana budi kuwa na imani, matumaini na mapendo thabiti kwa Mwenyezi Mungu, ambaye ni asili na chemchemi ya wema na utakatifu wote. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, matatizo na changamoto za maisha ya mwanadamu zimepata mwelekeo mpya.

Watu wa Mungu wanapaswa kuwa na ujasiri bila ya kukata wala kukatishwa tamaa. Waendelee kusali na kufuata ushauri wa madaktari na wataalam wa afya katika kupambana na Virusi vya Corona, COVID-19. Gonjwa hili limeonesha udhaifu wa binadamu na umuhimu wa kuendelea kushirikiana na kushikamana kama familia ya Mungu inayowajibika, kama njia ya kukabiliana na gonjwa hili la kutisha. Inasikitisha kuona kwamba, hata katika kukabiliana na janga la Virusi vya Corona, COVID-19, bado vita na mashambulizi ya kigaidi yameendelea kufanyika Barani Afrika. SECAM inapenda kuungana na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutoa wito wa kusitisha vita ili rasilimali na nguvu zaidi zielekezwe katika mapambano dhidi ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19. SECAM inapenda kuwashukuru na kuwapongeza watu wa Mungu Barani Afrika kwa kuendelea kujizatiti katika mchakato wa uinjilishaji wa kina licha ya changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza kila kukicha.

SECAM inazipongeza Serikali mbali mbali katika jitihada zao za kudhibiti ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Inawashukuru, madaktari, wahudumu wa sekta ya afya, wakleri na watawa waliojisadaka kwa ajili ya huduma makini kwa jirani zao. SECAM inawashukuru wafadhili na wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika kwa mchango wao. Ni matumaini ya SECAM kwamba, familia ya Mungu Barani Afrika itaendelea kupanua wigo wa maisha na utume wa SECAM na hivyo kuliwezesha Kanisa Barani Afrika kuwa ni chombo makini cha huduma, ili Bara la Afrika liweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. SECAM inawakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kusali na kuiombea kuanzia tarehe 29 Julai hadi tarehe 2 Agosti 2020, kilele cha Maadhimisho ya Siku ya SECAM kwa Mwaka 2020. SECAM inaendelea kupokea mchango kwa wale wote wanaoguswa na utume wake, kwani kwa mwaka 2020, mkazo umewekwa katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Siku ya SECAM 2020

 

27 July 2020, 09:50