Tafuta

Vatican News
Baraza la Makanisa Ulimwenguni Limetoa Tamko Kuhusiana na Serikali ya Uturuki kuligeuza Kanisa la Mtakatifu Sophia kuwa Msikiti kwa ajili ya waamini wa dini ya Kiislam. Baraza la Makanisa Ulimwenguni Limetoa Tamko Kuhusiana na Serikali ya Uturuki kuligeuza Kanisa la Mtakatifu Sophia kuwa Msikiti kwa ajili ya waamini wa dini ya Kiislam. 

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Tamko: Kanisa Kuu la Mt. Sophia!

Ni matumaini ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., kwamba, Kanisa kuu la “Hagia” yaani Mtakatifu Sophia halitakuwa tena ni sababu ya chokochoko, malumbano na mpasuko wa kidini kati ya Waislam na Wakristo nchini Uturuki. Mwaka 1934, Kanisa kuu la Mt. Sophia liligeuzwa kuwa ni Jumba la Makumbusho kwa watu wote wa Mungu nchini Uturuki; mahali pa kuwakutanisha watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Prof. Dr Ioan Sauca Kaimu Katibu Mkuu, Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., amemwandikia barua Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, akisikitishwa na uamuzi alioufanya wa kuligeuza Kanisa kuu la “Hagia” yaani Mtakatifu Sophia kuwa Msikiti kwa ajili ya waamini wa dini ya Kiislam. Ni matumaini ya Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwamba, Kanisa kuu la “Hagia” yaani Mtakatifu Sophia halitakuwa tena ni sababu ya chokochoko, malumbano na mpasuko wa kidini kati ya Waislam na Wakristo nchini Uturuki, bali chombo cha kuwaunganisha watu wa Mungu nchini Uturuki kama ilivyokuwa tangu mwaka 1934. Katika mwaka huo, Kanisa kuu la “Hagia” yaani Mtakatifu Sophia liligeuzwa kuwa ni Jumba la Makumbusho kwa watu wote wa Mungu nchini Uturuki; mahali pa kuwakutanisha watu kutoka ndani na nje ya Uturuki;  urithi wa watu wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo.

Jumuiya ya Kimataifa ilitamani kuona kwamba, Serikali ya Uturuki inaendelea kuheshimu uhuru wa kidini na hivyo kutorudia tena makosa yaliyotendwa katika historia ya Uturuki, ambako dini iligeuzwa kuwa ni chanzo cha vita, kinzani na mipasuko ya kidini. Baraza la Makanisa Ulimwengu ni chombo kinachoyaunganisha Makanaisa 350 kutoka katika nchi 110. Haya ni Makanisa yenye waamini zaidi ya nusu bilioni. Kumbe, barua hii ni kielelezo cha masikitiko ya waamini waamini wote wanaounda Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Kwa uamuzi wa Rais Recep Tayyip Erdogan, Uturuki  imejikuta ikitumbukia katika sera za utengano na migawanyiko kwa misingi ya kidini. Inasikitisha kuona kwamba, uamuzi huu umechukuliwa bila hata ya taarifa ya awali wala majadiliano na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) kwa sababu Kanisa kuu la Mtakatifu Sophia linatambuliwa na Umoja wa Mataifa kuwa ni sehemu ya urithi wa dunia kama ilivyobainishwa kwenye Itifaki ya Urithi wa dunia, “World Heritage Conversion”.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC katika miaka ya hivi karibuni, limekuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kudumisha misingi ya majadiliano ya kiekumene na kidini nchini Uturuki, ili kujenga na kudumisha madaraja ya watu kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi. Dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo nchini Uturuki, yanashirikishana tunu msingi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, licha ya tofauti zao msingi. Baraza la Makanisa Ulimwenguni, limeendelea kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini. Kumbe, uamuzi wa kuligeuza Kanisa kuu la Mtakatifu Sophia kuwa Msikiti kwa ajili ya waamini wa dini ya Kiislam kutoka kwenye matumizi yake ya awali yaani Jumba la Makumbuko nchini Uturuki, kumesababisha hofu, wasi wasi na hali ya kutokuaminiana na hivyo kuhatarisha juhudi za kutaka kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa waamini wa dini na madhehebu mbali mbali nchini Uturuki.

Uamuzi huu, utaathiri kwa kiasi kikubwa mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam na hivyo kudhohofisha ushirikiano miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali nchini Uturuki. Kinzani na mipasuko ya kidini ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Kitendo cha Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki kugeuza historia iliyokuwa imeandikwa kunako mwaka 1934 kwa kutambua Kanisa kuu la Mtakatifu Sophia kuwa ni Jumba la Makumbusho na urithi wa dunia ni hatari sana. Maelewano na mafungamano ya kijamii, uhuru wa kidini, majadiliano na ushirikiano ni mambo ambayo kwa sasa yameingia “mchanga”.Uamuzi wa mwaka 1934 ulisaidia sana kujenga na kuimarisha umoja wa kitaifa kwa kuondokana na kinzani pamoja chuki zisizokuwa na mvuto wala mashiko. Ni matumaini ya Baraza la Makanisa Ulimwengu kwamba, Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki ataweza tena kutafakari uamuzi wake na hatimaye kubatilisha uamuzi huu, ili Kanisa kuu la Mtakatifu Sophia, lisigeuzwe tena na kuwa ni chanzo cha vita, chuki na uhasama wa kidini, bali liwe ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa kitaifa, amana na urithi wa dunia nzima kama ilivyobainishwa kunako mwaka 1934.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC.
13 July 2020, 07:27