Tafuta

Familia ya Mungu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, tarehe 28 Julai 2020 imeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumsindikiza Marehemu Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwenye usingizi wa amani. Familia ya Mungu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, tarehe 28 Julai 2020 imeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumsindikiza Marehemu Rais Mstaafu Benjamin Mkapa kwenye usingizi wa amani.  

Yaliyojiri Ibada Ya Misa Takatifu ya Kumwombea Rais Ben Mkapa!

Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea na kumuaga Rais Mstaafu Bennjamin William Mkapa. Ibada ya Buriani kwa Marehemu ni kumkabidhi kwake kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa, kwa imani na matumaini ya ufufuko wa wafu. Ibada ya Buriani imeongozwa na Askofu mkuu mstaafu Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anasadiki na kufundisha kuhusu ufufuko wa wafu na uzima wa ulimwengu ujao. Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka la Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu, ambaye ndani mwake mna tumaini moja. Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu “huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Bwana” Kwa maana hii, kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo kwa kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme wa mbinguni uliotangulizwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi.

Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa Jimbo kuu la Dar es Salaam, tarehe 28 Julai 2020 amemsindikiza mtoto wake Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin William Mkapa mpaka mwisho wa safari yake, ili kumweka mikononi mwa Mwenyezi Mungu. Kanisa linamtolea Mwenyezi Mungu katika Kristo Yesu mtoto wa neema yake, na katika tumaini linaikabidhi ardhi mbegu ya mwili utakaofufuliwa katika utukufu. Katika wosia wake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mzee Benjamin William Mkapa, Mkristo Mkatoliki aliyekuwa anaishi katika Parokia ya Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, Upanga, Jimbo kuu la Dar es Salaam, alisema, siku atakapofariki dunia, apelekwe Parokiani Upanga, mahali alipokuwa anashiriki maisha na utume wa Kanisa, ili aweze kuombewa na kuagwa kwa Ibada ya Misa Takatifu. Katika maisha yake kama kiongozi mkuu wa nchi lakini zaidi kama mwamini mlei, Mzee Benjamin William Mkapa alishiriki Ibada mbali mbali kwa: Unyenyekevu, uaminifu, imani na uchaji.

Mzee Benjamin William Mkapa, alijijengea utamaduni wa kuwahi Kanisani ili kujiandaa kikamilifu kwa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu. Alikuwa ni mwanaparokia hodari na aliyeshiriki kikamilifu hata katika Jumuiya ndogondogo za kikristo. Na kwa njia hii, akamshuhudia Mwenyezi Mungu kwa njia ya imani thabiti, maisha ya sala, shukrani na majitoleo mbali mbali. Sasa waamini wa Parokia ya Upanga na Jimbo kuu la Dar es Salaam katika ujumla wake, wanamwomba Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze sasa kumpokea mtumishi wake Mzee Benjamin William Mkapa na hatimaye, kumstahilisha maisha na uzima wa milele. Mwenyezi Mungu awajalie watanzania wote kuupokea msiba huu kwa imani, matumaini na mapendo.

Marehemu Rais Mstaafu Mkapa alikuwa daima ni mtu wa shukrani kwani falsafa ya neno asante ni kuomba tena neema na baraka za Mwenyezi Mungu katika maisha. Kunako mwaka 1991 aliadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Ndoa yake Takatifu, akamshukuru Mungu. Mwaka 2005 alipong’atuka kutoka madarakani, akarudi tena Parokiani Upanga, kumshukuru Mungu kwa zawadi ya kuweza kuwaongoza watanzania katika misingi ya ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi. Kunako mwaka 2013, akamshukuru Mungu kwa zawadi ya Injili ya uhai kwa kutimiza miaka 75 tangu kuzaliwa kwake, Ibada ya Misa Takatifu ikaadhimishwa na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Tarehe 28 Julai 2020 imekuwa ni zamu ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Mzee Benjamin William Mkapa. Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea na kumuaga Rais Mstaafu Bennjamin William Mkapa. Kadiri ya Mapokeo ya Mama Kanisa, Ibada ya Buriani kwa Marehemu ni kumkabidhi kwake kwa Mwenyezi Mungu kwa njia ya Kanisa, kwa kuamini kwamba, wanaoishi kwa ajili ya Kristo na kwa sasa wameungana na Kristo na kwamba, siku moja wataenda wote na kuwa pamoja na Kristo Yesu. Ibada ya Buriani imeongozwa na Askofu mkuu mstaafu Josaphat Louis Lebulu wa Jimbo kuu la Arusha. Huyu ni kati ya viongozi wa Kanisa Katoliki Tanzania waliofanya naye kazi kwa karibu wakati akiwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Askofu mkuu Yuda Thaddaeus Ruwa'ichi katika mahubiri yake amewatafakarisha watu wa Mungu nchini Tanzania kuhusu Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, mwamini anafanywa huru toka dhambi na kuzaliwa upya kama mtoto wa Mungu, na hivyo kuwa ni kiungo cha Kristo Yesu na kuingizwa Kanisani anakofanywa kuwa ni mshiriki wa utume wake wa: kikuhani, kinabii na kifalme. Kwa Ubatizo, waamini wanakuwa ni Hekalu la Roho Mtakatifu. Waamini wanafarijika na kukumbushwa kwamba, kifo si hatima ya maisha ya binadamu, bali ufufuko na maisha ya uzima wa milele. Hii ni sehemu ya Fumbo la imani ambalo limefunuliwa kwao kwa njia ya Kristo Yesu. Waamini wanafundishwa na Kristo Yesu kuwa kweli ni watu wa shukrani kwa kusema, “Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendeza mbele zako.” Mt. 11: 25-26. Watu wenye hekima na akili wanaotajwa katika Maandiko Matakatifu ni wasomi na wajanja wa ulimwengu huu.

Lakini  hekima na ujuzi wa kweli, uwasaidie waamini kuunganishwa kwenye ufunuo wa Mungu. Mama Kanisa anatafakari kuhusu Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu kwa kuamini kwamba, Rais Mstaafu Benjamini William Mkapa atafufuka pamoja na wateule wa Mungu katika uzima wa milele. Hii ni imani katika ufunuo wa Mwenyezi Mungu ambaye ni: tumaini, faraja na kimbilio la mwanadamu. Kumbe, kuna haja kwa waamini kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kwa majonzi na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu; kwa furaha na yale yote wanayoyabeba katika maisha yao ya kila siku. Kristo Yesu anawaalika waja wake, akisema, “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.” Mt. 11: 28-30.

Msiba wa Rais Mstaafu Benjamini William Mkapa ni jambo na mzigo mzito sana kwa watanzania na watu wote wenye mapenzi mema, lakini watanzania wasiubebe peke yao, bali pamoja na Kristo Yesu aliyeshinda dhambi na mauti; huyu ndiye Mtakatifu wa Mungu. Yesu anawaalika waja wake kujitwika nira yake kwani mzigo wake ni mwepesi kuchukua na wajitahidi kujifunza kutoka kwake, kwa sababu yeye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo. Hata katika msiba na majonzi haya makubwa, watanzania wakimbilie na kujiaminisha kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili aweze kuwa ni faraja na kitulizo chao; imani na matumaini yao thabiti. Mwenyezi Mungu kwa wema, upendo na huruma yake ya daima, amjalie Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa mwanga na pumziko la milele.

Mwenyezi Mungu amsamehe yale yaliyopungua katika ufuasi wake kama Mkristo, majitoleo yake, katika kuamini na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika hali na mazingira haya, Mwenyezi Mungu pia awatazame kwa wema na huruma watanzania ambao nao wako bado safarini, ili siku moja waweze kuungana na Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa. Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, awasamehe pia dhambi na mapungufu yao ya kibinadamu! Ibada hii ya Misa takatifu imehudhuriwa pia na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga wa Jimbo kuu la Mbeya ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania pamoja na Maaskofu kadhaa bila kuwasahau watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania, wanaoshiriki tukio hili la huzuni na majonzi makubwa!

Mkapa 1938-2020

 

28 July 2020, 13:52