Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linawapongeza Rais pamoja na Makamu wake wa Rais bila kusahau juhudi na weledi uliotekelezwa na Tume ya Uchaguzi Nchini Malawi, MEC. Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linawapongeza Rais pamoja na Makamu wake wa Rais bila kusahau juhudi na weledi uliotekelezwa na Tume ya Uchaguzi Nchini Malawi, MEC.  (AFP or licensors)

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi Linampongeza Rais Chakwera!

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, ECM linapenda kuonesha matumaini yake kwamba, Dr. Chakwera ataweza kusimama kidete kutekeleza ahadi zake kwa wananchi wa Malawi. Hususan kwa kupambana na saratani ya rushwa, wizi na ufisadi wa mali ya umma. Kwa kujikita katika utekelezaji wa utawala bora unaoheshimu: katiba na sheria pamoja na kuendelea kuboresha maisha ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, ECM, linampongeza Dr. Lazarus McCarthy Chakwera, Rais wa Malawi na Dr. Saulos Klaus Chilima, Makamu wa Rais nchini Malawi kwa kuibuka kidedea kwenye uchaguzi mkuu wa marudio uliofanyika tarehe 23 Juni 2020 na hatimaye, mshindi kupatikana. Tume ya Uchaguzi nchini Malawi, ikamtangaza Dr. Lazarus McCarthy Chakwera kuwa Rais na hatimaye, kuapishwa rasmi, Jumapili tarehe 28 Juni 2020, huko Lilongwe, nchini Malawi. Dr. Lazarus McCarthy Chakwera Rais wa Malawi amesema, huu ni ushindi wa demokrasia na haki kwa wananchi wa Malawi wapatao milioni 18. Hiki ni kielelezo cha kiu ya wananchi wa Malawi, wanaotaka kushuhudia mageuzi makubwa katika medani mbali mbali za maisha yao.

Hii ni heshima kubwa kwa wananchi wa Malawi, kutoa fursa ya uongozi kwa Chama cha Upinzani. Serikali mpya kwa sasa ina jukumu la kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kuondokana na ndago ya ukabila, kikwazo kikubwa cha maendeleo, ustawi na mafao ya wengi. Huu ni wakati wa kupambana na umaskini, ujinga na njaa, ili kuwajengea wananchi uwezo wa kutimiza ndoto zao za maisha. Hii ni Serikali inayopaswa kuongoza; kwa kusikiliza na kujibu matamanio halali ya wananchi wa Malawi. Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, ECM linapenda kuonesha matumaini yake kwamba, Rais mpya wa Malawi ataweza kusimama kidete kutekeleza ahadi zake kwa watu wa Mungu nchini Malawi. Hususan kwa kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa, wizi na ufisadi wa mali ya umma. Atajikita zaidi katika utekelezaji wa utawala bora unaoheshimu na kuzingatia: katiba na sheria za nchi sanjari na kujielekeza zaidi katika maboresho ya huduma za kijamii, kiuchumi, kiafya na kielimu zinazotolewa na Serikali kwa watu wa Mungu nchini Malawi.

Dr. Lazarus McCarthy Chakwera kwa sasa ndiye kiongozi mkuu wa nchi, kumbe, anapaswa kuwa ni kielelezo cha umoja, mshikamano na mafungamano ya watu wa Mungu nchini Malawi, ili kuvunjilia mbali ukabila na upendeleo, mambo ambayo yalikuwa yameanza kuota mizizi katika akili na mawazo ya watu, kiasi hata cha kuhatarisha umoja na mshikamano wa kitaifa! Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linaipongeza Tume ya Uchaguzi nchini Malawi, MEC, kwa kuendesha mchakato mzima wa uchaguzi kwa weledi na kwa kuzingatia: sheria, kanuni na taratibu za nchi, jambo ambalo limeiwezesha Malawi kurudia tena uchaguzi mkuu hapo tarehe 23 Juni 2020 na hatimaye, mshindi wa halali kupatikana. Licha ya Tume ya Uchaguzi Nchini Malawi, MEC kukabiliwa na ukata wa fedha, lakini imeliwezesha Malawi kurudia uchaguzi mkuu, hali ambayo imesaidia kujijengea heshima kubwa mbele ya wananchi wa Malawi, katika umaskini wao, wameonesha ile kauli mbiu ya “Maskini Jeuri”.

Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi, linavipongeza Vikosi vya Ulinzi na Usalama nchini Malawi, kwa kusimama kidete kulinda usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda vituo vya kupigia kura pamoja na masanduku ya kura, ili kweli haki iweze kutendeka na mshindi kupatikana kadiri ya matakwa ya watu wa Mungu nchini Malawi. Jeshi la Polisi nchini Malawi, limewashughulikiwa wale wote waliokuwa wanataka kuvunja sheria kwa mujibu wa sheria, jambo ambalo linapaswa kupongezwa na kuungwa mkono na wapenda amani. Baraza la Maaskofu Katoliki Malawi linawapongeza wadau wote waliohakikisha kwamba, uchaguzi mkuu unafanikiwa kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi, haki na amani. Sasa ni wakati wa kuendelea kuombea mchakato wa ujenzi wa haki, amani, umoja wa kitaifa, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu nchini Malawi.

Maaskofu Malawi 2020
05 July 2020, 14:17