Tafuta

Vatican News
Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara, amewataka vijana kujitambua ili hatimaye, waweze kuziishi ndoto zao kikamilifu. Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara, amewataka vijana kujitambua ili hatimaye, waweze kuziishi ndoto zao kikamilifu.  (Vatican Media)

Askofu Titus Mdoe: Vijana Dunia ni Tambara Bovu! Jichungeni!

Askofu Mdoe amewataka vijana kujitambua jinsi walivyo na kujitahidi kuziishi ndoto zao ili waweze kufikia malengo yao, kwa kujibidiisha. Wanapaswa kuwa ni vijana safi na wachamungu kwa sababu wamepata malezi makini: kiroho, kiutu na kiakili. Wajitahidi kuwa ni wasomi wanaojali: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huko ulimwenguni wanakokwenda, wawe ni faida kwa jirani zao.

Na Godfrey Mahonge- Mtwara na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anawahamasisha vijana kufikiri na kutenda katika mwanga wa kweli za Kiinjili. Kwa njia hii, wataweza kupyaisha maisha, kwa kuuvua utu wa kale na hivyo kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Upya wa maisha katika Kristo Yesu ni kielelezo cha hekima na busara ya wafuasi wa Kristo wanaotoa mwanya ili huruma na upendo wa Mungu viweze kung’aa na kushuhudiwa hapa ulimwenguni. Kanisa lina utajiri na amana kubwa ya uzoefu na mang’amuzi ya watakatifu waliokuwa wadhambi, lakini wakatubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao, leo hii ni mifano bora ya kuigwa na familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Utakatifu wa maisha ni mapambano endelevu katika maisha ya waamini. Vijana wa kizazi kipya wanahimizwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kiinjili.Upendo wa Kikristo ni amana na utajiri unaotoa utambulisho wa maisha ya mwamini, kama sehemu ya maandalizi ya kurithi maisha na uzima wa milele.

Vijana wanatakiwa kujipatia muda, kwa kujiweka katika nafasi zitakazoweza kuwasaidia kujifahamu zaidi, kwamba wanataka kuwa nani katika maisha. Vijana wawe na msimamo thabiti katika maisha na wala wasiwe ni watu wa bendera kufuata upepo. Hili ni angalisho ambalo limetolewa hivi karibuni na Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara, wakati wa adhimisho la Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Mahafali ya Kidato cha Sita, kwenye Shule ya Sekondari ya Aquinas inayomilikiwa na Jimbo Katoliki la Mtwara na kuongozwa na Shirika la Masista Wamisionari Wabenediktini wa Tutzing. Askofu Mdoe amewataka vijana hao kujitambua jinsi walivyo na kujitahidi kuziishi ndoto zao ili waweze kufikia malengo yao, kwa kujibidiisha. Kazi ya waalimu na walezi ni kusaidia mioyo na dhamiri zao nyofu kuridhika, ili waweze kutimiza hamu ya mioyo yao. Wanapaswa kuwa ni vijana safi na wachamungu kwa sababu wamepata malezi makini: kiroho, kiutu na kiakili. Wajitahidi kuwa ni wasomi wanaojali: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huko ulimwenguni wanakokwenda, wawe ni faida kwa jirani zao.

Vijana wasijivunie tu elimu ya kidato cha sita, wakadhani kwamba, huo ndio mwisho wa mapambano ya maisha! Bali wajitahidi kufanana na kiwango cha elimu walichopata na kamwe wasiwe ni kero mitaani. Askofu Mdoe ametanabaisha kwamba, wasije wakalewa sifa kutoka kwa jamii na hatimaye, kupoteza, utu na heshima yao. Wanafunzi hawa wametakiwa kuwa ni mabalozi wema wa Shule ya Sekondari ya Aquinas, kwa waalimu na walezi, wajiojisadaka ili kuhakikisha kwamba, wanapata elimu bora itakayowasaidia kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Wakumbuke kwamba, wakilogwa na hatimaye, kukengeuka, watakuwa wanawaaibisha wazazi na hata walezi wao. Wawe ni mifano bora ya kuigwa kwa jamii kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao yenye mvuto na mashiko! Kamwe wasitumie majina na elimu yao vibaya, kwa kuwarubuni watu, bali wawe ni faida kwa jamii inayowazunguka kwa matendo mema. Wakumbuke kwamba, wameitwa na kutumwa katika ulimwengu mamboleo wenye mazuri, matatizo na changamoto zake.

Yote haya wayakabili kwa mwanga wa Injili. Wale watakaobahatika kuendelea na elimu kwenye taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu, waendelee kukuza na kudumisha kanuni maadili na utu wema; waendelee kuwa wachamungu na watu wenye hekima na busara katika kufikiri na kutenda. Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara amewakumbusha vijana kwamba, UKIMWI bado upo na janga la virusi vya Corona, COVID-19 bado linaendelea kuwatesa watu sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, wanapaswa kuwa makini kufuata ushauri wa madaktari na wataalam wa afya. Kamwe wasibweteke na kudhani kwamba, UKIMWI na CORONA kwa sasa vimepewa kisogo.

Askofu Titus Mdoe

 

 

 

11 July 2020, 07:22