Askofu Salutaris Melchior Libena, Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, baada ya kufuru Kanisa la Parokia ya Modeko, Jimbo Katoliki Morogoro, ametabaruku Kanisa hilo! Askofu Salutaris Melchior Libena, Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, baada ya kufuru Kanisa la Parokia ya Modeko, Jimbo Katoliki Morogoro, ametabaruku Kanisa hilo! 

Kufuru Parokia ya Modeko Morogoro: Tabernakulo na Kanisa Vyatabarukiwa!

Kitendo cha kuiba Tabernakulo ikiwa na Komunyo Takatifu ni tukio ambalo liligusa imani, kikawajaza waamini uchungu mkubwa. Tabernakulo ni mahali ambapo Ekaristi Takatifu inahifadhiwa kwa heshima kubwa. Ni mahali pa kusujudiwa na kuabudiwa kwani ndani mwake yumo Yesu Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai. Na Kanisa ni Hekalu la Mwenyezi Mungu, nyumba ya Ibada na Sala.

Na Angela Kibwana, Morogoro Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. –Vatican.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walifanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa mintarafuLiturujia Takatifu kwa kutambua nafasi ya Liturujia katika Fumbo la Kanisa, kwani, Liturujia ni chemchemi na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kanisa, kimsingi lina asili mbili: ile ya Kimungu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu na asili ya Kibinadamu kwa sababu linawaambata binadamu. Hivyo Liturujia ya kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa, wawe Hekalu la Roho Mtakatifu, Makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo. Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumtangaza  na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Lengo ni kujenga na kudumisha: umoja na mshikamano wa watoto wa Kanisa. Liturujia ni muhimu kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa kwa njia ya Kristo Yesu.

Liturujia ni utekelezaji wa kazi ya Kikuhani ya Kristo Yesu.Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Liturujia, Ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa Fumbo wa Kristo Yesu, yaani Kanisa. Hili ni tendo takatifu katika maisha na utume wa Kanisa. Mama Kanisa anaendelea kuwachangamotisha viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika malezi makini ya Kiliturujia pamoja na ushiriki hai wa waamini. Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya Liturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji! Hii ndiyo tabia ya Liturujia na kwa sababu ya Sakramenti ya Ubatizo, ni haki na wajibu wa waamini, ambao kimsingi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki wa Mungu. Liturujia ni chemchemi ya kwanza ambayo mwamini anaweza kuchota roho ya kweli ya kikristo.

Ni katika muktadha huu, hivi karibuni, Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara, Tanzania, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Idara ya Liturujia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC), amebariki Tabernakulo mpya na kutabaruku Kanisa la Parokia ya Bikira Maria Mtakatifu, Modeko, Jimbo Katoliki la Morogoro, baada ya wezi kufanya kufuru kwa mambo matakatifu Parokiani hapo kunako tarehe 26 Aprili 2020. Na Mheshimiwa Padre Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro nchini Tanzania, baada ya kuwasiliana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC) na Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania, kuanzia tarehe 27 Aprili 2020 Kanisa la Parokia ya Modeko likafungwa. Mababa wa Kanisa wanathibitisha kuwa, kwa nguvu ya imani ya Kanisa na uwezo wa Neno la Kristo Yesu, na tendo la Roho Mtakatifu, kwamba, mageuzo ya Mkate na Divai yanakuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo.

Kitendo cha kuiba Tabernakulo ikiwa na Komunyo Takatifu ni tukio ambalo liligusa na kutikisa imani, kikawajaza waamini majonzi na uchungu mkubwa. Kwa mwamini Mkatoliki, Tabernakulo ni mahali patakatifu sana, yaani ni mahali ambapo Ekaristi Takatifu inahifadhiwa kwa heshima kubwa. Ni mahali pa kutazamwa, kusujudiwa na kuabudiwa kwa sababu ndani mwake yumo Yesu Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai. Na Kanisa ni Hekalu la Mwenyezi Mungu, nyumba ya Ibada na Sala. Askofu Salutaris Melchior Libena katika mahubiri yake amewakumbusha waamini kwamba, wanao wajibu wa kuyalinda matakatifu ya Mungu yaliyomo ndani ya Kanisa. Wanao wajibu wa kulinda na kudumisha imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, Jengo la Kanisa, Sakramenti pamoja na Visakramenti vilivyomo. Waamini wasikubali kutoa mwanya kwa watu waovu kuvuruga msingi wa imani yao.

Baada ya huduma ya maisha ya kiroho na kichungaji kurejeshwa tena kwenye Kanisa la Parokia hii, Askofu Libena amewataka waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kuabudu Ekaristi takatifu, ili waweze kujichotea baraka na neema kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Waamini wajenge mazoea ya kuadhimisha Ibada mbali mbali nje na Ibada ya Misa Takatifu ili kuimarisha maisha yao ya kiroho na kiutu! Kumekuwepo na mahangaiko makubwa kwa waamini wa Parokia ya Modeko baada ya huduma za kiroho na kichungaji kusitishwa Kanisani hapo! Hali hii ilisababisha uchungu wa ndani na ukame wa maisha ya kiroho. Tukio hili la kihistoria, lilitanguliwa na semina kuhusu Umuhimu wa Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na maisha ya kiroho, ili kuwawezesha waamini kutambua uzito wa kufuru iliyokuwa imetendwa kwenye Kanisa hili.

Waamini wa Parokia hii, wamekuwa ni barua wazi inayoonesha mateso na mahangaiko ya ndani kutokana na kufuru kwa Ekaristi Takatifu. Huu ni wakati wa kuimarisha: imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, bila ya mkanganyiko wa mambo. Huu ni upendo unaodai sadaka na majitoleo makubwa kutoka kwa waamini wenyewe. Katika mateso na mahangaiko ya waamini wa Parokia ya Modeko, Jimbo Katoliki la Morogoro, wameonja pia umoja na mshikamano kutoka kwa waamini wa Majimbo mengine kwa kuguswa na kashfa hii. Kwa namna ya pekee kabisa, familia ya Mungu Parokia ya Modeko, inamshukuru na kumpongeza Mama Catherine Kagombola kutoka Parokia ya Kristo Mfalme, Tabata, Jimbo kuu la Dar es Salaam aliyejisadaka kununua Tabernakulo mpya na kumkabidhi Msimamizi wa Kitume, Jimbo Katoliki la Morogoro.

Waamini wengine walishiriki kwa hali na mali na mchango wao, umekuwa ni msaada mkubwa katika kulikarabati Kanisa la Parokia ya Modeko, leo hii lina mwonekano mpya kabisa. Mama Catherine Kagombola, amefananishwa na Mtakatifu Veronica aliyethubutu kujitokeza hadharani ili kuupangusa Uso wa Yesu uliokuwa umetapakaa damu bila kuogopa uwepo wa askari na maneno ya watu! Kimekuwa ni kipindi ambacho waamini mbali mbali wameibua vipaji vya ubunifu, ili kuhakikisha kwamba, hali ya maisha ya kiroho na shughuli za kichungaji zinarejea tena kama kawaida! Naye Mheshimiwa sana Padre Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro, amelishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa ushirikiano lililompatia tangu mwanzo wa tukio hili hadi kufikia hatua ya kutabaruku tena Kanisa la Parokia ya Modeko. Amewashauri waamini Parokiani hapo kuendelea kufanya toba na wongofu wa ndani, ili waendelee kupata neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ikumbukwe kwamba, kufuru ni matukio ambayo yanasababisha mateso na machungu makubwa katika imani ya watu, hasa kwa kuchezea mambo matakatifu. Hii ni hatari sana katika mshikamano na mafungamano ya kijamii, kama familia ya watu wa Mungu wanaojaliana na kusaidiana!

Itakumbukwa kwamba, Padre Nikodemas Masong, Paroko wa Parokia ya Modeko, Jimbo Katoliki la Morogoro alisema, watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi tarehe 27 Aprili 2020 walivamia na kuvunja mlango wa Kanisa la Parokia ya Modeko na kufanikiwa kuiba Tabernakulo iliyokuwa inahifadhi Ekaristi Takatifu na kutokomea mahali kusikojulikana. Walivunja pia milango ya ofisi za Parokia na kufanikiwa kuiba kiasi cha shilingi laki tatu na nusu, mali ya Chama cha Watumishi wa Altare Parokiani hapo. Walifanikiwa pia kuiba “Mixer” inayotumika kwa ajili ya mawasiliano Parokiani hapo! Familia ya watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Morogoro imesikitishwa sana na kufuru hizi dhidi ya mahali na mambo matakatifu yanayogusa undani wa imani ya watu! Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu kama inavyojulikana na wengi: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini, kwa mwaka 2019, aliwaalika waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa takatifu; Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kushiriki kikamilifu kwa ibada na heshima kuu wakati wa maandamano ya Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kristo katika maisha ya waja wake, Kristo anayeandamana na wafuasi wake, bega kwa bega!

Waamini waoneshe moyo wa upendo kwa kushikamana na Kristo katika safari ya maisha yao, kwa kujiandaa kikamilifu, ili kuweza kumpokea! Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini chakula cha uzima wa milele na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha, uzima na utukufu wa Baba wa milele! Ekaristi Takatifu inajenga fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila Mwaka Mama Kanisa anayofuraha kubwa ya kusherehekea na kushuhudia Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa kwa maandamano makubwa, ushuhuda kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuandamana na waja wake katika historia ya maisha yao ya kila siku hadi utimilifu wa dahali. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Umoja, inayowaunganisha waamini kuwa ni mwili mmoja na watu watakatifu wa Mungu. Mwamini anayepokea Ekaristi takatifu anakuwa ni chombo cha umoja, kwani ndani mwake kunaibuka “vinasaba ya maisha ya kiroho” vinavyosaidia kujenga umoja. Mkate wa Umoja unasaidia kuvunjilia mbali tabia ya kujiona kuwa ni bora zaidi kuliko wengine; watu wanaopenda kuwagawa wengine kwa mafao binafsi; watu wenye wivu na umbea unaohatarisha umoja na mshikamano. Waamini kwa njia ya kuliishi kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu: wana mwabudu na kumshukuru Kristo Yesu, kwa zawadi hii kubwa; kumbu kumbu hai ya upendo wake unaowaunganisha wote kuwa ni mwili mmoja na kuwaelekeza katika ujenzi wa umoja.

Parokia ya Modeko, Morogoro
11 July 2020, 14:12