Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi: Sakramenti ya Kipaimara inawaimarisha waamini kuwa: Manabii wa Ukweli wa Mungu, Walimu wa Imani na Watakatifu ili kuyatakatifuza malimwengu! Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi: Sakramenti ya Kipaimara inawaimarisha waamini kuwa: Manabii wa Ukweli wa Mungu, Walimu wa Imani na Watakatifu ili kuyatakatifuza malimwengu! 

Askofu mkuu Ruwaichi: Kipaimara: Manabii, Walimu na Watakatifu!

Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara waamini wameimarishwa na kuwa Manabii wa Ukweli wa Mungu wanaopaswa kuusimamia na kuutangaza. Wao wameimarishwa na kuwa ni walimu wa imani wanayopaswa kuwashirikisha jirani zao. Imani hii inapaswa kukomaa na kuwa sahihi na thabiti. Wamewekwa wakfu kwa njia ya Roho Mtakatifu ili kuyatakatifuza malimwengu na jirani zao, kazi kwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, Jumapili tarehe 19 Julai 2020 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Mtakatifu Francis Xaveri, Chango’ombe, Jimbo kuu la Dar Es Salam na kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 51. Waamini hawa wataendelea kupata katekesi ya kina kuhusu Sala ya Nasadiki kama msingi wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hii ni imani inayofafanuliwa kwa kina katika Katekesimu ya Kanisa Katoliki, muhtasari wa Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Maisha ya Sala. Lengo ni kuwawezesha waamini walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara, waweze kupalilia imani ambayo inapaswa kusimika mizizi yake katika maisha yao. Huko ambako wanaishi na kwa sasa wanatumwa na Mama Kanisa kushuhudia imani yao kuna: fursa, hatari na changamoto zake. Kuna watu wasiolipenda Kanisa, kuna watu watakaowarubuni na kuwapeleka “mchaka mchaka kama daladala iliyokatika usukani”.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi amewataka vijana walioimarishwa kamwe wasikuyakubali hayo! Bali wasimame imara katika imani, maadili na utu wema. Kwa sababu, kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara wameimarishwa na kuwa Manabii wa Ukweli wa Mungu wanaopaswa kuusimamia na kuutangaza. Wao wameimarishwa na kuwa ni walimu wa imani wanayopaswa kuwashirikisha jirani zao. Imani hii inapaswa kukomaa na kuwa sahihi na thabiti. Wamewekwa wakfu kwa njia ya Roho Mtakatifu ili kuyatakatifuza malimwengu na jirani zao. Kumbe, wanapaswa kupania kwa neema ya Mungu kuyatekeleza haya yote kwa ari na moyo mkuu! Sakramenti hii ni kielelezo cha wema na huruma ya Mungu kwa waja wake. Kumbe, waamini wanahitaji nguvu ya pekee, kuweza kupokea na kuambata wema na huruma ya Mungu. Nguvu hii ni zawadi ya Roho Mtakatifu ambaye huwasaidia waamini katika udhaifu wao, kwa maana hawajui kuomba jinsi ipasavyo.

Kwa mara ya kwanza, waamini hawa walimpokea Roho Mtakatifu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara muungano wa wabatizwa na Kanisa hufanywa kuwa mkamilifu zaidi, kwani wanatajirishwa kwa nguvu pekee ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuineza na kuitetea imani, kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu. Kwa njia ya Sakramenti hii, hupata “alama”, mhuri wa Roho Mtakatifu anayewaimarisha na kuwatuma kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Vijana walioimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara wanapaswa kuichukulia kwa uzito Sakramenti hii, kwani inawakomaza na kuwakirimia Roho Mtakatifu Mfariji na Zawadi ya Baba wa milele.

Huyu ndiye yule Roho wa kweli, anayewajalia akili ya kusikiliza na ujasiri wa kutekeleza maneno yake. Huyu ndiye Roho Mtakatifu, Paji na Upendo wa Baba wa Mbinguni anayemiminwa kwenye sakafu ya kila moyo wa Mkristo. Roho Mtakatifu Mfariji, anawaongoza, anawaangaza na kuwaimarisha, ili kila mmoja wao, aweze kutembea katika hija ya maisha bila wasi wasi na mashaka hata pale anapokumbana na adui pamoja na vikwazo; wakati wa raha na machungu, daima akiwa imara na thabiti katika njia ya Kristo Yesu. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi anasema, Roho Mtakatifu anawadai kunafsisha imani katika matendo, ili ushuhuda wao uweze kuwa thabiti, wakiwa na uelewa sahihi wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi amegusia kuhusu sifa kuu ya Mungu kuwa ni huruma inayofunuliwa katika uvumilivu. Kwa njia ya upendo wake usiokuwa na kikomo, Mwenyezi Mungu amemtuma Mwanaye wa Pekee, Kristo Yesu, ili aje ulimwenguni: kuwafundisha, kuwakomboa na kuwapatanisha watu na Mungu. Waamini watumie vyema zawadi ya uhai na imani, kutubu na kumwongokea Mungu. Hii ndiyo hekima ya Mungu anaporuhusu magugu kukua pamoja na ngano; wadhambi kustawi na waadilifu. Hii ni changamoto endelevu, ya kuacha dhambi, kujirudi na kuanza tena. Mwenyezi Mungu hamkatii mwanadamu tamaa, wala hataki kumpatiliza, bali anataka: ustawi, maendeleo na mafao ya waja wake. Anawatakia mema na wokovu wao, kama watoto wapendelevu wa Mungu!

Kipaimara DSM

 

20 July 2020, 13:48