Askofu Mkuu Renatus Nkwande amesema, Mapadre ni vyombo vya imani, matumaini na mapendo miongoni mwa watu wa Mungu waliowekwa chini ya usimamizi wao! Askofu Mkuu Renatus Nkwande amesema, Mapadre ni vyombo vya imani, matumaini na mapendo miongoni mwa watu wa Mungu waliowekwa chini ya usimamizi wao! 

Askofu mkuu Nkwande: Mapadre ni Vyombo vya Faraja na Matumaini

Askofu mkuu Nkwande amesema Mapadre wanaendeleza utume wa Yesu, ambaye ni Kuhani mkuu na mkombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unajionesha katika Fumbo la Umwilisho, kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu kati pamoja na waja wake. Yeye ndiye “Emmanuel yaani Mungu pamoja na nasi”.

Na Nikas Kiuko, Mwanza; Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuhusu dhana na utambulisho wa Mapadre, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili anasema, Mapadre ni wawakilishi wa kisakramenti wa Yesu Kristo, kiongozi na mchungaji ambao kwa mamlaka waliyopewa hutangaza Neno lake na huendeleza kazi yake ya ukombozi kwa njia ya Sakramenti za Kanisa. Lakini hasa ni Sakramenti za: Ubatizo, Kitubio na Ekaristi Takatifu wakiyatolea mapendo yao kama zawadi ya nafsi zao nzima kwa kundi walilokabidhiwa ili walikusanye na kulipeleka kwa Baba wa milele kwa njia ya Kristo Yesu katika Roho Mtakatifu. Kimsingi Mapadre wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Katika maisha na wito wao, Mapadre wakuze moyo wa sala, tafakari ya Neno la Mungu, maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kwa ibada na uchaji.

Mapadre wajenge utamaduni wa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Mapadre wawe ni chachu ya upendo ambao unafumbatwa katika: umoja, amani na mshikamano wa kweli. Mapadre wawe ni mashuhuda wa kutenda wema, kwa kutambua kwamba, hii ni changamoto kwa binadamu wote kutendeana wema, kwani wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, bila upendo yote ni bure!  Mapadre wanapaswa kumtambua na hatimaye kumuiga Kristo Yesu: kiongozi na mchungaji mwema, mwaminifu, mtiifu kwa Baba yake wa mbinguni na mwenye upendo usiokuwa na mipaka. Mapadre waoneshe na kushuhudia: uaminifu, upendo, unyofu, unyenyekevu na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake! Wawe ni watu wenye mvuto na mashiko kutokana na maisha na utume wao kwa familia ya Mungu. Wawe ni mfano bora wa kuigwa, daima wakijitahidi kumfuasa Kristo Yesu; mwalimu na mlezi wa Mapadre katika huduma takatifu kwa watu wa Mungu!

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania, tarehe 18 Julai 2020 ameongoza Ibada ya Misa takatifu na kutoa Daraja ya Upadre kwa Shemasi Deogratias Method Nyamwihula wa Jimbo kuu Katoliki la Mwanza kwenye Parokia ya Mtakatifu Francisko wa Assisi, Butimba, Jimbo kuu la Mwanza. Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Nkwande amesema kwamba, Mapadre wanaendeleza utume wa Kristo Yesu, ambaye ni Kuhani mkuu na mkombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unajionesha katika Fumbo la Umwilisho, kielelezo cha uwepo endelevu wa Mungu kati pamoja na waja wake. Yeye ndiye “Emmanuel yaani Mungu pamoja na nasi”.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, mwamini anapata neema ya utakaso na kuzaliwa upya katika Roho Mtakatifu na hivyo kufanyika kuwa ni mwana wa Mungu, mshirika wa tabia ya uungu, kiungo cha Kristo Yesu na Hekalu la Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Daraja Takatifu, Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake wachungaji wanaoupendeza moyo wake; wachungaji watakaojisadaka kwa ajili ya kuwalisha watu wa Mungu maarifa na ufahamu. Rej. Yer. 3:15. Haya ni maneno mazuri kuyatamka anasema Askofu mkuu Nkwande, lakini yanaweza kuwa magumu kuweza kuyanafsisha. Lakini, Padre Deogratias Method Nyamwihula amehamasishwa kujitahidi kuyamwilisha katika maisha na vipaumbele vyake, licha ya udhaifu na mapungufu ya kibinadamu. Ajitahidi kumtumikia Mwenyezi Mungu kwa akili na nguvu zake zote. Katika Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo inaonesha jinsi ambavyo Kristo Yesu alivyotenda miujiza, lakini bado Mafarisayo walimkataa na kufanya shauri jinsi ya kumwangamiza kama ilivyokuwa hata kwa Mfalme Herode. Hawa walikuwa wanamwinda Mtakatifu wa Mungu na maadili yake.

Hivi ndivyo ilivyo hata leo hii, kwa wale wanaojizatiti katika kusema na kutangaza ukweli. Watu wanaojipambanua kwa kukemea utepetevu wa maadili, utu wema na dhambi. Itasikitisha sana, ikiwa kama Mapadre watalindwa na Mafarisayo. Ikumbukwe kwamba, Kristo Yesu, hakuwa mwanaharakati, lakini alijipambanua kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi wa binadamu. Aliwaganga na kuwaponya wagonjwa; akawasamehe watu dhambi zao bila ya mbwembwe zozote. Tofauti na watu wanaohitaji: kushangiliwa na kupigiwa makofu. Mambo haya ni hatari sana kwa maisha na utume wa Mapadre. Kristo Yesu alipokataliwa kwenye mji mmoja, aliendelea na safari yake. Askofu mkuu Nkwande, aliwaomba waamini kumkumbuka na kumwombea Padre Deogratias Method Nyamwihula, ili Mwenyezi Mungu aweze kumsaidia na kumpatia ujasiri wa kusimama kidete kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu. Padre mpya ametakiwa asiwe ni kitisho kwa waamini wake, bali kiongozi anayeonesha dira na mwongozo wa kufuata kwenda kwa Baba wa mbinguni.

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, watu wataweza kuzaliwa tena kwa Maji na Roho Mtakatifu. Kwa Ekaristi Takatifu, watapata chakula cha maisha ya kiroho na kwa Sakramenti ya Upatanisho, watu wataondolewa dhambi zao na kupatanishwa na Mungu. Kwa Sakramenti ya Mpako mtakatifu, atawaonjesha waamini huduma ya uponyaji, faraja na matumaini. Atawaondoa wagonjwa katika enzi ya dhambi na kuwaweka huru na kwa njia ya wema wa Mungu, atawapatia nafuu katika mateso yao na hatimaye, kuwajalia neema, daima akiwa ameungana na Askofu mahalia. Kama kiongozi wa watu wa Mungu, ajitahidi kuwakusanya waamini wote ili waweze kuwa ni familia moja inayowajibika, kwa kuwaongoza kuelekea kwa Mwenyezi Mungu katika: haki, ukweli na utakatifu. Kama Padre anatumwa kuwahudumia watu wote wa Mungu bila ubaguzi. Atakutana na watu wema, watakatifu na waadilifu. Lakini pia, wamo waliokengeuka na wadhambi wa “kutupwa” wanaohitaji kuonjesha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Anatumwa kuwahudumia maskini na matajiri, ili wote waweze kusaidiana na kukamilishana. Asipende kujenga tabia ya ubaguzi kwani ni hatari kwa maisha na utume wake.

Watanzania, Jumatano tarehe 28 Oktoba 2020 watafanya uchaguzi mkuu kwa kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wabunge pamoja na Madiwani. Tume ya Taifa ya Uchaguzi, NEC, imesema kampeni za uchaguzi mkuu zitaanza rasmi tarehe 26 Agosti hadi tarehe 27 Oktoba 2020. Ni katika muktadha huu, Padre atambue kwamba, anao waamini ambao ni wanachama wa vyama mbali mbali za kisiasa nchini Tanzania. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, anasimamia Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa kujikita katika: Utu, heshima, haki msingi za binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Wanachama wa vyama vyote hivi watahitaji baraka za Mwenyezi Mungu. Kimsingi, “wote hawa ni abria wake”.

Itakumbukwa kwamba, Padre Deogratias Method Nyamwihula wa Jimbo kuu Katoliki la Mwanza, alizaliwa tarehe 4 Julai 1990 huko Butimba, Jimbo kuu la Mwanza. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, Mei Mosi 2019 katika Kanisa kuu la Mtakatifu Apolinari, Jimbo kuu la Roma, Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu alimpatia Daraja Takatifu ya Ushemasi wa mpito! Tarehe 18 Julai 2020, Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza akampatia Daraja Takatifu ya Upadre.

Askofu mkuu Nkwande: Upadrisho
23 July 2020, 14:17