Tafuta

Vatican News
Askofu Mkuu Beatus Kinyaia wa Jimbo Kuu la Dodoma ameipongeza Radio Maria Tanzania kwa kuchangia katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! Askofu Mkuu Beatus Kinyaia wa Jimbo Kuu la Dodoma ameipongeza Radio Maria Tanzania kwa kuchangia katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili! 

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya Aipongeza Radio Maria Tanzania!

Radio Maria imekuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa uinjilishaji wa kina nchini Tanzania kwa kugusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni Radio ambao imejipambanua kwa kusoma alama za nyakati na hivyo kujibu maswali msingi yanayowatatiza watu wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Imekuwa ni chombo cha faraja kwa wagonjwa na wazee. Kumenoga!

Na Rodrick Minja, Dodoma na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mwenyezi Mungu ni chanzo na kilele cha mawasiliano, kwani anataka kuwasiliana na waja wake jinsi alivyo, kutoka katika undani wake. Kumbe, wadau wa tasnia ya mawasiliano ya jamii wanapaswa kuwasiliana kwa kutumia akili, moyo na mikono yao; kwa maneno mengine, haya ni mawasiliano yanayomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili na kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha mawasiliano ni upendo wa Mungu ambao umemwilishwa kati ya waja wake. Mawasiliano yanayotekelezwa na Mama Kanisa si matangazo ya biashara wala wongofu wa shuruti. Kanisa linakuwa na kupeta kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

Mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa yanafumbatwa katika ushuhuda; ukweli, uzuri na wema. Huu ndio ushuhuda wa wafiadini na waungama imani; watu walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Mawasiliano ndani ya Kanisa ni mchakato unaofumbatwa katika ujasiri pasi ya kukata wala kukatishwa tamaa na hatimaye, kumezwa na malimwengu na hiki ni kishawishi cha Shetani, Ibilisi hata katika karne ya ishirini na moja. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu katika Sala yake ya Kikuhani, aliwaombea wafuasi wake, ili Mwenyezi Mungu aweze kuwatakasa kwa ile kweli kwani Neno la Mungu ndiyo ile kweli. Wametumwa ulimwenguni lakini wao si wa ulimwengu huu. (Rej. Yoh. 17: 12-19). Wadau wa tasnia ya mawasiliano wasishikwe na kishawishi cha kutaka kujifungia katika upweke wao, kwa kutaka kuendelea kubaki katika udogo wao.

Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba, wanahabari ni chumvi na chachu ya kuyatakatifuza malimwengu, kwa kuondokana na utamaduni wa watu kukata tamaa na kulalama kila wakati. Hata katika udogo na uchache wao, bado wanaweza kutenda makubwa kwa njia ya ushuhuda. Huu ni ushuhuda unaotangazwa na kushuhudiwa kwa njia ya tunu msingi za maisha ya Kikristo. Waandishi wa habari wanapaswa kutangaza ukweli wa Kikristo unaofumbatwa katika ukweli wa mambo, bila kuweka chumvi au kuwabeza wengine. Ndani ya Kanisa, watu wote wajisikie kuwa ni ndugu wamoja na watangaze uzuri. Hii ndiyo lugha ya mashuhuda wa imani na wafiadini, waliotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Waandishi wa habari wawe mashuhuda wa Kristo kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu, kama inavyoshuhudiwa katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Waandishi wa habari, wawe ni mashuhuda wa furaha ya Injili, changamoto changamani katika ulimwengu mamboleo.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, O.F.M. Cap., wa Jimbo kuu la Dodoma, amesema, familia ya Mungu Jimboni humo, itaendelea kuiwezesha Radio Maria Tanzania kuendeleza malengo yake ya kuwainjilisha watanzania wote bila kujali dini, kabila wala rangi ya mtu. Radio Maria imekuwa ni msaada mkubwa katika mchakato wa uinjilishaji wa kina nchini Tanzania kwa kugusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni Radio ambao imejipambanua kwa kusoma alama za nyakati na hivyo kujibu maswali msingi yanayowatatiza watu wa Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Imekuwa ni chombo cha faraja kwa wagonjwa na wazee. Ni Radio ambayo imeibukia kupendwa na watu wengi kutokana na mchango wake katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania.

Askofu mkuu Beatus Kinyaiya ameyasema haya hivi karibuni, alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Radio Maria, Jimbo kuu la Dodoma waliofika ofisini kwake, ili kumpatia taarifa ya kampeni ya Mariathon kwa mwaka 2020 Nyota ya Mashariki, iliyomalizika rasmi mwishoni mwa mwezi Juni 2020. Hii ni kampeni ambayo imewashirikisha wapenzi wa Radio Maria Tanzania kutoka katika mikoa mbali mbali, ambamo Radio hii inasikika. Lengo ni kuijengea uwezo Radio Maria iweze kuwafikia watanzania wengi zaidi, kwa kuendelea kufungua vituo vya kurushia matangazo. Wasikilizaji wa Radio Maria Jimbo kuu la Dodoma wamechangia kiasi cha shilingi milioni kumi na tatu na hivyo kuvuka kiwango cha milioni kumi, walichokuwa wamepangiwa hapo awali. Bibi Leonia Odilo Bishoge, Mwakilishi Kiongozi wa Radio Maria Jimbo kuu la Dodoma, amempongeza Askofu mkuu Beatus Kinyaiya kwa kukubali kuipokea na kuendelea kuilea Radio Maria Tanzania.

Radio Maria Tanzania

 

 

09 July 2020, 14:08