Jimbo Katoliki la Musoma kwa Mwaka 2020 linatarajia kupata Mapadre Wapya 7 na hivyo kuandika historia mpya ya Jimbo la Musoma mintarafu Wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. Jimbo Katoliki la Musoma kwa Mwaka 2020 linatarajia kupata Mapadre Wapya 7 na hivyo kuandika historia mpya ya Jimbo la Musoma mintarafu Wito wa Daraja Takatifu ya Upadre. 

Maajabu ya Jimbo Katoliki la Musoma 2020! Kumenoga Hadi...!

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Jimbo Katoliki la Musoma katika kipindi cha Mwaka 2020 linatarajia kupata Mapadre wapya 7. Tayari Askofu Msonganzila amekwisha kuwapatia Daraja Takatifu Shemasi Alexander Muganyizi Mujuni na Shemasi Joakim Abel Makaya, wote kutoka Parokia ya Musoma Mjini! Watoto wa Mujini! Wametakiwa wawe wajumbe wa Habari Njema ya Wokovu! Yaani!

Na Padre Alfred Stanslaus Kwene, Tume ya Uinjilishaji, TEC, -Musoma, Tanzania.

Kwa mara ya kwanza tangu kuumbwa ulimwengu, Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania linategemea mwaka huu wa 2020 kupata mapadre wapya saba, wakiwemo sita wanajimbo na mmoja mwanashirika. Katika kuelekea kutimia kwa ndoto hii, tayari siku ya Alhamisi tarehe 09 Julai, 2020, familia ya Mungu ya Jimbo la Musoma ilishuhudia upadrisho wa mashemasi wawili wa kwanza kati ya hao saba wanaotarajiwa kupadrishwa mwaka huu. Mashemasi waliopadrishwa tarehe hiyo ni Alexander Muganyizi Mujuni na Joakimu Abel Makaya wa Kanisa Kuu, Musoma Mjini. Tukio hilo nalo lilikuwa ni la kihistoria kwani kwa mara ya kwanza kabisa rekodi inavunjwa kwa kushuhudia mapadre wawili wa jimbo wa parokia moja wakipewa daraja siku moja. Imewahi kutokea kuwepo upadrisho wa mapadre zaidi ya mmoja kwa siku moja katika parokia, lakini ni mara ya kwanza kabisa kwa wote kuwa ni mapadre wa jimbo (by incardination). Itakumbukwa, mwaka 2012 walipadrishwa mapadre wawili katika Kanisa Kuu, ila mmoja alikuwa wa jimbo la Musoma na mwingine mwanashirika la Msalaba Mtakatifu. Kuwapata mapadre wawili wa parokia ile ile wa jimbo la Musoma, kwetu hii ni habari mpya.

Hakika, kila Mwana-Musoma anayo kila sababu ya kukiri kama Mzaburi alivyofanya: “Jambo hili limefanywa na Mungu nalo ni la ajabu mno kwetu” (Zab.118:23). Kwa kuzingatia ukuu na upekee wa tukio hilo la upadrisho, siku hiyo ilipambwa kwa maadhimisho mazuri sana ya kiibada yaliyoandaliwa vizuri na kwa heshima inayostahili; mahudhurio makubwa ya mapadre, watawa, walei na watu wengi wenye mapenzi mema; shamrashamra za aina mbalimbali na mengine kama hayo. Yote haya yalilenga kuienzi siku hii na kumrudishia Mungu shukrani kwa zawadi hii kubwa ya wachungaji kwa Kanisa mahalia la Jimbo Katoliki la Musoma. Kati ya mambo yatakayobaki katika kumbukumbu ya wengi vizazi hata baada ya vizazi, ni homilia nzuri na ya kina iliyotolewa siku hiyo na Mhashamu Baba Askofu Michael Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma aliyeongoza Misa hiyo na kutoa daraja hiyo takatifu ya upadre kwa hao wakandidati wawili. Huku akijawa na furaha na shukrani kwa Mungu kwa zawadi hiyo ya mapadre wawili kati ya saba wanaotarajiwa mwaka huu wa 2020, Baba Askofu Msonganzila alikuwa na haya ya kutufundisha sote - mapadre watarajiwa na kila mmoja wetu:

Katika homilia yake ya siku hiyo, Baba Askofu Msonganzila alianza kwa kufanya rejea katika utabiri wa Nabii Isaya kadiri ya somo la kwanza la siku hiyo: Isaya 61:1-3. Nabii Isaya anamsimulia yule ajaye kuwa ni mtumishi mnyenyekevu, aliyetumwa kuwaganga waliovunjika moyo, ametumwa kuwatangazia uhuru mateka na waliofungwa kufunguliwa kwao. Vile ambavyo utabiri huu wa nabii Isaya ulipata utimilifu wake katika Kristo, Baba Askofu Msonganzila aliwaasa mapadre watarajiwa wajitazame ya kuwa utabiri huu unawalenga na wao kadhalika. Wameitwa kuwa watumishi mithili ya Kristo ambaye anajitambulisha kuwa mtumishi kadiri pia ya Injili ya siku hiyo (Mt. 20:25-28). Hivyo, wanaalikwa kuwa wanyenyekevu, waleta matumaini kwa waliokata tamaa na kuvunjika moyo na watangazaji wa habari njema kwa wale walio kifungoni. Aidha, Baba Askofu alihimiza kuwa, wateule hawa wawili ni vijana ambao wanafahamika kwa watu wengi kwani ni wanajimbo, wanaparokia na familia zao zinafahamika vema. Kristo amependa kuwaita kuwa watumishi ndani ya Kanisa. Huku akifanya rejea katika Somo la Pili la siku hiyo – Efe. 4:1-7,11-13.

Baba Askofu alikazia kuwa, hadi kufikia hatua hii mapadre hao watarajiwa wamelelewa katika tunu mbalimbali kama vile ukweli, unyenyekevu, uvumilivu katika maisha yao, upole, pamoja na kuchukuliana kwa upendo. Wametayarishwa ili kuwa wapatanishi ndani ya jamii na kwa sakramenti ya upatanisho wanafanyika kuwa kweli wapatanishi wakuu kwa sababu wao ndio waadhimishaji wakuu wa sadaka inayotolewa Altareni. Ni vema waendelee kutambua umuhimu wa tunu hizi katika maisha na utumishi wao kwani hata jamii wanayoenda kuihudumia inawategemea wapambwe na tunu hizi. Baba Askofu Msonganzila aliendelea kwa kuwakumbusha mapadre watarajiwa kuhusu mazingira yao ya utume wanayotegemea kuingia na kufanya kazi. Wanaenda kuihudumia jamii ambayo kitu uhuru na kudai haki, hata wakati mwingine kudai haki bila kutimiza majukumu ni masuala ya kila siku. Ni jamii inayodai haki kuliko kuwajibika katika maisha yetu. Aliwaaalika kuwatazama hawa wote kuwa ni kondoo wao na kuwaongoa! Ni jamii ambayo haina uoga tena kwa baadhi ya dhambi, hasa haithamini tena tunu ya uhai kiasi cha kuiharibu tunu hii; jamii inayoona kuwa hata kuua ni jambo la kawaida na hata kupambwa na maneno kama vile: “uzazi wa mpango”. Badala yake aliwahimiza mapadre watarajiwa wajitahidi kutoa mafundisho yanayofaa na kuhimiza juu ya mpango wa uzazi na sio uzazi wa mpango.

Askofu Msonganzila aliendelea kukazia kuwa hii ni jamii ambayo pamoja na mapambano yaliyopo dhidi ya rushwa, lakini bado inabobea katika rushwa. Mapadre watarajiwa walialikwa kuwatazama hawa wote kuwa ni kondoo wao na hivyo wanahitaji kuwaganga mioyo na pia kuwapatanisha nafsi zao na Mwenyezi Mungu. Jamii ambayo sasa kama taifa tunaelekea katika uchaguzi mkuu. Kadiri ya uzoefu wake, alidokeza kuwa huwa kuna dalili nyingi za fujo wakati wa uchaguzi hivi kwamba watu wanafikia hatua ya kupigana na hata familia zinatengana kwa sababu tu ya kushabikia chama au mtu fulani. Baba Askofu aliwaaasa mapadre watarajiwa wafanye bidii ya pakee katika kuleta mapatano baina ya makundi haya yanayoweza kusigana kwa misingi ya kisiasa kwani watu wa pande zote mbili ni watoto wao. Ni jamii ambayo bado inasumbuliwa na janga la ugonjwa wa homa kali inayosababishwa na unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hata kama changamoto za ugonjwa huu si kubwa sana kwa sasa, lakini ugonjwa bado upo. Baba Askofu aliwaasa mapadre watarajiwa kutumia habari njema kuwafundisha watu wa Mungu juu ya hitaji la kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya janga hili.

Ni vema mapadre watarajiwa wawahimize wazazi juu ya wajibu wa kuzilinda familia zao dhidi ya janga hili kama sehemu ya wajibu wao katika kuwalea watoto wao katika maadili na utu wema. Inashangaza kuona kuwa wakati mashule yamefungwa kutokana na janga hili baadhi ya maeneo yalishuhudia wazazi kushindwa kutimiza vema wajibu wao wa malezi hadi baadhi ya wanafunzi wa kike kuishia kupata mimba. Hii inaashiria ya kuwa wazazi wanazidiwa na shule katika malezi kwani mabinti wanapokuwa mikononi mwa wazazi ndipo wanapata mimba tofauti na wanapokuwa shuleni. Ni vema wazazi wakawafundisha watoto wao kuheshimu uhuru wao na wa wengine, kutambua maslahi yao na ya wengine, na kuwa hakuna uhuru usio na ukomo kwani uhuru kamili tutaupata tutakapoungana na Mwenyezi Mungu. Pia wazazi wawahimize watoto wao kutambua alama za nyakati na kijitahidi kuendana nazo. Hivyo, aliwaasa mapadre watarajiwa wawakumbushe tena wazazi juu ya wajibu wao wa kutoa malezi bora kwa watoto wao.

Vile vile, katika homilia yake, Baba Askofu Msonganzila hakusita kuwakumbusha mapadre watarajiwa juu ya wajibu wao wa kuhamasisha miito kwa vijana. Aliwahimiza kuwaalika vijana wengine wafuate wito huu kwani zizi lisipokuwa na ndama limekwisha. Aliwasihi wawasaidie vijana wenzao wafikie maamuzi ya kina ya kujiona wameitwa na Mungu na wajitahidi kuitika. Pamoja na himizo hilo, waliombwa wawakumbushe vijana wasiitikie bila kuitwa! Baba Askofu aliwasihi mapadre watarajiwa wawatafute vijana kokote waliko, hasa huko mitaani wanakozungukazunguka na kuishia katika ujambazi, uvutaji wa sigara kubwa na hata utumiaji wa dawa za kulevya. Alikazia sana na kusema ya kuwa hao nao ni kondoo wao, wawaalike katika kazi ya Bwana ili waingie katika miito hii mitakatifu ili wawe nyenzo muhimu ya kumtumikia Mwenyezi Mungu. Watambue kuwa, kuharibika kwao sio mwisho bali wokovu wao utapatikana kupitia huduma iliyotukuka ya mapadre hao watarajiwa.

Baba Askofu alihitimisha homilia yake kwa kuwaombea Baraka za Mungu mapadre watarajiwa katika wito wao walioitikia, ambao kimsingi ni jibu kwa wito mama wa zawadi ya uhai. Vile ambavyo zawadi ya uhai haiji kwa bahati mbaya bali kadiri ya mpango wa Mungu, kadhalika hata wito wa hawa mapadre watarajiwa ni matokeo ya mpango wa Mungu. Mwenyezi Mungu ana mpango na wito wao na anawaalika kuwa punda wake ili wambebe Kristo na kumfikisha katika jamii yetu ya sasa ambayo kwa bahati mbaya haina tena woga dhidi ya uovu, haimuheshimu Mungu vya kutosha na imekumbwa na mazingira mengi tatanishi. Ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii yetu, Baba Askofu aliwaalika mapadre watarajiwa kumbeba Kristo kwa unyenyekevu, upole na uvumilivu kabisa na kumfikisha kwa watu. Aliwaalika wajifunze kutoka kwa Kristo aliye mpole na mnyenyekevu wa moyo ili waweze kupata furaha nafsini mwao. Wajifunze daima kuja kumwomba na kuongea naye mubashara.

Katika kuhitimisha homilia yake, aliwahimiza mapadre watarajiwa wayapokee kwa dhati mashauri haya kwani yalitoka ndani ya uketo wa moyo wa padre ambaye sasa ana miaka 36 ya upadre, yaani yeye mwenyewe. Japo upadre ni ule ule, lakini mang’amuzi ni mbalimbali. Hatimaye, alihitimisha kabisa homilia yake kwa maneno haya yaliyosheheni upendo wa kweli na yanayodhihirisha moyo wake wa ubaba: “Karibuni kwenye ukoo wa urika wa upadre”.

Jimbo la Musoma 2020

 

14 July 2020, 14:12