Vatican News
Abate Placidius Mtunguja wa Abasia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo Ndanda, tarehe 11 Julai 2020 amepokea nadhiri 3 za daima na 8 za muda. Abate Placidius Mtunguja wa Abasia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo Ndanda, tarehe 11 Julai 2020 amepokea nadhiri 3 za daima na 8 za muda. 

Wabenediktini wa Ndanda, Mtwara: Watawa 11 Waweka Nadhiri!

Abate Placidius Mtunguja ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Abasia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, Ndanda, Jimbo Katoliki la Mtwara. Katika ibada hii amepokea nadhiri za daima kutoka kwa watawa watatu na wengine wanane wameweka nadhiri za muda. Amewataka watawa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na huduma makini kwa Kanisa na Jirani zao!

Na Godfrey Mahonge, Ndanda, Mtwara Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba, wingi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na Karama zao mbali mbali yamechangia sana kukamilisha Kanisa katika huduma za kiroho na kimwili kama sehemu ya mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Katika wingi huu wa karama, wale wote wanaoitwa na Mwenyezi Mungu kutekeleza mashauri ya Kiinjili na kuyatimiza kiaminifu wanajiweza wakfu kwa Mungu, kwa kumfuasa Kristo Yesu ambaye akiwa: fukara, mseja na maskini, aliwakomboa wanadamu na kuwatakatifuza kwa njia ya utii wake mpaka kufa Msalabani. Kumbe, kwa njia ya upendo wa Mungu uliokwisha kumiminwa katika nyoyo za watawa, wanawajibika kuishi zaidi kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake, ili hatimaye, waweze kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Mwenyezi Mungu ndiye anayemwita mja wake, anamweka wakfu na kumtuma kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Wakristo wote wanaitwa na kutumwa kushiriki maisha na utume wa Kanisa, lakini kuna baadhi ya watu ambao wamedhaminishwa utume maalum. Kitendo cha kuwekwa wakfu, tayari ni sehemu ya mchakato wa utume, changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, mambo msingi kama vile: udugu, utume na karama yanazingatiwa ili kutoa mwelekeo sahihi kwa kila mtawa katika maisha na utume wake ndani ya Kanisa. Mababa wa Kanisa wanakazia umuhimu wa: karama ya maisha ya kitawa mintarafu mwelekeo sahihi wa ufahamu wa Kanisa na maisha ya Kisakramenti, ili kukuza na kudumisha uzuri wa upendo wa Mungu kwa waja wake. Watawa hawana budi kuwa na uelewa sahihi wa Taalimungu ya Agano, Taalimungu ya Sakramenti za Kanisa, Taalimungu ya Roho Mtakatifu pamoja na Mambo ya Nyakati. Haya ni mambo yanayotegemeana na kukamilishana katika maisha na utume wa kitawa.

Hili ni Agano katika Fumbo la Utatu Mtakatifu linalomwilishwa katika maisha ya mtawa binafsi na hatimaye katika jumuiya na shirika zima. Hii ni changamoto na mwaliko wa kuwa ni mashuhuda, wamisionari na manabii wanaotumwa kushuhudia na kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati zote. Maisha ya Kisakramenti kwa kila mtawa ni chachu ya utakatifu inayopaswa kuvaliwa njuga na wote kwa kutambua kwamba, kwa njia ya nadhiri, wanawekwa wakfu na Roho Mtakatifu ili kumshuhudia Kristo Yesu kwa namna ya pekee kabisa, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu sanjari na kujiandaa kwa maisha ya uzima wa milele!

Mama Kanisa, tarehe 11 Julai 2020 ameadhimisha Sikukuu ya Mtakatifu Benedikto, Abate na Msimamizi wa Bara la Ulaya. Huyu alikuwa ni mjumbe wa amani, upendo na mshikamano. Ni mwalimu aliyebobea katika ustaarabu unaobubujika katika amana na utajiri wa maisha na utume wa Kristo Yesu. Ni muasisi wa umonaki kwa Kanisa la Magharibi. Mtandao wa Mashirika ya Kibenediktini ulioenea sehemu mbali mbali za dunia ni sehemu ya urithi wa maisha ya kiroho na kitamaduni kutoka kwa Mtakatifu Benedikto, Abate. Ni katika muktadha huu, Abate Placidius Mtunguja ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Abasia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, Ndanda, Jimbo Katoliki la Mtwara. Katika ibada hii amepokea nadhiri za daima kutoka kwa watawa watatu na wengine wanane wameweka nadhiri za muda.

Abate Placidius Mtunguja, amewataka watawa hawa waliofunga nadhiri zao kutambua kwamba, wanahitaji kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumfuasa na kumtumikia Mungu kwa njia ya Shirika la Wabenediktini! Hii ni sadaka kubwa inayohitaji nguvu na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwani kwa nguvu za kibinadamu si rahisi sana. Kama watawa wameitwa na kupewa dhamana na wajibu wanaopaswa kuutekeleza. Wito wowote ule kutoka kwa Mwenyezi Mungu unadai:  upendo kamili, imani thabiti, utii na nidhamu katika maisha ya kitawa kama ushuhuda kwa majirani wanaowazunguka. Watawa walioweka nadhiri zao watambue kwamba, Mwenyezi Mungu anayo makusudi katika maisha yao.

Kumbe, watawa wanapaswa kuwa ni sadaka safi inayompendeza Mungu na jirani. Wawe ni baraka na chemchemi ya neema katika huduma kwa watu wa Mungu, ili Mungu aendelee kupewa sifa, enzi, utukufu na heshima kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wameteuliwa, wakawekwa wakfu na sasa wanatumwa kwenda kuwatumikia watu wa Mungu. Katika maisha na utume wao, daima wajitahidi kujenga udugu wa kibinadamu; umoja na upendo, daima wakimtanguliza Mwenyezi Mungu kuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao. Watambue kwamba, maisha ya Jumuiya si tatizo bali ni fumbo ambalo wanaalikwa kulimwilisha kila kukicha katika maisha na vipaumbele vyao, katika hali ya upole, uvumilivu, udumifu, unyenyekevu, imani, matumaini na mapendo kamili. Kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili, waendelee kushikamana na kuandamana na Kristo Yesu aliye njia, ukweli na uzima.

Wabenediktini wa Ndanda, Mtwara

 

15 July 2020, 13:39