Vatican News
Rev. Dr. Sr. Martine Shayo wa Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, CDNK amtetea kazi yake ya utafiti kwa weledi, ushupavu na ujasiri mkubwa! Rev. Dr. Sr. Martine Shayo wa Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, CDNK amtetea kazi yake ya utafiti kwa weledi, ushupavu na ujasiri mkubwa! 

Rev. Dr. Martine Shayo: Atetea kazi yake ya utafiti kwa ushupavu

Rev. Dr. Sr. Martine Shayo, wa Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, CDNK, tarehe 16 Juni 2020 amefaulu kutetea kazi yake ya utafiti. Amejikita zaidi kuhusu amana na utajiri wa Shirika la Kitawa Mintarafu Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, CDNK kulingana na Sheria za Kanisa Namba 578. Baada ya kutwangwa maswali mazito na magumu, akayajibu kwa weledi na ubunifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika tamko lao kuhusiana na Maisha ya Kitawa: “Perfectae Caritatis”, yaani “Upendo mkamilifu”, wanawataka watawa kupyaisha maisha yao, kwa kutoa nafasi ya kwanza katika maisha ya kiroho, mashauri ya kiinjili, maisha ya kijumuiya pamoja na malezi makini, kwa wale wote wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Hii ni changamoto na mwaliko wa kufanya mageuzi ya kina, kwa kusoma alama za nyakati pamoja na kuendelea kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kushuhudia ile furaha na unabii unaofumbatwa katika nadhiri, umoja na udugu katika maisha ya kijumuiya, ushuhuda wenye mvuto! Rev. Dr. Sr. Martine Shayo, wa Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, CDNK, tarehe 16 Juni 2020 amefaulu kutetea kazi yake ya utafiti.

Amejikita zaidi kuhusu amana na utajiri wa Shirika la Kitawa Mintarafu Shirika la Masista wa Bibi Yetu wa Kilimanjaro, CDNK kulingana na Sheria za Kanisa Namba 578. Baada ya kutwangwa maswali mazito na magumu, akayajibu kwa weledi, ubunifu na ufasaha, hatimaye, akaweza kuwatoa watanzania kimasomaso kwa kutunukiwa Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma. Kazi ya utafiti imesimamiwa na Prof. Ndiaye Antoine na kusaidiwa na Prof. Lorusso Lorenzo pamoja na Prof. Attila Yawovi Jean. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican Rev. Dr. Sr. Martine Shayo anasema, kwa ufupi sana, kazi yake ya utafiti imezingatia karama ya maisha ya Shirika la kitawa, jinsi ya kuitunza, kuiendeleza na kuitamadunisha kwa kuendelea kusoma alama za nyakati mintarafu katiba ya Shirika, Sheria, Taratibu na Kanuni za Kanisa Katoliki.

Rev. Dr. Sr. Martine Shayo ambaye amekuwa mwanafunzi wa kwanza kutetea kazi yake kutoka Tanzania baada ya vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kufunguliwa hivi karibuni anasema, umefika wakati kwa watawa wa Mashirika mbali mbali kujiimarisha kwa kuwa na watalaam wao wenyewe na hasa zaidi katika Sheria za Kanisa ambazo, watawa wengi wanaziona kuwa ni jambo lisilowezekana sana! Penye nia pana njia na wala hakuna sababu ya kujikatia tamaa kwani kila kitu, kinawezekana kwa neema ya Mungu. Sheria za Kanisa ni kwa ajili ya wokovu war oho za watu. Kumbe, watawa wanapaswa kujifunza sheria hizi ili wafahamu wajibu na haki zao msingi kadiri ya karama, katiba na Sheria za Kanisa. Sheria za Kanisa ziwawezeshe watawa kujenga na kuimarisha mahusiano mema na yenye tija na Maaskofu mahalia kama yanavyofafanuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwenye hati ya “Perfectae Caritas” yaani “Mapendo Kamili”.

Wataalam wa Sheria za Kanisa wawasaidie wakuu wa Mashirika kutambua kwamba, uongozi ni huduma kwa ajili ya watu wa Mungu na kwamba, wanapaswa kukuza na kudumisha uongozi na utawala bora kwa kuzingatia karama, katiba na sheria za Kanisa. Kwa njia hii, viongozi wa Kanisa wataweza kutenda kwa haki na usawa, kwa kuzingatia na kuheshimu dhamiri nyofu. Rev. Dr. Sr. Martine Shayo anawaalika watawa wa mashirika mbali mbali kujizatiti kikamilifu ili kujiendeleza katika Nyanja mbali mbali za maisha kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu wanaowahudumia. Baada ya kusoma, sasa umefika wakati wa kumwilisha elimu na hekima hii, ili kusaidiana na watawa wenzake kuendelea kusoma alama za nyakati. Kwa namna ya pekee, anawashukuru watu mbali mbali waliochangia katika hija ya maisha yake, hadi kufikia hatua hii ya kutunukiwa shahada ya uzamivu katika sheria za Kanisa.

Wambea hawana Bunge: Baada ya patashika nguo kuchanika, watanzania wanaosoma mjini Roma, baadhi yao walibahatika kuhudhuria hafla fupi ya kumpongeza Rev. Dr. Sr. Martine Shayo. Baada ya muda mrefu wa kuwekwa karantini, Waswahili walipata nafasi ya kuonja tena “Mtori safi uliotengenezwa kwa umalidadi mkubwa”, Ubwabwa kama kawaida na wakauteremshia kwa kwa kinywaji kutoka Moshi, Kilimanjaro, maarufu kama….!

REV. DR. SR. MARTINE SHAYO
17 June 2020, 13:57