Siku ya maombi nchini Hispania:Na Maria katika moyo wa Kanisa!
Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican
Na Maria katika Moyo wa Kanisa ndiyo kauli mbiu iliyochaguliwa na Baraza la Maaskofu wa Hispania kuongozwa katika Siku ya Maombi ambayo imeadhimishwa siku ya Jumapili tarehe 7 Juni 2020 sambamba na Mama Kanisa kuadhimisha Siku Kuu ya Utatu Mtakatifu. Katika fursa ya siku hiyo, Maaskofu hao wametangaza Ujumbe wao uliotiwa sahini na Askofu Luis Ángel de las Heras Berzal, Rais wa Tume ya Maaskofu kwa ajili ya Maisha ya Watawa ambapo anawaalika watazame Maria kama “mfano wa maisha ya watawa wa ndani kwa kutafakari kama Yeye, yaani kukaribisha mwili wao uwe makao ya ibada ya Kristo, katika Kanisa ambalo linawasindikiza watoto wake kwa upendo wa umama kila wakati, hasa nyakati zile ngumu.
Kutafakari ni maisha yaliyofichwa na yenye kuzaa matunda katika ulimwengu
Kama Bikira Maria, katika Jumuiya kiukweli maisha ya ndani yabaki mafichoni kwa yote na kila kitu lakini katika uwepo hai kwa yote na kila kitu. Hakika, Mama wa Yesu ni “kumbukumbu ya kwanza ya upendo wa Mungu katika Mwana na maisha ya kutafakari ni wito wa upendo wa Yesu katika Kanisa”. Uwepo wa kutafakari, kwa mujibu wa Maaskofu wa Hispania ni maisha yaliyofichwa na yenye kuzaa matunda katika ulimwengu, ambao unaonyesha mwanga wa Mungu, hasa wakati giza linapoukumba ubinadamu”.
Kuna aina tatu ya maisha ya kutafakari kwa mujibu wa maaskofu
Maaskofu katika ujumbe wao hata hivyo wanabainisha kuwa kuna sifa tatu za kutafakari na iliyo ya kwanza ni kulinda kwa dhati ukweli wa kiini cha imani ambayo ni upendo wa Kristo. Kwa hakika, tafakari inadumisha uhai wa imani kwa Mungu ambaye, kwa upendo wetu, katika ukimya na ubaridi wa usiku, katika kona ya kimaskini kabisa ya ulimwengu huu, amejifanya mtoto kwa ajili ya wokovu wa wote.
Tafakari inatia moyo wa kuwa na matumaini bila kuchoka
Sifa ya pili ya kutafakari ni kwamba uwepo wa tafakari unatia moyo bila kuchoka kuhusu tumaini kuu la Kanisa, ambalo ni huruma ya Baba, kwa sababu ni shukrani kwa watu waliowekwa wakfu na kwamba unaamsha ule uvumilivu na kuhifadhi ambaye anajua kuwa amekaribishwa kwa moyo wenye huruma ya Mungu Baba katika kila hali, hata katikati ya mateso makubwa kama haya ya sasa yaliyosababishwa na janga la virusi vya corona.
Maisha ya wakfu uangaza ulimwengu furaha ya kuishi Injili
Hatimaye sifa ya tatu ya maisha ya kutafakari yaliyowekwa wakfu, kama Bikira Maria, yanaangazia ulimwengu ile furaha ya kuishi kwa mujibu wa Injili na neema ya Roho na kama Bikira Maria katika harusi Kana, alitoa divai ya Habari Njema katika ulimwengu, katika kubadilisha kila siku matarajio mazuri ya karamu ya Ufalme wa Mungu ”.