Tafuta

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Ufunuo wa upendo wa Mungu kwa binadamu! Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Ufunuo wa upendo wa Mungu kwa binadamu! 

Sherehe ya Utatu Mtakatifu: Ufunuo wa Upendo wa Mungu

Sherehe ya Utatu Mtakatifu: Tunatafakari sura halisi ya Mungu kadiri ya Kristo, Mwana pekee wa Mungu Baba. Sura ya Mungu kama anavyoifunua Yesu mwenyewe: ‘’Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele’’. Kristo anamtambulisha Mungu Baba kwa kitenzi kile cha kupenda pasi na upeo!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Somo la Injili ya leo ingawa ni aya tatu tu za majadiliano kati ya Yesu na Nikodemo, kiongozi wa kundi la mafarisayo bado linabeba ujumbe mzito na mkubwa kwetu na hasa leo katika Sherehe ya kuadhimisha Fumbo la Utatu Mtakatifu. Nikodemo anakwenda kwa Yesu usiku, si tu kwa kuwa alikuwa anajificha kutoonekana na mafarisayo wengine kuwa ni mfuasi wa siri wa Yesu wa Nazareti, bali pia kwa desturi za marabi au walimu wa kiyahudi, walitumia muda wa usiku kwa kusoma na kutafakari Maandiko Matakatifu, ulikuwa ni muda muafaka na wenye utulivu mkubwa kwa ajili ya kujifunza Maandiko Matakatifu. Nikodemo alifika kwa Yesu si tu kwa nia ya kujifunza ila pia yawezekana alitaka kumfundisha Yesu maana sahihi ya Maandiko kadiri ya mapokeo ya marabi, hivyo Yesu anatumia fursa hii kumfundisha na kumfunulia kwa uwazi zaidi sura halisi ya Mungu. Nikodemo anapewa katekesi nzito juu ya fumbo la upendo wa Mungu kwa mwanadamu, ili imsaidie kuwa na sura au picha ya Mungu inayokuwa sahihi.

Yawezekana kabisa hata nasi leo bado tuna sura ya Mungu isiyokuwa sahihi, ndio ile ya Mungu mkali na hakimu asiye na huruma kwa yeyote yule. Katika tafakari yetu ya leo ya Dominika ya Utatu Mtakatifu, Mama Kanisa anatualika kutafakari sura halisi ya Mungu kadiri ya Kristo, Mwana pekee wa Mungu Baba. Sura ya Mungu kama anavyoifunua Yesu mwenyewe aliye, Mwana pekee wa Mungu Baba. ‘’Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele’’. Kristo anamtambulisha Mungu Baba kwa kitenzi kile cha kupenda, ambacho kwa lugha ya Kigiriki ni αγαπαν(agapan) kwalo leo tuna neno ‘’agape’’, ni upendo usio na masharti, ni upendo kamili usiotegemea malipo au kujitafuta kwa mpendaji, ni Mungu anatupenda kiasi hicho hata wakati tunapokuwa mbali naye, ni Yeye anawaka mapendo kiasi cha kuwa wa kwanza kumtafuta kila mmoja wetu. Sio mwanadamu anayemtafuta Mungu bali Mungu anayemtafuta mwanadamu kwa nafasi ya kwanza.

Yesu anatuonesha jinsi Mungu Baba anavyoupenda ulimwengu, anavyompenda kila mmoja wetu bila kuweka masharti yeyote, sio kwa sababu sisi tulimpenda na kumtafuta Mungu kwanza, bali Mungu daima ndiye anayenitafuta mimi na wewe kwa nafasi ya kwanza. Mtume Yohane ambaye aliona kwa macho yake na kumshika kwa mikono yake Neno la uzima (1Yohane 1:1), anamtambulisha ‘’Mungu ni upendo’’. (1Yohane 4:8) Mwinjili Yohana anatuonesha kile ambacho yeye alikishuhudia kutoka kwa Kristo Mfufuka, ndio sura halisi ya Mungu inajifunua kwetu kama Upendo. Mungu anaupenda ulimwengu, neno ulimwengu hapa ni vema tukitilia mkazo, hasemi amelipenda Kanisa, au Taifa, au rangi fulani, au dini fulani au watu fulani bali Mungu anaupenda ulimwengu, anampenda kila mmoja wetu bila ubaguzi wowote ule. Na hili yafaa sana kama Kanisa kulitilia maanani tunapoutangaza wema wa Mungu wa watu wake. Ni wajibu wa Kanisa kila mara kutambua kuwa ulimwengu wote ni wa Mungu na hivyo utume na misheni yake ni kwa ulimwengu mzima na kamwe tusifungwe na tofauti zetu.

Kanisa la Mwanzo kwa kweli lilienea sio kwa ufasaha wa mafundisho bali kwa ushuhuda wa maisha na ndio changamoto kwetu leo.  Labda tunashawishika kuona ulimwengu unasubiri mafundisho mazuri na yenye kutolewa kwa lugha na falsafa ya hali ya juu, ni kishawishi kwangu na kwangu na hivyo kutupelekea kusahau kuwa wajibu wetu wa kwanza ni kuwa mashahidi kwa maisha yetu, maisha yetu yambebe Kristo Mfufuka, maisha yetu yanukie harufu nzuri ya upendo usio na masharti kwa Mungu na kwa jirani, tuwe kweli watu wa agape! Jinsi ya kupenda kwa Mungu bado inatushangaza hata nasi leo, kwani Mungu anamtoa Mwana sio kati ya wana wengi bali Mwana pekee ili kwa njia yake sisi tuweze kupata uzima wa milele, yaani ukombozi wetu. Mungu hamtumi mtumishi au malaika au malaika mkuu bali anamtuma Mwana tena pekee. Anamtoa Mwana pekee kuwa zawadi ya ulimwengu. Anamtoa Mwana pekee kuwa zawadi kwa kila mmoja wetu, kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu mzima bila kumbagua yeyote yule. Mwana pekee ni zawadi ya Mungu kwa mwanadamu. Si tu Mungu ameupenda ulimwengu kwa kumtoa Mwanae wa pekee kwa kuzaliwa na kufanyika mwanadamu na kukaa kwetu bali zaidi sana kwa kufa pale juu msalabani ili atupatanishe na Mungu Baba, ili tuupate uzima wa milele. Uzima wa milele ndio kushiriki maisha ya Kimungu tangu tukiwa hapa duniani.

Na ndio tunaona Mtume Paolo kwa kutambua upendo usio mfano wa Mungu kwetu anakiri: ‘’Lakini Mungu amethibitisha kwamba anatupenda, maana wakati tulipokuwa bado wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu’’. Warumi 5:8 Na si amekuja na kufa na kufufuka siku ya tatu na kupaa mbinguni kwa maana ya kutuacha peke yetu na kurejea katika hali yake ya awali ya utukufu, bali anabaki daima na Kanisa lake kwa njia isiyoonekana ndio Roho Mtakatifu ambaye kwake sisi tunahuishwa na kujaliwa uzima wa kimungu kwa kushiriki maisha ya Kimungu. Kristo ni Mungu pamoja nasi milele yote, Mathayo 28:20. Wayahudi walikuwa bado na sura ya Mungu anayekuja kama hakimu mkali kuhukumu ulimwengu, anayekuja ili kuwatenga wema na waovu, kuja kuangamiza waovu. Na yawezekana hata kati yetu leo tulio wafuasi wa Kristo bado tuna sura ya Mungu kama ile ya wayahudi, kwa kweli tunaalikwa kila mara kubadili vichwa vyetu kwani kinyume chake tutakuwa tunafanya kufuru. Mungu anajifunua kwetu kupitia kwa njia ya Mwana pekee sio kama hakimu mkali bali kama upendo kamili, upendo usio na masharti.

Mwinjili Yohane anatusaidia kila mara anapotuonesha Mungu Baba, na hata Mungu Mwana daima kuwa sio hakimu anayekuja kuhukumu ulimwengu bali ni mwokozi na mkombozi anayempenda kila mmoja wetu. ‘’Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwengu ili auhukumu ulimwengu, bali aukomboe’’. Yohana 3:17 ‘’Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki, mimi sitamhukumu; maana sikuja kuuhukumu ulimwengu bali kuukoa’’. Yohane 12:47 Hivyo Mungu sio hakimu bali ni Upendo, anayekuja sio kuangamiza bali ili tupate uzima wa milele, ndio uzima wa kushiriki maisha ya Mungu, umilele sio kwa maana ya muda bali nje ya muda kwani tunashiriki maisha ya Mungu mwenyewe ambaye haishi katika muda bali nje ya muda. Hukumu ya Mungu kwetu wanadamu ni ukombozi, ndio kutukomboa kutoka utumwa wa dhambi na uovu, na kutupatia uzima wa milele. Ni kwa kusikia Neno lake na kulishika Yesu anatuhakikishia uzima wa milele. Ni sawa na mmoja anayepuuza maelekezo ya tabibu kwa ajili ya afya yake, hapo wa kumlaumu sio tabibu bali ni mgonjwa mwenyewe kwa kuharibu afya yake kwa kutokusikiliza na kutii maelekezo ya mganga. Ni mwanadamu anayejihukumu mwenyewe kwa kumuasi Mungu na Neno lake na kufuata mapenzi yake na ya yule muovu.

Na ndio tunaona aya ya mwisho ya somo la Injili ya leo inasema: ‘’Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa, kwa sababu hakumwamini Mwana pekee wa Mungu’’. Hukumu inayozungumziwa hapa sio ya siku ya mwisho bali ni wajibu wa kila mmoja wetu mbele ya upendo wa Mungu. Ndio kusema asiyeupokea upendo wa Mungu basi huyo anajihukumu mwenyewe, kwa kufuata njia ile ya kifo isiyokuwa na uzima wa milele. Hivyo ni mimi na wewe tunawajibika kwa kuamua leo kuisikiliza Sauti na hasa Neno lake na kuliishi na hapo tunajaliwa maisha ya kweli, maisha yasio na mwisho, kwani hata kama tutakufa bado sisi maisha yetu yataendelea kuwa hai kwani tumeyashikamanisha na maisha ya Mungu mwenyewe. Hivyo hukumu haitoki kwa Mungu bali kwa sisi wenyewe kukataa upendo wake na kuamua kufuata njia zetu. Hukumu ni kumkataa Mungu na Neno lake, na badala yake kugeukia uovu na muovu. Hukumu ni kukubali kwa utashi wetu kuharibu maisha yetu kwa kukataa mahusiano ya upendo na Mungu. Mungu daima anakuja kwetu na sura ya upendo na kamwe sio kama hakimu anayekuja kutuhukumu na kutuangamiza.

Na ndio Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, tunaalikwa nasi kushiriki maisha ya umoja na upendo wa Kimungu, kama vile Mungu mmoja katika nafsi tatu, kama wao walivyo umoja nasi tunaalikwa kuunganisha maisha yetu na Mungu. Ndio kuishi maisha ya kitakatifu, maisha ya kuwa kweli wana wa Mungu kwa njia ya Mwana pekee.  Ni kwa kumtafakari Mungu kama Upendo hapo tunaweza kuona jinsi Mungu katika Utatu Mtakatifu anavyojifunua na kujidhihirisha kwetu.  Ni fumbo hivyo ni kwa kutafakari fumbo la upendo wake, hapo tunaweza kuuona uso halisi wa Mungu, na kamwe tusishawishike kuwa tunaweza kuufikia uso halisi wa Mungu kwa akili zetu bali kwa msaada wa Mungu Mwenyewe anayejifunua kwetu katika Maandiko Matakatifu. Ni kwa njia ya Neno lake, Mungu anajifunua kwetu nasi kwa msaada wa Maandiko pekee hapo tunaweza kumtambua Mungu mmoja katika nafsi zile tatu, Mungu anayejifunua kwetu kama Baba, kama Mwana na kama Roho Mtakatifu. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni Fumbo la Upendo wa Mungu kwa mwanadamu na ndio maana leo somo la Injili linatualika kuutafakari upendo wa Mungu ili tuweze kuwa na sura halisi ya Mungu.

Mungu Baba anajifunua kwetu hasa katika uumbaji hasa katika Agano la Kale, na katika fumbo la umwilisho, Mungu Mwana anajifunua na kujidhihirisha kwetu na kwa kuuonja upendo wa Mungu Baba na Mwana hapo Roho Mtakatifu anajifunua na kujidhihirisha kwetu, ni Yeye atokaye kwa Baba na Mwana, ndio upendo ule wa milele unaokuwa kati ya Baba na Mwana. Ni fumbo ili kuweza kulionja hatuna budi kama nilivyotangulia kusema tunaalikwa nasi kushiriki katika maisha ya kuungana na Mungu mwenyewe, ni kwa njia hiyo pekee fumbo hilo linajifunua na kujidhihirisha kwetu.Ni kwa kushiriki upendo huo wa Mungu nasi tunaweza kutafakari vema Fumbo la Mungu mmoja katika Nafsi Tatu. Nawatakia tafakari na Dominika njema ya Utatu Mtakatifu.

04 June 2020, 14:25