Tafuta

Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Hili ni Fumbo la msingi la imani na maisha ya Kikristo! Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu: Hili ni Fumbo la msingi la imani na maisha ya Kikristo! 

Fumbo la Utatu Mtakatifu: Msingi wa Imani na Maisha ya Kikristo!

Imani ya Wakristo inafumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni fumbo la msingi la imani na la maisha ya Kikristo. Hili ni fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Baba na Mwana wamefunuliwa na Roho Mtakatifu. Kwa ufupi tunaweza kusema: Utatu ni mmoja, Nafsi za Mungu zinatofauti ya kweli kati yao na zina uhusiano moja kwa nyingine kwa sababu Umoja wa Mungu ni Utatu. Fumbo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote. Hii ni Salamu ya Mtakatifu Paulo kwa Wakorintho inayobeba uzito wa juu kwa siku ya leo. Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Katika utangulizi wa Ibada ya Misa Takatifu katika Sherehe hii, tunasali tukisema, Wewe Mungu Baba Mwenyezi pamoja na Mwanao wa pekee Kristo Yesu na Roho Mtakatifu, u Mungu mmoja na Bwana mmoja, siyo katika umoja wa Nafsi, ila katika Utatu wa Umungu mmoja! Imani ya Wakristo wote inafumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni fumbo la msingi la imani na la maisha ya Kikristo. Hili ni fumbo la Mungu ndani yake mwenyewe. Baba na Mwana wamefunuliwa na Roho Mtakatifu. Kwa ufupi tunaweza kusema: Utatu ni mmoja, Nafsi za Mungu zinatofauti ya kweli kati yao na zina uhusiano moja kwa nyingine kwa sababu Umoja wa Mungu ni Utatu.

Ufunuo wa imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu unamwilishwa katika maadhimisho ya Liturujia na Sakramenti mbali mbali za Kanisa. Ni mwaliko wa kujua ukuu na utukufu wa Mungu; ni kuishi kwa shukrani pamoja na kujua Umoja na heshima ya kweli ya watu wote, sanjari na kutumia vyema viumbe vya Mwenyezi Mungu na kuendelea kumtumainia Mungu kwa kila namna. Kumsadiki Mungu kunatufanya tumwelekee Yeye peke yake, kama chanzo chetu na kikomo chetu, bila kupenda kitu kingine badala yake. Mwenyezi Mungu hata anapojifunua mwenyewe anasema Mtakatifu Augustino anabaki ni Fumbo lisiloelezeka, kama tungemwelewa asingekuwa Mungu. Mungu wa imani yetu amejifunua mwenyewe katika kazi ya uumbaji, ukombozi na ujio wa Roho Mtakatifu kielelezo cha uwapo wake ambao ni ukweli na upendo! Rej. KKK. 222- 231.

Tunaposali “Mtakatifu” tunakiri utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Katika Kanuni ya Imani, Kanisa linafundisha na kukiri kwa Mungu mmoja, Baba Mwenyezi, Muumba wa Mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Kanisa linasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu, aliyezaliwa kwa Baba, tangu milele yote, Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa Mungu. Aliyezaliwa bila kuumbwa wenye umungu mmoja na Baba; ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kanisa linasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima; anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana; aliyenena kwa vinywa vya manabii! Kanuni hii ya imani, muhtasari wa imani ya Kanisa, imeandikwa kwa mateso na shuhuda za Mababa wa Kanisa.

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha historia nzima ya wokovu wa mwanadamu. Ni ufunuo wa upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani kama Mungu mwenyezi alivyojifunua mbele ya Waisraeli pale kwenye mlima wa Sinai kama ambavyo tunasikia kutoka katika Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Kutoka 34: 4-6; 8-9. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli. Hiki ni kiini cha Agano kati ya Mungu na wateule wake, licha ya wao kuteleza na kuanguka dhambini mara kwa mara. Mwenyezi Mungu ni mwaminifu daima na anatekeleza ahadi zake, kwa kuwakirimia waja wake neema na baraka katika maisha; kiasi cha kuwafungulia matumaini ya maisha ya uzima wa milele. Huu ni mwaliko wa kuabudu Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa ibada na uchaji, tayari kupokea ufunuo wa wokovu wa Mungu.

Ufunuo wa: Ukweli, huruma na upendo wa Mungu umeletwa kwetu kwa njia ya Kristo Yesu na kwa Roho Mtakatifu. Amana na utajiri unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu unawaunganisha binadamu wote na hivyo kujisikia kuwa ni watoto wa familia moja ya binadamu. Mtakatifu Paulo anatualika kuwa ni watu wapya, tukitambua dhamana na wajibu wetu. Waamini wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha kama kielelezo cha uwepo wa Mungu ndani mwao, hata kama bado kuna mateso yanayoendelea kumwandama mwanadamu. Anawataka Wakristo watimilike, wafarijike na kunia mamoja, huku wakiishi kwa amani, hivyo Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nao. Re. 2 Kor 13: 11-14.

Mwinjili Yohane katika Sura 3: 16-18 anaturejesha tena kwenye mazungumzo kati ya Kristo Yesu na Nikodemu ili kutufunulia asili ya Mungu, huruma, upendo na wokovu unaofumbatwa kwa namna ya pekee kwenye Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake kwenye Fumbo la Pasaka. Hapa, mwamini anakumbushwa kwamba, mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kumbe anauwezo wa: kufahamu, kupenda na kuhurumia. Kumbe, ukosefu wa imani ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha mwanadamu kuukataa ukweli kutokana na kiburi na jeuri yake. Mwana falsafa mmoja aliwahi kusema kwamba, kiburi na jeuri vinawea kumpandisha mwanadamu juu kama manyoya, lakini iko siku jeuri hii itampromosha na kuvunjika kama nazi na hapo ndipo kutakapokuwepo na kilio na kusaga meno. Unyenyekevu utusaidie kulitafakari Fumbo la Utatu Mtakatifu na kumwabudu Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu pamoja na kuendelea kujiaminisha kwenye upendo wenye huruma!

Utatu Mtakatifu

 

05 June 2020, 13:51