Tafuta

Vatican News
Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha imani ya Kanisa. Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kiini cha imani ya Kanisa. 

Fumbo la Utatu Mtakatifu: Kiini cha Imani ya Kanisa

“Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, mwumba wa mbingu na Dunia… Nasadiki kwa Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu, ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu…Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima…” Imani inatuambia kwamba nafsi hizo tatu za Mungu siyo Miungu watatu bali Mungu mmoja. Mungu mmoja katika Nafsi tatu!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Neno la Mungu, katika sherehe ya Utatu Mtakatifu. Utatu Mtakatifu ni fumbo la imani kuwa katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu yaani Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu. Hizi nafsi tatu za Mungu mmoja, zote ni sawa katika uasili. Na kwa kuwa ni fumbo la imani, imani tu, imani tu, yaelewa. Kumbe lengo la tafakari katika sherehe hii siyo kuwaelewesha namna ambavyo nafsi tatu katika utatu mtakatifu zilivyoungana na kufanya Mungu mmoja. La hasha. Shabaha ni kujaribu kutufahamisha jinsi Utatu Mtakatifu unavyofanya kazi katika maisha yetu na kutukuza Utatu Mtakatifu ambao ni Mungu mmoja.

Misa na sala zingine zinaanza na kumalizika kwa maneno haya: “Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.” Ni ishara tosha ya kumkiri Mungu katika nafsi tatu. Katika hii sala rahisi, tunakiri kile tunachokiamini kwa kirefu katika Kanuni ya Imani katika sehemu kuu tatu tukianza kwa kusema: “Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi, mwumba wa mbingu na Dunia… Nasadiki kwa Yesu Kristo, Mwana wa pekee wa Mungu, ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu…Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima…” Imani inatuambia kwamba nafsi hizo tatu za Mungu siyo Miungu watatu bali Mungu mmoja. Kwa namna gani? Hili ni fumbo la imani na imani tu yaelewa.  Wimbo wa mwanzo unatoa wasifu wake ukisema: Asifiwe Mungu Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; kwa sababu ametufanyizia huruma yake na wimbo wa katikati unatoa sifa kwa Mungu ukisema “Umehimidiwa, Ee Mungu wa Babu zetu. wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele” (Dan. 3:52).

Ukweli kuhusu Fumbo la Utatu Mtakatifu: Siri ya fumbo la Utatu Mtakatifu ni fumbo la Imani. Kuuelewa muungano na umoja uliopo katika nafsi hizi tatu katika Mungu mmoja kwa akili za kibindamu ni jambo lisilowezekana kwani fumbo hili lapita uwezo wa ufahamu wetu. Ni Mungu pekee ndiye anayetuwezesha kulifahamu kwa njia ya ufunuo wake mwenyewe kama vile Mtakatifu Augustino alivyojaribu kwa akili yake yote kupembua siri hii kuu lakini Mungu mwenyewe alimuweka wazi kupitia malaika katika mfano wa mtoto mdogo na kumwambia wazi akili ya mwanadamu ni ndogo kiasi kwamba haiwezi lolote ndiyo maana anatufundisha akisema inatupasa kusadiki kwa sababu Mungu ametufunulia. Lakini mafumbo kama haya katika imani yetu ni kama mifupa katika nyama. Kama tusivyoitupilia mbali mifupa moja kwa moja na nyama iliyo juu yake bali tunakwangua nyama yote na kuachana na mifupa, na haya mafumbo hatuwezi kuyakimbia moja kwa moja tutafanya tuwezalo ili kuelewa kinachoweza kueleweka; pale tutakapokwama na kushndwa, hatuna budi kupiga magoti na kusadiki.

Mtakatifu Thomaso wa Akwino aliyejaliwa uelewa mkubwa na wa hali ya juu wa mambo yamhusuyo Mungu katika wimbo tunaouimba wakati wa kuabudu Ekaristi Takatifu anasema; “waficha Umungu msalabani, na ubinadamu altareni, mafahamu yangu yadanganya yanapokuona, nami nasadiki bila haya. Mtume Paulo naye anasema: “Basi, sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa na hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho. Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtumpu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho. Maandiko yasema, nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Lakini sisi tunayo akili ya Kristo (1Kor.2:13-16). Thomaso wa Akwino anashauri kwamba: “ukikutana na lolote ambalo hulielewi ama katika Biblia au katika mafundisho ya Kanisa usiseme mambo haya hayaeleweki au yamekosewa bali useme akili zangu ni ndogo kuelewa ukweli huu.” Fanya juhudi kuelewa utakavyoweza. Yatakayokushinda “Inamisha kichwa mpaka nchi na kusema pamoja na mtakatifu Hipoliti kuwa; “nasadiki kwa kuwa sina uwezo wa kueleza” (Nasadiki kwa kuwa ni upuuzi).

Kumbe, basi katika sherehe hii ya Fumbo hili la Imani yatosha kujikumbusha mafundisho yatolewayo na mamlaka funzi ya kanisa. Fundisho la Utatu Mtakatifu ni moyo na kiini cha imani yetu ya kikristo. Ni fumbo asili la imani na maisha ya Kikristo. Kwa Utatu Mtakatifu tunafunuliwa upendo, wema, ukuu, mamlaka na huruma ya Mungu katika Nafsi hizi tatu. Ni katika Utatu Mtakatifu ndimo tunamopata ufupisho na simulizi la asili yetu tangu kuumbwa hata ukombozi kwa njia ya Yesu Kristo nafsi ya pili ya Mungu, ndimo zinamolala sala zetu na matumaini yetu kufikia utimilifu wa upendo kwa kuungana na yule aliye asili ya upendo.

Msingi wa fundisho la Utatu Mtakatifu: Imani katika Utatu Mtakatifu imefunuliwa kwetu na Mungu mwenyewe katika maandiko matakatifu. Mtume Paulo anapowasalimu wakristo katika Salamu-tangulizi za barua zake haachi kusema “neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na upendo wa Mungu Baba na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote.” Katika kitabu cha Mwanzo 1:1-2 tunasoma; “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji. Roho wa Mungu akatulia juu ya uso wa Maji.” Hili ni dokezo la udhihirisho wa uwepo wa Roho Mtakatifu tangu mwanzo. Katika kitabu cha Methali 8: 1-36 kinamtaja Hekima (Neno wa Mungu ambaye ni Kristo) akisema; “Kabla Mungu hajaumba dunia na mashamba yake, nilikuwa pamoja naye kama fundi stadi”. Mwanzo 1:24 “Mungu akasema, Natumfanye mtu kwa sura na mfano wetu. Mungu akasema (ni mmoja anayesema), kwa sura na mfano wetu (ni wingi). Hii tayari inatuonyesha kuwa Mungu ni Mmoja katika Nafsi zaidi ya moja ndiyo maana Kumbukumbu la Torati 6:4 liliwakumbusha Waisraeli likisema; “Sikiliza ee Israeli Bwana Mungu wetu Bwana ndiye Mmoja”. Katika Yohane 14: 15-17, Yesu anasema; “Mkinipenda mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine ndiye Roho wa Ukweli.” Pale Filipo alipomwuliza tuonyesha Baba yatutosha, Yesu anajibu kama anavyoandiaka Yohane 14:8-10 akisema; “Filipo; aliyeniona mimi amemwona Baba, Mimi ni ndani ya Baba na Baba yu ndani yangu.” Jibu hili ni gumu kuelewa kwa akili ya kibinadamu, imani tu yaelewa. Na huu ni udhibitisho wa Kibibilia wa ufunuo wa Utatu Mtakatifu kwa sababu aliyetufunulia ni Mungu mwenyewe Yesu Kristo aliye nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu hatuna budi kuamini na kusadiki.

Kutangaza na kukiri imani yetu juu ya Utatu Mtakatifu: Katika maisha yetu ya kila siku tunakiri na kuutangaza Utatu Mtakatifu. Kila mara katika sala zetu tunaanza na kuhitimisha kwa ishara ya msalaba huku tukitamka waziwazi maneno; “Kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu.” Tunapaswa kufanya hivyo kabla ya kulala na kila tunapoamka, kabla na baada ya kula, kabla na baada ya kazi, na nyakati mbalimbali katika maisha yetu yak ila siku. Ni kwa njia hii tunatangaza waziwazi msingi wa imani yetu. Mtakatifu Augustino anasema, ‘‘Roho Mtakatifu anatoka kwa Baba kama chanzo cha kwanza, na ni paji la milele analolitoa Baba kwa mwana, anatoka katika umoja wa Baba na Mwana’’. Kupelekwa kwa Roho Mtakatifu ambaye Baba anamtuma kwa jina la Mwana na ambaye Mwana anamtuma toka kwa Baba, kunafunua kwamba yeye pamoja nao ni Mungu huyo huyo mmoja (Yon. 14:15-17) katika nafsi tatu. Ni kwa upendo wa Mungu dunia na vyote vilivyomo, vinavyoonekana na visivyoonekana vilifanyika (Yon.1:2). Ni kwa upendo wa Mungu taifa la Israeli liliandaliwa kwa ajili ya wokovu wa wanadamu.

Ni kwa upendo wa Mungu Baba, “Kristo alijinyenyekeza akawa mtii mpaka mauti, naam hata mauti ya msalaba” (Wafilipi. 2:8) na ni kwa upendo wa Mungu Baba, Kanisa liliimarishwa na kuendelea kukua kutokana na ujio wa Roho Mtakatifu aliyetoka kwa Baba na Mwana siku ya Pentekoste (Mdo.1:8; 2:1-13). Na huu ndio ufunuo wa Utatu Mtakatifu. Na kwa kuwa Mungu ndiye aliyetufunulia hatuna budi kuamini na kusadiki yote kuwa ni kweli tupu. Tunaposherehekea Fumbo la Utatu Mtakatifu tuombee umoja katika familia kama kanisa la nyumbani na katika Kanisa kwa ujumla. Yesu aliomba: Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma” (Jn 17:21). Ufunuo huu wa Utatu Mtakatifu unatuonyesha kuwa Baba ni Muumbaji, Mungu Mwana ni Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu ni Mfariji. Lakini katika yote haya hawakuachana. Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu walikuwepo na kushiriki katika uumbaji kama anavyotufahamisha Yohane: “Hapo mwanzo kulikuwa Neno naye Neno alikuwa kwa Mungu naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo, wala pasipo yeye hakikufanyika chochote kilichofanyika(Yoh.1:1). Katika kutukomboa Mungu Baba na Mungu Roho mtakatifu hawakumwachia Mungu Mwana ahangaike peke yake.

Wote walikuwepo:Yesu akasema, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanywa kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yangu yu pamoja nami(Yn.16:32). Luka anatuambia tena kuwa Yesu alipokuwa Gethseman alisali akasema: “Baba, kama wapenda, ukiondoe kwangu kikombe hiki, hapo malaika kutoka mbinguni akamtokea ili kumtia moyo(Lk.22:42-43). Basi tuzingatie wosia wa Paulo: “Hatimaye ndugu, kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi katika Utatu Mtakatifu. Salimianeni kwa busu takatifu” (2Kor 13:11-14). Tumsifu Yesu Kristo.

04 June 2020, 14:42