Tafuta

Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. 

Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Fumbo la Imani na Upendo

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha. Kwa kumpokea Kristo Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo: Fumbo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Mwokozi wetu, Kristo Yesu katika Karamu ya mwisho, usiku alipotolewa, aliweka sadaka ya Ekaristi ya Mwili wake na Damu yake Azizi. Alifanya hivyo ili kuendeleza Sadaka ya Msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibiarusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa kifo na ufufuko wake: Sakramenti ya utakatifu (Sacramentum pietatis), ishara ya umoja, kifungo cha mapendo karamu ya Pasaka “ambamo Kristo huliwa, na roho hujazwa neema, na hutolewa amana ya uzima wa milele”. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unawaalika waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Kwa sababu hiyo, Mama Kanisa anajibidisha kwa namna nyingi kusudi waamini wasihudhurie fumbo hilo la imani kama wageni au watazamaji bubu, bali waishiriki ibada takatifu kwa akili, kwa moyo na kwa matendo, wakielewa vizuri fumbo hilo kwa njia ya matendo ya kiliturujia na sala.

Waamini waelimishwe katika Neno la Mungu; walishwe katika karamu ya Mwili wa Bwana; wamtolee Mungu shukrani; wakitolea hostia isiyo na doa, siyo kwa mikono ya padre tu, bali pia pamoja naye, wajifunze kujitolea wenyewe. Tena, siku kwa siku, kwa njia ya Kristo mshenga, wakamilishwe katika umoja na Mungu na kati yao ili hatimaye, Mungu awe yote katika wote. Rej. SC. 47-49. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Kristo Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha kama ilivyo kwa wakati huu wa maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Na hatimaye, Kristo Yesu anawaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu ili kujenga ufalme wa Mungu hapa duniani.

Kila mwaka, Kanisa lina furaha kubwa ya kuadhimisha Sherehe ya Ekaristi Takatifu, kiini cha imani, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa kwa kumwabudu Kristo Yesu anayejisadaka na kujitoa kwa waja wake kama chakula na kinywaji cha wokovu! Sherehe ya Ekaristi Takatifu kama inavyojulikana na wengi: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini, ni Sherehe kubwa inayokwenda sanjari na maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu kuzunguka vitongoji mbali mbali kama ushuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake. Kwa bahati mbaya kwa mwaka 2020, maadhimisho haya hayatakuwa na kishindo cha ushuhuda wa mwonekano wa nje kama desturi yake kutokana na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Lakini Sherehe hii pia inapaswa kuadhimishwa kwa moyo wa ibada na uchaji wa Mungu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe, linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa mara ya kwanza Sherehe hii iliadhimishwa kunako mwaka 1246 huko Lie’ge nchini Ufaransa kama ushuhuda wa imani ya Kanisa kwa Fumbo la Ekaristi Takatifu na uwepo endelevu wa Kristo Yesu kati ya waja wake kwa njia ya: Ekaristi Takatifu, Neno la Mungu na Roho wake Mtakatifu. Kunako Mwaka 1264 Papa Urban IV akatamka kwamba, Sherehe hii iadhimishwe na Kanisa zima. Papa Urban IV alimwomba Mtakatifu Thoma wa Akwino (1224-1274) ambaye alikuwa mtaalamu sana katika taalimungu kuandika sala na tenzi zote za Sherehe ya Ekaristi Takatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walifanya mabadiliko makubwa kwa kuwataka waamini kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inafumbatwa katika alama ya Mkate na Divai. Yesu katika maisha na utume wake, ametumia alama hizi kuwa ni kiini cha mafundisho yake makuu mintarafu imani, matumaini na mapendo.

Ni fundisho linalojitokeza mintarafu mavuno na watenda kazi katika shamba la Bwana, yaani miito! Yesu alipowalisha watu kwa mikate mitano na samaki wawili, anaonesha umuhimu wa ukarimu na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Mfano wa Maskini Lazaro alivyotamani kujishibisha kwa makombo yaliyokuwa yanadondoka mezani kwa yule tajiri; hapa alikazia umuhimu wa kuwajali maskini kwani wao ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Alizungumzia pia kuhusu Baba Mwenye huruma na Mwana mpotevu na mwishoni katika Sherehe hii, Yesu anasema Yeye ni chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Anaendelea kufafanua kwamba, chakula atakachotoa ni Mwili na Damu yake Azizi. Rej. Yn. 6: 51-58. Mwili wake ni chakula na Damu yake ni kinywaji cha kweli. Ukweli huu, unafumbatwa kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Ikumbukwe kwamba, Ekaristi Takatifu ni mazao ya nchi na kazi ya mikono ya wanadamu; ni sadaka na matoleo ya mwanadamu kwa Mwenyezi Mungu na kuwekwa wakfu na baadaye, tunarejeshewa tena kama zawadi na sadaka ya Kristo Yesu kwa ajili ya Kanisa lake. Ni mkate ambao ni chemchemi ya maisha na uzima wa milele na Yesu anasema, atamfufua siku ya mwisho. Hiki ni chakula cha wasafiri, kinachowaimarisha waamini katika Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Somo la kwanza kutoka katika Kitabu cha Kumbukumbu la Torati Sura ya 8: 2-3; 14-16 linawakumbusha waamini jinsi ambavyo Waisraeli walivyopata upendeleo wa pekee kwa kulishwa jangwani kwa mana na maji kutoka mwambani kwa muda wa miaka arobaini. Hapa tunakumbushwa kwamba, jangwa la maisha ya mwanadamu ni kama watu wanavyoishi kwenye karantini; watu wanaondamwa na magonjwa sugu kama ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19; ajali za barabarani; vifo vya ghafla na katika hali ya upweke hasi hasa miongoni mwa wazee. Ukosefu wa fursa za ajira pamoja na hali ya kujikatia tamaa ya maisha. Hata maisha yenyewe ni jangwa linalotisha sana!

Ekaristi Takatifu iwe kwetu chemchemi ya imani, matumaini; umoja, upendo na mshikamano na zaidi sana iwe kisima cha wokovu wa roho zetu! Mtakatifu Paulo katika Waraka wake kwanza kwa Wakorintho 1Kor.11:29-30 anazungumzia kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu. Hata leo hii kuna waamini wadhaifu na wagonjwa kwa sababu hawawezi kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa kutokana na uvivu wao wenyewe au kwa sababu ya vizuizi mbali mbali. Kwa bahati mbaya sana, kuna waamini wanaopokea Ekaristi Takatifu kwa mazoea bila ya maandalizi ya kina, yaani toba na wongofu wa ndani unaofumbatwa katika moyo wa ibada na uchaji wa Mungu. Hivyo basi, Ekaristi Takatifu iwe ni chemchemi ya furaha, amani ya ndani, imani na matumaini, ili kila mwamini aweze kujisadaka na kujimega kwa kuwa Ekaristi kwa ajili ya Mungu, jirani, ustawi na maendeleo ya Kanisa zima.

Corpus Domini 2020
11 June 2020, 14:27