Kardinali Berhaneyesus D. Souraphiel: Barua ya Kichungaji Kuhusu Mapambano Dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Kardinali Berhaneyesus D. Souraphiel: Barua ya Kichungaji Kuhusu Mapambano Dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. 

Kardinali Souraphiel: Barua ya Kichungaji: Vita ya COVID-19

Anawataka watu wa Mungu kutafakari kuhusu: Sala na Neno la Mungu. Waendelee kujenga na kudumisha familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma na mapendo kwa jirani zao, kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kipindi cha watu kuwekwa karantini iwe ni fursa ya toba na wongofu wa ndani; kwa kukazia maana ya maisha

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mama Kanisa anatumia silaha mbali mbali katika vita ya adui asiyeonekana. Mama Kanisa anakazia umuhimu wa Kufunga na kusali na Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbali mbali. Anawahimiza waamini kufanya Tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa kwenye matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kanisa linakazia Ibada ya Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa nchini Ethiopia ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ethiopia ameandika barua ya kichungaji kuhusu janga la COVID-19. Anawataka watu wa Mungu kutafakari kuhusu: Sala na Neno la Mungu. Waendelee kujenga na kudumisha familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma na mapendo kwa jirani zao, kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kipindi cha watu kuwekwa karantini iwe ni fursa ya toba na wongofu wa ndani; kwa kukazia maana ya maisha mintarafu mwanga wa Neno la Mungu. Waamini waendelee kuimarisha amani na utulivu wa ndani kwa kusali na kutafakari zaidi; sala ambayo hatimaye, inamwilishwa katika kipaji cha ubunifu.

Huu ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia familia kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa kutambua kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Huu ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha. Ni wakati wa kukaa pamoja na wanafamilia ili kukazia malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana. Ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia. Familia inapaswa kuwa ni mahali pa usalama, haki na amani. Huu ni wakati wa kuambakizana Injili ya upendo, ilikweli familia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kushinda matatizo na changamoto za Virusi vya Corona, COVID-19. Familia zijenge utamaduni wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kardinali Souraphiel anakaza kusema kwamba, huu ni muda muafaka wa kuendelea kutafakari Waraka wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, uliozinduliwa hapo tarehe 18 Juni 2015 mjini Vatican. Baba Mtakatifu pamoja na mambo mengine anakazia: Umuhimu wa kutunza mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini; anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo ni sawa na chanda na pete na kamwe hayawezi kutenganishwa. Anapembua kwa kina na mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote.

Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote! Ni muda wa kusikiliza na kujibu kilio cha Mama Dunia na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi, yaani maskini! Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa anawashukuru na kuwapongeza madaktari, wauguzi na wafanyakazi wote katika sekta ya afya ambao wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia watu wa Mungu nchini Ethiopia. Katika Injili ya huruma ya upendo, waamini wanaweza kutangaza na kushuhudia kwamba, kwa hakika Mungu ni upendo.

COVID-19-Ethiopia
13 June 2020, 11:35