2020.05.21  Askofu Valentine Kalumba wa Jimbo la  Livingstone, Zambia 2020.05.21 Askofu Valentine Kalumba wa Jimbo la Livingstone, Zambia 

Zambia:saidia parokia yako kifedha hata katika nyakati hizi za COVID-19!

Ikiwa Makanisa bado yamefungwa nchini Zambia,Askofu Valentine Kalumba,OMI,wa Jimbo la Livingstone,amewahimiza waamini wa jimbo hilo kuendelea kuunga mkono parokia na makuhani wao hata kwa wakati huu wa janga la ugonjwa wa COVID-19.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Askofu Valentine Kalumba, OMI wa Jimbo katoliki la Livingstone nchini Zambia hivi karibuni alitoa ombi na kuwakumbusha waamini kwamba mapadre wao na parokia bado walikuwa na bili za umeme na mahitaji mengine ambayo yanategemea ukarimu wao. “Mbali na majukumu yetu ya msingi wa imani, hatupaswi kusahau kusaidia parokia zetu katika malipo ya bili, umeme, maji, na mengine pale yanapotumika. Jukumu lako la parokia lazima liendelee licha ya janga la virusi vya corona. Kwa maana hiyo, ninawahimiza sana kila parokia kuunda mikakati na kupata njia sahihi ya kuchangia, kwa pesa au kwa namna nyingine ya kuchangia kwa ajili ya kusaidia makuhani wao. Tafadhali tuwe wakarimu katika suala hili”.  Askofu Kalumba amebainisha hayo kwa njia ya barua yake iliyosambazwa kwa waamini wa Jimbo la Livingstone.

Shukrani kwa mipango ya kichungaji wakati wa covid-19

Hata hivyo Askofu huyo aliwapongeza wachungaji katika jimbo lake kwa kuanzisha harakati zao za kichungaji kusaidia kukaa karibu na wanaparokia wao hata kama Makanisa mengi bado yamefungwa nchini kote. Vile vile amekipongeza kituo katoliki cha matangazo ya nchini humo kiitwacho 'Musi-O-Tunya FM', kwa kuto nafasi ya kuendesha vipindi vya kiliturujia hewani. “Sasa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu tulipoacha kukusanyika katika parokia zetu kwa ajili ya  ibada na huduma nyingine kwa sababu ya COVID-19. Mmekosa Misa, sakramenti na sala ya pamoja kwenye parokia. Katika muktadha huu, tunamlilia Mungu pamoja na Mtunga Zaburi: ‘Kama vile kulungu atamanivyo vijito vya maji ndivyo roho yangu inavyotamani wewe, Ee Mungu…' (Zab. 42: 1-4), Askofu alisema. Kwa kuongeza, “Katika parokia za jiji, utumiaji wa Radio ya Musi-O-Tunya, umesaidia sana watu katika maeneo yanayofunikwa na masafa ya redio ambapo wameweza angalau kufuatilia Misa na programu nyingine za kiroho kwenye redio. Tunawashukuru makuhani ambao wamejitolea kwa kazi hii ya uinjilishaji kupitia redio na njia nyingine za kielektroniki za mawasiliano. Tunaweza pia kufanya zaidi katika suala hili. Ninawatia moyo kila mtu kuwa mbunifu zaidi, "alisisitiza Askofu wa jimbo la Livingstone.

Zipo changamoto za kichungaji katika kuhudumia vijijini

Askofu hakukosa kukubali juu ya changamoto za kichungaji za kuhudumia vijijini wakati wa COVID-19 zilizopo. “Walakini, swali ni jinsi gani tunaweza kuendelea kuwasiliana kiroho licha ya umbali wa kijamii na umbali wa kijiografia kati yetu? Inawezekanaje mapadre na viongozi waliowekwa wakawasiliana na waamini (hasa walioko vijijini), kwa kutumia simu zao, mahali ambapo kuna mtandao, na njia za kiutamaduni za mawasiliano katika vijiji ambazo bado zinazaweza kushirikisha Neno la Mungu na imani nyingine ili kumwilishwa  kwa  habari na vifaa.

Kila siku makuhani katika jimbo na askofu wanawaombea waamini

Askofu Kalumba katika ujumbe wake aliwahakikishia wanaparokia wote kwamba ingawa Makanisa yamefungwa, Askofu na mapadri wanabaki katika huduma ya kila mtu katika jimbo hilo. Misa ya kila siku zinaombwa kwa ajili ya waamini wote wa Jimbo. "Tunaendelea kuomba kwa Mwenyezi Mungu na Upendo Mungu atuokoe na janga hili tunapojitunza sisi wenyewe na wapendwa wetu". Alihitimisha.

Hatari ya njaa nchini Zambia 

Nchini Zambia inasemekana kuwa zaidi ya watu milioni moja wako hatari ya kufa kwa njaa kufuatia na mafuriko kaskazini na mashariki mwa nchi. Baada ya ukame mwaka 2019  na virusi vya corona, mvua kubwa sasa zimeongezeka katika hali halisi ambayo tayari ni dhaifu kwa watu.

21 May 2020, 15:13