Tafuta

Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani WUCWO, linaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 103 tangu kuanzishwa kwake kwa kushiriki Sala ya kuomba huruma ya Mungu dhidi ya COVID-19. Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani WUCWO, linaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 103 tangu kuanzishwa kwake kwa kushiriki Sala ya kuomba huruma ya Mungu dhidi ya COVID-19. 

WUCWO Miaka 110: Sala Maalum Dhidi ya COVID-19

Mama Evaline Malisa Ntenga katika sala hii, amewaalika wanawake wakatoliki popote pale walipo watambue kwamba, wao ni wanawake wa imani, wanaitwa na kuchangamotishwa kubaki imara na thabiti wakiwa wameungana na Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kufikia utakatifu wa maisha kwa njia ya Sakramenti. Kwa kutafakari Neno la Mungu pamoja na kujenga utamaduni wa sala binafsi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Evaline Malisa Ntenga kutoka Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania, ni kati ya wajumbe wa Bodi ya Shirikisho la Vyama Vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, walioshiriki katika sala ya udugu wa kibinadamu tarehe 14 Mei 2020 kwa njia ya mtandao! Hii ni sala ambayo imeandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, ili kuunga mkono wito uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kukimbilia huruma na upendo wa Mungu, ili aweze kuwaokoa watu wake wanaoendelea kuteketea kwa janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Hii pia ilikuwa ni Siku ambayo WUCWO walikuwa wanakumbukia miaka 110 tangu lianzishwe. Kwa pamoja wamesali sala hii ambayo ilitungwa na Baba Mtakatifu Francisko kwa heshima ya Bikira Maria, wakati wa Mwezi Mei 2020 uliotengwa kwa heshima na Ibada kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa!

“Tunakimbilia ulinzi wako, Mama Mtakatifu wa Mungu, katika hali tete na majonzi ambayo yameugubika ulimwengu mzima, tunakimbilia kwako Mama wa Mungu na Mama yetu, tunatafuta usalama chini ya ulinzi wako. Ee Bikira Maria, utuangalie kwa macho yako yenye huruma katika Janga hili la Virusi vya Corona, na uwafariji wale wanaohuzunika na kuomboleza kutokana na vifo vya ndugu zao; waliozikwa hata wakati mwingine katika mazingira yanayo uchoma moyo. Wahurumie wale wote wanaoteseka kwa ajili ya wagonjwa, ili kuzuia maambukizi hawawezi kuwa nao karibu. Wajalie imani watu wenye hofu kwa kutokuwa na uhakika wa maisha yao kwa siku za mbeleni kutokana na athari za kiuchumi na kazi. Mama wa Mungu na Mama Yetu, tuombee kwa Mwenyezi Mungu, Baba wa huruma, ili kwamba, majaribu haya mazito yaweze kufikia ukomo na kuanza kurejea tena upeo wa matumaini na imani. Kama ilivyokuwa kwenye Harusi ya Kana ya Galilaya, ingilia kati na uwaombee mbele ya Mwana wa Mungu, ili aweze kuzifariji familia zenye wagonjwa na waathirika; afungue nyoyo zao ili ziweze kuwa na imani.

Walinde madaktari, wauguzi, wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na watu wa kujitolea ambao katika Janga hili wamekuwa mstari wa mbele, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao, ili kuokoa maisha ya wengine. Wasindikize katika mahangaiko yao ya kishupavu; wajalie nguvu, wema na afya. Uwe pembeni mwa wale wote ambao usiku na mchana wanawasaidia wagonjwa, na mapadre wakisukumwa na ari ya kichungaji na utume wa Kiinjili, wanajitahidi kuwasaidia na kuwahudumia wote. Bikira Maria angaza akili za wanasayansi, ili waweze kupata suluhu ili kushinda Virusi hivi. Wasaidie Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, ili waweze kutenda kwa hekima, huruma na ukarimu, kwa kuwasaidia wale wote wanaokosa mahitaji msingi ya maisha; kwa kuandaa programu zitakazotoa suluhu za kijamii na kiuchumi kwa kuwa na malengo ya muda mrefu wakiwa na moyo wa mshikamano.

Bikira Maria Mtakatifu, gusa dhamiri za watu ili kiasi kikubwa cha fedha kinachotumika kutengeneza na kuboresha silaha za maangamizi, badala yake, fedha hii, itumike katika tafiti muhimu ili kuzuia majanga kama haya kwa siku za usoni. Bikira Maria Mama mpendelevu, saidia kukuza ulimwenguni utambuzi kwamba, watu wote wanaunda familia kubwa ya binadamu; ili kwamba, wote wakiwa wameunganishwa na mshikamano na udugu waweze kusaidia kupambana na umaskini na hali mbaya ya maisha ya mwanadamu. Waimarishe waamini katika imani, daima wakidumu katika sala na huduma. Bikira Maria Faraja ya wanaoteseka, wakumbatie wanao wote wanaoteseka, waombee kwa Mwenyezi Mungu ili kwa mkono wake wenye nguvu aweze kuwaokoa watu wake kutoka katika Janga hili, ili hatimaye, maisha yaweze kuanza tena katika hali ya kawaida na utulivu. Tunakutumainia, ili katika safari yetu uwe ni alama ya wokovu na matumaini, Ee mpole, Ee mwema Ee mpendevu, Bikira Maria. Amina.

Kwa upande wake, Mama Evaline Malisa Ntenga katika sala hii, amewaalika wanawake wakatoliki popote pale walipo watambue kwamba, wao ni wanawake wa imani, wanaitwa na kuchangamotishwa kubaki imara na thabiti wakiwa wameungana na Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kufikia utakatifu wa maisha kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti za Kanisa; Kwa kusikiliza, kutafakari na kunafsisha Neno la Mungu pamoja na kujenga utamaduni wa sala binafsi. Wanawake Wakatoliki ni wanawake wa shoka katika mambo ya imani, wanataka kujitahidi kuhakikisha kwamba, wanamwilisha upendo wa Kristo katika uhalisia wa maisha yao.

Ni wanawake wa imani wanaotaka kujizatiti katika mchakato wa kurithisha imani kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa kutambua kwamba, wao kimsingi ni mashuhuda na vyombo vya upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani. Ni wanawake wanaojitambua kwamba kwa hakika ni “majembe” ya msaada kwa jirani zao wakati wa raha na shida. Ni wanawake wa imani walioteuliwa na Kristo Yesu ili kusimama kidete kulinda na kudumisha zawadi ya imani katika maisha. Hawa ni wanawake wa imani ambao wamejiweka wazi ili kutafuta njia mpya zinazosimikwa katika ubunifu, ili kutoa nafasi kwa vijana wa kizazi kipya kukutana, kukua na kukomaa mahali ambapo wataweza kugundua na hatimaye kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu wito wao mintarafu wito na dhamana ya Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO.

Katika mkutano huu wa sala kwa njia ya mtandao, wajumbe wameshirikishana alama mbali mbali kama ushuhuda wa imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Wametumia fursa hii kwa ajili ya kuzikumbuka na kuziombea familia zinazokabiliana na changamoto mbali mbali za maisha. Watu wanaoteseka kwa baa la umaskini, athari za mabadiliko ya tabianchi; vita, kinzani, misigano, dhuluma na nyanyaso mbali mbali. Wamewaombea wanawake wakatoliki duniani, ili kweli waweze kuwa: wema, watakatifu, waadilifu na wenye ujasiri tayari kujitoa bila ya kujibakiza katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao katika medani mbali mbali za maisha. Katika kumbukizi la Miaka 110 tangu Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, lianzishwe, wanamshukuru na kumwomba Mwenyezi Mungu ili asaidie mchakato wa kumtangaza Mwenyeheri Pilar Bellosillo kuwa Mtakatifu. Huyu ndiye muasisi wa Shirikisho la Vyama vya Wanawake Wakatoliki Duniani. Wajumbe hawa wameshirikishana sala katika makundi, wakatoa shuhuda za maisha yao kuhusu umuhimu wa Shirikisho hili na hatimaye, wakasali ile Sala ya Kikristo kwa Ushirika na Mazingira iliyotungwa na Baba Mtakatifu Francisko na kuwekwa mwishoni mwa Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote”.

Wanawake Wakatoliki Duniani

 

14 May 2020, 13:48