Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume: Utimilifu wa Pasaka ya Bwana na Mwanzo wa Kanisa: Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume: Utimilifu wa Pasaka ya Bwana na Mwanzo wa Kanisa: Umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! 

Sherehe ya Pentekoste: Roho Mtakatifu: Karama na Ushuhuda

Sherehe ya Pentekoste ni adhimisho llinalohitimisha kipindi cha Pasaka ya Kristo Yesu kwa kumminina Roho Mtakatifu ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu. Ni siku ya kutafakari juu ya uwepo wa Roho Mtakatìfu katika Kanisa na katika maisha ya waamini na ni siku ya kuomba kuimarishwa kwa mapaji yake saba na kujazwa na matunda yake! Ushuhuda!

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

Utangulizi: Karibu ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika kipindi hiki cha Tafakari ya Neno la Mungu. Dominika hii, Kanisa linaadhimisha sherehe ya Pentekoste, yaani tukio la Roho Mtakatifu kuwashukia kwa pamoja Mitume na wafuasi. Sherehe hii ya Pentekoste ndiyo inayohitimisha kipindi cha Pasaka na kuashiria kuanza kwa kipindi kipya cha maisha ya ushuhuda kwa Kristo kwa mafumbo yake makuu. Kwa jinsi hii, Pentekoste husherehekewa pia kama siku ya kuzaliwa kwa Kanisa kama jumuiya inayomshuhudia na kumtangaza Kristo. Katika Kanisa la Tanzania, Pentekoste ni sherehe pia ya Halmashauri ya Walei, sherehe inayolenga kuendeleza mwaliko uleule wa Kanisa zima kuutwaa utume wake wa kumshuhudia Kristo.

Somo la Kwanza (Mdo. 2:1-11) kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume linaelezea tukio lenyewe la Pentekoste. Ni muhimu kujua kuwa Wayahudi walikuwa na sherehe yao ya Pentekoste hata kabla ya kuzaliwa Yesu. Pentekoste hiyo ya wayahudi ilikuwa ni sherehe ya shukrani ya mavuno na iliitwa Pentekoste kwa sababu ilisherehekewa siku 50 baada ya Pasaka yao, yaani kumbukumbu ya kutolewa utumwani Misri. Sherehe hii ilikuwa ni mojawapo ya sherehe za hija ambapo kila Myahudi alilazimika kwenda Yerusalemu kuhiji. Siku hiyo ya Pentekoste, Mitume na wafuasi wengine wa Yesu akiwemo Bikira Maria walikuwa pamoja katika nyumba wakisurbiri ujio wa Roho Mtakatifu. Ndipo ukaja upepo, ukaijaza nyumba yote na ndimi za moto zikawakalia kila mmoja wao. Wakajazwa Roho Mtakatifu. Wakatoka nje kwa ujasiri na nguvu wakaanza kunena kwa lugha na kutangaza matendo makuu ya Mungu. Umati mkubwa wa watu uliokuwapo kwa sherehe ya Pentekoste kutoka sehemu mbalimbali wakashangaa namna kila mmoja alivyowaelewa katika lugha yake mwenyewe.

Somo linaonesha kuwa mojawapo ya alama za ujio wa Roho Mtakatifu ni kunena kwa lugha. Jambo hili linakumbushia tukio lile la mnara wa Babeli katika kitabu cha Mwanzo (rej. Mwa 11:1-9). Kitabu cha Mwanzo kinaelezea tukio la mnara wa Babeli kama dhambi ya mwanadamu dhidi ya agizo la Mungu la wanadamu kuenea na kwenda kuijaza dunia (Mwa 1:28). Kinyume na agizo la Mungu, tukio la Babeli linaelezwa kuwa ni makusudio ya mwanadamu kujikusanya pamoja, kujijengea mji na kuunda umoja ili kujinasua kutoka  maongozi ya kimungu na kumfanya mwanadamu atende kama anavyoona yeye sawa. Hapo ndipo Mungu akaamua kuwatawanya kwa kuwachanganya lugha. Kwa jinsi hii, kunena kwa lugha kunakofuatia ujio wa Roho Mtakatifu Sherehe ya Pentekoste kunakuwa ni alama ya uumbaji mpya wa jamii ya wanadamu inayokubali kuongozwa na Roho mwenyewe wa Mungu katika kutekeleza matakwa yake.

Somo la Pili (Kor 12:3b-7, 12-13) ni kutoka katika Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorinto. Katika somo hili, Mtume Paulo anafafanua kuwa Roho Mtakatifu ndio kiini cha utendaji wa Kanisa na ndio chemichemi ya karama, huduma na utume wote wa Kanisa. Pamoja na fundisho hilo, Paulo haachi kusisitiza kuwa karama mbalimbali ambazo Roho anawajalia waamini ni kwa ajili ya Kanisa na hasa zaidi kwa ajli ya kuujenga umoja wa Kanisa. Huu si umoja kama ule mwanadamu alioutafuta wakati wa mnara wa Babeli ili ajiimarishe yeye kinyume na mapenzi ya Mungu. Umoja huu wa Kanisa ni umoja unaolitambulisha Kanisa kama mwili wa Kristo ambao una viungo vingi na kila kiungo kinafanya kazi kwa ajili ya faida ya mwili mzima. Somo hili linatualika kuzipokea karama mbalimbali ambazo Roho amezimwaga katika Kanisa na kuwa tayari kuzitumia kwa ajili ya Kanisa. Hii ni pamoja na kutambua karama mbalimbali walizonazo wenzetu na kuzipa nafasi kwa ajili ya ustawi wa Kanisa na jamii kwa ujumla.

Injili (Mt 20:19-23) Katika Injili ya leo, Kristo mfufuka anawatokea mitume wake na kuwavuvia Roho Mtakatifu. Kadiri ya mwinjili Yohane, tendo hili lilitokea jioni ya siku ile ile ya Pasaka Kristo alipofufuka. Mitume wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu ya wayahudi Yesu anawatokea,  anawatoa hofu na hapo hapo anawapa Roho Mtakatifu ambaye alikuwa amewaahidia. Injili inaonesha wazi kuwa waliopokea Roho Mtakatifu katika siku hii ni Mitume peke yao. Na Roho huyu waliyempokea ni Roho anayewapa nguvu na mamlaka ya kutenda yale ambayo Kristo mwenyewe aliyatenda. Kristo aliponya roho za watu kwa kuwaondolea dhambi. Uwezo huu, sasa anawapa pia mitume anapowaambia “wowote mtakaowaondolewa dhambi wataondolewa na wowote mtakaowafungia dhambi watakuwa wamefungiwa”. Maneno haya huashiria nguvu ya kisakramenti ambayo Mitume wanapewa katika kuondolea dhambi. Kumbe kwa njia ya Roho Mtakatifu nguvu na uwepo ule ule wa Kristo unaendelea kuwa hai katika Kanisa kwa njia ya Sakramenti ambazo Mitume wanaziadhimisha kwa Jina lake.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, Sherehe ya Pentekoste ni adhimisho llinalohitimisha kipindi cha Pasaka ya Kristo kwa kumminina Roho Mtakatifu ambaye amedhihirishwa, ametolewa na kushirikishwa kama Nafsi ya Mungu. Ni siku ya kutafakari juu ya uwepo wa Roho Mtakatìfu katika Kanisa na katika maisha ya waamini na ni siku ya kuomba kuimarishwa kwa  mapaji yake saba na kujazwa na matunda yake ambayo ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu , upole na kiasi kama anavyofundisha mtume Paulo (Rej Gal 5:22). Roho Mtakatifu ni Nafsi ya tatu ya Mungu mmoja. Ni jina halisi la yule ambaye tunamwabudu na kumtukuza pamoja na Baba na Mwana. Kanisa limempokea Roho Mtakatifu kutoka kwa Bwana na linamuungama katika ubatizo wa watoto wake wapya.  Licha ya jina lake hili halisi, Roho Mtakatifu anaitwa pia: Mfariji, Msaidizi, Mtakasa, Roho wa Bwana, Kidole cha Mungu na Roho wa Mungu.

Roho Mtakatifu yupo tangu hata kabla ya nyakati akitenda kazi katika umoja na Baba na Mwana. Utume wake huu hata hivyo ulibaki umejificha hadi ulipowadia utimilifu wa nyakati alipomiminwa ulimwenguni. Roho Mtakatifu amekuwapo katika uumbaji ikitulia juu ya uso wa maji (Mwa 1::2). Ameshiriki kumuumba mwanadamu pamoja na vitu vyote. Mtakatifu Ireneo anasema “Mungu amemuumba mwanadamu kwa mikono yake mwenyewe yaani Mwana na Roho Mtakatifu na juu ya mwili ulioumbwa alitengeneza sura yake mwenyewe hivi kwamba kile kilichoonekana kilichukua sura ya Mungu” (Rej. KKK 704). Ni Roho Mtakatifu aliyewaongoza waisraeli kutoka Misri kuelekea nchi ya ahadi, mchana akiwa mbele yao kama wingu na usiku kama mnara wa moto. Roho huyu ndiye aliyenena kwa vinywa vya manabii akiwafundisha kulishika Agano na kumtumainia masiha ajaye.

Wakati wa kuja kwake Masiha ni Roho huyu aliyemtayarisha Maria kwa neema yake ili awe “amejaa neema”. Ndani ya Bikira Maria ni Roho Mtakatifu aliyetekeleza mpango wa Baba uliojaa upendo wa kuzaliwa duniani Mwanae wa Pekee. Katika Bikira Maria, Roho Mtakatifu alimdhihirisha mwana wa Baba aliyefanyika mwili na kwa njia ya Bikira Maria Roho Mtakatifu akaanza kuwaweka watu katika ushirika pamoja na Kristo ambao ndio lengo la pendo la huruma ya Mungu.  Kristo mwenyewe ametekeleza utume wake katika ushirika na Roho Mtakatifu. Baba alimpaka mafuta kwa Roho Mtakatifu alipobatizwa Yordani na kumuongoza daima. Naye Kristo ndiye aliyemfunua Roho Mtakatifu na kummimina kwa wanafunzi wake na kwa kanisa lake katika utumilifu wa nyakati, adhimisho tunalolifanya katika Sherehe ya Pentekoste hii. Sherehe hii ya Pentekoste inakuhakikishia kuwa Roho huyu huyu yupo pamoja nasi na yupo pamoja na Kanisa zima kama kiini na nguvu yake ya utendaji. Uwepo wa Roho Mtakatifu katika Kanisa ni matumaini tosha kabisa kwamba hata katika changamoto nyingi ambazo Kanisa linazipitia, Roho huyu atalitunza na kulihifadhi salama katika misingi yake nalo litaendelea kung’ara na kuwa sakramenti ya wokovu kwa ulimwengu mzima.

Liturujia: Pentekoste

 

30 May 2020, 07:45