Tafuta

Vatican News
Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol, hivi karibuni amekimbilia huruma na upendo wa Mungu ili kuwaombea waathirika wote wa Virusi vya Corona, COVID-19. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol, hivi karibuni amekimbilia huruma na upendo wa Mungu ili kuwaombea waathirika wote wa Virusi vya Corona, COVID-19.  (AFP or licensors)

Patriaki Bartolomeo wa Kwanza: Sala Kuomba Huruma ya Mungu

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Costantinopol, hivi karibuni, katika hali ya unyenyekevu mkubwa, kwa kutambua udhaifu wa binadamu na kwa kukiri: wema, ukuu wa Mungu, mwenye haki, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake, alikimbilia huruma ya Mungu kwa sala kama sehemu ya mapambano ya Kanisa dhidi ya COVID-19 kwenye Madhabahu ya Mama wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mama Kanisa anaendelea kusoma alama za nyakati kwa kutumia silaha zifuatazo: Kufunga na kusali; Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbali mbali; Tafakari ya Neno la Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha; Matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na Ibada ya Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Tangu kulipotokea Janga la Corona, COVID-19, waamini wa dini na madhehebu mbali mbali wameendelea kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, aweze kuwaepusha watu wake na janga hili la Corona, COVID-19, awaponye wagonjwa wote kwa mkono wake wenye nguvu na matumaini; awakinge watu wa Mataifa yote wasipate na maambukizi mapya ya Corona. Awajalie wanasayansi, watafiti na wanasiasa mang’amuzi sahihi ili waweze kushirikiana na kushikamana kama Jumuiya ya Kimataifa, ili waweze kupata chanjo na hatimaye, tiba ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Ni katika muktadha huu, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Costantinopol, hivi karibuni, katika hali ya unyenyekevu mkubwa, kwa kutambua udhaifu wa binadamu na kwa kukiri: wema, ukuu wa Mungu, mwenye haki, mwingi wa huruma na mapendo kwa waja wake, alikimbilia huruma ya Mungu kwa sala kama sehemu ya mapambano ya Kanisa dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwenye Madhabahu ya Mama wa Mungu, “Theotokos” yaliyoko huko Balikli mjini Istanbul nchini Uturuki. Katika sala hii anatambua na kukiri kwamba, Kristo Yesu, Neno wa Baba wa milele ana upendo usiokuwa na kifani kwa binadamu, kwa sababu ameshiriki ubinadamu wao kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu lakini hakutenda dhambi. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu, amemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na kifo. Akawaimarisha katika hija ya imani na matumaini kwa kuwapelekea Roho Mtakatifu, anayeungaza ulimwengu wote kwa mwanga wa ukweli!

Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Costantinopol, kwa kupiga magoti kwa unyenyekevu mkuu, anamwomba Mwenyezi Mungu mwenye nguvu, mjuzi wa mambo yote na ambaye yuko sehemu zote, aweze kusikiliza sala na dua za watu wake. Anamtambua Mwenyezi Mungu kuwa ni chemchemi ya wema, utakatifu na mweza wa yote, aweze kunyoosha mkono wake wenye nguvu na kuwasaidia waja wake kwani wanatambua kwamba, ataweza kuwakirimia zaidi hata kile ambacho hawakuthubutu kumwomba! Anamwomba Mwenyezi Mungu aweze kuwaokoa watu wake na Janga la homa kali inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na madhara yake. Ashushe neema na baraka kwa wagonjwa; awafariji na kuwapatia nafuu kutokana na mateso yao na hatimaye, aweze kuwaponya haraka ili hatimaye, waweze kurejea tena katika shughuli zao za kila siku.

Patriaki Bartolomeo wa kwanza anamwomba Mwenyezi Mungu kuwasaidia na kuwaenzi madaktari, wauguzi na wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa. Awalinde watu wote na kuwapatia tunza yake ya kibaba. Mwenyezi Mungu, daktari mkuu wa mwili na roho, awajalie waja wake kuwa na afya ya roho na mwili. Wawe na hekima na busara na wanyoofu wa moyo ili waweze kupata neema na baraka za mbinguni. Mwenyezi Mungu aendelee kuwapatia na kuwafundisha Amri zake! Awakirimie imani tendaji inayomwilishwa katika matendo; matumaini kwa wale wenye mashaka na wasi wasi mkubwa, ili Jina yake tukufu na takatifu lipate kujidhihirisha. Kristo Yesu, Mwana mpendwa wa Mungu, asikilize sana za waja wake! Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, awasaidie waamini kupyaisha tena Amri za Mungu, kwa njia ya maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu, “Theotokos”, chemchemi ya upyaisho wa maisha inayowawezesha waamini kupata tiba na uponyaji wa magonjwa yanayowasumbua. Mwishoni Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Costantinopol anawaomba watakatifu wote wa Mungu waliopata upendeleo mbele ya uwepo wake, wawasaidie watu wa Mungu wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu kama sehemu ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Patriaki COVID-19

 

07 May 2020, 13:53