Tafuta

Vatican News
Radio Vatican inaungana na Padre Agapito Mhando kuomboleza kifo cha Mama Elizabeth Bernard Seuta, kilichotokea Dar es Salaam, tarehe 29 Mei 2020. RIP. Radio Vatican inaungana na Padre Agapito Mhando kuomboleza kifo cha Mama Elizabeth Bernard Seuta, kilichotokea Dar es Salaam, tarehe 29 Mei 2020. RIP. 

Tanzia: Mama Elizabeth Seuta: Mtu wa watu, Mchapakazi na Sala!

Radio Vatican inapenda kuungana na Padre Agapito Mhando, kuomboleza kifo cha Mama Elizabeth Bernard Seuta, Mama Mzazi wa Padre Agapito Mhando, kilichotokea Jijini Dar es Salaam, Alfajiri ya tarehe 29 Mei 2020. Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican wanapenda kutoa salam za rambi rambi kwa mzee Bartholomeo Luizo Mhando, kwa kuondokewa na asali wa moyo wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sakramenti zote, na hasa zile za kuingizwa katika Ukristo, zina kama lengo, Pasaka ya mwisho ya mtoto wa Mungu, ile ambayo kwa kifo inamwingiza katika uzima wa Ufalme wa mungu. Sasa kinatimilizika kile alichokisadiki katika imani na matumaini: “Nangojea ufufko wa wafu na uzima wa ulimwengu ujao”. Maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, ambaye ndani mwake, waamini wanachota tumaini lao moja, yaani kwa kutoka katika maisha ya hapa duniani ili kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kanisa linafundisha kwamba, kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo kwa kufanana kamili na “sura ya Mwana” kulikotolewa kwa mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme wa Mungu, uliotangulizwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.  Hata kama analazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi.

Mama Elizabeth Bernard Seuta, aliyezaliwa tarehe 21 Agosti 1951 amekuwa ni nguzo na kiungo thabiti cha familia yake. Amejitahidi kuwa ni shuhuda na chombo cha umoja, mshikamano na upendo katika mchakato wa ujenzi wa familia kama Kanisa dogo la nyumbani. Alikuwa ni Mama mpole, asiyependa makuu! Aliwapenda na kuwathamini jirani zake. Alikuwa ni mchapakazi, aliyejitahidi kuitegemeza familia yake: kiroho na kimwili. Alikuwa ni mtu wa sala na Bikira Maria alikuwa ni tegemeo lake la daima wakati wa raha na shida. Alipenda sana kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Msaada wa Wakristo. Itakumbukwa kwamba, Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Wakristo, Maskati, Jimbo Katoliki la Morogoro, kunako mwaka 2009 imeadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Ukristo. Kumbe, si haba kumwona Mama Elizabeth Seuta, akiwa na Ibada kwa Bikira Maria, Msaada wa Wakristo. Ibada ya mazishi imefanyika tarehe 30 Mei 2020 na kuongozwa na Padre Joseph Shukuru na mahubiri kutolewa na Padre Salvinus Kwembe, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Patris, Jimbo Katoliki la Morogoro.

Radio Vatican inapenda kuungana na Padre Agapito Mhando, kuomboleza kifo cha Mama Elizabeth Bernard Seuta, Mama mzazi wa Padre Agapito Mhando, aliyefariki dunia, alfajiri ya tehe 29 Mei 2020, huko Jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu. Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili wanapenda kutoa salam za rambi rambi kwa Mzee Bartholomeo Luizo Mhando kwa kuondokewa na asali wa moyo wake, waliopendana upedo! Tunamwombea Padre Mhando moyo mkuu, ili aweze kuubeba msiba huu kwa imani na matumaini katika ufufuko, maisha na uzima wa milele. Kwa Padre Mhando hali ni ngumu kwa sababu hawezi kwenda kumsindikiza Mama yake mpendwa kwenye nyumba yake ya milele kutokana na itifaki ya kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona. Roho ya Marehemu Mama Elizabeth Bernard Seuta ipate, raha ya milele na mwanga wa milele, upate kumwangazia na apumzike kwa amani. Amina. 

Tanzia
29 May 2020, 14:13