Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa tarehe 10 Mei 2020 inaadhimisha Siku ya Mama Duniani ili kuenzi tunu msingi za maisha ya kimama, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za wanawake duniani! Jumuiya ya Kimataifa tarehe 10 Mei 2020 inaadhimisha Siku ya Mama Duniani ili kuenzi tunu msingi za maisha ya kimama, kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za wanawake duniani! 

Siku ya Mama Duniani 2020: Injili ya Uhai! Utu na Heshima!

Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, linasema, hii ni siku muhimu ya kuwaheshimu na kuwaenzi akina mama kutokana na mchango wao mzito katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu mwaliko wa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo tangu pale mtoto anapotunga mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika! Uhai!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelium vitae” yaani “Injili ya uhai” kwa ufupi anakazia kuhusu: Thamani ya maisha, ukuu na utu wa binadamu kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni Injili ya upendo wa Mungu kwa binadamu; utu na heshima yake, mambo msingi yanayofumbatwa katika Injili. Katika ulimwengu mamboleo kuna mambo ambayo yanaendelea kutishia Injili ya uhai kwa kukumbatia utamaduni wa kifo. Haya ni matokeo ya watu kukengeuka pamoja na kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema. Kuna sera na mikakati mbali mbali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii inayotishia Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Mtakatifu Yohane Paulo II anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete: kuheshimu, kulinda na kuhudumia Injili ya uhai, ili kukuza na kudumisha haki, maendeleo fungamani ya binadamu, uhuru wa kweli, amani na furaha ya kweli inayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu. Waamini wanapaswa kujipambanua kuwa ni watu wanaotetea Injili ya uhai kwa ajili ya maisha.

Kardinali Timothy Dolan aliwahi kusema kwamba, wananchi wengi nchini Marekani wanatamani kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya uhai kwa kuwapokea, kuwalea na kuwatunza watoto. Wamarekani wanasema, fedha inayotumika kugharimia mchakato mzima wa utoaji mimba, ingeweza kusaidia kuenzi na kudumisha uhai wa mtoto ambaye hajazaliwa bado. Mashuhuda wa Injili ya uhai wanapaswa kuwa na mwelekeo sahihi kuhusu uhai wa binadamu ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kutunzwa na kudumishwa na wote! Kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema ambao wameguswa na kutikiswa na utamaduni wa kifo unadhalilisha basi huu ni wakati wao muafaka wa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa utamaduni na Injili ya uhai.

Jumapili, tarehe 10 Mei 2020 Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Siku ya Mama Duniani na Waswahili wanachombeza kwa kusema “eti ni nani kama Mama”? Katika maadhimisho haya, Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani, USCCB, linasema, hii ni siku muhimu sana ya kuwaheshimu na kuwaenzi wanawake kutokana na mchango wao mzito katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni changamoto ya kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri mapenzi ya Mungu. Ni fursa ya kuwakumbuka na kuwaombea akina mama ambao wamepewa dhamana ya kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai. Kwa wale wanawake ambao wamepitia kipindi kigumu wakati wa ujauzito, wafarijike kwa sala na sadaka inayotolewa na watu wa Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Familia ya Mungu nchini Marekani katika maadhimisho ya Mwezi Mei, 2020 uliotengwa maalum kwa ajili ya heshima na ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, inapenda kuwaweka wanawake wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria!

Bikira Maria awe ni mfano bora wa kuigwa katika kutimiza wajibu wao kama mama ndani ya familia na jamii katika ujumla wake. Awe ni mwombezi wa akina mama wote wenye ujauzito kwa wakati huu, ili waweze kuwalinda na kuwatunza watoto wao ili hatimaye, waweze kuzaliwa salama salimini. Si akina mama wote wanaadhimisha Siku hii kwa amani na utulivu wa ndani! Kuna baadhi ya wanafamilia wanapambana na ugumba katika familia; kuna baadhi ya wazazi wamepoteza watoto wao au hata wazazi wao hasa katika kipindi hiki cha janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna baadhi ya akina mama wamejikuta wakitumbukia na kumezwa kwenye utamaduni wa kifo kwa kukumbatia vitendo vya utoaji mimba. Kwa kuzingatia uzuri na utakatifu wa maisha; dhamana na wajibu wa akina mama katika maisha ya familia na jamii katika ujumla wake, Siku ya Mama Duniani ni muda muafaka wa kuwaenzi akina mama duniani!

Siku ya Mama Duniani 2020

 

09 May 2020, 07:45