Tafuta

Injili ya Jumapili ya V ya Kipindi cha Pasaka ni mwaliko wa kufanya tafakari ya kina kuhusu Wosia wa Kristo Mfufuka kwa wafuasi wake: Njia, Ukweli na Uzima! Injili ya Jumapili ya V ya Kipindi cha Pasaka ni mwaliko wa kufanya tafakari ya kina kuhusu Wosia wa Kristo Mfufuka kwa wafuasi wake: Njia, Ukweli na Uzima! 

Jumapili ya V ya Pasaka: Wosia wa Kristo Yesu: Njia, Ukweli na Uzima!

Injili ya leo ni wosia unabeba maelezo ya msingi au mambo ya kuzingatia kama mwongozo wa maisha mara baada ya kuondoka kwake hapa ulimwenguni, ni jinsi ya kuenenda na kutenda wakati anapokuwa hayupo pamoja nasi, hivyo ni maneno yenye uzito mkubwa kabisa kwa kila mmoja. Kristo Yesu anasema, Yeye ni Njia, Ukweli na Uzima! Ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Injili ya leo inaanza na maneno ya Yesu ya kuwafariji wanafunzi wake, ni moja ya hotuba za Yesu za kuwaaga na hivyo kuwahusia wanafunzi wake. Ni hotuba inayowaacha wanafunzi wake wakiwa na mioyo yenye mashaka na wasiwasi, wanakuwa na huzuni kuwa kiasi Mwinjili anatumia kitenzi cha Kigiriki cha ‘’ταρασσειν’’ (tarassein) kitenzi kinachohashiria pale bahari inapochafuka kabisa, hivyo mioyo yao ilikuwa si tu na huzuni bali na machafuko ya ndani kabisa kiasi cha kupoteza si tu amani na utulivu wa akili bali hata na mwili pia. Labda ndio hali tunayokuwa nayo katika ulimwengu wetu wa leo tunapopambana sote na janga la COVID-19. Si tu mashaka na huzuni bali ni hofu kubwa inayosumbua si tu akili zetu bali hata na mioyo na miili yetu. Yesu kama alivyowatuliza mitume wake wawe na kuwaalika kuwa na imani kwake hivyo hivyo leo ananialika mimi na wewe kuwa na amani na utulivu na kuwa na imani naye.

Sehemu ya Injilli ya Dominika ya leo ni moja kati ya hotuba tatu za Yesu alizowaachia wanafunzi wake wakati wa Karamu ile ya Mwisho kabla ya mateso, kifo na ufufuko wake. Ni maneno ya buriani na wosia kwa wanafunzi na rafiki zake. Na maneno ambayo karibu kila mmoja weu angetamani ayasikie kutoka kinywani kwa mzazi wake kabla ya kulala katika usingizi wa milele. Ni wosia unabeba maelezo ya msingi au mambo ya kuzingatia kama mwongozo wa maisha mara baada ya kuondoka kwake hapa ulimwenguni, ni jinsi ya kuenenda na kutenda wakati anapokuwa hayupo pamoja nasi, hivyo ni maneno yenye uzito mkubwa kabisa kwa kila mmoja. Hivyo ni maneno pia kwako na kwangu, ni wosia wa kila mmoja wetu. Mama Kanisa anatualika leo kutafakari wosia huu wa Yesu baada ya ufufuko wake kwani kama tunavyojua hata katika tamaduni zetu za kiafrika huwa tunaufungua na kuusoma wosia mara baada ya kifo cha huyo anayetuusia. Hivyo leo ni nafasi muafaka nasi tunaalikwa kuyasikia na kuyatafakari maneno yale ya wosia wa Yesu kwetu baada ya mateso, kifo na ufufuko wake. Ni mwaliko wa kukaa na kuanza kuzingatia maneno yake.

Si tu Yesu anatualika kutofadhahika na kuhuzuznika mioyoni mwetu bali pia anatuhakikishia kuwa: ‘’…Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama isingekuwa hivyo, ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi. Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi. Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda’’. Yohane 14:2-4 Mara nyingi maneno haya ni magumu kueleweka hasa maana yake, si tu kwa mitume nyakati zetu bali hata nasi leo. Wengi tunaposoma mara moja tunapata picha kuwa Yesu anazungumzia nafasi kule mbinguni anakokwenda baada ya kupaa kwake. Lakini kwa kweli haileti maana sana kwani mbinguni nafasi zipo tayari kwa nini basi anasema anakwenda kuziandaa? Mbinguni pia si mahali hivyo kuanza kufikiria juu ya nafasi kwa kila mmoja kama vile nafasi tunazoweza kuzizungumzia katika ulimwengu huu wa muda na nafasi? Hakika mbinguni ni makazi ya milele yasiyo akisi uhalisia wa maisha ya hapa duniani kwani ni muunganiko na Mungu, ni maisha ya umilele na utukufu pamoja na Mungu kwenye nafasi kwa kila mmoja wetu ila sio nafasi kwa maana tunayoweza kuifikiria katika ulimwengu huu wa sasa.

Kwa kweli maana ya maneno hayo ya Yesu yanaakisi ukweli wa maisha yetu ya sasa, ndio maisha ya huduma ya upendo katika jumuiya ya wanakanisa. Zaidi anatualika nasi kushiriki na kutembea katika njia ile aliyopitia yeye. Njia ile anapita Yeye kwa nafasi ya kwanza lakini pia anatualika nasi tulio wafuasi na rafiki zake kupitia njia ile. Pia ni hakika kuwa kila mmoja wetu ana nafasi au mahali katika Upendo na Huruma yake ya Kimungu kwetu. Wokovu sio wito wa wachache bali wa kila mwanadamu wa kila nyakati na rangi na kabila na taifa. Ni Upendo wa Mungu usimbagua hata mmoja wetu. Mwinjili Luka leo anatuonesha wanafunzi wawili wa Yesu nao ni Tomaso na Filipo. Kwa kweli zaidi ya kutuonesha kama wanafunzi waliokuwepo katika historia bali pia ni ishara kwa kila mmoja wetu. Tomaso anajulikana pia kama Pacha (Didimo) ndio kusema ananialika mimi na weye kuwa pacha wake. Ni Tomaso wakati Yesu alipopewa taarifa za ugonjwa wake Lazaro na kutaka kurejea Yudea tunaona anadiri kusema waende pamoja naye ili hata ikimpasa kufa basi wafe naye. Yohane 11: 16 Lakini Tomaso anajulikana zaidi kwa tukio la kutoamini baada ya ufufuko wake Yesu. Yohane 20

Tomaso aliyejulikana pia Pacha ni kielelezo cha mfuasi wa Yesu ambaye daima ili kufikia imani lazima aone na athibitishe pasi na mashaka. Na ndio hata leo tunamwona Tomaso akisema: ‘’Tomaso akamwuliza, Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?’’ Yohane 14:5 Labda hata nasi tunapokuwa na huzuni na mashaka makubwa yawezekana kabisa katika sala na maombi yetu tunamuomba Yesu ajifunue na kujidhihirisha waziwazi ili ulimwengu upate kumwamini na kuokoka, tunataka tuone uwezo na ukuu wake kwa kututoa na kutuokoa katika janga hili la COVID-19. Jibu la Yesu kwa Tomaso ndilo jibu lake pia kwangu na kwako leo tunapokuwa na maswali mengi na zaidi sana tukiwa na mioyo yenye kujaa na fadhaa na mashaka mkubwa. ‘’Εγω ειμι η οδος και η αλεθεια και η ζωη’’ ‘’ Mimi ni njia, na ukweli na uhai’’ Maneno yale ya Kigiriki anayotumia Yesu kujitambulisha ni ‘’Ego eimi’’ yenye maana ya ‘’Mimi ndimi’’ ni maneno yanayomtambulisha Mungu hivyo kwa myahudi mara moja anaposikia maneno hayo ni maneno yenye maana ya kusema ‘’Mimi ni Mungu’’, hivyo Yesu pia anajitambulisha kwetu leo kuwa Yeye mfufuka ni Mungu wetu. Ni muweza na mwenye ukuu wote.

Yesu ni Njia! Njia anayozungumzia Yesu sasa tunaweza kuielewa kuwa ni ile inayotuongoza katika Pasaka, ni njia ngumu kwani inatudai nasi kutoa maisha yetu kwa upendo kama alivyofanya yeye. Yesu aliwaalika na hata leo anatualika nasi ili ilikuwa ngumu kwa mitume kumuelewa kama vile ilivyo ngumu kwetu leo kuuelewa wito na mwaliko wa Yesu wa kushiriki na kutembea katika njia ile. Njia ya kuwa tayari kutoa maisha yetu kama Yeye alivyoyatoa kwa ajili yetu. Siyo njia ya kufikirika bali ni Yeye mwenyewe. Pale Antikoa kabla wakristo kuanza kujulikana kwa jina la wakristo waliitwa watu wa njia, ndio kusema wale wanaenenda katika njia ya Kristo msulubiwa. Yesu ni Ukweli. Ukweli anaozungumzia sio kweli ya kiakili bali maana ya maswali na mashaka yetu yote, Yeye ni jibu na suluhisho la kila jambo linalotusibu kutupelekea kufadhaika katika maisha ya siku kwa siku. Yeye ndiye nuru na mwanga wa mashaka yetu na maswali yetu yote. Anatualika kumwangalia Yeye pale tunapokosa majibu ya maswali ya maisha.

Yesu ni uhai! Ni mwaliko tena kwa kila mmoja wetu kumwangalia Yesu mfufuka kwani ni kwake tunajaliwa maisha ya kweli na hasa maisha ya umilele. Hivyo hata kama tutakufa na kwa hakika tutakufa ili tunajawa na matumaini kuwa kwake tutaishi milele yote, kifo hakina neno la mwisho kwani sisi tunaoalikwa kumwamini tunakuwa na hakika na maisha ya umilele. Ila kila mmoja anayekubali kutembea katika njia ile anahakikishiwa nafasi katika nyumba ya Baba, yaani Jumuiya ya wanakanisa. Ni katika jumuiya hapo kuna nafasi kwa kila mmoja wetu wa kutoa huduma na kutumikia wengine kwa upendo, hakuna mmoja anayekosa nafasi ya huduma katika nyumba ya Mungu Baba yaani Jumuiya ya Wanakanisa. Kila mmoja anaitwa kutoa huduma kwa upendo. Ni leo tunaona Mama Kanisa anatualika sote wabatizwa kila mmoja kuchukua nafasi na kutumikia wengine bila kujali tofauti zetu mbali mbali. Sote kila mmoja anaitwa na kualikwa kuchukua nafasi yake katika kuujenga Mwili Fumbo wa Kristo yaani Kanisa. Hakuna hata mmoja anayeitwa kuwa mtazamaji bali mawe hai katika Mwili Fumbo wa Kristo Mfufuka. Sote tunaalikwa kutoa huduma hizo kama ndugu bila kutafuta sifa au masilahi binafsi.

Tofauti na mtindo wa kidunia au mantiki ya ulimwenguni ambapo nafasi ni kwa ajili ya sifa na masilahi binafsi. Leo mmoja anapokuuliza unafanya kazi gani ni sawa na kusema unapata kiasi gani na labda elimu yako na nafasi yako ni ipi kati ya macho ya ulimwengu huu. Bali sisi tunaalikwa kuongozwa sio na mantiki ya dunia hii. Sisi tunaalikwa sote bila kujali tofauti za huduma kutumikia wengine na si kutafuta nafasi za sifa au masilahi binafsi. Kila mmoja bila kujali anaalikwa kutumikia kwa upendo katika kuujenga Mwili Fumbo wa Kristo. Kila mmoja kadiri ya wito alioitiwa katika Kanisa hatuna budi kufanya yote kwa sifa na utukufu wa Mungu. Sehemu ya pili ya Injili ya leo ni ombi la Mtume Filipo kwa Yesu. Yohane 14:8-12 ‘’Bwana, tuoneshe Baba, nasi tutatosheka’’.  Filipo ni mtume pekee wa Yesu mwenye jina lenye asili ya Kigiriki likiwa na maana mpenda farasi. Ndiye huyu aliyetokea kijiji kimoja na Mtume Petro.  Na baada ya kukutana na Yesu mara moja anakwenda na kumwalika Nathanieli wa Kana. Si tu ana jina la kigiriki lakini inaonekana ndiye mtume pekee aliyezungumza pia lugha ya Kigiriki kwani Wagiriki walifika kwake na kumuomba awaoneshe Kristo. Yohane 12:21.  Yesu pia anaonekana akiwa na majadiliano na Filipo wakati wa kulisha watu mikate. Yohane 6:5,7 Pale Yesu anapoomuliza ni wapi wanaweza kununua mikate ili watu wale naye anamjibu kuwa pesa walizo nazo ni kidogo kwa kununua mikate ya kulisha umati mkubwa ule.

Mjadala wa leo na Yesu haukuwa tena rahisi kama ule wa muujiza wa mikate kwani Yesu anasikitishwa pamoja na kukaa na Filipo muda wote huo karibu miaka mitatu bado alikuwa mbali kumtambua Yesu kama Mungu na Bwana. Filipo bado hajafaulu kumtambua Yesu kwani aliishia kwa kumwangalia tu juu juu na kwa nje, hakufungua macho ya imani na kukutana na Bwana wake. Ni kishawishi hata kati yetu leo, kukosa kufungua macho ya imani ili tuweze kukutana na Mungu. Kushindwa kuuona utukufu wa Mungu katika maisha yetu kwani tunaishia kuangalia kwa macho ya nyama na akili zetu za kibinadamu, na hivyo kushindwa kuuona utukufu na ukuu wa Mungu. Ombi la Filipo ni sawa na kusema utuoneshe utukufu wako nasi tutatosheka kama vile Musa alivyoomba kuuona uso wa Mungu. Kutoka 33:18,20 Na hapo Mungu anamjibu Musa kuwa hakuna anayeweza kuuona uso wa Mungu na kubaki anaishi. Lakini tunaona kiu na tamaa hiyo ya mwanadamu ya kutaka kumuona Mungu inabaki si tu katika Agano la Kale bali hata katika nyakati zetu leo.

Mzaburi anasali kuonesha kuwa hamu na shauku yake ni kuuona uso wa Mungu, Zaburi 27:8-9 na hata anaonesha tena moyo wake una kiu, kiu ya Mungu aliye hai, Zaburi 42:3 ‘’Nitafika lini kwake na kuuona uso wake?’’ Kiu na tamaa ya Filipo ni kiu na tamaa yangu pia leo. Tunaona Yesu anamjibu Filipo na pia mimi na wewe kuwa ili kumuona Mungu hatuna budi kumuona Yeye. Aliyemuona Yesu hakika huyo amemuona Baba. Yesu ni sura halisi ya Mungu Baba asiyeonekana kwa macho yetu ya nyama. Kumwangalia Yesu ni kuwa na mahusiano naye ya ndani kabisa, ni kuwa rafiki yake, ni kukubali kuunganika na hata kutembea katika njia ile aliyotembea Yeye. ‘’Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana’’ Wakolosai 1:15. ‘’Yeye ni mng’ao wa utukufu wa Mungu, na mfano kamili wa hali ya Mungu mwenyewe…’’ Waebrania 1:3. Hivyo Yesu anatuonesha njia na jinsi ya kumuona Mungu Baba, ya kuuona utukufu wake ni kwa kumwangalia Yesu, sio kwa macho ya nyama bali kwa macho ya imani. Sio kwa akili zetu na falsafa bali kukubali kuongozwa na Neno lake na Masakramenti yake na huku tukiongozwa na Sakramenti ile ya Kwanza yaani Jumuiya ya Kanisa. Tumwangalia Yes una tujifunze kutoka kwake, kile alichofanya, alichofundisha, kwani kazi zake ni kazi za Baba yake na yetu. Yohana 14:10

Ni saa ya Yesu pale Msalabani pia Mungu Baba anajifunia na kuudhihirisha utukufu wake kwetu. Ni pale anaufunua upendo wake kwetu, ni katika saa ile ya upendo pia anaufunua kwetu utukufu na ukuu wake. Waebrania 1:3 na 2Wakorintho 4:6 Ni kwa kumwangalia Yesu kwa jicho la imani hapo tunamuona Mungu Baba. Ni jicho lisiloishia kwa yale tunayoyaona tu kwa kuonekana bali kwa kwa kuonja upendo wake kwetu. Ni mwaliko nasi leo katika Dominika hii kila mara kusaka wasaa wa kumwangalia Yesu kwa jicho la imani hasa tunapokuwa mbele ya Yesu wa Ekaristi ili hapo tuweze kuuona utukufu wa Mungu kwetu na ndio upendo wake kwetu ambao ananialika mimi na weye pia kutoa maisha yetu kwa ajili ya wengine. Nawatakia tafakari na Dominika njema.

 

07 May 2020, 14:24