Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Siku ya 57 ya Kuombea Miito: Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa! Seminari Kuu ya Nazareti 2020 Pamoja na Mfuko wa Maafa wa Papa Francisko. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Siku ya 57 ya Kuombea Miito: Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa! Seminari Kuu ya Nazareti 2020 Pamoja na Mfuko wa Maafa wa Papa Francisko. 

Maaskofu Katoliki Tanzania: Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaadhimisha Jumapili ya Mchungaji Mwema 2020 Sanjari na Siku ya 57 ya Kuombea Miito Duniani kwa kukazia ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya; Maandalizi ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa, huko Tabora, Uzinduzi wa Seminari kuu ya Nazareti pamoja na umuhimu wa kuchangia Mfuko wa Dharura wa Papa.

Na Askofu Mkuu Damian Denis Dallu, - Dar Es Salaam.

Ndugu zangu wapendwa, Baba Mtakatifu Francisko, katika Siku ya 57 ya Sala kwa ajili ya Kuombea Miito duniani, anatualika katika tafakari yetu tuongozwe na mawazo makuu yenye maneno haya: maumivu, shukrani, hamasa na sifa. Anasema maneno haya yawe dira ya kuwashukuru na kuwatia moyo wale wote ambao wamejikita katika uinjilishaji wa aina mbalimbali. Baba Mtakatifu anaelekeza maneno haya kwa Taifa zima la Mungu ili kulinganisha mporomoko wa uenezaji wa Injili unaohitaji uzoefu mkubwa wa Yesu na Mtume Petro usiku ule wa dhoruba kali katika Bahari ya Galilaya (Mt. 14: 22-33). Bwana wetu Yesu Kristo aliongeza mikate na kuwalisha watu wote waliokuwepo kwenye mkutano. Jambo hili liliwashangaza wengi.

Baada ya tendo hili, Yesu aliwaagiza Mitume wake waingie kwenye mashua na watangulie ng’ambo ya pili. Safari ya wafuasi wake kuelekea ng’ambo ya pili ambayo inalinganishwa na safari ya Wakristo kuelekea mbinguni na safari ya wale wanaoitwa kuelekea miito mbalimbali. Anasema watu hao wanaosafiri katika mashua mbalimbali, maisha yao husonga mbele taratibu huku wasafiri wakiwa na wasiwasi kama kweli bandarini watafika salama. Wasafiri hao wapo tayari kupambana na dhoruba mbalimbali za baharini na pamoja na hayo, wanaamini kuwa kiongozi wao atawahifadhi wafike salama. Baba Mtakatifu anaongeza kuwa wale wote wanaoitwa kumfuata Mwalimu wa Nazareti, wanatakiwa kubadilika na kuacha kabisa aina za usalama binafsi, ili waweze kurudi na kuwa wafuasi wa Bwana. Maana katika safari hiyo wanakutana: usiku wa giza nene, upepo mkali unaovuma, dhoruba kali na mambo mengine mazito.

Wapendwa, tukumbuke kuwa wito unakuwa shukrani kwa sababu wito wetu ni mwitikio wa sauti kutoka juu. Katika mwito huu Bwana anatuelekeza kuwa mwisho wa safari yetu ni upande wa pili wa bahari, na anatupa ujasiri wa kupanda mashua (boti). Kwa kitendo cha kutuita, Yeye mwenyewe anakuwa ndiye Kiongozi wetu; anatusindikiza na kutuongoza; anazuia tusikwame kutokana na changamoto ndogo ndogo wakati tunajaribu kufanya maamuzi stahiki. Baba Mtakatifu anaendelea kukutueleza kuwa mwito wetu ni zaidi ya chaguo letu binafsi, na fadhila ya kupokea mwito wa Bwana ambao pengine hatukustahili. Tukifanikiwa kutambua na kukumbatia huu wito wetu ikiwa tutafungua mioyo yetu kwa shukrani na kupokea kwa dhati maelezo ya Mungu katika maisha yetu.

Baba Mtakatifu anatukumbusha kuwa licha ya changamoto nyingi katika maisha yetu, Kristo anakuja akitembea juu ya bahari iliyojaa dhoruba akituwashia mwanga wa kututia moyo katika changamoto zetu za maisha ya upadri, utawa, ndoa na wakfu. Yeye anatushika mkono ili atuokoe kama alivyofanya kwa Mtume Petro, na tena yeye anatuambia: “Jipeni moyo, ni mimi, msiogope: (Mt. 14:27). Hapa Kristo anatupatia hamasa ya kusonga mbele. Kwa imani yetu tunafahamu kwamba Bwana yupo pamoja nasi hata kama bahari itachafuka kwa mawimbi makali. Katika utume wetu tutakutana na maumivu ambayo yanaendana na majukumu ya wito. Hata hivyo imani itatuwezesha kutembea kuelekea kwa Bwana Mfufuka na tutashinda kila aina ya dhoruba. Ikitokea uchovu ama hofu ikatusababishia tuanze kuzama, basi Yesu atatunyooshea mkono wake. Anatupatia ari/hamasa tunayohitaji kuuishi wito wetu kwa furaha na utulivu mkubwa.Tunapouacha wito tuliojaliwa, ule upepo mbaya unaweza kutuharibu kabisa.

Baba Mtakatifu anasema anawafikiria wale wenye majukumu muhimu katika asasi za kijamii na wenza wa ndoa. Baba Mtakatifu anaongeza kuwa siyo bila sababu kuwataja hao kuwa mashujaa maana kwa njia ya pekee, wale walioitika katika maisha ya kitawa ama Daraja la upadri. Baba Mtakatifu anatambua pia ugumu wa kazi yao na kujitenga kwao na jamii ambako wakati mwingine kunaongeza mzigo mioyoni mwao, pia hofu ya kuangukia kwenye dimbwi la taka na taratibu kusababisha kuzimika kwa ari za kuuishi utume, kujisikia amebeba mzigo mzito wa kutokuwa na uhakika na usalama wake. Hata pengine kuwa na wasiwasi wa usalama na kujutia maisha yake ya baadaye. Baba Mtakatifu anawahamasisha akisema wajipe moyo, wasiogope! Yesu yuko upande wao, wamkubali kuwa yeye ni Bwana pekee wa maisha yao, Yeye ataunyoosha mkono, atawashika na kuwaokoa.

Hata katika bahari iliyozongwa na mawimbi makubwa, hapo maisha yao yako wazi kwa ajili ya kumpa Bwana sifa. Mfano mzuri unaoeleza wazo hili ni Mama Bikira Maria, Yeye licha ya kuwa na wimbi la hofu na misukosuko mingi, alikuwa bado na ujasiri mkuu na alikumbatia wito wake, ambao unafanya maisha yake kuwa wimbo usiokoma wa kumsifu Bwana. Baba Mtakatifu analialika Kanisa siku ya leo kuombea miito na kugusa mioyo ya waamini ili kila mmoja aweze kutambua na kutoa shukrani kwa wito ambao Mungu amemjalia katika maisha yake. Watu wapate ujasiri wa kumwambia Mungu “ndiyo” na kushinda udhaifu wote kupitia imani kwa Kristo na kugeuza maisha yao kuwa nyimbo za kutoa sifa kwa Mungu, sifa kwa ndugu zao  na kwa ajili ya ulimwengu wote. Mwisho anamwomba Mama Bikira Maria atuongoze na awe mtetezi wetu mkuu.

KONGAMANO LA EKARISTI TAKATIFU KITAIFA: Ekaristi Takatifu, Chemchemi ya Uzima wetu: Wapendwa katika Kristo, mwaka huu tunatarajia kuadhimisha Kongamano la Nne la Kitaifa la Ekaristi Takatifu katika Jimbo Kuu la Tabora. Katika Kongamano hilo tunaenda kukutana na Kristo anayetuambia: “Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu kwa ajili ya uzima wa ulimwengu” (Yn 6: 51). Tunawaalika kujitayarisha kwenda huko. Tujiandae kiroho na kimwili twende katika maadhimisho hayo ili tukutane na chemchemi ya uzima wetu, Mwalimu wetu, Kristo, aendelee kutufundisha kuishi upendo, unyenyekevu, maisha ya sala na umoja miongoni mwetu. Pia tunaenda kuabudu Ekaristi Takatifu, kuishi Maisha ya Kiekaristi miongoni mwetu, kutoa ushuhuda juu ya Sakramenti ya Ekaristi na kuishi duniani hapa kwa ajili ya utukufu wa Mungu na wokovu wa nyoyo zetu. Kwa ufupi, twende tukaishi Kauli-Mbiu ya Kongamano hilo inayosema: Ekaristi Takatifu, chemchemi ya uzima wetu. Ili kufanikisha Kongamano letu kitaifa, tunaalikwa kutoa ukarimu wetu mapema kutoka majimbo yote kama tulivyoombwa.

KUANZISHWA KWA SEMINARI KUU YA NAZARETI JIMBONI KAHAMA: Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania mwaka huu, mwezi Oktoba 2020, linategemea kuanzisha (kufungua) Seminari Kuu itakayoitwa Seminari Kuu ya Nazareti katika Jimbo Katoliki la Kahama. Seminari hii itakuwa na taaluma mbili: Falsafa na Taalimungu. Baraza la Maaskofu limeamua kuanzisha seminari hii kutokana na ongezeko la miito nchini kwetu. Seminari tano tulizo nazo haziwezi kupokea zaidi waseminari, maana tayari zimejaa na idadi ya wanafunzi tulio nao katika nyumba za malezi katika majimbo yetu inazidi nafasi tulizo nazo katika seminari zetu kuu.  Kama suluhu ya changamoto hii, ambayo ni Baraka, Maaskofu wameona ni vema waanzishe seminari hii mpya.

Wapendwa katika Kristo, ongezeko la miito katika nchi yetu ni Baraka za Mwenyezi Mungu kwa Kanisa letu la Tanzania na Kanisa la dunia nzima. Tunawaomba tuunganike kumshukuru Mungu kwa Baraka hizo. Nchi za Mabara ya Ulaya, Amerika na Makanisa ya nchi nyingine hayana miito kama hiyo.  Baadhi ya nchi zimelazimika kufunga seminari hizo kutokana na uhaba wa miito. Wapendwa, tuwaunge mkono Maaskofu wetu kwa sala, na kwa hali na mali katika kuchangia ujenzi wa seminari hii mpya tunayotarajia kuianzisha Oktoba 2020. Seminari hiyo ikiishaanzishwa itakuwa ni tegemeo la kulea miito ya upadri ya Kanisa la Tanzania na hata nje ya nchi yetu, kwani ndiyo tabia ya kimisionari ya Kanisa letu Katoliki.  Tunawaomba kuitikia mwaliko wa Mababa Askofu wetu kwa Parokia zote katika Kanisa la Tanzania kutoa ukarimu wetu wa Sala, Sadaka na Matoleo yetu kama ilivyopangwa, Dominika ya Pili ya Pasaka, ya Huruma ya Mungu, tarehe 19 Aprili 2020, kwa lengo la kuanza rasmi muhula wa kwanza wa masomo 2020/2021 katika Seminari hiyo mpya.

MFUKO WA MAAFA WA BABA MTAKATIFU FRANCISKO DHIDI YA   UGONJWA UNAOSABABISHWA NA VIRUSI VYA CORONA (COVID - 19). Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha “Mfuko wa Maafa” kwa ajili kusaidia nchi za Kimisionari (Majimbo, Mashirika ya Watawa na Taasisi za dini) ili kuweza kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Lengo la Baba Mtakatifu ni kwamba, kwa kupitia mfuko huo atoe mkono wake wa huruma na upendo kwa wale walioathirika na kuteswa na ugonjwa unaoletwa na virusi hivyo. Wapendwa, jukumu la kukusanya ukarimu utakaowekwa kwenye mfuko huo limekabidhiwa kwa Ofisi ya Mashirika ya kipapa. Ili kuweza kutekeleza jukumu hilo Rais wa Mashirika ya Kipapa ya Kimisionari ulimwenguni, Mhashamu Askofu Mkuu Giampietro Dal Toso, ametuandikia barua ya mwaliko ili kutuomba tuchangie mfuko huo kwa Sala, Hali na Mali. Wapendwa waamini, sote tunaona na kuguswa na madhara ya ugonjwa huu hatari, hivyo tunaleta ombi kwenu tutoe ukarimu wetu kuunga mkono jitihada za Baba Mtakatifu, ili kupitia yeye Kanisa lote la Mungu liweze kutoa mkono wa heri kwa wahanga wa ugonjwa huu.

Tunaombwa kama tunataka kutuma ukarimu wowote kwenye Mfuko huu wa Dharura, tunaweza tukatuma kwenye Akaunti iliyofuguliwa rasmi kwa lengo hili la Baba Mtakatifu la kukabiliana na janga la Ugonjwa huu hata hatari unaosababishwa na Virusi vya CORONA (Covid-19). Weka lengo la Ukarimu wako kuwa ni MSHIKAMANO KUKABILI MAAFA YA VIRUSI VYA CORONA. “Kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha; nalikuwa uchi, mkanivisha; nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia … Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi” (Mt 25: 35 - 40). Tunatanguliza shukrani kwenu nyote mtakaochangia Mfuko huu. Tunawaalika tuendelee kumwomba Mungu atuondolee ugonjwa huu hatari unaoleta hofu, mahangaiko na kututenga kimahusiano kati ya mtu na mtu, kusimamisha kabisa matendo yote yanayoendana na Ibada ya kumwabudu Mungu katika Kanisa, pia kuwanyima hadhi ya kimazishi wale wanaofikiriwa kufariki kwa ugonjwa huu.

Mkombozi commercial BankJina la Akaunti wa Mfuko huu ni: PMS-Corona Virus Pandemic Fund

Namba ya Akaunti ni: 00111501981801

SHUKRANI KWA UKARIMU WENU: Kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kwa niaba ya Tume na kwa niaba yangu mimi mwenyewe, tunatoa shukrani kwa wote waliotegemeza Miito Mitakatifu kwa kutoa Ukarimu wenu Mwaka 2019. Kama mnavyoona kwenye Majedwali yetu kwa Upendo na Mshikamano wetu tumesimama hapo tulipo. Hivyo tunawashukuru sana wote mnaounga mkono juhudi za Baba Mtakatifu na Mashirika yake katika Uinjilishaji. Tunatoa shukrani za dhati kwa Majimbo, Mashirika ya watawa wa Kike na wa Kiume, na wenye Maisha ya wakfu, Parokia, Taasisi za Elimu ya juu, Seminari Kuu na Ndogo na Marafiki wa Baba Mtakatifu (Mashirika ya Kipapa) kwa kutoa ukarimu wenu kwenye Mfuko wa Mshikamano (Solidarity Fund). Tunaomba Mungu awajalie Baraka mnazohitaji katika maisha yenu na ajaze pale mlipotoa. “Apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu” (2 Kor. 9:6). Kushukuru ni kuomba tena: Hivyo tunawaalika tena Majimbo, Mashirika ya Watawa wa Kike na wa Kiume, na wenye Maisha ya wakfu, Parokia, Taasisi za Elimu ya juu, Seminari Kuu na Ndogo na Marafiki wa Baba Mtakatifu na Mashirika yake, kutoa kwa moyo wa furaha katika Dominika ya Miito ya Mwaka huu 2020, ili kusaidia kulea Miito Mitakatifu.

Askofu Mkuu Damian Denis Dallu,

Mwenyekiti Tume ya Kimisionari

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Askofu Mkuu Dallu
02 May 2020, 13:30