Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawaalika waamini kuanza tena kushiriki kwa ari na moyo mkuu; kwa ibada na uchaji maadhimisho ya Misa Takatifu kuanzia tarehe 18 Mei 2020. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawaalika waamini kuanza tena kushiriki kwa ari na moyo mkuu; kwa ibada na uchaji maadhimisho ya Misa Takatifu kuanzia tarehe 18 Mei 2020. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia: Maadhimisho ya Misa Takatifu

Maaskofu Katoliki kutoka Italia wanasema, maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu yaanze kwa nguvu, ari na kasi mpya; kwa kujikita katika fadhila ya amani ya ndani, utulivu, hekima na busara; kwa kuendelea kuwajibika ili kukuza na kudumisha upendo! Kwa hakika, maisha na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa yamebadilika sana kutokana na changamoto ya janga la Virusi vya Corona.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanakumbusha kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Upendo; zawadi na sadaka ya Kristo Yesu Msalabani; kielelezo cha huduma inayonafsishwa na kuwasha mapendo kwa Mungu na jirani. Ni Sakramenti ya Altare, mahali pa kukutana mubashara na Kristo Yesu katika maumbo ya Mkate na Divai, Mwili na Damu yake Azizi. Ekaristi Takatifu ni Fumbo na muhtasari wa imani ya Kanisa; ni chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Hii ni zawadi ya upendo inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, na kwa namna ya pekee kabisa linamwonesha Yesu kuwa kweli ni mwanakondoo wa Mungu na sadaka inayotolewa kwa ajili ya maondoleo ya dhambi na maisha ya uzima wa milele! Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha Kristo anayejitoa mwenyewe kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa pamoja na utendaji wake. Hii ni Sakramenti ya umoja wa Kanisa, inayoimarisha na kudumisha upatanisho kati ya Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Wosia wake wa Kitume “Sacramentum Caritatis” yaani “Sakramenti ya Upendo” anakaza kusema, Ekaristi Takatifu ni Fumbo linalopaswa: Kusaidikiwa, Kuadhimishwa kwa Ibada, Uchaji wa Mungu na Uaminifu, ili kuonja: uzuri, ukuu na utakatifu wa Sakramenti hii ya ajabu inayoonesha Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu. Hili ni Fumbo linalopaswa Kunafsishwa katika maisha ya Kikristo kwa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa! Katika kumbu kumbu ya Miaka 100 tangu kuzaliwa kwa Mtakatifu Yohane Paulo II, huko Wadowice nchini Poland tarehe 18 Mei 1920 na kupewa jina la Karol Josef Wojtyla, familia ya Mungu nchini Italia inaanza tena kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu hadharani kwa ushiriki mkamilifu wa waamini. Makubaliano haya yamefikiwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya Serikali ya Italia na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI.

Maaskofu Katoliki kutoka Italia wanasema, maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu yaanze kwa nguvu, ari na kasi mpya; kwa kujikita katika fadhila ya amani ya ndani, utulivu, hekima na busara; kwa kuendelea kuwajibika ili kukuza na kudumisha upendo! Kwa hakika, maisha na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa yamebadilika sana kutokana na changamoto ya janga la Virusi vya Corona, COVID-19. Kumbe, kuna haja ya kuwa ni muda wa majaribio, upembuzi yakinifu na marekebisho msingi ili maadhimisho haya yasiwe ni sababu ya kuzuka tena kwa kasi kubwa maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Maadhimisho ya Komunio ya Kwanza na Sakramenti ya Kipaimara yamehailishwa hadi wakati mwingine, ili kuangalia mwenendo wa ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kipindi hiki ni muhimu sana kwa familia ya Mungu nchini Italia kufanya tathmini ya kina ili kuangalia madhara yaliyosababishwa na gonjwa hili la Corona, COVID-19, ili hatimaye, kufanya mang’amuzi ya kina kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu kwa sasa na kwa siku za mbeleni.

Maisha, utume na mtindo wa Kanisa kwa sasa umebadilika. Kumbe, kuna haja ya kuibua na kuimarisha sera na mbinu mkakati wa kunafsisha Injili ya huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu. Kanisa linapaswa kusoma alama za nyakati kwa kujikita katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni muda wa kutekeleza kwa vitendo Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayokazia: utu, heshima na haki msingi za binadamu! Masuala ya kitamaduni na kijamii yanapaswa kuangaliwa na kupimwa mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa!

Maaskofu CEI
16 May 2020, 13:15