Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limefikia muafaka na Serikali ya Italia na sasa Ibada ya Misa Takatifu yenye ushiriki wa waamini itarejea tena tarehe 18 Mei 2020. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limefikia muafaka na Serikali ya Italia na sasa Ibada ya Misa Takatifu yenye ushiriki wa waamini itarejea tena tarehe 18 Mei 2020. 

Kanisa Katoliki Italia: Ibada ya Misa Kuanza tena kuadhimishwa 18 Mei 2020

Kanisa Katoliki nchini Italia litaanza kuadhimisha tena Ibada ya Misa Takatifu hadharani, kwa ushiriki mkamilifu wa waamini kuanzia tarehe 18 Mei 2020. Makubaliano haya yamefikiwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya Serikali ya Italia na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Ili kudhibiti maambukizi ya Corona, shughuli na ibada mbali mbali zilisitishwa nchini Italia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI na Serikali ya Italia tarehe 7 Mei 2020 yanabainisha kwamba, Kanisa Katoliki nchini Italia litaanza kuadhimisha tena Ibada ya Misa Takatifu hadharani, kwa ushiriki mkamilifu wa waamini kuanzia tarehe 18 Mei 2020. Makubaliano haya yamefikiwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya Serikali ya Italia na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI. Itakumbukwa kwamba, Serikali ya Italia kama sehemu ya mbinu mkakati wa kudhibiti maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 iliamua kwamba, raia wake wote wabaki majumbani mwao pamoja na kusitisha shughuli za hadhara zikiwemo Ibada mbali mbali. Tangu tarehe 4 Mei 2020, Serikali ya Italia imeanza kutekeleza awamu ya pili ya Protokali inayodhibiti maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuruhusu baadhi ya shughuli za uzalishaji kurejea tena katika hali yake ya kawaida. Serikali ikawa imeruhusu dini kuendesha Ibada za mazishi ambazo zingehudhuriwa na watu wasiozidi 10.

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia likatoa na Tamko Kali dhidi ya Serikali ya Italia kwa kutozingatia umuhimu wa uhuru wa watu kuabudu! Huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa majadiliano kati ya Serikali na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Makubaliano yaliyofikiwa yamegawanyika katika sehemu kuu tano: Mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa wakati waamini wanapohudhuria kwenye nyumba za ibada; umuhimu wa kunyunyizia dawa katika nyumba za ibada pamoja na kuzingatia usafi wa mazingira. Maaskofu mahalia ndio watekelezaji wakuu wa protokali ya makubaliano kati ya Serikali ya Italia na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na mwishoni ni mapendekezo ili kudumisha ulinzi na usalama wa waamini wakati wa mikusanyiko ya Ibada mbali mbali nchini Italia! Waamini wanaohudhuria Ibada wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanazingatia umbali uliotengwa ili kuhakikisha usalama wa kila mwamini dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19.

Mahudhurio ya waamini kwenye nyumba za Ibada yataratibiwa na watu wa kujitolea ili kuhakikisha kwamba, kila mwamini anavaa barokoa ili kujikinga na kuwakinga wengine kwani Corona inazuilika! Idadi ya waamini wanaohudhuria Ibada inapaswa kuratibiwa na viongozi wa Kanisa katika maeneo yao. Pale ambapo kuna idadi kubwa ya waamini, basi idadi ya Ibada iongezwe ili kupunguza msongamano wa watu katika Ibada. Umbali wa mita moja na nusu unapaswa kuzingatiwa na wote. Kwa waamini wanaojisikia kuwa na dalili za homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 wanashauriwa kubaki nyumbani. Kwa waamini wote walioambukizwa Virusi vya Corona, hawapaswi kuhudhuria kwenye nyumba za Ibada kwa kuhakikisha kwamba, wanaziangatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa wakati wa Karantini.

Kila baada ya maadhimisho ya Liturujia na Ibada mbali mbali, usafi wa nguvu unapaswa kufanyika pamoja na kuhakikisha kwamba, nyumba za Ibada zinakuwa na hewa safi. Vyombo vya maji ya baraka vitaendelea kubaki tupu hadi itakapoamriwa vinginevyo! Wakati wa maadhimisho ya Ibada mbali mbali, kwaya kwa wakati huu zimepigwa rufuku. Hakuna kupeana amani kwa kushikana mikono. Wakati wa kukomunisha, wahudumu wa Ekaristi Takatifu watapaswa kuvaa vifaa vya kuzuia maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 pamoja na kuzingatia umbali unaotakiwa. Sadaka itatolewa na waamini kwenye vyombo maalum vitakavyokuwa vimetengwa kwenye nyumba za Ibada.

Sakramenti ya Upatanisho itolewe kwenye maeneo ya wazi kwa kuzingatia pia umbali unaotakiwa, daima waungamishaji na waamini wanaokimbilia kiti cha toba na huruma ya Mungu wanapaswa kuvaa barakoa. Maaskofu mahalia ndio waliopewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, makubaliano ya protokali hii yanatekelezwa kwa uaminifu kabisa. Nje ya Kanisa kuwepo na matangazo yanayoonesha idadi ya waamini wanaopaswa kushiriki. Waamini wenye dalili za ugonjwa wa Virusi vya COVID-19 wasiruhusiwe kushiriki kwenye Ibada. Maaskofu wanaweza kuamua mahali pengine panapofaa kwa ajili ya Ibada, lakini sheria, kanuni na taratibu za kudhibiri maambukizi ya Virusi vya Corona-COVID-19, hazina budi kuzingatiwa! Makubaliano haya yametiwa sahihi na Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, Giuseppe Conte, Waziri Mkuu wa Italia pamoja na Luciana Lamorgese, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Utekelezaji wa makubaliano haya ni hapo tarehe 18 Mei 2020, kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 100 tangu alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II.

Maaskofu Katoliki Italia

 

08 May 2020, 14:19