Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawataka watu wa Mungu nchini humo kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu unakuwa huru, wa haki na amani, kielelezo cha ukomavu wa demokrasia ya kweli. Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawataka watu wa Mungu nchini humo kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu unakuwa huru, wa haki na amani, kielelezo cha ukomavu wa demokrasia ya kweli.  (AFP or licensors)

Maaskofu Katoliki Burundi: Tamko Kuhusu Uchaguzi Mkuu 2020

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawataka wananchi kutumia vyema haki yao ya kupiga kura ili kurejesha tena misingi ya haki, amani na maridhiano ya kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawataka viongozi wa serikali, vyama vya kisisasa pamoja na wapambe wao kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya amani na utulivu; upendo na mshikamano wa kitaifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawataka watu wa Mungu nchini Burundi kuhakikisha kwamba uchaguzi mkuu unakuwa wa amani, huru na haki kama kielelezo cha ukomavu wa kisiasa nchini Burundi. Huu si muda wa kuendekeza kinzani za kikabila kwani madhara yake ni makubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Burundi. Bado watu wa Mungu nchini Burundi wanakumbuka athari za vurugu na mipasuko ya kisiasa iliyojitokeza kwenye uchaguzi mkuu wa Mwaka 2015, ulioitumbukiza Burundi katika ombwe na machafuko ya kisiasa. Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawataka wananchi kutumia vyema haki yao ya kupiga kura ili kurejesha tena misingi ya haki, amani na maridhiano ya kitaifa. Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi linawataka viongozi wa serikali, vyama vya kisisasa pamoja na wapambe wao kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha misingi ya amani na utulivu; upendo na mshikamano wa kitaifa.

Maaskofu wanapongeza kwamba, hadi wakati huu, kampeni za uchaguzi mkuu zimefanyika kwa amani na utulivu, jambo ambalo linapaswa kuendelezwa: wakati wa uchaguzi, wakati wa kutangaza matokeo na baada ya kutangazwa kwa matokeo. Maaskofu wanasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitumia lugha chafu katika kampeni zao na kutishia kususia matokeo ya uchaguzi mkuu. Maaskofu wanawataka watu wa Mungu nchini Burundi, kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maaskofu wanawataka viongozi wa Serikali na vyama vya kisiasa kuhakikisha kwamba, wanafuata sheria, kanuni na taratibu zote za uchaguzi mkuu, ili Burundi iweze kuwapata viongozi watakaosongesha mbele gurudumu la maendeleo fungamani ya binadamu. Kwa waandishi wa habari wawe makini katika taarifa zao na kamwe wasiwe na mawakala wa: chuki, vurugu na uhasama wakati na baada ya uchaguzi mkuu.

Wanasiasa wanaowania nafasi mbali mbali za uongozi wawe tayari kukubaliana na matokeo na kama kuna watu watakaopinga basi watumie taratibu zilizopo ili kudai haki yao. Uchaguzi mkuu wa Mwaka 2020 uwe ni chemchemi ya matumaini kwa watu wa Mungu nchini Burundi. Itakumbukwa kwamba, Kampeni za uchaguzi Mkuu nchini Burundi zilianza hapo tarehe 27 Aprili 2020. Uchaguzi unatarajiwa kufanyika tarehe 20 Mei 2020. Kampeni ziliazna na kutimua vumbi licha ya tishio la ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni uchaguzi wa: Rais, Wabunge na Madiwani. Kwa upande wa uchaguzi wa urais, wagombea saba wamejitokeza kuwania nafasi ya Urais: Hawa ni pamoja na Jenerali Evariste Ndayishimiye, ambaye amechukuwa mikoba ya Rais Pierre Nkurunziza, anayemaliza muda wake wa uongozi na ndiye atakayepeperusha bendera ya chama tawala cha CNDD-FDD. Atapambana na Bwana Agathon Rwasa ambaye anaonekana kuwa kati ya wapinzani wenye nguvu zaidi huku akipeperusha bendera ya chama cha CNL ambacho kilisajiliwa mwaka mmoja uliyopita kama Chama cha Siasa.

Uchaguzi Mkuu Burundi 2020

 

16 May 2020, 14:58