Tafuta

Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, tarehe 24 Mei 2020 amerejesha tena Ibada ya Misa Takatifu iliyokuwa imesitishwa kuanzia tarehe 19 Aprili 2020. Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, tarehe 24 Mei 2020 amerejesha tena Ibada ya Misa Takatifu iliyokuwa imesitishwa kuanzia tarehe 19 Aprili 2020. 

Askofu Niwemugizi: Arejesha Ibada ya Misa Takatifu Rulenge-Ngara

Kuanzia tarehe 24 Mei 2020, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, ameruhusu kuanza tena kwa Ibada za Misa Takatifu, kwa kufuata mwongozo uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Sala za Jumuiya vifuate utaratibu huo. Nia ni kuepusha waamini wasiambukizane Virusi vya Corona, COVID-19 Kanisani, kwani kinga ni bora zaidi kuliko tiba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge Ngara, Tanzania, tarehe 19 Aprili 2020 alisitisha maadhimisho yote ya hadhara yanayowaleta waamini wengi pamoja, Kanisani na kwenye Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo kwa muda wa mwezi mzima. Baada ya kutafakari kwa kina na mapana mwenendo mzima wa maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuanzia tarehe 24 Mei 2020, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, ameruhusu kuanza tena kwa Ibada za Misa Takatifu, kwa kufuata mwongozo uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Hii ikiwa ni pamoja na waamini kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka nje ya Kanisa; waamini wavae barakoa na wakae umbali wa mita moja toka mtu hadi mtu Kanisani. Barokoa zivuliwe wakati wa kupokea Ekaristi Takatifu tu! Idadi ya Ibada za Misa iongezwe hasa Parokiani kadiri iwezekanavyo, ili waamini wachache wachache waweze kuingia na kuadhimisha mafumbo ya Kanisa, bila ya kusongamana. Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa na Sala za Jumuiya vifuate utaratibu huo pia.

Nia kuu anasema Askofu Severine Niwemugizi ni kuepusha waamini wasiambukizane Virusi vya Corona, COVID-19 Kanisani, kwani kinga ni bora zaidi kuliko tiba. Ugonjwa wa Corona, COVID bado upo na wale wanaojisikia hali za afya zao kuwa mbaya, wasifike Kanisani au kwenye Sala za Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo. Anawaalika waamini kuendelea kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kusikia kilio cha watanzania na walimwengu katika ujumla wao, ili aweze kuwaepusha na janga hili mapema iwezekanavyo, ili waendelee kuishi maisha ya kawaida na kumtukuza Mwenyezi Mungu kama ilivyo desturi. Askofu Severine Niwemugizi wa Jimbo Katoliki Rulenge Ngara anasema, kumekuwepo na giza kubwa kuhusu taarifa za maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19 nchini Tanzania kwa sababu ya Serikali kutokutoa taarifa za kuaminika kwa muda wa majuma mawili sasa. Kumbe, imekuwa vigumu kwake, kuweza kufanya tathmini, ili kubaini ongezeko au kupungua kwa maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna hofu zaidi kwa sababu watu wanaonekana kutojali, licha ya kuambiwa kuchukua tahadhari. Kwa kutambua umuhimu wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa maisha ya kiroho kwa waamini wake, ameamua kuruhusu tena maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Lawama ibebwe na mamlaka husika za kutoa taarifa kuhusu hali halisi ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19.

Wakati huo huo, Prof. Abel Makubi, Mganga Mkuu wa Serikali nchini Tanzania amewataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari juu ya maambukizi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Hadi sasa ugonjwa huu hauna chanjo na kwamba, dawa iliyotolewa nchini Madagascar hivi karibuni bado inafanyiwa uchunguzi ili Serikali ya Tanzania iweze kujiridhisha zaidi. Wananchi katika ujumla wao na hasa vijana wanapaswa kukumbuka kwamba, Virusi vya Corona, COVID-16 havibagui umri wala mahali anapotoka mtu! Ugonjwa huu ni rahisi sana kusambaa na kuenea kwa watu sehemu mbali mbali, kumbe, kuna haja kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kama inavyoelekezwa na Serikali, Wataalam wa Afya pamoja na Shirika la Afya Duniani. Amewataka viongozi mbali mbali kuweka mikakati itakayowasaidia wananchi kuendelea na shughuli za kiuchumi kwa kuzingatia masharti yaliyowekwa. Amewataka wananchi waepuke mikusanyiko isiyo na ulazima na kama hakuna lazima ya kwenda kwenye mikusanyiko wananchi watulie majumbani mwao.

Askofu Niwemuguzi

 

 

 

25 May 2020, 14:04