Mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19: Watanzania watakiwa kuzingatia ushauri wa madaktari pamoja na kuendelea kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza. Mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19: Watanzania watakiwa kuzingatia ushauri wa madaktari pamoja na kuendelea kumpatia Mwenyezi Mungu kipaumbele cha kwanza. 

COVID-19: Watanzania Jihadharini! Na mtangulizeni Mwenyezi Mungu!

Katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali inayosababishwa na Virusi vya Corona, watanzania wametakiwa kuhakikisha kwamba, wanazingatia ushauri wa madaktari na viongozi wa Serikali sanjari na kumtanguliza Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, ili aweze kuwaepusha na janga hili, awajalie wanasayansi na watafiti ulimwenguni uwezo wa kupata chanjo na tiba!

Na Ofisi ya Waziri ya Waziri Mkuu, - Dodoma.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa amewataka Watanzania waendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19) huku wakimtanguliza Mungu. “Hakuna njia nyingine yoyote isipokuwa kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu. Tuendelee kuchukua tahadhari wakati bado tunaendelea kumtumainia Mungu. Ni heri kumwishia Mungu, na Roho Mtakatifu atatupa njia ya kutoka hapa tulipo,” alisema. Ametoa kauli hiyo Jumapili, Aprili 26, 2020 wakati akizungumza na viongozi wa dini mbalimbali walioshiriki Maombi Maalum ya Kitaifa kwa mkoa wa Dodoma dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona (COVID-19) yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha VETA, Dodoma.

Amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ambaye ana hofu ya Mungu na ndiyo maana aliomba Watanzania kwa imani zao wafanye maombi kwa siku tatu. Alisema Serikali inatambua mchango wa viongozi wa kiroho na akawataka waliombee Taifa kwani mwaka huu 2020 linajiandaa kwa uchaguzi mkuu. “Mwaka huu tunatarajia kufanya uchaguzi mkuu, kwa hiyo tunaomba tumtangulize Rais wetu, tumuombee sana kwa yale anayoyafanya kwa nchi yetu.” Akizungumza wakati wa kufungua maombi hayo, Rais wa Chama cha Maaskofu na Wachungaji (Tanzania Pastors’ Association – TPA), Askofu Samson Mlawi alitoa maombi akimwomba Mungu aifute COVID-19 kwenye mipaka ya Tanzania.

Naye mwakilishi wa Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Sheikh Kisusu Mvumbo alisema dunia huwa inaandika historia kila kunapotokea tukio kubwa akitolea mfano wa Vita Kuu ya Dunia. “Vita ya Kuu ya Kwanza ya Dunia iliandika historia, ikaja Vita Kuu ya Pili ya Dunia nayo ikapita. “Sasa hivi, tishio juu ya mdudu huyu Corona pia inaendelea. Dunia haiendi imesimama, imekwama kiuchumi sababu ya mdudu corona. Tumsihi Mwenyezi Mungu atuepushe na hili janga,” alisema katika maombi yake. Kwa upande wakemwakilishi kutoka madhehebu ya Khoja Shia mkoa wa Dodoma, Ustaadh Haidary Bakari alisema anamwomba Mungu aiponye Tanzania na pia akaombea uchaguzi Mkuu ujao uwe wa heri na amani.

Akimalizia maombi hayo, Mwenyekiti wa Mtandao wa Maombezi wa Wanawake Barani Afrika, Prof, Margareth Kilimali alisema anamshukuru kwa kuwakutanisha viongozi hao wa dini wa mkoa wa Dodoma bila kujali tofauti zao za dini. “Tunamshukuru Mungu kwa kuwa ana uwezo wa kutokomeza janga hili kwa nchi yetu ya Tanzania na bara zima la Afrika. Asante ka fursa ya uchaguzi mkuu kwani umeshapanga ni jinsi gani utaendeshwa kwa amani wakati ukifika,” alisema. Alisema Tanzania haitaaibika na janga la corona kwa sababu imemtumaini Mungu. “Tanzania haitaaibika kwa sababu tumekujua wewe ni Mungu na unaweza kutuponya, Afrika haitaaibika kwa sababu nao wamekukimbilia wewe,” alisema.

Wakati huohuo, Mratibu wa TPA, Askofu Gerald Nzwalla alisema neno kuu la maombi hayo ya kitaifa ni limetoka nyakati wa pili, sura ya saba mstari wa 14 na wa 15 (2Nya.7: 14-15) na waliona ni muhimu maombi hayo yafanyike jijini Dodoma kwa sababu ni makao mkuu ya nchi na ndipo mahali anaishi Rais wa nchi. Maombi hayo maalum yaliandaliwa na TPA kwa kushirikiana na BAKWATA, SHIA, HAMADIA, HINDU, AGA KHAN, KKKT, EAGT, FPCT, MENONITE NA MOROVIAN.

28 April 2020, 09:26