Tafuta

Vatican News
Fumbo la Ufufuko wa Kristo ni mwanzo wa mapambazuko katika maisha ya mwamini, changamoto ya kuandamana daima na Kristo Yesu! Fumbo la Ufufuko wa Kristo ni mwanzo wa mapambazuko katika maisha ya mwamini, changamoto ya kuandamana daima na Kristo Yesu!  (ANSA)

Sherehe ya Pasaka ya Bwana Wetu Yesu Kristo! Kiini cha Imani!

Pasaka ya Mwaka 2020 inatualika turudi na kuitafakari ile Pasaka ya kwanza kabisa pale mjini Yerusalemu ambapo Mitume wanashuhudia Bwana na Mwalimu wao akikamatwa, akiteswa na kusulubiwa na hata kufa Msalabani. Hii ni Pasaka ambayo Mitume wa Yesu hawakuaidhimisha katika Makanisa bali wakiwa wamejifungia na kupata taarifa na kukimbilia pale penye kaburi wazi.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

ALLELUIA! ALLELUIA! ALLELUIA! Mapema asubuhi, siku ile ya kwanza ya juma, ikiwa bado giza na ukimya mkuu tunakutana na Maria Magdalena anakwenda kaburini. Baada ya kifo cha Yesu ile siku ya Ijumaa basi ni kama kila kitu sasa kimefikia ukomo na mwisho wake, ni giza, ni ukimya, ni mashaka na ndio tunaona anajihimu mapema kungali giza akiwa amejaa na uoga anaenda kaburini. Kifo kinaonekana kushinda katika hali na mazingira ya namna hiyo. Utawala wa mabavu, ubaguzi, rushwa, ufisadi, kukosa haki na mengi maovu yanaoneka kushinda katika ulimwengu wetu wa leo. Ni kama ulimwengu ulisimama, hakukuwa na uhai tena baada ya kifo chake Yesu. Ni leo tunapokuwa katika ulimwengu uliosimama kwa amri ya lockdown, hakuna uhai, hakuna maisha kila mmoja anaalikwa kujifungia ndani mwake kwa hofu ya kuambukizwa au kuambukiza COVID-19. Pasaka ya Mwaka huu wa 2020 inatualika turudi na kuitafakari ile Pasaka ya kwanza kabisa pale mjini Yerusalemu ambapo Mitume wanashuhudia Bwana na Mwalimu wao akikamatwa, akiteswa na kusulubiwa na hata kufa kifo cha aibu pale juu Msalabani.

Pasaka ile ambayo kwa hakika wanafunzi wa Yesu hawakuaidhimisha katika Makanisa makubwa, bali wakijawa na woga na mashaka wakiwa wamejifungia na kupata taarifa na kukimbilia pale penye kaburi wazi na bado wanashindwa kuelewa maana yake mambo yale. Ndio Pasaka ya mwaka huu tuliposafiri safari ile ya Kwaresima ya siku arobaini tukiwa na mateso makali ya maambukizi makubwa ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kama Kwaresima ilivyo siku arobaini na leo tunashuhudia viongozi wa ulimwengu huu wakiatualika kuwa katika ‘’karantini’’, ni neno linalotokana na lugha za Kilatini hasa Kiitalia yaani’’Quarentina’’ likimaanisha bado siku arobaini. Ni mwaliko kumbe, kwa ulimwengu mzima kusafiri pamoja na Yesu katika tafakari ya mateso yake kwa siku arobaini, labda bila wengi kujua ni mwaliko wa maisha yote kwani namba 40 ni kuonesha sio tu siku 40 bali muda wote wa maisha yetu, ni mwaliko sio tu kujitenga na kuwa peke yetu bali kubaki pamoja na Mungu ili tupate majibu ya maana ya mateso na maisha yetu. Kwaresima ni mwaliko wa maisha ya kila siku ya kila mfuasi na rafiki yake Yesu Kristo.

Kwa Upande mwingine mara baada ya Maria Magdalena kufika pale kaburini na kukuta kaburi li wazi tunaona kila kitu sasa kinabadilika na kuchukua sura nyingine. Maria Magdalena akimbia kwa kasi na kwenda kwa Simon Petro, na pia kwa yule mwanafunzi mwingine. Nao pia wanatoka na kukimbia kwa pamoja kuelekea kaburini. Uhai unaanza tena! Ni mwanzo mpya kutoka katika kila kitu kusimama sasa kila kitu kwa mbio na kasi ya ajabu. Ni kama vile tunapokuwa katika karantini leo kila mmoja wetu anasubiri kwa hamu kubwa ifike siku ile tutakapotangaziwa kuwa tusalama tena na hivyo maisha kuchukua sura yake ya kawaida, ni kurudi katika maisha ya furaha na matumaini jinsi kila mmoja anavyosubiri kwa hamu. Hata hivyo Maria Magdalena anafikiri kuwa wamemwiba Bwana kaburini, hivyo bado giza nene, bado ana safari ndefu ya kufikia imani kamili. Mwinjili Yohana kwa mshangao hatuoni tena nini kilijiri kwa upande wa mwanamama Maria Magdalena na badala yake sasa anawaleta mbele yetu magwiji wawili, ndio Mitume Petro na yule mwanafunzi mwingine bila jina ila kivumishi kuwa alipendwa na Bwana.

Pamoja na wataalamu wa Maandiko wengi kukubaliana kuwa pengine mwanafunzi aliyependwa na Yesu ndiye Yohana Mtume, lakini bado tunajiuliza kwa nini daima Mwinjili Yohane katika Injili yake hamtambulishi kwa jina? Akiwa na Andrea walimwona Yesu akipita na walimfuata na kukaa naye na ndiyo hapo tunaona pia anamtangulia Simon Petro katika kukutana na Yesu. Yohane 1:35-40 Ni mwanafunzi aliyependwa anatangulia kuwa mfuasi na kuomba kukaa na Bwana. Hatusikii tena habari zake mpaka wakati wa kalamu ya mwisho. Ni hapo Yesu anapowaonya wanafunzi wale kumi na wawili kuwa kati yao mmoja atamsaliti. Ni huyu mwanafunzi aliyependwa na Bwana anafanyiwa ishara na Simon Petro ili amuulize Yesu. Yohane 13:23-26 Mwanafunzi huyu aliyependwa yupo kifuani mwa Yesu, anabaki na mahusiano ya karibu na Bwana na Mwalimu wetu. Wakati wa mateso ya Yesu, Petro alisimama mbali na kwa hofu alimkana Yesu, ila mwanafunzi aliyependwa na Yesu alibaki kumfuasa Yesu kiaminifu, hata kuingia katika nyumba ya Kuhani mkuu na mpaka pale chini ya Msalaba. Yohane 18:15-27 Mwanafunzi aliyependwa na Bwana anabaki mwaminifu hata katika nyakati ngumu na za kutisha na kuogofya.

Yesu akiwa anasulubiwa pake Kalvari, Mtume Petro hakuwepo kwa hofu ila mwanafunzi yule aliyependwa alisimama chini ya Msalaba pamoja na Mama wa Yesu. Yohane 19:25-27 Habaki tu karibu na Bwana wake bali hata karibu na Mama wa Yesu. Na hata katika Injili ya leo tunaona anakimbia zaidi ya Mtume Petro na anakuwa wa kwanza kufika pale kaburini na haishi hapo tu bali hata katika mbio au safari ya kiimani anakuwa wa kwanza kuona na kuamini. Yohane 20:3-10 Kama alivyokuwa wa kwanza kukuta shauri na kumfuata Yesu na anabaki daima karibu na mwaminifu sio tu kwa siku chache mpaka hata baada ya mateso na kifo na leo ufufuko anakuwa wa kwanza kuona na kuamini. Hata wanapokuwa katika bahari ile ya Tiberia au Galilaya huyu mwanafunzi aliyependwa na Yesu anakuwa wa kwanza kumtambua Kristo Mfufuka. Yohane 21:7. Na hata alipoitwa na Yesu kumfuasa, tunaona Petro anakosa ujasiri wa kumfuata peke yake bali pamoja na huyu mwanafunzi aliyependwa na Yesu. Yohane 21:20-25 Ni mfuasi ambaye daima anaona haja ya kuwasindikiza wengine kwa maisha na sadaka yake ili wengine waweze kumfuata Bwana.

Hivyo tunaweza sasa kujiuliza mwanafunzi aliyependwa anamwakilisha nani kwa hakika? Ni nani huyu mwanafunzi asiye na jina bali kivumishi sifa kuwa alipendwa na Yesu? Kwa kweli ni kila mfuasi wa kweli wa Yesu, yule anayekutana na Yesu anamwamini bila kuwa na safari ndefu yenye mashaka na hofu nyingi, ndiye anajisahau yeye mwenyewe na kuvutwa na ule upendo wa Yesu, anayeitikia kwa upendo wa Yesu kwa kumpenda pia bila masharti na kujitafuta. Hatajwi jina kwani kila mmoja wetu anapaswa kuwa huyu aliyependwa na Yesu. Kuwa tayari kufuata njia ile ya Bwana na Mwalimu wetu bila kujibakiza. Ni mfano na kielelezo cha kila mmoja wetu anayetaka kuwa mwanafunzi na mfuasi wa Yesu Kristo, Mfufuka. Tunaona mitume hawa wawili baada ya kupokea ujumbe kuwa kaburi li wazi kutoka kwa Maria Magdalena wanakimbia kwa kasi kuelekea kaburini. Yule mwanafunzi aliyependwa na Bwana anafika wa kwanza na anainama na kuchungulia na kuona vitambaa ila hakuingia. Na mwisho anafika Petro na hivyo anaingia wa kwanza kaburini na kuona vitambaa na yote ila pasipo kuuona mwili wa Yesu.

Mtakatifu Yohane Krisostomo anasema labda mitume nao walikuwa mwanzoni na mawazo haya yafuatayo: Kama mwili wake umechukuliwa kutoka kaburini basi kwa hakika waliouhamisha hawakupaswa kuuvua mwili sanda na leso, hivyo wangembeba pamoja na sanda na leso alizozikwa nazo, hivyo hawakuwaza kuwa mwili wake umeibiwa kutoka kaburini. Kwa nini kuuvua nguo ikiwa ni rahisi zaidi kuuhamisha ukiwa pamoja na nguo zake. Mtume Petro ambaye mwana tahalilimungu Hans Urs Von Balthasar anamtambulisha kama ‘’ecclesial office’’ na yule mwanafunzi mwingine aliyependwa kama ‘’ecclesial love’’, naomba ninukuu hapa maneno yake bila kuyatafsiri: ‘’Both disciples run there together yet not together, for, unburdened by the cares borne by the office, Love runs faster. Yet Love yields to Office when it comes to examining the tomb, and Peter thus becomes the first to view the cloth that had covered Jesus’ head and establish that no theft had occurred. That is enough to permit Love to enter, who sees and believes.’’ (Cfr. Hans Urs Von Balthasar, Light of the Word, p. 71). Tunaona tofauti na Injili ya Luka hapa mitume wanajikuta ni wao tu wenyewe bila ya ufunuo au msaada wa mwanga kutoka mbinguni au uwepo wa malaika wa Bwana. Wanabaki wanakutana na ishara za kawaida tu na mbaya zaidi ishara za umauti ndio sanda na leso na jiwe na kaburi tupu.

Na ndio tunaona Mtume Petro hata baada ya kuingia anabaki amesimama bila kuelewa nini maana yake, kwa maneno mengine alikuwa naye bado katika giza nene. Yule mwanafunzi mwingine ambaye mwanateolojia von Balthasar anamtambulisha kama ‘’ecclesial love’’ baada ya kuingia na kuona anapiga hatua nyingine mbele anaamini. Hata mbele ya ishara zile za kifo, mwanafunzi aliyependwa na Bwana anafaulu kupiga hatua ya kufikia imani. Anaona ushindi dhidi ya umauti. Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko, sentesi hii Mwinjili anaiweka hata baada ya yule mwanafunzi aliyependwa kuwa ameona na kuamini na kwa kweli sio kupinga alichoandika kabla, ila ni kuonesha jinsi gani jumuiya ya rafiki zake Yesu walikuwa bado na safari ya kufikia ukweli wa Pasaka ambao ni kwa Maongozi ya Maandiko Matakatifu tunaweza kuufikia na si nje ya hapo. Ni ukweli wa kiimani hata kama ulitokea katika historia ya mwanadamu. Hivyo mfuasi wa kweli wa Yesu daima anaongozwa na Neno la Mungu, ni kwa njia hiyo pekee nasi tunaweza kufikia imani na sio kama Tomaso aliyetaka ukweli wa ufufuko uwe sawa na ukweli wa kisayansi kwa kuuona kwa macho yake na kuushika kwa mikono yake. Wapendwa ni ujumbe wa Pasaka leo katika nyakati hizi ngumu na hofu kuwa kila mmoja wetu anaalikwa kutoka katika maisha yenye ishara za umauti kwa kuamini katika ufufuko wake Yesu.

Tunaalikwa kuwa watu wa Pasaka, kwani Kristo amefufufuka kweli kweli hayumo tena kaburini, ameyashinda mauti kwa ufufuko wake. Tunaalikwa kuishi kwa matumaini kwani sisi tuna maisha hata baada ya maisha ya hapa duniani, ndio maisha ya umilele pamoja na Kristo Mfufuka, Kifo sio mwisho bali mwanzo mpya wa kwenda kuanza maisha mapya pamoja na Kristo Mfufuka anayetualika nasi kutembea na kuishi naye milele. Hofu na mashaka ni ishara za kifo, ni ishara za mtu wa kale, sisi tunaalikwa kutembea kifua mbele kwani maisha yetu yanapata maana kwake Kristo Mfufuka hata kama tunaugua, hata kama tunateseka, hata kama tunakufa kwani Kristo amefufuka. Wakarudi nyumbani kwao, ni baada ya kukutana na Yesu Kristo Mfufuka kila mmoja wetu anaalikwa kurejea nyumbani kwake na kutoa ushuhuda huo mkubwa. Ni mimi na wewe baada ya kukutana na Yesu Mfufuka katika Neno lake na meza yake ya Ekaristi tunaalikwa kurudi na kushirikisha wengine furaha ya Upendo wa Mungu kwa watu wake.

Ni vile inakuwa ni habari ya kukeleketa, hivi hatuwezi kubaki nayo sisi tu wenyewe bila ya kuwashirikisha wengine. Ni habari inayotuacha na mshangao chanya hivyo hatuna budi kutoka kwa haraka na kushirikisha wengine na hayo ndio maisha ya ushahidi. Kwetu Kristo ni Habari  Njema ya Wokovu, kwani amefufuka kweli kweli, ameyashinda mauti na hayupo tena kaburini. Kama tunavyokuwa na shauku kuwahabarisha wengine habari nzuri katika maisha yetu hatuna budi na leo kujawa na shauku hiyo hiyo na kuwashirikisha wengine kwa kuwa na maisha ya mwanga na nuru, kuwa chumvi na mwanga kwa maisha yetu. Pasaka inatualika kuwa na maisha ya mwanga, maisha ya imani na matumaini na mapendo ya kimungu ndani mwetu. Nawatakia tafakari njema na sherehe njema za Pasaka.

11 April 2020, 16:05