Tafuta

Mheshimiwa Padre Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S, Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Morogoro amefunga Kanisa la Parokia ya Modeko kutokana na kufuru kwa Ekaristi Takatifu. Mheshimiwa Padre Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S, Msimamizi wa Kitume Jimbo Katoliki la Morogoro amefunga Kanisa la Parokia ya Modeko kutokana na kufuru kwa Ekaristi Takatifu. 

Kanisa la Parokia ya Modeko, Morogoro lafungwa kwa kufuru!

Kuanzia tarehe 27 Aprili 2020 Kanisa la Parokia ya Modeko limefungwa na halitaweza kutumika kwa sasa hadi pale, Tabernakulo mpya itakapowekwa wakfu. Ibada hii inatarajiwa kuadhimishwa wakati wa Sherehe ya Ekaristi Takatifu, fursa makini kwa waamini kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa kuhusu Ekaristi Takatifu, yaani uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai.

Na Angela Kibwana, Morogoro Na P. Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mheshimiwa Padre Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Morogoro nchini Tanzania amefunga Kanisa la Parokia ya Bikira Maria Mtakatifu baada ya kuwasiliana na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania. Kuanzia tarehe 27 Aprili 2020 Kanisa la Parokia ya Modeko limefungwa na halitaweza kutumika kwa sasa hadi pale, Tabernakulo mpya itakapowekwa wakfu. Ibada hii inatarajiwa kuadhimishwa wakati wa Sherehe ya Ekaristi Takatifu, fursa makini kwa waamini kutangaza na kushuhudia imani ya Kanisa kuhusu Fumbo la Ekaristi Takatifu, yaani uwamo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai. Mababa wa Kanisa wanathibitisha kwamba, kwa nguvu ya imani ya Kanisa na uwezo wa Neno la Kristo Yesu, na tendo la Roho Mtakatifu, kwamba, mageuzo ya Mkate na Divai yanakuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo.

Padre Nikodemas Masong, Paroko wa Parokia ya Modeko, Jimbo Katoliki la Morogoro amesema, watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi tarehe 27 Aprili 2020 walivamia na kuvunja mlango wa Kanisa la Parokia ya Modeko na kufanikiwa kuiba Tabernakulo iliyokuwa inahifadhi Ekaristi Takatifu na kutokomea mahali kusikojulikana. Walivunja pia milango ya ofisi za Parokia na kufanikiwa kuiba kiasi cha shilingi laki tatu na nusu, mali ya Chama cha Watumishi wa Altare Parokiani hapo. Walifanikiwa pia kuiba “Mixer” inayotumika kwa ajili ya mawasiliano Parokiani hapo! Familia ya watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Morogoro imesikitishwa sana na kufuru hizi dhidi ya mahali na mambo matakatifu yanayogusa undani wa imani ya watu!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu kama inavyojulikana na wengi: “Corpus Domini” au “Corpus Christi” kwa lugha ya Kilatini, kwa mwaka 2019, aliwaalika waamini kujenga na kudumisha utamaduni wa kuhudhuria na kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa takatifu; Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na hatimaye, kushiriki kikamilifu kwa ibada na heshima kuu wakati wa maandamano ya Ekaristi Takatifu, kielelezo makini cha uwepo endelevu wa Kristo katika maisha ya waja wake, Kristo anayeandamana na wafuasi wake, bega kwa bega! Waamini waoneshe moyo wa upendo kwa kushikamana na Kristo katika safari ya maisha yao, kwa kujiandaa kikamilifu, ili kuweza kumpokea! Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini chakula cha uzima wa milele na upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, ili hatimaye, kuweza kushiriki katika maisha, uzima na utukufu wa Baba wa milele! Ekaristi Takatifu inajenga fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa; ni chemchemi ya utakatifu wa maisha ya waamini, kumbe linapaswa lisadikiwe kwa dhati, liadhimishwe kwa ibada na uchaji na limwilishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kila Mwaka Mama Kanisa anayofuraha kubwa ya kusherehekea na kushuhudia Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa kwa maandamano makubwa, ushuhuda kwamba, Kristo Yesu anaendelea kuandamana na waja wake katika historia ya maisha yao ya kila siku hadi utimilifu wa dahali.

Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Umoja, inayowaunganisha waamini kuwa ni mwili mmoja na watu watakatifu wa Mungu. Mwamini anayepokea Ekaristi takatifu anakuwa ni chombo cha umoja, kwani ndani mwake kunaibuka “vinasaba ya maisha ya kiroho” vinavyosaidia kujenga umoja. Mkate wa Umoja unasaidia kuvunjilia mbali tabia ya kujiona kuwa ni bora zaidi kuliko wengine; watu wanaopenda kuwagawa wengine kwa mafao binafsi; watu wenye wivu na umbea unaohatarisha umoja na mshikamano. Waamini kwa njia ya kuliishi kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu: wana mwabudu na kumshukuru Kristo Yesu, kwa zawadi hii kubwa; kumbu kumbu hai ya upendo wake unaowaunganisha wote kuwa ni mwili mmoja na kuwaelekeza katika ujenzi wa umoja.

Kufuru Parokia ya Modeko, Morogoro
29 April 2020, 13:02