Vatican News
Mkesha wa Sherehe ya Pasaka ni Mama wa mikesha yote inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia yake! Mkesha wa Sherehe ya Pasaka ni Mama wa mikesha yote inayoadhimishwa na Mama Kanisa katika Liturujia yake!  

Kesha la Jumamosi Kuu: Fumbo la Ufufuko wa Kristo Yesu!

Ufufuko wa Yesu Kristo tofauti na mateso na kifo chake hatuwezi kuuelezea kama vile ni tukio la kimwili, ni tukio linalopita ufahamu wetu wa kimwili, sio tukio la macho na mikono bali ni tukio la ulimwengu wa kiroho, lazima kuliona kwa macho ya imani na kamwe si macho ya nyama au akili zetu au dadisi za kihistoria na kisayansi. Tunahitaji jicho la imani ili kulielewa Fumbo la Ufufuko!

Na Padre Gaston George Mkude, -Roma.

ALLELUIA! ALLELUIA! ALLELUIA! Wainjili wote wanatupa Simulizi la Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo kwa kutuonesha muda na hasa siku husika, alfajiri siku ya kwanza ya Juma. Na pia wanatutajia wahusika waliokwenda kaburini asubuhi na mapema na ndio Maria Magdalena na wale wanawake wengine.  Katika somo la Injili ya Mkesha wa leo tunasoma kutoka Mwinjili Matayo ambaye anawataka Maria Magdalena na Maria mwingine. Ikiwa Wainjili Marko, Luka na Yohane wanatuonesha kuwa wanawake wale walipofika kaburini walijawa na mshangao, kwa kukuta jiwe limeondolewa kaburini, ila Mwinjili Mathayo leo anatuonesha kuwa walifika na kushuhudia ishara za kutisha za kuondolewa jiwe pale kaburini. Palikuwa na tetemeko la nchi, malaika wa Bwana, aliyeshuka kutoka mbinguni, alifika na kuliondosha jiwe na kukaa juu yake. Umbo lake likaonekana kama umeme na mavazi yake meupe kama theruji. Walinzi wanajawa na hofu hata mwinjili kutuonesha kuwa walionekana kama wamekufa.

Kwa kweli kama tutachukulia hizi taarifa kama kweli za kihistoria tutajikuta na wakati mgumu kulinganisha Injili ya Mathayo na wainjili wengine. Simulizi la ufufko wake Yesu Kristo kutoka kwa Injili ya Mathayo sio masimulizi ya matukio yaliyojiri kihistoria hivyo kuchukuliwa jinsi yalivyo na badala yake lazima kutambua kuwa ni katekesi yenye taalimungu kubwa ndani mwake. Ni lugha ya ishara kutuonesha jinsi Kristo Mfufuka alivyoshinda nguvu zote za kifo na mauti. Ni yale yaliyojiri ila sio katika ulimwengu wa macho bali ulimwengu wa kiroho. Ufufuko wa Yesu tofauti na mateso na kifo chake hatuwezi kuuelezea kama vile ni tukio la kimwili, ni tukio linalopita ufahamu wetu wa kimwili, sio tukio la macho na mikono bali ni tukio la ulimwengu wa kiroho, lazima kuliona kwa macho ya imani na kamwe si macho ya nyama au akili zetu au dadisi za kihistoria na kisayansi. Ni kwa macho ya imani pekee ndio tunaweza kuelewa maana kamili ya ufufuko. Ni kwa kukubali kuongozwa na mantiki ya kimungu na hasa Maandiko Matakatifu pekee tunaweza kufikia ukweli huo na kamwe sio kwa milango ya ufahamu ya kimwili na kibinadamu. Kerygma ya Ufufuko inapita akili zetu zetu zote, sayansi zetu zote, na falsafa zetu zote.

Hivyo tukio la ufufuko wa Yesu kama lilivyoshuhudiwa na wanawake wale na baadaye Mitume sio kweli ya kihistoria inayokuwa rahisi hata nasi leo kuweza kuielezea kwa ufasaha wa maneno na kifalsafa au akili zetu. Mwinjili Mathayo anatumia lugha hiyo katika kuelezea “Kerygma ya ufufuko”, kwani ilieleweka vema na walengwa wa Injili yake. Anatumia lugha ya ishara zinazojulikana katika Agano la Kale na pia wasikilizaji wake wa pale mwanzo. Na ndio nasi leo tunapotafakari ufufuko wake Kristo hatuna budi pia kuangalia kwa makini maana ya lugha ya ishara anazotumia Mwinjili Matayo katika kutufikishia ukweli huu wa kiimani juu ya Ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Tetemeko la nchi katika Agano la Kale linaonesha uwepo wa Mungu, ni ufunuo wa Mungu kila mara anapoonesha nguvu na uweza wake kati ya watu wake. Mlimani Sinai tunaona mlima wote ulitetemeka kuonesha uwepo wa Mungu. Kutoka 19:18-19 Tunaona pia Zaburi 18:7-8 “Hapo dunia ikatetemeka na kutikisika…’’ Ni ishara inayotumika mara nyingi katika Maandiko Matakatifu kuonesha nguvu na uweza wake Mungu, ni ishara ya kuonesha uwepo wa Mungu. Hivyo tetemeko katika kaburi, ndio kusema ni Mungu mwenyewe anamfufua Yesu kutoka wafu.

Kama ambavyo katika tukio la kifo cha Yesu pale juu Msalabani anaonesha pia nchi ilitetemeka na leo katika tukio la ufufuko pia anatuonesha juu ya uwepo wa Mungu kwa ishara ile ile ya tetemeko la nchi. Mathayo 27:51-52 Mwinjili Mathayo anatumia ishara hii kuonesha kuwa saa ile ya kifo na ufufuko ni saa ya mwanzo mpya kwa ulimwengu mzima, nchi inatetemka kutoka katika misingi yake ndio ishara ya ulimwengu mpya, ni ishara ya ushindi kwa kutuonesha nguvu na uwezo na uwepo wa Mungu. Ni katika Saa ile ya Yesu ilipowadia hapo kila kitu kinakuwa kipya, ni mwanzo wa ushindi, ni mwanzo mpya, ni mwanzo wa dunia mpya. Anatumia ishara nyingine ambazo tunazikuta pia katika Maandiko Matakatifu ndizo za Malaika wa Bwana, mavazi meupe na umbo la umeme, na hofu kuu. Danieli 7:9; 10:6; Waamuzi 6:11 na 13:22. Mwinjili Matayo anatumia ishara zitokanazo na Maandiko hasa sehemu hizi za Agano la Kale katika kuelezea "Kerygma" ya ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Malaika wa Bwana ni vema ieleweke katika lugha ya Biblia ni sawa na kusema uwepo wa Mungu mwenyewe katika tukio. Kila mara tunaposoma juu ya mjumbe wa Mungu au malaika wa Mungu hapo ni Mungu mwenyewe anayeshuka na kujifunua kwa mwanadamu.

Pale mwanzoni tunaona ishara za kifo zinaonekana kutawala, leo tungesema hofu ya mauti itokanayo na janga la COVID-19, linaonekana kushinda kwani hata baadhi ya nchi waamini wanashindwa kuadhimisha mafumbo haya ya mateso, kifo na ufufuko kwa pamoja katika nyumba za ibada. Wengi leo wanajifungia kwa hofu bila kutoka katika makazi yao kwa hofu ya corona, corona kiumbe kidogo sana ambacho hata hatuwezi kukiona kwa macho ya nyama, lakini wanasayansi wanatuambia kipo na jinsi kinavyoweza kuathiri maisha yetu wanadamu, dunia nzima imesimama na kukumbwa na sintofahamu hiyo. Labda kwa macho yetu ya ulimwengu ambapo makanisa leo yamefungwa katika baadhi ya nchi inaweza kuonekana kuwa Mungu ameshindwa, na hata wasioamini leo wanatuuliza kwa kebehi, yupo wapi basi Mungu wenu, kwa nini Mungu wenu asiingilie kati na kuwakinga na hili janga ili nasi tuweze kumwamini? Kanisa leo kama Pasaka ile ya mwanzo ambayo haikuadhimishwa katika makanisa bali pale kaburini, kaburi lililowekewa ulinzi mkali, hivi kuonekana kuwa huo ndio mwisho wa Yesu wa Nazareti waliyemsulubisha na kufa kifo cha aibu pale juu msalabani. Waliweka jiwe kubwa pale kaburini na ulinzi juu. Mathayo 27:62-66.

Kanisa linapitia mwaka huu wa 2020 kwa namna ya pekee majaribu makuu kabisa ya kutoka na kushuhudia kwa ulimwengu mzima kuwa Kristo ni Mzima, ameyashinda mauti, hayupo kaburini hivyo ameyashinda mauti. Ni nani leo kwa ujasiri na uthubutu mkubwa anaweza kutoka na kushuhudia kweli hiyo ya imani mbele ya walimwengu katikati ya mateso na mahangaiko yetu ya Virusi vya Corona, COVID-19. Wanawake wanafika kaburini alfajiri mapema wakati wa mapambazuko, ndio saa ya matumaini baada ya giza nene la usiku, giza la hofu na mashaka makubwa, giza la hofu ya umauti na kifo, hofu ya maradhi na mapambano ya maisha ya kila siku. Wapendwa wanawake wanakwenda kumtafuta Yesu kaburini, nasi yawezekana bado tunashawishika kutokana na magumu ya leo kwenda kumtafuta Yesu katika makaburi ya ulimwengu wa leo.

Malaika wa Bwana anashuka na kuliondosha jiwe pale kaburini na kuketi juu, ni ishara ya ushindi. Malaika anawaalika wanawake kubadili vichwa vyao na mtazamo wao, kwani Yesu hayupo kaburini bali amefufuka, ni mzima, yu hai. Ni habari njema lakini bado wanakuwa na mashaka na hofu ya kuamini. Ndio nasi leo tunapoenda kaburini kumtafuta Yesu tunakutana na Habari Njema kuwa Yesu Kristo ni mzima, hayupo tena kaburini, ameyashinda mauti, ni hai na hafi tena. Ni ukweli ambao hatuwezi kuuthibitisha kisayansi wala kwa kutumia akili na mawazo yetu bali hatuna budi kumsikiliza Yesu Mfufufuka mwenyewe. Ni kwa kukubali kuongozwa naye mwenyewe hapo kwa hakika tutafika kilele cha imani yetu, kuwa Kristo yu hai, hayupo kaburini, hayupo katika ishara zile za kifo kama maradhi na magonjwa. Hayupo katika giza la kaburi wala pale juu Msalabani anatualika kumtafuta katika Neno lake na Sakramenti na katika Kanisa. Ni huko tunakutana na Yes una kupokea ujumbe wake wa furaha na amani. Kinyume chake tutakuwa bado tumebaki kaburini, tunabaki kumtafuta Yesu kati ya wafu huko makaburini. Hatuna budi kutoka makaburini na kuanza maisha mapya.

Malaika bila kupoteza muda anawaalika na kuwatuma kwenda kuwa mashahidi wa Habari Njema kuwa Yesu Kristo amefufuka. Sio misheni rahisi ya kutoka kwa haraka bila kupoteza muda na kwenda kushuhudia “Kerygma hii ya imani”, juu ya ufufuko wake Bwana wetu Yesu Kristo. Wanawake wale hata labda bila kuelewa vema ila wanatii kutoka kaburini na ndio mwaliko kwetu leo, kutoka kaburi la COVID-19, kutoka kwenda kule tunakoongozwa na Mungu mwenyewe. Sio kufuata akili na falsafa zetu bali kuongozwa na mantiki ya Mungu mwenyewe. Hata leo nasi hakuna ugumu wala shida kuzungumzia mateso na kifo chake Bwana wetu Yesu Kristo, kwani ni kweli ya kihistoria inayoweza kuthibishwa hata na kweli za kisayansi, leo hii tunazungumzia hata Sanda ya Torino, kuwa ni moja ya shahidi za mateso na kifo chake Bwana wetu Yesu Kristo. Kwa wanajimbo Kuu Dar es salaam, karibu kila mwaka mara moja tunapata nafasi ya kusali mbele ya nakala ya sanda ya Yesu pale katika kituo cha hija, Pugu. Lakini leo tunaalikwa sio kuzungumzia juu ya mateso na kifo cha Yesu bali ufufuko wake, kuwa yu mzima hayumo kaburini na hatupaswi kumtafuta kaburini kwani yu hai, mzima. Mfufuka hatuwezi kumuona katika ulimwengu huu wa mwili, hatuwezi kumuona wala kumgusa leo kwa milango yetu ya fahamu.

Ni ukweli unaotualika kuufikia sio kwa akili zetu, wala njia za kisayansi, wala falsafa za kibinadamu bali kwa macho ya imani pekee. Ni ukweli zaidi ya kweli za kisayansi na kifalsafa. Ufufuko sio falsafa wala kweli ya kisayansi ni kweli ya Kimungu inayotutaka kuuona kwa macho ya imani tu. Ni kwa yule tu anayekubali kuongozwa na Neno lake pekee anaweza kuufikia ukweli huu wa kiimani. Kama wanawake walivyoweza kukubali kuongozwa na Mungu mwenyewe ndio wanapata ujasiri wa kutoka kwa kasi na kushuhudia ukweli huo wa imani. Kaburini tunaona kuna makundi mawili ya watu, na ndio wanawake na walinzi. Ni makundi yanayowakilisha dunia au mantiki mbili tofauti. Walinzi wanawakilisha wale wote wanaodhani na kufikiri kuwa kifo chake pale juu msalabani ilikuwa ndio mwisho wake, na sasa wanaingiwa na hofu karibu wanakuwa sawa na kufa wanapokutana na kweli hii ya kiimani, kweli ya ufufuko wa Yesu Kristo. Ni kweli unaowagusa na kuwabadili mtazamo wale wote wanaokuwa tayari kuongozwa sio na mantiki ya ulimwengu huu bali na Mungu mwenyewe. Mathayo 28:4

Wanawake badala yake wanawakilisha jumuiya ya wale wanaoamini, ya wale wanaokubali kuongozwa na mantiki ya Mungu na hasa Neno lake na sio mantiki na namna za ulimwengu huu. Ni wao wanaalikwa na Malaika wa Bwana wasiogope, anawahakikishia usalama na matumaini mapya. Kila mmoja anayekubali kuongozwa na Mungu anapata faraja na utulivu wa ndani kwani daima anakuwa pamoja naye. Ujumbe ule unaoshuka kutoka mbinguni kwa wale wanawake ni ujumbe kwa kila mmoja wetu. Ni ujumbe wa ushindi wa Mungu tunaoalikwa kuupokea hasa leo tunapoadhimisha Pasaka katika mazingira yenye mashaka na hofu ya umauti itokanayo na maambukizi makubwa ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kila mmoja anayekubali kuongozwa na Mungu hatamwacha kamwe kaburini, hatamwacha katika giza la uvuli wa mauti bali atatufufua pamoja na Yesu Kristo. Kama wanawake kwa haraka wakatoka kaburini na kwenda kushuhudia ukuu na upendo wa Mungu ndivyo nasi leo tunaalikwa kutoka kaburini na kwenda kumtangaza Kristo Mfufuka tukiwa na amani na matumaini makubwa. Walinzi kinyume chake wanashindwa kukubali kukubali kuwa mashahidi wa ufufuko wa Kristo na badala yake kama Yuda Isakariote wanakubali kuvutwa na pesa.

Ni Pasaka inayotualika nasi kujiangalia ndani mwetu na kujihoji kama tunatoka kwa haraka kwenda kumtangaza Kristo Mfufuka au tunakimbia kwa haraka kusaka na kutafuta pesa na mali za ulimwengu huu.  Tunabaki kuongozwa na ishara za umauti badala ya kukubali kuongozwa na ishara za uzima wa milele. Walinzi pamoja na kuona nguvu na uwepo wa Mungu bado wanabaki na mioyo migumu, mioyo inayovutwa zaidi na mali na vitu kuliko kufungua mioyo yao na kuukubali ukweli ule wa kiimani wa Ufufuko wake Yesu Kristo. Waamini hata kama tunakufa tuna tumaini kuwa mauti sio mwisho wa maisha yetu kwani sisi ni watu wa umilele, mateso na kifo daima havina kauli ya mwisho, kwani mbele yetu na tunasubiriwa na maisha ya umilele pamoja na Kristo Mfufuka. Nawatakia tafakari njema na Pasaka njema yenye kila furaha na tumaini la umilele.

11 April 2020, 15:34