Tafuta

Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbi kuu la  Addis Ababa-Ethiopia anasema, Kwaresima ni kipindi cha kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani! Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbi kuu la Addis Ababa-Ethiopia anasema, Kwaresima ni kipindi cha kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani! 

Kwaresima 2020: Jipatanisheni na Mungu na Jirani!

Kauli mbiu ya Kwaresima 2020: “Twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: Mpatanishwe na Mungu.” 2 Kor. 5:20. Papa anasema, Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ndicho kiini cha toba na wongofu wa ndani, unaowawezesha waamini kumgusa Kristo Yesu kwa njia ya imani kati ya watu wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kwa njia ya huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020 unaongozwa na kauli mbiu “Twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo: Mpatanishwe na Mungu.” 2 Kor. 5:20. Anasema, Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ndicho kiini cha toba na wongofu wa ndani, unaowawezesha waamini kumgusa Kristo Yesu kwa njia ya imani, wale wote wanaoteseka. Anawahamasisha waamini kufanya toba ya kweli kwa njia ya sala, ili kumwongokea Mungu na kuwa tayari kutenda mapenzi yake katika maisha yao. Ni kipindi cha kuingia katika undani wa jangwa la utupu wa maisha yao, tayari kuanza majadiliano ya kina, kwa kuwapenda jirani lakini zaidi kwa kuwapenda adui zao pamoja na kua na matumizi sahii ya vyombo vya mawasiliano ya jamii. Utajiri na amana ya Fumbo la Pasaka ni tunu shirikishi katika ujenzi wa amani, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kusimama na kujizatiti katika utu, heshima na haki msingi za binadamu dhidi ya biashara haramu ya binadamu na viungo vyake pamoja na utumwa mamboleo. Ni mwaliko wa kujenga na kudumisha uchumi shirikishi unaofumbatwa katika kanuni ya upendo!

Kwa upande wake, Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Addis Ababa nchini Ethiopia katika kipindi hiki cha Kwaresima kwa mwaka 2020, anawaalika watu wa Mungu nchini Ethiopia kutubu na kumwongokea Mungu. Anatambua kwa kina kwamba, watu wote ni wadhambi na kwamba, kwa hakika wanahitaji neema na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini, ikumbukwe kwamba, toba na wongofu wa ndani ni mwaliko kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni wakati wa toba na wongofu wa ndani unaofumbatwa katika maisha ya sala, matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kusali na kufunga pamoja na kujenga utamaduni wa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu linalopaswa kuwa ni dir ana mwongozo wa maisha. Ni muda muafaka wa kuondokana na tabia ya uchoyo, ubinafsi pamoja na hali ya kubweteka kiasi hata cha kumezwa na malimwengu pamoja na tabia ya ukanimungu.

Kwaresima iwe ni fursa ya watu wa Mungu nchini Ethiopia kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma, upendo na upatanisho wa Mungu, tayari kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi nchini Ethiopia. Waamini wathubutu kuingia ndani mwao na kuomba msamaha wa kweli kwa Mwenyezi Mungu kutokana na dhambi zao. Wawe tayari kuwasamehe jirani zao waliowakosea kwa njia ya Kristo Yesu, aliyeyamimina maisha yake, ili kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kuwashirikisha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani! Kardinali Berhaneyesus Demerew Souraphiel, anawakumbusha waamini kwamba, Kwaresima ni kipindi muafaka cha kujenga na kuimarisha mafungamano na tunu msingi za maisha ya kifamilia; kwa kukazia zaidi maisha ya kiroho.

Ni muda wa kusali pamoja kama familia; kusoma, kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Wazazi na walezi, watumie muda huu kuwaelimisha watoto wao maana ya Kipindi cha Kwaresima katika maisha na utume wa Kanisa pamoja na umuhimu wa kujinyima kama kielelezo cha upendo kwa jirani. Huu ni muda uliokubalika wa kutoka katika ubinafsi na kuanza kujiachia kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Kardinali Souraphiel, anasema waamini watambue kwamba, wao ni vyombo na wahudumu wa neema na upendo wa Mungu wanaopaswa kuwashirikisha na kuwamegea wengine. Ni kipindi cha kuthubutu kuwashirikisha maskini na wanaoteseka rasilimali fedha, vitu na muda kama wafuasi amini wa Kristo Yesu bila ya kujibakiza hata kidogo. Kutoa sadaka kwa maskini ni tendo jema linalowataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa makini, ili wasiwe na uchu na tamaa ya kutaka kumiliki mali ya watu wengine kinyume cha sheria.

kard. Souraphiel

 

03 April 2020, 12:11