Tafuta

Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa Maadhimisho ya Jumaa kuu linalowaingiza waamini katika Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu! Hii ni Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa mwaka 2020 Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa Maadhimisho ya Jumaa kuu linalowaingiza waamini katika Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu! Hii ni Siku ya Vijana Ulimwenguni kwa mwaka 2020 

Tafakari Neno la Mungu, Jumapili ya Matawi: Siku ya XXXV ya Vijana

Jumapili ya Matawi, Kanisa linamshangilia Kristo Yesu anapoingia mjini Yerusalemu, tayari kukabiliana mubashara na Fumbo la Mateso, Kifo na hatimaye, Ufufuko wake kutoka kwa wafu! Hii ni Siku ya XXXV ya Vijana Ulimwenguni inayoongozwa na kauli mbiu: "Kijana, nakuambia: Inuka". Lk. 7:14. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kuinuka na kuanza mchakato wa kupyaisha maisha yao!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya matawi mwaka A wa kanisa. Ni siku sita kabla ya Pasaka, wakati Bwana alipoingia mjini Yerusalemu, watoto walimlaki; nao walichukua matawi ya mitende mikononi, wakapaaza sauti wakisema: Hosana juu mbinguni: Mbarikiwa wewe uliyekuja na wingi wa rehema yako. Kumbe domenika hii Kanisa linaadhimisha matukio makuu mawili. La kwanza ni kuingia kwa shangwe Bwana wetu Yesu Kristo mjini Yerusalemu kama mfalme na mkombozi ambapo mwaka huu kutokana na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na virusi aina ya korona sehemu kubwa duniani wataifanya bila maandamano.

Pili ni simulizi la Mateso ya Yesu Kristo yanayotuingiza katika katika Jumaa kuu la kuadhimisha Fumbo la ukombozi wetu, Fumbo la Pasaka tunaloliadhimisha kwa siku tatu mfululizo yaani: Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Jumamosi kuu. Tunazama katika tafakari ya fumbo la msalaba, fumbo la wokovu wetu, yaani Mateso, Kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Hili ni adhimisho Kuu moja linalodumu kwa muda huo wa siku tatu. Alhamisi Kuu, tutaadhimisha karamu ya mwisho yaani mlo wa mwisho aliokula Yesu na wanafunzi wake muda mfupi tu kabla ya kukamatwa na kuteswa hadi kufa msalabani. Ni siku aliyoweka Sakramenti za Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Upadre na Amri ya mapendo. Ijumaa Kuu Kanisa linaadhimisha: mateso na kifo cha Kristo Msalabani na Jumamosi Kuu Kanisa linaomboleza kwa masikitiko makuu likingojea ufufuko wake katika mkesha wa Pasaka ambapo kunakuwa na ibada ya mwanga na kupigwa kwa mbiu ya kumshangilia Kristo mfufuka. Maadhimisho haya yanakuwa na maana kwa walioziishi vyema siku hizi arobaini za kwaresma, siku za mfungo mtakatifu, siku za kujipatanisha na Mungu.

Katika somo la kwanza Nabii Isaya anamwonesha Yesu Kristo kuwa ni mfalme wa amani, sio mfalme wa vita, ni mpole, mnyenyekevu, mvumilivu na hana makuu. Ili kudhihirisha hili anaingia Yerusalemu kwa shangwe na furaha akiwa juu ya mwanapunda, mnyama mpole na mtaratibu asiye na makuu ambaye kwa wayahudi alikuwa ni mnyama aliyetumiwa na watu duni, maskini na wanyonge kwa safari na kazi, tofauti kabisa na farasi aliyetumiwa na wafalme na majemedari wa vita. Punda ambaye hajatumiwa bado kwa kazi au safari za kawaida, alitumika kwa mambo matakatifu. Ndiyo maana Yesu aliagiza mwanapunda ili kuonyesha kuwa yeye ni Mtakatifu na yote anayoenda kuyafanya ni Matakatifu. Tukio hili linatimiza utabiri wa nabii Zekaria ukisema; “Furahi sana Ee binti Sayuni, piga kelele ee binti Yerusalemu! Tazama Mfalme wako anakuja kwako. Ni mwenye haki, naye ana wokovu, ni mnyenyekevu amepanda punda, naam, mwana punda, mtoto wa punda” (Zek.9:9).

Watu waliochukua matawi kama ishara ya ushindi na matumaini kwa Masiha wanatandika nguo zao huku wakiimba nyimbo za furaha. Kundi hili la watu linalomshangilia Yesu ni la wanyonge, watu toka mashambani, watu duni, wenye kipato cha chini, nao wanafanya mji wote wa Yerusalemu utikisike kwa kelele za shangwe na hivyo kuamsha hasira za wakuu wa Makuhani, Mafarisayo na Waandishi ndiyo maana wakaanza mikakati ya kumkamata Yesu tena wakati wa usiku, wakati wa giza, wakiwa na taa na mienge, marungu na mikuki na silaha za kivita huku wamejaa hofu na mashaka. Kristo anakamatwa akiwa bustanini Gethsemane akisali, naye bila ubishi anaanza safari ya ukombozi kuelekea Golgota kusulubiwa. Safari yenye mateso makubwa, anabebeshwa msalaba mzito, anafanyiwa dhihaka njiani, anapigwa mijeledi, anatemewa mate, anatukanwa na pale msalabani anapigiliwa misumari mikononi na miguuni hatimaye anakufa kwa sababu ya dhambi zetu kama mtu aliyelaaniwa na Mungu.

Tunasoma hivi katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati: “Ikiwa mtu ametenda dhambi ipasayo kufa, nawe ukamtundika juu ya mti, mzoga wake usikae usiku kucha juu ya mti; lazima utazikwa siku hiyohiyo. Kwani aliyetundikwa amelaaniwa na Mungu, asije akatia unajisi katika nchi yako akupayo Bwana Mungu wako iwe urithi wako” (Kum.21:22-23). Ni mateso makali mno na kifo cha aibu mbaya mno. Lakini kwa kifo chake kilivyokuwa cha pekee, dunia ilitetemeka, jua lilififia, kukawa giza, pazia la hekalu likapasuka mara mbili, walioshuhudia walisadiki uaguzi wa manabii na kusema hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu. Haya yote aliyotendewa mwana wa Mungu yanatufundisha kuwa hakuna utukufu pasipo mateso na hakuna Pasaka bila Ijumaa kuu. Mateso na mahangaiko ya maisha yetu hapa duniani yanaakisi tu mateso ya Kristo kwa ajili ya dhambi zetu. Kwa kujua ukweli huu Kanisa linahimiza waamini kuvumilia mateso na magumu yanayotupata katika kumfuata Kristo ili tuufikie utukufu wa milele. Mateso tuyapatayo katika kuikiri na kuishuhudia imani yetu yanatushahilisha kuingia katika ufalme wa mbinguni kama tukiyapokea kwa imani na bila kunung`unika.

Kuna mateso yanayosababishwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambayo yanaleta mabadiliko ya tabia nchi yasababishwayo na ufidhuli wa mwanadamu. Kwa mfano: mafuriko na ukame, matetemeko, magonjwa ya mlipuko kama homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya korona nyakati zetu, wengine wanateseka kwa vita, umaskini, manyanyaso kazini, ugomvi wa kifamilia. Mateso haya, yasitufanye tukate tamaa bali yaimarishe imani yetu tukijua kuwa Kristo yupo kwa ajili yetu, anayajua hayo yanayotukabili na tukimwamini yeye, atatusaidia. Lakini tutambue kuwa majukumu yanayotukabili katika maisha ya kila siku sio mateso. Mfano ili kuleta mafanikio, maendeleo, kulisha familia, kusomesha watoto ni lazima kuhangaika, kufanya kazi kwa bidii, kuvumilia, kutumia nguvu wakati mwingine kukatisha usingizi utoke usiku uenda mbali, unalazimika kuacha starehe na kufurahi na wenzetu, unahangaika na kutoka jasho na wakati mwingine kuumia. Haya ni majukumu na sio mateso ndiyo maana Mtume Paulo anatuambia asiyefanya kazi na asile, kwani kazi ni agizo la Mungu kwa Mwanadamu la kuutiisha ulimwengu. Na tukiwajibika vizuri ipasavyo tutafaidika na kupata furaha tele mbele za Mungu.

Tutambue pia, mateso na mahangaiko tunayojisababishia wenyewe kwa kukiuka amri na maagizo ya Mungu, mateso yatokanayo na dhambi zetu wenyewe, hayawezi kutuletea wokovu bali yatatupeleka kwenye moto wa milele kwani yanazidi kumtesa Kristo. Hii ni baadhi ya mifano ya matatizo na mateso tunajisababishia ambayo ndiyo yatakayotupeleka motoni tusipotubu dhambi zinazotusababishia mateso haya: umeenda kuiba, umetoka nje ya ndoa, kijana hujaoa au hujaolewa umekamatwa katika uasherati na uzinzi ukapiga kwa nzuri wakatokea wasamaria wakakuokoa ukabaki na maumivu na makovu, huna meno yote ya sebuleni, reception ineharibiwa umebaki na chongo, mdomo uko upande, au umelewa ukaanguka ukavunjika; Je, haya nayo tuyaite mateso yaletayo wokovu? Unaendesha gari, pikipiki au baiskeli kwa mwendo kasi ukaanguka ukavunjia, tunaambiwa madawa ya kuzuia mimba yana madhara katika miili yetu yanaharibu mfumo wa uzazi, utashindwa kupata mtoto utakapomhitaji na tena ni dhambi na chukizo kwa Mungu yanapinga kazi ya Mwenyezi Mungu, kutoa mimba ni dhambi na chukizo kwa Mungu, kupiga ramli, ulevi, uvivu, uzembe kazini unasababisha kufukuzwa kazi, rushwa ni mbaya utafia genezani, imani na "sera za freemasons" kama kutoa kafara za watu, sio tu ni dhambi na chukizo kwa Mungu bali pia yanatuletea shida na matatizo katika maisha yetu.

Licha ya kuwa tunaambiwa juu ya hayo yote hatusikii wala kuelewa kwasababu ya kiburi, majivuno na ukaidi tunajikuta tuna matatizo na masumbuko mengi na watu waliowajanja wanaongozwa na Ibilisi wanayatumia matatizo yetu na kutufanya tuasi imani yetu. Haya ni mateso ya kujitakia wala Mungu hahusiki na haya wala hayatuletei wokovu bali yatatupeleka katika moto wa milele aliyetayarishiwa ibilisi na malaika zake tangu awali. Katika simulizi la mateso ya Yesu, umati wa watu walipiga makelele wakisema asulubishwe, asulubishwe. Kwetu sisi kwa mawazo yetu, kwa maneno yetu, kwa matendo yetu maovu, kwa kutokutimiza nyajibu zetu za kikristo, kwa dhambi zetu tunatoa mlio na makelele hayo hayo, msulubishe, msulubishe. Petro anajaribu kupambana na nguvu za giza kwa upanga. Kristo anapambana na kumshinda shetani si kwa mapanga na vitisho bali kwa uvumilivu wake, kwa unyenyekevu wake, kwa upole wake na kwa utii wake kwa Mungu Baba. Kila mmoja wetu ajitafakari na kujiuliza, je mimi sina fikra kama za Petro za kupambana na nguvu za shetani na Ibilisi kwa ubanga wa giza, maseng’enyo, malumbano, mapigano, visasi na fitina. Je, sisemi kila siku katika makundi ya watu msulubishe, msulubishe, mwondoshe, mwondoshe. Tukumbuke ufalme wa Kristo si wa Dunia hii hivyo hatupaswi kumpigania kwa jeshi bali kwa ushuhuda wa maisha yetu mema. Tuwe werevu kama nyoka na wapole kama njiwa.

Mtakatifu Petro hakuishia hapo bali mara tatu amemkana Kristo akisema mimi si mfuasi wa mtu huyu, akasisitiza mimi simjui mtu huyu. Sisi pia tunafanya jambo hili hili katika maisha yetu pale tunapoionea aibu Injili, tunaporudi nyuma kiimani tunapokumbana na matatizo na magonjwa mbalimbali, tunakosa imani na matumaini kwa nguvu na uweza wa Kristo, tunatafuta suluhu katika dhambi na wakati mwingine tunapongezana na kushukuriana kwa baadhi ya dhambi tuzitendazo. Jogoo amekwisha wika mara ya tatu, tunaalikwa kujirudi, tujiweke chini ya msalaba kwani hatuna tumaini lingine, japo kwao wanaopotea msalaba ni kikwazo na upuuzi, kwetu ni nguvu ya Mungu, kwetu ni nguvu ya Kristo, kwetu ni alama ya ushindi, tuutazame msalaba kwa imani kuu na moyo wa toba. Tumwombe Mungu atujalie moyo thabiti na wa ujasiri wa kuyapokea mateso na mahangaiko kwa uvumilivu na imani kuu kama Kristo alivyoyapokea na hata pale tunaposikia hatumjui huyu! Mwondoshe! Mwondoshe! Msulubishe! Msulubishe!

Tusikatishwe tamaa au kukwazwa, na kurudi nyuma, bali mahangaiko ya magonjwa na mateso tunayoyapata yatuimarishe na kutuunganisha zaidi na Kristo aliyevumilia mateso kwa ajili yetu sisi wadhambi ili mwisho wa yote tukamsifu Mungu pamoja na malaika zake huko mbinguni milele yote.Tuingie juma hili kuu kwa moyo wa majuto. Tuombe neema ya kuwa wasikivu na watii kama Isaya alivyoimba katika somo la kwanza “Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi…huniamsha sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao”. Tukubali kufundishwa na kuelekezwa. Tuwe watii. Tujipatanishe na Mungu ndipo tutakapokuwa na sababu ya kufurahia siku ya Pasaka na tunuie kutorudi nyuma tena mpaka tutakapomaliza safari yetu na kufurahi milele katika Pasaka ya Mbinguni.

02 April 2020, 13:56