Jumapili ya Huruma ya Mungu ni chemchemi na neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sakramenti za Huruma ya Mungu kwa waamini waliojiandaa kikamilifu Jumapili ya Huruma ya Mungu ni chemchemi na neema na baraka zinazobubujika kutoka katika Sakramenti za Huruma ya Mungu kwa waamini waliojiandaa kikamilifu 

Jumapili ya Huruma ya Mungu: Chemchemi ya neema na baraka!

Kazi ya Kristo ya Ukombozi hudhihirika katika Sakramenti Takatifu, na Liturujia ya Dominika ya Pili ya Pasaka inazungunzia Sakramenti hizo. Ubatizo, Kitubio na Ekaristi Takatifu. Hivi ni visima vya huruma ya Mungu visivyokauka. Kanisa huviongoza vizazi vyote vya dunia nzima kuelekea katika visima hivi vya neema. Kilele cha ibada yetu kwa Mungu, katika Jumapili ya Huruma ya Mungu.

Na Padre Wojciech Adam Koscielniak, Hekalu la Huruma ya Mungu, -Musoma.

"Natamani Jumapili ya kwanza baada ya Pasaka iwe Sikukuu ya Huruma." (Shajara, 299) Wapendwa Mahujaji, Kwa mara ya kwanza Bwana Yesu alipozungumza kwamba anatamani Sikukuu hii ya Huruma iadhimishwe katika Jumapili ya kwanza baada ya Pasaka, ilikuwa mwaka 1931 katika kanisa la Plock, Poland alipoagiza picha ya Yesu mwenye Huruma ichorwe. Katika miaka iliyofuata baada ya hapo, alirudia agizo hili zaidi ya mara 14, akieleza nafasi ya Sikukuu hii katika kalenda ya Kiliturjia, sababu za kuanzishwa kwake, namna ya kuiandaa na kuiadhimisha. Wazo la Huruma ya Mungu ndilo hutawala katika mwaka mzima wa Liturujia ya Kanisa. Sababu ya kuchagua Jumapili ya kwanza baada ya Pasaka, ambayo ni kilele cha siku nane tangu siku ya ufufuko, huonesha uhusiano wa karibu kati ya Fumbo la Pasaka la ukombozi na Sikukuu ya Huruma. Kwa nini? Kwa sababu Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo ni matendo makuu yanayoonesha Huruma ya Mungu kwa binadamu.

Uhusiano huu pia husisitizwa kwa Novena ya Huruma ya Mungu, ambayo huitangulia Sikukuu; novena hii huanza Ijumaa Kuu, siku ambayo Yesu aliteseka na kufa Msalabani. Tunasoma katika kitabu cha kumbukumbu cha Sista Faustina kwamba Yesu alisema: ‘Nawajulisha watu kilindi cha Huruma yangu kupitia kwa Neno aliyefanyika mwili’ (88). Kazi ya Kristo ya Ukombozi hudhihirika katika Sakramenti Takatifu, na Liturujia ya Dominika ya Pili ya Pasaka inazungunzia Sakramenti hizo. Ubatizo, Kitubio na Ekaristi Takatifu. Hivi ni visima vya huruma ya Mungu visivyokauka. Kanisa huviongoza vizazi vyote vya dunia nzima kuelekea katika visima hivi vya neema. Ndiyo maana, tunafikia kilele cha ibada yetu kwa Mungu, katika Liturujia ya Jumapili ya Huruma ya Mungu. Vile vile, Bwana wetu alitoa sababu za tamaa yake ya kuanzishwa kwa Sikukuu hii: ‘Licha ya mateso yangu makali bado roho zinaangamia. Nazipatia tumaini la mwisho la wokovu; yaani, sikukuu ya Huruma yangu. Zisipoiabudu Huruma yangu, zitaangamia milele yote’ (Shajara, 965).

Sikukuu ya Huruma haitakuwa tu siku maalum ya kumwabudu Mungu katika Fumbo hili, bali pia siku ya neema nyingi kwa ajili ya watu wote, hasa siku ya kuwakomboa wakosefu: ‘Natamani Sikukuu ya Huruma iwe kimbilio na makao ya roho zote, hasa za wadhambi’ (Shajara, 699). Yesu alisema, ‘ye yote atakayejisogeza karibu na kisima hiki cha uzima katika siku hii atajaliwa ondoleo kamili la dhambi na adhabu zake’ (Shajara, 300). Hivyo, wapokeao Komunyo Takatifu katika siku hiyo hujaliwa neema ya pekee, neema ya ‘ondoleo kamili la dhambi na adhabu zake.’ Neema hii ni kubwa zaidi kuliko rehema kamili, ambazo huondoa tu adhabu za muda za dhambi zilizotendwa, lakini hazitoi msamaha wa kosa. Hakika, neema hii maalum kabisa, inazidi hata rehema zile zitolewazo na Sakramenti sita, isipokuwa Sakramenti ya Ubatizo kwa sababu neema ya kuondoa dhambi na hatia ni tunda la Sakramenti ya Ubatizo. Katika ahadi zilizotajwa hapo juu, Kristo alisema Komunyo Takatifu katika Sikukuu ya Huruma itaambatana na neema hizo.

Ni wazi kwamba, ili Komunyo Takatifu itoe ondoleo la dhambi na msamaha wa adhabu, lazima ipokewe katika hali inayostahili  ya hali ya neema ya utakaso rohoni na katika kutimiza masharti muhimu ya Ibada ya Huruma ya Mungu. Ikipokewa isivyostahili - katika hali ya dhambi bila tumaini katika Huruma ya Mungu na bila tendo lo lote la huruma kwa jirani, badala ya kuleta neema za pekee sana inaweza kuleta hasira na ghaghabu ya Mungu kwa aliyekomunika (Mwanataalimungu wa Huruma ya Mungu - Padre I. Różycki). Ukarimu wa Bwana Yesu Kristo haukuishia hapo tu. Kwa maana alishasema kwamba anazimwagia bahari nzima roho zinazoikaribia chemchemi ya Huruma yake kwa sababu ‘…katika siku hiyo, milango yote ya kimungu ambamo Huruma yangu hupita inapotiririka, hufunguka na kukaa wazi. Roho yo yote isiogope kunikaribia hata kama ina dhambi kubwa kiasi gani’ (Shajara, 699).

Leo, dunia inazama katika dhambi, katika damu ya watoto wasiozaliwa (mimba zinazotolewa), katika machozi ya wanaosumbuliwa na kudhulumiwa, na Wakristo wanaojihusisha na Kanisa juu juu tu. Wanakaa miaka mingi bila kupokea Sakramenti, hawashiriki Misa Takatifu Jumapili, hawabatizi watoto wao, wala kujishughulisha na malezi yao ya Kikristo. Mara nyingi, tabia hii ya kutojali haitokani na nia mbaya, bali uelewa mdogo au kutokuelewa kabisa umuhimu wa neema za Huruma ya Mungu. Neema hizi hupatikana kwa wingi sana katika Sakramenti zote na katika matendo mengine ya kiroho. Kutambua ukuu wa Huruma ya Mungu ndiko kunapaswa kulipia hasara inayoletwa na ubaridi na kutojali kwa Wakristo wa nyakati hizi. Kunapaswa kuwafurahisha, kuwajaza matumaini na furaha ya kimungu. Bwana Yesu anasema: “Sikukuu ya Huruma yangu imetoka katika vilindi vyangu kwa ajili ya kuifariji dunia nzima”. (Shajara, 1517).

Maandalizi kwa ajili ya Sikukuu ya Huruma ni pamoja na kuadhimisha Novena ya Huruma ya Mungu kuanzia Ijumaa Kuu hadi Jumamosi kabla ya Sherehe ya Huruma ya Mungu. Katika Kitabu cha kumbu kumbu cha Sista Faustina, imo pia Novena ambayo Yesu aliagiza isaliwe kwa ajili ya mahitaji na matumizi binafsi. Waamini wanaweza pia kuisali Novena hii kama aina mojawapo ya kuonyesha uchaji. Hata hivyo, kuadhimisha Novena kwa kutumia Rozari ya Huruma kunaleta manufaa makubwa sana kwa dunia nzima. Yesu mwenyewe alituahidi yafuatayo: “Kwa novena hii, nitazipatia roho neema zote zinazowezekana” (Shajara, 796). Kuhusu namna ya kusherehekea Sikukuu ya Huruma, Bwana Yesu alitoa masharti mawili yafuatayo: kwanza, katika siku hii, picha ya Yesu Mwenye Huruma ibarikiwe kwa heshima na itukuzwe hadharani, yaani, kiliturujia (Shajara, 49 na 88); pili, katika siku hiyo “Mapadre wamwambie kila mtu juu ya Huruma yangu kuu na isiyo na mwisho” (Shajara, 570). Bwana Yesu Kristo, si tu anatudai kuiheshimu Huruma hii ya Kimungu, bali pia kuwapenda jirani zetu (Shajara, 742).

Neema nyingi na kuu za namna hiyo hazikuambatanishwa katika aina yo yote ile nyingine ya ibada kwa Huruma ya Mungu, hivyo ni jambo jema kwa waamini kujua ukuu wa neema wanazoweza kupokea katika Sikukuu ya Huruma ya Mungu na masharti yanayoendana nazo ili kuzipata. Ninawashukuruni nyote kwa kusherehekea Siku kuu ya Huruma ya Mungu mwaka huu ama katika Kituo hiki cha Kitaifa cha Hija cha Huruma ya Mungu ama katika Makanisa yenu. Natumaini kabisa kila mmoja wetu atakuwa amebadilika na kujaa ukamilifu wa mapaji, karama na huduma za Roho Mtakatifu wa Huruma. Natumaini janga la gonjwa la COVID-19 litakwisha mapema na tutaweza tena kufunga safari za hija za kuelekea Kituo cha Kitaifa cha Hija cha Huruma ya Mungu – Kiabakari, Jimbo Katoliki la Musoma. Hivyo, ninawakaribisheni sana kwa hija maalum kwa heshima ya Mitume wa Huruma ya Mungu - Mtakatifu Sista Faustina na Mtakatifu Yohane Paulo II tarehe 3-4/10/2020. Hija ya siku mbili ya malezi endelevu ya wachaji wa Huruma ya Mungu na ya Wanashirika waliojiunga na wanaopenda kujiunga rasmi na Shirika la Mitume wa Huruma ya Mungu. Tuombeane na kutiana moyo katika utume huu na wala tusikate tamaa bali - tukiwa tumejawa Roho Mtakatifu - tutende yampendezayo Yesu wa Huruma.

Tafakari: Huruma
16 April 2020, 13:00