Ijumaa Kuu: Mama Kanisa anatafakari juu ya: Ukuu na Utukufu wa Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu, kiini cha wokovu wa ulimwengu! Ijumaa Kuu: Mama Kanisa anatafakari juu ya: Ukuu na Utukufu wa Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu, kiini cha wokovu wa ulimwengu! 

Ijumaa Kuu: Utukufu na Ukuu wa Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu!

Ijumaa Kuu, Mama Kanisa anatafakari mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalaba. Fumbo la Msalaba ni ufunuo wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu kwa ajili ya wokovu wa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Leo Mama Kanisa anatafakari mng'ao wa Fumbo la Msalaba "Fulget crucis mysterium". Ni kilele cha ile Saa ya Yesu anayetukuzwa na Baba yake wa mbinguni!

Na Padre Gaston George Mkude, -Roma.

Amani na Salama! ‘’Fulget crucis mysterium’’ ni maneno ya lugha ya Kilatini ambayo naomba tuanze nayo katika tafakari yetu ya leo. Maneno haya kwa tafsiri sisisi ni fumbo la kung’aa kwa msalaba. Kwa kweli kwa tafsiri yake tunaona ni maneno yanayokinzana, iweje msalaba ung’ae?! Kuna utukufu gani katika mateso ya msalabani. Tunajua kifo cha msalaba ni adhabu ya kifo cha aibu kwa waarifu wakubwa katika enzi za utawala wa kirumi katika dola lao. Na hata leo hatuoni kuna thamani gani katika mateso kwa mwanadamu, leo dunia inasimama na kujiuliza maswali magumu kwa nini magonjwa kama hili la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Kuna utukufu gani katika janga la CORONA? Tunapotafakari juu ya utukufu wa Msalaba siku ya leo, Mwinjili Yohane katika masimulizi ya mateso ya Yesu anatusaidia kupata maana ya matukio yaliyojiri kwa masaa yale matatu ya mateso makali na kifo cha aibu pale juu msalabani. Mwinjili Yohana anatusaidia kuelewa maana na sababu za mateso na kifo chake, kwani kwa kila aliyepata kuona mafundisho na matendo yake haoni sababu za kuhukumiwa kifo kile tena kwa njia ya mateso yenye ukatili usioelezeka. Ni Yesu aliyeponya wagonjwa, aliyewakumbatia watoto, aliyewapenda maskini na kujifanya mtumishi na haswa mtumwa wa wote. Mtu wa haki leo anapata tuzo la kupigiliwa pale msalabani na kutemewa mate na kudhihakiwa?

Kwa nini Yesu ateseke na afe pale juu Msalabani?  Ni kosa gani amefanya? Mwinjili Yohana tangu mwanzoni kabisa na hasa katika Utangulizi wake ujulikanao kama ‘’Prologue’’, anamtambulisha Yesu kama NURU Iliyokuja ulimwenguni kuwaangaza watu wote lakini si wote wamechagua nuru na badala yake wamechagua kubaki gizani. (Yohana 1:4-5, 9 na 3:19). Miale ya nuru/mwanga ule umekuwa kero baada ya kuangaza baadhi ya mioyo iliyo gizani, inasumbua na kuchosha macho yaliyozea kubaki gizani. Upande mwingine, miale ya mwanga ule umekuwa msaada kwa mioyo minyofu iliyoupokea na hivyo kuweza kutembea katika nuru. Hivyo tangu mwanzoni mwa Injili ya Yohana tunakutana na makundi haya mawili. Miale ya Nuru hii tunaona inagusa kwa namna 4 kwa makundi mawili yenye madaraka ya kidini na kisiasa. Ni hasa kwa sababu za kisiasa na za kidini tunaona Yesu anahukumiwa na hata kuonekana anapaswa afe tena kifo cha aibu pale juu Msalabani.

Muale wa kwanza ni juu ya sura halisi ya Mungu: Yesu alikutana na ukinzani mkubwa kwani viongozi wa dini kwa mapokeo daima walifundisha watu juu ya Mungu aliye hakimu mkali asiye na huruma na yeyote yule aendaye kinyume na amri na maagizo yake. Kinyume chake Mungu anayehubiriwa na Yesu ni Baba Mwema na si kingine bali Mwema. (Mathayo 5:45, Mathayo 6:25-31 na Mathayo 6:8 na kuendelea) Hivyo ni Mungu mwenye Huruma hivi hakuna mdhambi yeyote aendaye kwake bila kupokea huruma na upendo wake wa Kimungu. Na ndio anamtuma mwanae ulimwenguni ili kila amwaminiye asipotee bali ajaliwe kuwa na uzima wa milele. (Yohane 3:16-17) Mungu ni mwenye huruma ipitayo vipimo vyote na ndio maana naendelea kuwakumbusha kila mara tuepuke na tafsiri zinazomkufuru Mungu hasa siku hizi wapo wahubiri wanaothubutu kusema gonjwa la homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 ni adhabu ya Mungu kwa mwanadamu kwa dhambi na makosa yetu kwake! Niseme waziwazi hapana, kusema na kuamini hilo ni kufuru kwa Mungu wetu aliye mwema na mwenye upendo na huruma isiyo na mipaka, tunaalikwa daima kukimbilia huruma na upendo wake usio na mipaka wala masharti.

Kwa Waandishi na Mafarisayo kwao Yesu ni sawa na “mwendawazimu” na “mpotoshaji” kwani Mungu kwao ni hakimu mkali asiye na huruma na hivyo yupo mbali na wadhambi kama watoza ushuru na makahaba. (Yohane 8:48, 59 na Yohane 10:31, 39) Kwao Yesu ni mtu hatari na hivyo ni vema kumwondoa katika sura ya nchi kwani anahatarisha imani ile waliyorithi kutoka mababu zao. Tukumbuke jinsi Yesu alivyokula na kutembea na hata kukaa katika nyumba za wadhambi, ni Yesu anayetaka kuja na kukaa ndani mwa kila mmoja wetu anayekiri na kukubali kuwa ni mdhambi ili tuweze kuponywa kwa kupokea huruma na upendo wake wa kimungu. Muale wa pili wa hiyo nuru unaangaza katika dini potofu. (False Religion) Kuna aina mbili za kuishi dini, aidha kuishi imani kwa namna ambayo inaleta amani katika nafsi ya mtu au ile dini iliyojaa amri na maagizo na masharti mengi hivyo kukiuka moja ya amri na maagizo hivyo kuishia kuwa ni mzigo mzito kwa mtu. (Mathayo 11:28-30) Ni dini inayokuwa mzigo kwani mahusiano na Mungu siyo yale yanayojengeka katika upendo bali katika amri na maagizo mengi ya kufuata. Yesu kinyume chake anatualika kuhusiana na Mungu kwa upendo na kwa si kingine bali upendo. Siyo tena dini inayojikita katika amri na sheria bali katika roho na kweli, ni mahusiano ya upendo na Mungu aliye Baba yetu mwema na mwenye upendo na huruma. (Marko 7:7 na Yohane 2:13-22). Ni mwanga huu unawasumbua kiasi cha Kaifa aliyekuwa kuhani mkuu kuwaalika wengine kuwa ni heri mtu huyu afe kwa ajili ya watu. (Yohana 11:50)

Muale wa tatu ni ule unaoangaza juu ya mtu kweli ni yupi, "the authentic person". Ni mtu wa aina gani anasimama kama mfano wa kweli katika jamii. Yesu anatupa kielelezo ambacho nacho kinaamsha hasira kali. Wakati wa Yesu, watu walioonekana waliishi maisha adilifu na ya mfano ndio wakuu wa “Sinedrio”, makuhani wa hekaluni, marabi na hivyo walivaa mavazi marefu na kupewa heshima wasalimiwapo na kuchukua nafasi za mbele katika masinagogi na katika sherehe. Hawa ni watu wa mfano. (Marko 12:38-39 na Yohane 5:44) Hata Yesu aliomba kutukuzwa na Baba yake lakini utukufu wake haupo katika kushangiliwa kama alivyoingia katika mji ule mtakatifu kama tulivyoadhimisha Dominika ya Matawi bali katika saa yake pale Msalabani, Mlimani Kalvario. Ni pale juu Msalabani Yesu aliweza kuonesha ulimwengu nuru na mwanga wa Huruma na Upendo wa Mungu kwa mwanadamu dhaifu na mdhambi (Natumai neno dhaifu halitelata ukakasi kama inavyosikika siku hizi katika nchi yetu) Tukiri sisi sote ni dhaifu na hivyo Ijumaa Kuu ni siku ya kuinuliwa kwetu ili nasi tuweze kushiriki: ukuu na utukufu wa Mungu.

Ni katika udhaifu na unyonge hapo utukufu wa Mungu unaonekana na kujidhihirisha. Kwa Yesu maisha yetu hayana budi kuwa kama mbegu ili yatoe matunda kusudiwa hatuna budi kufa kama mbegu inayosiwa ardhini, na anayeokoa maisha yake anayaangamiza ile yule anayeyaangamiza maisha yake anayaokoa. Ni mantiki ya Mungu na hivyo kinyume na mantiki yetu ya kiulimwengu. Kuwa mfuasi wa Yesu ni kukubali nasi kuishi na kuenenda katika njia ile ya Yesu mwenyewe. (Yohane 12:24-25). Hivyo Yesu anatualika kubadili vichwa vyetu kwa maana ya mitazamo yetu inapofika kuhusu mtu kweli (authentic person), si yule anayeshinda bali anayepoteza, asiyetawala bali anayetumikia, siye yule anayehesabu faida yake bali anayejitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Ni yule asiyeenenda kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu bali daima anayeongozwa na mantiki ya kimungu.

Na muale wa nne uliangaza jamii nzima. Sisi tunaishi katika ulimwengu wa ushindani. Na tangu tungali wadogo tunalelewa katika namna hiyo ya lazima kupambana ili kufanikiwa maishani. Ni lazima tuibuke washindi iwe shuleni mzazi anaalika watoto lazima wafaulu zaidi kuliko wengine na hivi kila mzazi kudiriki kusema enzi zangu shuleni nilikuwa wa kwanza daima yote ni kuwapa hamasa watoto wapambane shuleni hata mtaani katika michezo kila mzazi anamuhimiza mwanae asikubali kuonewa na wengine, hivyo ikibidi apambane pale anapopigwa au kufanyiwa vibaya na mtoto mwingine. Leo tunaposalimiana hata kwa njia ya jumbe za simu ni kawaida kusikia au kupata majibu kuwa tunapambana na maisha, ni mantiki inayotawala na kutuongoza wengi wetu. Na ndipo siku moja Yesu akaketi na kumpakata mtoto mdogo na kuwaalika wanafunzi kuwa anayempokea mtoto yule basi anampokea yeye na hivyo Baba aliyemtuma ulimwenguni. (Marko 9:36-37) Wakati wa Yesu watoto walikuwa ni ishara ya udhaifu kwani ni tegemezi kwa kila hali, ni muhitaji maana bado hajafika umri wa kujitegemea.

Ni katika ulimwengu mpya wa Ufalme na Utawala wa Mungu tunaona wadogo na wanyenyekevu ndio wanakuwa kielelezo cha maisha yetu. Ni wadogo ndio wanaoheshimika katika macho ya Mungu. Ni hawa wanaoonekana dhaifu na wadogo ndio wanapewa kipaumbele na ndio Kanisa leo linaalikwa daima kuwalinda watoto katika kila hali, na ndio linaalikwa daima kutenga kwa umakini na upendo mkubwa katika kuwalea na kuwakuza watoto hawa. Maskini kwa namna ya pekee kabisa wanapaswa kuwa kipaumbele cha jumuiya zetu, iwe ndogo ndogo, kiparokia na majimboni mwetu. Katika mipango yetu ya Kichungaji lazima kuona kwa namna ya pekee tunawapa nafasi ya kwanza makundi ya wote wanakuwa wanasahaulika katika jamii. Yesu anawakumbatia hawa wadogo na kuwabusu! Ni mara ngapi katika parokia zetu tunawapa nafasi ya kwanza makundi haya ya wanaosahaulika, japo mfano mdogo tu tunapokuwa na sherehe zetu mfano siku za Upadrisho, uwekwaji nadhiri, au sherehe yeyote ile tunakumbuka maskini na walio wadogo kwa kila hali! Katika maisha yetu ya kila siku kama wanakanisa hatuna budi kukumbuka na kutenga nafasi kwa ajili ya wale wanaokuwa wanyonge na maskini. Leo katika mapambano dhidi ya COVID-19 iko wapi nafasi ya maskini wasiokuwa na makazi wala uwezekano wa kupata mkate wa kila siku, ni makundi yanayokuwa katika hatari kubwa ya kupoteza uhai wao kwa hatari za kirusi Corona. Je, ni mara ngapi tunawakumbuka hawa iwe ni jirani zetu mtaani, kijijini au mijini mwetu?

Yesu angeweza kuepa kifo chake pale Msalabani kwa kuzima miale ya mwanga wake. Angejikalia kimya kuepusha shari! Angekubaliana na fikra na mitazamo ya wengine tu! Labda hata nasi leo mara ngapi tunaepuka shari kwa kuacha kuangaza kwa maisha yetu uzuri wa Injili/ Habari Njema? Masimulizi ya Mateso ya Yesu kama yalivyoandikwa na kusimuliwa na Mwinjili Yohane tunaona tangu mwanzoni mwa kukamatwa kwake pale Bustani ya Getsemani, tofauti na Wainjili wengine wanaotuonesha kuwa Yesu alikuwa na huzuni kubwa kiasi cha kufa na hivyo kuwaalika wanafunzi wake kukesha naye katika sala na badala yake anatuonesha kuwa Yesu alikuwa na utulivu na kuonekana kujua mwisho wa hatima yake. Hivyo Mwinjili Yohana anatuonesha sio maaskari wanaomkamata Yesu bali ni yeye mwenyewe anajikabidhi kwa watesi wake. Hivyo Yesu kwa ujasiri na utulivu anawaambia watesi kuwa ‘’Mimi ndimi’’ (Yohane 10:17-18). ‘’Mimi ndimi’’ katika Maandiko ni utambulisho wa Mungu, Mungu ambaye yupo, ndio uwepo wenyewe. Mwinjili Yohana anatualika kuelewa kukamatwa kwake Yesu kwa kuongozwa na Zaburi ya 9:4 na ile ya 27:2.

Wakati Injili Pacha zinatuonesha baada ya kukamatwa kwa Yesu anapelekwa katika nyumba ya kuhani mkuu Kaifa. Ni hapo wazee na waandishi wanajadiliana usiku mzima jinsi ya kutoa mashitaka yao mbele ya Ponsio Pilato. Yohana anatupa picha kidogo tofauti na hiyo. Yohana anatuonesha kuwa majadiliano yalifanyika mbele ya Anna, mkwe wa Kaifa. (Yohane 18:12-24) Anna aliwahi kuwa Kuhani mkuu na hata baada ya kumaliza muda wake alibaki kuwa ni mtu mwenye nguvu kimaamuzi na ushawishi. Hivyo alikuwa ni mzee wa familia na mwenye ushawishi mkubwa katika mambo yahusuyo hekaluni. Ni yeye aliyehusika na uangalizi wa sadaka pale hekaluni, wabadili fedha, wauzaji wa wanyama walionunuliwa ili kutolewa sadaka ya damu. Kitendo cha Yesu kuwafukuza Hekaluni wabadili pesa tunaona ni kuhatarisha uchumi wa familia ile. Hivyo Anna anabaki kuwa ni ishara ya uongozi wa dini uliokuwa kinyume na Yesu mgalilaya, mwana wa mselemala. Hivyo Mwinjili Yohana anamtumia Anna kuwakilisha wale wote waliokuwa kinyume na Yesu mintarafu dini. Wale wote wanaotumia dini kwa ajili ya manufaa yao binafsi, labda nasi leo hapo tunajiuliza Je tunakubali kupokea mwaliko wa Yesu hata ikiwa unagusa usalama wa uchumi wetu?

Katika mahojiano Yesu anamjibu bila uoga, kwa nini waniuliza mimi, waulize wale waliosikia mafundisho yangu. (Yohane 18:21) Mmoja wa watumishi wake anampiga kofi Yesu kwa kumjibu hivyo kuhani mkuu. Tunaona bado kuna utulivu mkuu kwa upande wa Yesu na anawaalika waonesha kama amefanya ubaya wowote. (Yohane 18:23) Ndiyo hali tunayoalikwa kuwa nayo hata nasi wanafunzi wa Yesu hasa pale tunapotendewa kinyume na haki bila kosa lolote. Mtumishi huyu anatumika kama kibaraka kulinda masilahi ya bwana wake, ni kielelezo kwangu na kwa kwako ni mara ngapi hata bila kuwa na ufahamu wa jambo na hasa ukweli wake tunachukua upande kwa kulinda masilahi yetu na hasa kwa kutetea masilahi ya wakubwa wetu? Ni mara ngapi tunajitoa kupigania wakubwa wa ulimwengu huu kwa madai ya kutetea dini au uzalendo na kujikuta tukimpiga kofi Yesu, tutafakari!

Mwinjili Yohane anatusimulia kwa marefu sana zaidi ya Mwinjili   Marko Yesu akiwa mbele ya Pilato. Mwinjili Yohane anatuonesha kwa msisitizo mkubwa kabisa jinsi Pilato, mtawala wa Kirumi alivyokuwa anaingia na kutoka ndani ya Praetorio. Ni kwa sababu za kidini wayahudi hawapaswi kuingia katika nyumba ya mpagani kwani kufanya hivyo wangenajisika na wao walikuwa wapo wanajiandaa na Sabato ya Kiyahudi. Mwinjili Yohane anatoa msisitizo hapa ili kukazia Ufalme wake Yesu. Tunakutana na wahusika mbali mbali mbali ya muhusika mkuu Yesu tunakutana na Pilato, wayahudi, maaskari, Barabba. Na lengo la Mwinjili ni kuhusu Ufalme wa Yesu. Pilato anawakilisha ufalme wa ulimwengu huu kinyume na ule wa Yesu. Ni mfano wa yule anayeamini katika madaraka yake kiasi hata ya kumtoa mtu sadaka ikiwa sheria inataka hivyo, mmoja anayelinda sheria zisizo na haki. Labda hata nasi leo ni mara ngapi tunakumbatia sheria zinazokiuka na kwenda kinyume na utu wa mwanadamu, na hata pengine kuzitetea na kuzipigania?

Wayahudi hawa ni wawakilishi wa wale wote wasikuwa tayari kubadili vichwa vyao mintarafu sura halisi ya Mungu. Ni wale wanaoamini katika Mungu anayeshinda kwa kutumia nguvu na si kwa upendo, hivyo hawapo tayari kumpokea mfalme aliye mpole na mwema. Maaskari hawa ni wawakilishi wa wale wote wanaokumbwa kwa bahati mbaya na kwa ujinga wao katika makosa. Wapo mbali na nchi yao na familia zao na hata kudhalilishwa huku wakikubali kuuvua ubinadamu na kuuvaa unyama kwa ajili ya kulinda matakwa ya watawala. Ni wale wanaoamini katika nguvu za mabavu na si utashi na upendo kwa jirani. Hapa pia tuna mifano mingi hata katika nchi na taifa letu ambapo vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinapokiuka haki za watu kwa kuwapiga na kuwadharirisha, wakristo tupo wapi au nasi tunaona sawa na kukubaliana na udhalilisha na uonevu wa wale wanaokuwa wanyonge na wadogo?

Barabba jina lake likiwa na maana ya “mwanaharamu”, mwana asiye na baba anayejulikana. Ni mwalifu, ni mwana wa yule muovu, ni mwakilishi wa wale wote wanaofanya ukatili mkubwa katika historia ya mwanadamu lakini kuna nyakati wanaonekana kuwa ni watu hodari na majasiri wa kuigwa. Baada ya kuangalia wahusika mbali mbali sasa tuone pia muda wa matukio haya.  Ilikuwa alfajiri (Yohane 18:28), ni mwanzo wa siku mpya, ndio jua linaanza kuangaza tena dunia baada ya kuisha kwa giza la usiku ule ambao Yuda Iskariote alitoka pale kwenye chumba cha kalamu ya mwisho na kwenda kumuuza Yesu. Yuda anatoka na kwenda kwa wakuu wa wayahudi usiku, wakati wa giza. Pia ni usiku maaskari wanafika kumkamata Yesu pale bustani, ni usiku tunaona Petro anamkata sikio kijakazi wa kuhani mkuu, usiku pia Kaifa na Anna wanafanya mashauri ya kumshitaki Yesu, na hata usiku tena Petro anamkana Yesu mara tatu. Hatimaye giza la usiku ule linaishia kwa kuanza kwa siku mpya. Mwanga na nuru ya mchana unaleta matumaini mapya.

Ilikuwa mchana wa saa 6 (Yohane 19:14) Ni mchana wa jua kali ndipo Pilato atatangazwa ukweli wa imani: Mwangalieni mfalme wenu (Ecce Rex vester) Katika sura hizi mbili yaani ya 18 na 19 Mwinjili Yohane anatumia neno mfalme kumuhusu Yesu mara 12. Mwinjili Yohane pia anatupa pia ishara ya ufalme wa Yesu nazo ndio taji la miiba, vazi la zambarau na pia kukiri kwa Pilato kuwa Yesu ni mfalme wa wayahudi. Yesu mwanzoni aliyehoji kofi la kijakazi wa Anna tunaona hapingi wala hahoji ufalme wake unaotamka na Pilato. Anakiri kuwa yeye kweli ni mfalme ila ufalme wake sio kwa mantiki ya ulimwengu huu, kutawala kwa mabavu na kujichukulia nafasi ya heshima. Mtu kweli na mfalme kweli ni yule anayejitoa sadaka kwa ajili ya huduma kwa wengine! Kadiri ya mantiki ya ulimwengu huu, Yesu anaonekana kuwa ameshindwa na hasa katika wakati huu wa mashitaka na mateso na kifo chake. Yesu anapoteza sifa ya kuwa jembe, kuwa jiwe, kuwa mpambanaji wa kweli, kuwa mwanaume wa shoka asiyekubali kushindwa kirahisi.

Yesu anabaki pale kimya hajibu neno wala hasemi kitu, hajitetei mwenyewe, anaonekana kushindwa na watesi wake. Yesu anabaki na kuonekana dhaifu kabisa. Yesu dhaifu mbele ya Pilato, mbele ya wayahudi na maaskari! Mwinjili Yohane anatueleza kwa ufupi kabisa safari ya Yesu kuelekea Kalvario. Yesu anachukua msalaba wake na kupanda kwenye Kalvario. (Yohana 19:17) Hatusikii juu ya wanawake wanaomlilia wala Simone wa Kirene anayemsaidia kubeba Msalaba. Wakati wa mateso yake Mwinjili Yohane kinyume na Wainjili Pacha anatupa tena baadhi ya kweli ambazo hatuzisikii kwa Wainjili wengine. (Yohana 19:18-37). Anwani iliyoandikwa juu ya msalaba wake kuonesha aina ya mashitaka yake. Anwani hii iliandikwa kwa lugha tatu yaani Kiebrania (Lugha takatifu ya Wayahudi), Kilatini (Lugha ya watawala wa kirumi), Kigiriki (lugha ilyoongelewa katika sehemu kubwa ya himaya ya Kirumi, hii ni lugha ya Wasomi na wana zuoni!)

Bila kufahamu Pilato anafanya unabii unaobaki na kudumu siku zote kuwa hakika Yesu ni Mfalme wa Wayahudi na Mfalme wa Ulimwengu mzima sasa na hata milele. Baada ya Yesu kusimikwa katika kiti chake cha ufalme yaani pale juu msalabani nini kinajiri? Mwinjili Yohana hatuambii juu ya matusi dhidi ya Yesu kutoka kwa wapita njia, makuhani wakuu, waandishi na wazee. Ni kwa sababu moja tu kuwa Yesu ni mfalme kweli hata kama ni ujinga kwa wayunani na makwazo kwa wayahudi. (1 Wakorintho 1:23) Ukweli unabaki daima iwe unapokelewa au unapingwa. Ni ukweli kwa wenyewe hivyo hautegemei mimi na weye bali unasimama na kuangaza daima. Na ndio maneno niliyoanza nayo tafakari yetu ya leo kuwa pale juu msalaba tunakutana mwanga wa mfalme wa ulimwengu huu. Ni fumbo la upendo na huruma ya Mungu kwetu wanadamu, hivyo tunabaki na mshangao mkubwa tunapoutafakari wema na huruma ya Mungu kwetu wadhambi na dhaifu, anakubali kubeba dhambi na udhaifu wetu ili sisi tuweze kupata wokovu. Tunakiri ‘’fulget crucis mysterium’’!

Yohaea Mwinjili anatueleza kuwa joho lake waliligawa katika sehemu nne na ndio kusema ukombozi wake ni kwa ulimwengu mzima. Katika ulimwengu wa nyakati za Yesu joho pia linabeba nafsi ya mtu mwenye nalo, kazi zake, tabia yake na hata namna ya kuhusiana na wengine. Na ndio tunaona hata siku ya ubatizo tunavalishwa vazi jipya, vazi jeupe likimaanisha cheo chetu kipya cha kufanyika wana wa Mungu. Ni kumvaa Kristo mwenyewe, msulubiwa na anayekufa pale juu msalabani lakini tunafufuka naye. Pale Msalabani pia Mwinjili Yohane anatuambia alikuwepo Mama yake na Yesu. Uwepo wa Mama yake pale chini ya Msalaba ni ukweli unaokuwa mgumu kuuelezea kiuhalisia kwa sababu nitakazojaribu kuzitaja hapa chini. Mwinjili Marko anaonesha kuwa kulikuwepo wanawake waliosimama kwa mbali na anawataja kwa majina na hataji uwepo wa Maria wala wa Yohane. Sheria ya Kirumi pia ilikataza uwepo wa ndugu wa karibu karibu na eneo la kutesea washitakiwa na hata kwa fikra za kawaida wanawake wale wasingeruhusu Maria kuwepo katika mazingira yale ya mateso makali kabisa kwa mwanae. Ni mama gani anaweza kusimama na kushuhudia dhulma ile na ukatili usio kifani kwa mwanae? Hili kwetu linaendelea kubaki fumbo katika maisha na utume wa Bikira Maria, mwanafunzi mwaminifu wa Kristo Yesu!

Hata hivyo tunaona Yesu hamuwiti mama bali mwanamke kama alivyotamka katika sherehe za harusi ya Kana ya Galilaya. Na kwa kadiri ya tamaduni za Kiyahudi hakuna mtoto angeweza kumwita mama yake bimkubwa (kwa kweli kwa tafsiri sahihi ni mwanamke – ‘’Mulier, ecce filius tuus – Γυναι, ιδε ο νιος σου.’’ Neno la Kigiriki ‘’Lunai’’ linamaanisha Mwanamke (Woman). Hivyo lazima kupata maana ya maneno haya kwani Mwinjili kwa hakika hakuwa na maana ya uwepo wake wala wa mama yake.  Najua mara nyingi wahubiri wengi wanaelezea uwepo halisi wa Maria, Mama wa Yesu na Yohane kama mfuasi aliyependwa na Bwana. Kwa Mwinjili Yohane, Mama ni lugha ya picha inayoashiria Israeli mwaminifu kwa Mungu. Katika Biblia Israeli ni bikra, mchumba na mama. Ni kutoka katika taifa hili sasa linazaliwa taifa jipya la Kimasiha. Hivyo Yesu anaalika kwanza taifa la Israeli kama watangulizi wa kupokea ahadi za Mungu kumpokea yeyote katika taifa hilo la kimasiya. Na pili anageukia kwa ile jumuiya mpya inayowakilishwa na yule mwanafunzi aliyependwa ili kumpokea mama Israeli ambapo kwayo imezaliwa na ndio kuona misingi ya imani kuanzia Agano la Kale kutoka kwa wale waliopokea awali ahadi za Mungu.

Kadiri ya Mwinjili Yohane tunaona kifo chake Yesu kinajiri kwa utulivu na ukimya mkubwa. Mwinjili Yohana haoneshi ishara za kutisha kama kulia kwa sauti pale juu Msalabani, tetemeko la nchi, au giza juu ya sura ya nchi. Mwinjili Yohana katika simulizi la mateso na kifo cha Yesu ni tofauti na simulizi tulilolisikia katika Dominika ya matawi kutoka Mwinjili Mathayo. Yesu pale juu Msalabani anakamilisha misheni yake ya kuja kutufunulia kikamilifu juu ya sura halisi ya Mungu yaani Mungu aliye upendo na mwingi wa huruma. Naona kiu, ni maneno anayotamka pale juu msalabani akionesha kiu na hamu na tamaa yake ya kuupa ulimwengu maji ya uzima kama alivyomwambia mwanamke msamaria pale kisimani. Ni kiu ya Yesu pale msalabani kuwa ulimwengu mzima hatuna budi kwenda kwake ili nasi tuweze kushiriki pamoja naye maisha mapya ya kuwa wana wa Mungu. Kiu yake sasa inakamilika pale juu msalabani, yaani kutukumboa kwa kutupatanisha na Mungu Baba. YAMETIMIA ni maneno anayotamka kumaanisha ukamilifu wa misheni yake, na ndio kukidhi kiu ya ulimwengu, maji ya uzima yenye kumaliza kiu ya mwanadamu, maji yaliyo chanzo cha uzima wa kweli, yanayowafikia wale wote wanaokuwa tayari kukaribia Msalaba wa Yesu.

Huu mti wa Msalaba ambao juu yake umetundikwa wokovu wetu. Baada ya kifo cha Yesu yote yamekamilika na Yesu anaikabidhi roho yake mikononi mwa Baba yake.  Ni katika Maandalio ya Pasaka Mwinjili Yohane anatuonesha kuwa amechinjwa, ametolewa sadaka, Mwanakondoo wa Pasaka. Kwa kumwaga damu yake azizi, Yesu anatukomboa kutoka katika utawala wa yule mwovu kwa kutuacha huru ili nasi tushiriki maisha mapya yaani kuishi kwa kuongozwa na Neno la Mungu. Mwinjili Yohane pia anatuonesha kuwa Askari mmoja anachoma ubavu wake kwa mkuki na humo inatoka damu na maji. Damu kwa wayahudi ni ishara ya uzima, hivyo kumwagika mpaka tone la mwisho ni sawa na kutoa uhai wake. Ni kwa kutoka maji ishara ya kumiminwa kwa Roho yake.  Mwili wake wanaupaka manukato ya gharama kubwa na hii yote ni kuashiria kuwa huyu kweli ni mfalme maana hawakutumia manukato ya kupaka maiti bali manukato yaliyotumika kupaka maharusi kama alivyofanya Maria dada wa Lazaro pale Betania, walimpaka Nardo yenye harufu nzuri. Ni kumtambua kama Kristo, Mpakwa mafuta wa Mungu.

NB: Niwakumbushe na kuwasisitiza wahubiri wenzangu kuwa lengo na shabaha ya Injili sio kugusa hisia zetu kwa kusisitiza ukatili na mateso ya kimwili kwani kama ni hilo basi Injili inakoma kuwa Habari Njema na kuwa sawa na vitabu vya masimulizi ya kihistoria, kila mara hatuna budi kusisitiza ujumbe kusudiwa na kwa leo ndio Upendo na Huruma ya Mungu kwa mwanadamu mdhambi na dhaifu. Ni pale msalabani tunaalikw akuutafari upendo wa Mungu kwetu na si kuishia tu kuona mateso na ukatili aliofanyiwa Yesu na wakuu wa makuhani na maaskari. Nawatakia Maadhimisho mema ya Fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.

09 April 2020, 17:41