Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Ujumbe wa Pasaka 2020: Ugonjwa wa Corona na Uchaguzi Mkuu 2020. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Ujumbe wa Pasaka 2020: Ugonjwa wa Corona na Uchaguzi Mkuu 2020. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Ujumbe wa Pasaka 2020

Hii ni fursa kumrudia Mungu na kusimama imara katika imani. Kuomba neema ya kuwa na moyo wa ibada na uchaji. Pamoja na hayo, wapendwa, kipindi hiki cha maadhimisho ya Sherehe za Pasaka ningependa kusisitiza mambo mawili muhimu kwa nafasi hii ya salamu: Ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID- 19 pamoja na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Na Askofu Antony Lagwen wa Jimbo la Mbulu, - Mbulu, Tanzania.

Wapendwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Leo waamini Wakristo tumeadhimisha kwa furaha Sherehe ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, yaani Pasaka kama wengi tulivyozoea kuiita. Ninapenda kuwatakia waamini Wakristo na Watanzania wote heri na Baraka za Mwenyezi Mungu katika siku hii na wakati wote wa Sherehe za Pasaka. Aleluya, Bwana amefufuka kweli kweli, tufurahi na kushangilia.Tuungane na Malaika kuimba utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema. Sherehe ya Pasaka ni kubwa mno katika historia ya ukombozi wanadamu. Ni siku takatifu inayofunua kwetu Nuru na Ushindi wa Mungu, ambayo ni furaha na amani ya roho. Ni Nuru inayoangaza akili na mioyo ya wanadamu yenye giza la dhambi na kuijalia mwanga baada kutubu na kuamini.

Pasaka ni adhimisho la ushindi wa Kristo unaolenga ukombozi wa wanadamu, Kristo aliteseka na hata kufa Msalabani na baada siku tatu akafufuka. Huu ni uthibitisho wa  uwezo wa Mungu usioweza kufungwa na mipango ya binadamu.  Uwezo wa Mungu daima unashinda yote, Kristo ameshinda dhambi ambayo matokeo yake ni mauti na kutujalia wanadamu uwezo wa kushinda hayo na kupata uzima mpya, uzima wa neema. Kauli ya kuvuka bahari inayotumika katika Maandiko Matakatifu mfano katika Kitabu cha Kutoka: Sura ya 12: inaashiria mabadiliko yanayoletwa na Mungu kwa mwanadamu anayezingatia maongozi yake, hasa anayeamini na kutubu kwamba atamvusha katika bahari ya mahangaiko ya dunia. Atamjalia matumaini mapya, upendo na amani katika ukamilifu wake.

Kwa hiyo wapendwa watanzania adhimisho hili liwe fursa ya kutafakari mahusiano yetu na Mungu na hata na Wenzetu, na kuona kama yanaleta matumaini mapya, na mabadiliko yanayoweza kulinganishwa na ufufuko. Hii ni fursa kumrudia Mungu na kusimama imara katika imani. Kuomba neema ya kuwa na moyo wa ibada na uchaji wa Mungu zaidi. Pamoja na hayo, wapendwa, kipindi hiki cha maadhimisho ya Sherehe za Pasaka ningependa kusisitiza mambo mawili muhimu kwa nafasi hii ya salamu: Ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID- 19 pamoja na Uchaguzi Mkuu mwa mwaka 2020.

Dunia yetu inasherekea Pasaka, msingi wa imani yetu Wakristo mwaka huu, 2020 ikiwa inapitia mazingira magumu yaliyosababishwa na ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Suala hili limekuwa janga kwa dunia. Tatizo lilianza na nchi mmoja na baadaye kusambaa kwa haraka katika nchi nyingi duniani kwa viwango tofauti, (wengine kiwango kikubwa sana, kikubwa wastani, kidogo) ikiwepo nchi yetu ya Tanzania kutokana na mwingiliano wa huduma na shughuli za kibinadamu. Ugonjwa umetisha dunia kwa maambukizi na idadi ya vifo kwa baadhi ya nchi wakiwemo wataalamu, wahudumu wa afya na wa kiroho. Tumeguswa wote kama familia nzima ya wanadamu bila kujali bara, nchi, rangi, n.k. elimu, uchumi, teknolojia, mazingira nk, wote tumekosa amani kwa sababu ya ugonjwa huu, wakati mwingine tumekaa bila matumaini... tumejaa hofu. Juhudi za pamoja za kitaalamu kuhusu namna ya kukinga virusi na kutibu kabisa ugonjwa kwa dunia nzima zinaendelea…Pengine tunajiuliza msaada wetu utatoka wapi?

Wapendwa Watanzania: Msaada wetu utatoka kwa Mungu tu, (Zab. 121: 1-2) yeye aliyeumba mbingu na dunia. Mosi, ni yeye tu anaweza kuondoa tishio hili na kuturudishia amani. Kwa hiyo tuungane kama familia ya Mungu hapa Tanzania kwa sala. Tumwombe Mungu atukinge, atuondelee kabisa janga hili –ili tuwe salama, tupate amani na utulivu tunaohitaji.  Pamoja na hayo msaada wa Mungu tuupe ushirikiano kwa kuwajibika kwetu. Pili, tuzingatie maelekezo yote yaliyotolewa na Shirika la Afya Duniani, WHO, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wadau wengine wote wenye nia njema kama tahadhari kujikinga na maambukizi ya virusi hivyo. Huu ni ushirikiano muhimu tunaoweza kuutoa kwa ajili ya usalama wetu.

Jambo la Pili: Uchaguzi mkuu 2020. Kama tunavyofahamu mwaka huu nchi yetu ya Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Hili ni tukio muhimu sana linalogusa maisha ya watanzania wote. Hivyo basi tunawasihi watanzania kushiriki inavyopasa kwa kadiri ya nafasi zetu kutayarisha mazingira mazuri ya kufanyika zoezi hili kwa kuzingatia misingi iliyo huru na ya haki ambayo matunda yake yatakuwa amani. Kila anayehusika mfano anayeratibu, anayetaka kuchaguliwa, anayepiga kura, anayesimamia, anayehesabu kura n.k awe mwaminifu, aongozwe na dhamiri safi. Tutumie haki yetu ya kugombea nafasi mbali za uongozi kadiri ya vigezo vilivyopo kwa mujibu wa sheria za uchaguzi. Pia tutumie haki ya kuchagua kwa uhuru viongozi tunaotaka wachukue dhamana ya kuiongoza nchi yetu. Tuwachague viongozi tunaowataka sisi watanzania siyo wanaojileta wenyewe, kwa tamaa ya madaraka bila uwezo, kwa njia ya rushwa na ambao baadaye inawezekana wakaendekeza rushwa na ufisadi.

Viongozi tutakaowachagua wawe ni wale wanaomcha Mungu, sio wanaotegemea udanganyifu wa nguvu zao, wenye fikra za upuuzi kama ushirikina n.k. Ukweli ni kwamba viongozi wanaochaguliwa kwa uhuru, haki na usawa kwa kadiri ya matazamio ya wote ni wa mpango wa Mungu kwani Sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. (War.13:1ff) ... Wenye mamlaka wamewekwa na Mungu. Wawe ni watu wanaojali na kutanguliza maslahi mapana ya nchi yetu siyo wenye tabia ya ubinafsi na ubaguzi wa aina yoyote. Kwa ujumla tunahitaji viongozi waungwana, waliopambwa kwa fadhila njema za kimungu na wenye kuheshimu tunu muhimu za kijamii za kujali ukweli, uhuru, haki na usawa kati ya raia wote. Tuishi na kuwajibika kwa upendo kulinda, kutunza na kuiombea amani ya nchi yetu. Neema na Baraka za Mungu tunazotakiana wakati huu Pasaka zitusaidie.

Ninawatakia tena heri na Baraka za Pasaka. Mwenyezi aibariki nchi yetu.

Katika Kristo,

+ Antony Lagwen

Askofu wa Jimbo la Mbulu.

12 April 2020, 14:40