Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linawashukuru na kuwapongeza Mapadre kwa ushuhuda wa huruma na upendo katika kipindi hiki cha Janga la ugonjwa wa Corona-covid-19 Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linawashukuru na kuwapongeza Mapadre kwa ushuhuda wa huruma na upendo katika kipindi hiki cha Janga la ugonjwa wa Corona-covid-19 

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina: Ushuhuda wa Upendo wa Mapadre

Katika shida, mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu, Mapadre wameendelea kuonesha uwepo wao wa dhati kati pamoja na watu wa Mungu. Wamekuwa wakisadaka maisha yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wameshuhudia watu wakifariki dunia kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Huu ni ushuhuda wa upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kama binadamu Mapadre wanatambua udhaifu na uwepo wa dhambi katika maisha yao, changamoto kubwa mbele yao ni kutubu na kuongoka, ili kuanza hija ya utakatifu inayokita mizizi yake katika mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu. Mapadre wanapaswa kuwa ni wachungaji wema, kwa mfano wa utakatifu wa maisha yao, wawasaidie waamini walei kuiona njia ya hija ya utakatifu wa maisha, kwa kukazia umoja, maisha ya kisakramenti, kazi na utume wa mashirika na vyama mbali mbali vya kitume parokiani, bila kusahau, nidhamu na wajibu wa kila mwamini. Uaminifu wa Mapadre na walei uwawezeshe kuuona utakatifu, kwa njia ya maisha ya Sakramenti, liturujia na sala, kila upande ukijitahidi kutekeleza wajibu wake. Katika Maadhimisho ya Miaka 160 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Yohane Maria Vianney, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Mapadre wote duniani, barua ya upendo na mshikamano wa kibaba, akiguswa na furaha ya huduma inayotolewa na Mapadre sehemu mbali mbali za dunia, kila kukicha!

Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina katika Waraka wake wa Kichungaji, linawashukuru Mapadre kwa ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo wanayoendelea kuwaonesha watu wa Mungu ndani na nje ya Argentina. Ukuu, uzuri na utakatifu wa maisha na utume wa Kipadre unapata chimbuko lake katika maisha ya: Sala, Tafakari, Sakramenti, Sadaka na Huduma ya Upendo kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Argentina. Katika shida, mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu, Mapadre wameendelea kuonesha uwepo wao wa dhati kati pamoja na watu wa Mungu. Wamekuwa wakisadaka maisha yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wameshuhudia watu wakifariki dunia kwa ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Hata Mapadre wameguswa na kutikiswa na janga hili kwa baadhi yao kufariki dunia;  kuondokewa na Mapadre wenzao, wanaparokia na hata ndugu na jamaa zao wenyewe. Wameonesha ujasiri kwa kuambatana daima na wafanyakazi katika sekta ya afya kwa ajili ya huduma kwa wagonjwa na wale wote waliokuwa kufani! Wamewatembelea na kuwafariji wazee! Kwa Mapadre walioambukizwa Virusi vya Corona, COVID-19 walijitenga kwa ridhaa “Self isolation” na kuachia itifaki dhidi ya Virusi vya Corona, ishike mkondo wake. Maaskofu wanawashukuru, wanawapongeza na kuwatia shime Mapadre kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu licha ya hali ngumu ya uchumi wanayokabiliana nayo kwa wakati huu! Waraka wa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina unaongozwa na kauli mbiu “Watulizeni mioyo, watulizeni mioyo, watu wangu asema Mungu wenu”.

Kwa hakika Mwenyezi Mungu anawatuliza na atawaokoa watu wake kutoka katika Janga la homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu Francisko anasema mashujaa wa kweli wanaanza kuonekana kila kukicha! Hawa si watu wanaotaka kujikweza wala “kujimwambafai”, hawatafuti fedha wala mafanikio, bali ni watu wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina linasema, kwa hakika Mapadre hawa wamelisimamisha Kanisa kwa njia ya ushuhuda wao; wakaonesha uhalisia wa maisha na utume wa Kikasisi; kwa kukuza na kuendeleza ari na mwamko wa kimisionari; kama faraja, huruma na upendo wa Mungu kwa wagonjwa na wale wote walioko kufani!

Kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, Mapadre wamewasaidia watu wa Mungu kukuza na kuimarisha imani yao kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Mapadre wamekuwa ni vyombo vya huruma na faraja kwa maskini, wagonjwa, wazee na walemavu, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao. Hawa ni vyombo na mashuhuda wa utu wema, udugu wa kibinadamu, upendo na mshikamano wa watu wa Mungu. Maaskofu Katoliki Argentina wanakiri kwamba, upendo huu wa Kipadre ni matunda ya mshikamano kati ya Wakleri na watu wa Mungu katika ujumla wao; upendo unaofumbatwa katika sadaka na huduma makini. Katika maadhimisho ya Juma Kuu, Mapadre wameonesha kipaji cha ubunifu wa hali ya juu kwa kugeuza makazi yao kuwa ni Makanisa madogo ya nyumbani, mahali pa sala, tafakari na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Hii ndiyo nguvu ya Mwenyezi Mungu inayoyofunika huduma wanayoitoa hata kama wakati mwingine, wametumbukia katika ubinafsi wao.

Kuhusu mateso: Baba Mtakatifu Francisko katika Barua yake kwa Mapadre Wote Duniani anasikitika kusema kwamba, katika miaka ya hivi karibuni mapadre wamekuwa wasikivu kwa kilio na mateso ya ndugu zao na wakati mwingine katika hali ya ukimya. Hawa ni watu waliokumbwa na nyanyaso za kijinsia zilizosababishwa na matumizi mabaya ya madaraka. Wahanga, familia pamoja na watu wote wa Mungu katika ujumla wao, wameteseka sana. Kanisa limedhamiria kujikita katika utamaduni wa shughuli za kichungaji kwa kukazia mfumo wa kukinga ili kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto kwa watu wote wa Mungu kuwajibika barabara. Baba Mtakatifu anakazia wongofu wa ndani, ukweli na uwazi sanjari na mshikamano kwa waathirika wa nyanyaso za kijinsia. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kujenga utamaduni wa kuwa sikivu kwa shida na mahangaiko ya walimwengu.

Shukrani kwa Mapadre: Baba Mtakatifu anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wito wa Upadre kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ambao si kwa mastahili yao wenyewe, bali wameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kipindi cha shida na magumu ya maisha, iwe ni fursa ya kurejea tena katika zile nyakati angavu za sadaka na huduma kwa watu wa Mungu, ili kugundua tena neema za Mungu katika maisha na utume wao, ili kuwasha tena furaha inayokita mizizi yake katika unyenyekevu, ili kamwe majonzi na uchungu wa moyo, yasizime ile furaha na uungwana! Huu ni wakati wa kusimama tena na kusema, Mimi hapa Bwana, nipe nguvu ya kusimama tena ili nitoe huduma kwa watakatifu majirani; tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Mapadre wazee wagundue tena ndani mwao, ile furaha waliyokuwa wanapata walipozitembelea familia za Kikristo; walipokuwa wanakwenda kutoa Sakramenti za Kanisa kwa wazee na wagonjwa.

Neno la Faraja kwa Mapadre: Baba Mtakatifu anataka kuwafariji Mapadre wote ili kupyaisha tena ari na moyo wa kipadre, ambao ni matunda ya Roho Mtakatifu anayetenda kazi ndani mwao. Katika shida, magumu na changamoto za maisha, kuna haja ya watu kufarijiana na kutiana shime, ili kuweza kuzipokea changamoto hizi kwa unyenyekevu na kutoa nafasi kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kuzigeuza na kuzitumia kadiri anavyotaka, mambo yanayosimikwa katika sala pamoja na kutambua udhaifu wa kibinadamu. Mapadre kama wachungaji wachunguze ndani mwao, jinsi ambavyo wanakabiliana na mateso yanayowasonga katika maisha na utume wao! Je, ni watu wanaothubutu “kufunika kombe, ili mwana haramu apite? Je, ni watu wanaokimbia matatizo na changamoto za maisha?

Baba Mtakatifu Francisko anasema, mwelekeo huu wa maisha unaweza kupachikwa majina mengi kama vile: Ubinafsi, upweke hasi pamoja na hali ya mtu kujifungia katika undani wa ulimwengu wake. Madonda ya maisha na utume wa Mapadre, yawasukume kukimbilia ili kugusa Madonda Matakatifu ya Yesu, chemchemi ya huruma, upendo na faraja ya Mungu kwa watu wake! Kamwe Mapadre wasikubali kukata wala kukatishwa tamaa, bali waonje uwepo mwanana wa jirani zao, ili wasitumbukie katika upweke hasi unaoweza kuwatumbukiza hata katika kifo! Uchungu wa moyo utawanyima Mapadre kutekeleza utume wao kwa ari na moyo mkuu; watashindwa kuona umuhimu wa sala na hapo kwa hakika maisha yatakuwa ni magumu na machungu sana!

Utukufu na Ukuu wa Mungu: Baba Mtakatifu anasema,  anaendelea kumshukuru Mungu kwa ajili ya Mapadre wanaojisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Ana uhakika kwamba, Mwenyezi Mungu atawarejeshea tena matumaini pamoja na kuwaondolea kizingiti cha maisha ili kukutana na Kristo Yesu, Jiwe hai, aliyefufuka kwa wafu. Kristo Yesu ni msingi wa Kanisa lake yuko tayari kupyaisha Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Mapadre waendelee kuwa ni vyombo vya shukrani, kwa kupyaisha ari na mwamko wa shughuli za kichungaji, ili kuwapaka watu wa Mungu mafuta ya matumaini; sanjari na kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Maaskofu Argentina

 

29 April 2020, 13:48