Tafuta

Vatican News
Askofu mkuu mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki wa Jimbo kuu la Nairobi aliyeafriki dunia tarehe 30 Machi 2020 atazikwa tarehe 7 Aprili 2020 kwenye Kanisa kuu la Familia Takatifu, Nairobi. Askofu mkuu mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki wa Jimbo kuu la Nairobi aliyeafriki dunia tarehe 30 Machi 2020 atazikwa tarehe 7 Aprili 2020 kwenye Kanisa kuu la Familia Takatifu, Nairobi.  (ANSA)

Marehemu Askofu Mkuu Ndingi Mwana a'Nzeki kuzikwa 7 Aprili 2020

Askofu mkuu mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki alizaliwa tarehe 25 Desemba 1931 huko Mwala, Machakos nchini Kenya. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi nchini Tanzania, akapewa daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 31 Januari 1961. Akawa Askofu wa kwanza mzalendo kuwekwa wakfu nchini Kenya kunako tarehe 31 Januari 1969: Motto: “Mwamini Mungu si mtovu”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linasikitika kutangaza kifo cha Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki wa Jimbo kuu la Nairobi, kilichotokea hapo tarehe 30 Machi 2020, baada ya kuugua kwa muda mrefu, hali iliyochangiwa pia na uzee. Amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 88. Mazishi ya Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki yanatarajiwa kufanyika Jumanne, tarehe 7 Aprili 2020 kwenye Kanisa kuu la Familia Takatifu Jimbo kuu la Nairobi. Kutokana na janga la ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID, -19, kutakuwepo na idadi ndogo sana ya waamini watakaoshiriki katika Ibada ya mazishi ili kuzingatia itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19.  

Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki alizaliwa tarehe 25 Desemba 1931 huko Mwala, Machakos nchini Kenya. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi nchini Tanzania, akapewa daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 31 Januari 1961. Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki ndiye Askofu wa kwanza mzalendo kuwekwa wakfu nchini Kenya kunako tarehe 31 Januari 1969, wakati wa hija ya Mtakatifu Paulo VI, Barani Afrika. Motto yake ya Kiaskofu ilikuwa: “Mwamini Mungu si mtovu”. Hii ikawa ni dira na mwongozo wake wa maisha. Katika maisha na utume wake, amewahi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Machakos kuanzia mwaka 1969-1971; Jimbo Katoliki la Nakuru kuanzia mwaka 1996-1997.

Baadaye Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi wa Jimbo kuu la Nairobi na kusimikwa rasmi tarehe 21 Aprili 1997. Tarehe 6 Oktoba 2007 Askofu mkuu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki akang’atuka kutoka madarakani. Daima amejitambulisha kuwa ni Baba wa wote, mtumishi mwaminifu wa watu wa Mungu nchini Kenya, kiongozi mwenye msimamo katika maisha yake! Alijitahidi kusimama kidete katika misingi ya imani, kanuni maadili na utu wema. Alipigania haki, amani, umoja wa kitaifa dhidi ya siasa na sera za ubaguzi wa kikabila sanjari na demokrasia nchini Kenya.  Ndiyo maana Baba Mtakatifu Francisko anasema, Mapadre watambue kwamba, wamepakwa mafuta ya wokovu, ili kuwahudumia jirani zao na kamwe wasikate tamaa, Baba Mtakatifu Francisko anasema haachi kutoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya wito wa Upadre, ambao si kwa mastahili yao wenyewe, bali wameitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Kipindi cha shida na magumu ya maisha, iwe ni fursa ya kurejea tena katika zile nyakati angavu za sadaka na huduma kwa watu wa Mungu, ili kugundua tena neema za Mungu katika maisha na utume wao, ili kuwasha tena  na tena furaha inayokita mizizi yake katika unyenyekevu, ili kamwe majonzi na uchungu wa moyo, yasizime ile furaha na uungwana! Baba Mtakatifu Francisko katika shukrani zake kwa Mapadre wote duniani, tunamwona pia ndanimwe, Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki, ambaye alichakarika usiku na mchana kufundisha katekesi; akawekeza nguvu na akili zake katika sekta ya elimu, ili kuwakomboa watu wa Mungu nchini Kenya kutoka katika lindi la ujinga, umaskini na magonjwa. Licha ya shughuli zote hizi, lakini bado alikuwa ni mwana michezo wa kutupwa, ndiyo maana Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1999, akamteuwa kuwa ni mjumbe wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha watu wa Mungu kwamba, wazee kama Askofu mkuu Mstaafu Raphael S. Ndingi Mwana a'Nzeki wana ndoto lakini vijana wana utabiri!

Askofu Mkuu Ndingi
03 April 2020, 12:28