Tafuta

Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda, OSB: Wosia kwa watu wa Mungu. Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda, OSB: Wosia kwa watu wa Mungu. 

Abate Mstaafu Alcuin Nyirenda: Wosia kwa watu wa Mungu

Hii ni tafakari ya kina juu ya Fumbo la Kifo iliyowahi kutolewa na Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda, OSB aliyefariki dunia tarehe 4 Aprili 2020 na kuzikwa tarehe 8 Aprili 2020 katika Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki la Njombe na mahubiri kutolewa na Askofu Mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea. Sikiliza wosia wake!

Na Padre Agapito Mhina Mhando na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Nangojea na ufufuko wa wafu. Na uzima wa milele ijayo. Amina. Kanisa lina amini na kutumaini kwa uthabiti kabisa kama vile Kristo Yesu alivyofufuka kweli kutoka wafu na anaishi daima, vivyo hivyo wenye haki baada ya kifo chao, wataishi daima na Kristo Yesu Mfufuka, naye atawafufua siku ya mwisho. Ufufuko wa waamini ni kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Neno mwili, linamwelezea mtu katika hali yake ya udhaifu, yaani kifo! Mfu na marehemu ni maneno mawili tunayotumia kumwita mtu aliyekufa, na mwili wake unaitwa maiti. Mfu ni jina la heshima kwa mtu aliyekufa. Kumbe, neno Marehemu linatokana na rehema-huruma: linamaanisha mtu aliyerehemiwa au kuhurumiwa. Neno hilo lingefanana na la kilatini “defungor” (defungi) au kwa Kiingereza “defunct” lenye maana ya kufikia kilele, mwisho, hatima, kukomaa, kuiva au ukamilifu. Kwa hiyo mwisho wa maisha haya ya mwili (ulimwengu) siyo kufa bali ni kukomaa na kufikia ukamilifu zaidi.

Ndugu zangu kifo ni kizungumkuti. Binadamu anayahangaikia sana maisha yake lakini mwisho wa pilikapilika zote hizi na “patashika nguo kuchanika” anaona uhai wake unagota na kufikia hatima. Ama kweli, asiyejua kifo aangalie kaburi”. Kwa hiyo kutokana na akili zake, binadamu daima amejiuliza, kulikoni maisha yagote wakati bado kuna matumaini ya kuishi? Ama kweli binadamu anao ugonjwa wa kusahau “Arzheimer”. Binadamu anashindwa kukumbuka kuwa akitaka kuwa na maisha ya kiutu, hana budi kuikabili pia hatima yake. Yaani kuyafuatilia maisha yake na kufikiria hatima yake kutoka pale anaposherekea siku yake ya kuzaliwa kwa umombo “birthday”. Bila hivyo maisha yanakosa maana na matumaini na mtu anaishia kuhangaika, mambo yanapomwendea kombo.

Ndivyo inavyokuwa pale kifo kinapokubana kwenye kona hadi usijue mahali pa kukimbilia, unabaki kuhaha kama “Ngiri” aliyezingirwa na Mbwa pamoja na wawindaji. Hapo unamwona mkristo anashika moyo, anahangaika kumwomba Mungu na watakatifu ili wairushie mbele mihadi ya kifo, yaani kifo kisogezwe mbele. Ndivyo walivyofanya Martha na Maria walipomwijia juu Bwana Yesu wa sababu hakukizuia kifo kumfika kaka yao Lazaro. Kumbe, wasijue kwamba Yesu hakufika duniani kuyaendeleza maisha ya kibaolojia bali kushinda dhambi na mauti! “Binadamu kumbuka kuwa wewe ni mavumbi na mavumbini utarudi” na wakati wa kutia udongo kaburini kwa marehemu wakati wa mazishi kiongozi wa Ibada anasema: “Binadamu wewe ni mavumbi na mavumbini utarudi, lakini Bwana atakufufua siku ya mwisho.” Fikra hii ni nzuri lakini hakieleweki. Yaani haileti matumaini kwani tunanaendelea kujisikia bado gizani mwa ulimwengu huu, kama mtuhumiwa anayesota lumande. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, mateso na kifo vimepata maana na mwanga mpya!

Hii ni tafakari ya kina juu ya Fumbo la Kifo iliyowahi kutolewa na Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda, OSB aliyefariki dunia tarehe 4 Aprili 2020 na kuzikwa tarehe 8 Aprili 2020 katika Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Askofu Alfred Leonhard Maluma wa Jimbo Katoliki la Njombe na mahubiri kutolewa na Askofu Mkuu Damian Denis Dallu wa Jimbo kuu la Songea. Askofu mkuu Dallu amewakumbusha waamini kwamba, hapa duniani wao ni wasafiri tu na wala hawana muda mrefu wa kuishi. Hivyo wanapaswa kukita maisha yao katika haki na kila mtu akijitahhidi kutekeleza dhamana na wito wake, ili kusudi la Mwenyezi Mungu liweze kutimia katika maisha ya mwanadamu. Mwanadamu ajitahidi kujishikamanisha na kuambatana na Mwenyezi Mungu katika hija ya maisha yake hapa duniani; kwa kutenda mema, ili hatimaye, aweze kufika mbinguni!

Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa Abate Mstaafu Nyirenda ni zawadi kubwa kutokana na huduma yake kwa watu wa Mungu! Kwa hakika maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na yanapata maana zaidi, ikiwa kama yanamwilishwa katika huduma makini kwa Mungu na jirani. Kwa maana hakuna mtu anayeishi kwa ajili yake binafsi na kama anaishi, anaishi kwa ajili ya Bwana na wanapoitupa dunia mkono, bado wanaendelea kuwa ni mali ya Bwana! Kuna umuhimu kwa waamini kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na Fumbo la Kifo! Waamini wasikubali kuelemewa wala kumezwa na malimwengu. Watu wa Mungu wajitahidi kupamba maisha yao kwa fadhila na karama mbali mbali kama vile: huruma, upendo, ukarimu, utu wema na usafi wa moyo! Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 67 ya kuzaliwa, Miaka 40 ya Nadhiri za daima miaka 33 ya Daraja Takatifu ya Upadre.

Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda, alizaliwa tarehe 9 Oktoba 1953 huko Lugagala, Parokia ya Mtakatifu Yakobo, Mgazini, Jimbo kuu la Songea. Baada ya masomo yake ya Sekondari kunako mwaka 1977 alijiunga na Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa kwa kipindi cha mwaka mmoja yaani kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1978. Akapiga kwata ya nguvu, huko Oljoro, Arusha na Buhemba, JKT, mkoani Mara wakati wa Operesheni Mazoezi hadi raha! Tarehe 15 Agosti 1980 akaweka nadhiri zake za kwanza! Akaendelea na masomo ya falsafa kwenye Seminari kuu ya Kibosho, Jimbo Katoliki la Moshi na Taalimungu, Seminari kuu ya Peramiho, Jimbo kuu la Songea. Kunako mwaka 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kati ya Mwaka 1991 hadi mwaka 1993 alipelekwa Roma ili kujiendeleza zaidi na masomo na aliporejea nchini Tanzania akapewa dhamana ya malezi kwa ajili ya watawa wenzake. Tarehe 2 Januari 1994 akateuliwa kuongoza Monasteri ya Hanga, Jimbo Kuu la Songea kwa muda wa miaka 9 hadi mwaka 2004 alipong’atuka kutoka madarakani. Baada ya kung’atuka kutoka madarakani alitumwa kwenda Roma kuwa Mshauri wa wanafunzi katika Taasisi ya Kipapa ya Liturujia, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Anselm. Akiwa Chuoni hapo, alijiendeleza na kuhitimu masomo yake hapo tarehe 3 Mei 2018.

Abate Mstaafu Alcuin Nyirenda alikuwa ni mchangiaji sana wa tafakari na makala mbali mbali za maisha ya kiroho na kiutu kwenye viunga vya Radio Vatican! Siku ya kutetea kazi yake, Radio Vatican ilikuwa na haya ya kusema: Shirika la Wabenediktini wa Monasteri ya Hanga, Jimbo kuu la Songea, Tanzania likabahatika kupata “chuma cha Mjerumani” katika taaluma baada ya Mheshimiwa sana Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda, tarehe 3 Mei 2018 kutetea kazi yake ya shahada ya uzamivu kutoka kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana kilichoko mjini Roma. Jopo la Maprofesa lililokuwa linaongozwa na Prof. Oborji Francis Anekwe likampongeza kwa kazi nzuri ambayo inajikita zaidi katika ushuhuda endelevu wa kimisionari unaotolewa na Monasteri ya Hanga, kama mahali muafaka pa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Hii sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa utume na umisionari wa Kanisa unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa watu wake. Hii ni jumuiya inayojikita katika huduma makini kama kielelezo cha imani tendaji.

Watawa wameitwa na wanatumwa kutangaza na kushuhudia Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Kwa mtindo wake wa maisha, Jumuiya inakuwa ni mahali pa majadiliano, utamadunisho na huduma makini kwa watu wa Mungu. Sheria ya Mtakatifu Benedikto imekuwa ni nguzo na mhimili mkuu wa ushuhuda kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji Jimbo kuu la Songea. Utetezi wa kazi hii, ulishuhudiwa na “vigogo wa Shirika la Wabenediktini kutoka ndani na nje ya Roma, bila kuisahau familia ya Mungu kutoka Tanzania. Kwa hakika Mheshimiwa sana Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda amekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa wanafunzi wanaoendelea kujitaabisha katika masomo, ili siku moja waweze kuibuka kidedea kutetea kazi zao, tayari kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Tanzania. Abate Mstaafu Alcuin Nyirenda alibahatika kuwa na karama na mapaji mbali mbali katika maisha yake. Alipewa kipaji cha akili ambacho alikitumia sana kwa ajili ya ustawi, maendeleo ya watu wa Mungu. Alibahatika kuzifahamu lugha za kimataifa kwa ufasaha kabisa!

Alipokuwa akizungumza “Umombo” watu walishika tama! Alipogeuza kibao na kutamba kwa Lugha ya Kifaransa, utadhani alizaliwa mjini Paris, Ufaransa. Kwake lugha ya Kijerumani ilikuwa ni sawa na maji kwa glasi! Alipiga michapo, hadi Wajerumani wakasimama dede! Kilatini ilikuwa ni Lugha ya majigambo kwa wasomi wenzake, lakini kwa “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” alimung’unya Kiswahili barabara! Alipenda sana ustawi na maendeleo ya vijana wengi, akawahamasisha kujiunga na miito mbali mbali. Alikuwa ni mwandishi aliyebobea! Kwa bahati mbaya, baadhi ya vitabu vyake, alivyokuwa anakusudia kuviandika ameondoka navyo! Ama kwa hakika mwanadamu hapa duniani ni mpita njia tu!

Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., amesema, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilifurahia kusikia kamba, Abate Mstaafu Alcuin Nyirenda alikuwa anarejea nchini Tanzania baada ya kuhitimisha utume wake wa kimisionari nje ya nchi. Maaskofu walikuwa na matumaini makubwa kwamba, Kanisa la Tanzania lingeweza kufaidika sana kwa karama na mapaji aliyokuwa amekirimiwa Abate Nyirenda katika maisha na utume wake kwa nafasi mbali mbali ndani ya Baraza. Lakini mipango ya mwanadamu si mipango ya Mungu. Mwenyezi Mungu amependa kumwita mtumishi wake, ili akapumzike kwa amani. Ni matumaini ya Askofu mkuu Nyaisonga kwamba, Mwenyezi Mungu atayakumbuka mema aliyotenda Abate Nyirenda katika maisha na utume wake na hivyo kumstahilisha maisha na uzima wa milele miongoni mwa wateule wake!

Abate Mstaafu Alcuin Nyirenda alirejea nchini Tanzania akitokea Korea ya Kusini, tarehe 2 Machi 2020. Tarehe 18 Machi 2020 akafunga safari na kuelekea Mbeya kwenye nyumba ya Shirika, “Domus Religiosa” iliyoanzishwa kunako mwaka 1993. Tarehe 20 Machi 2020 alianza kujisikia vibaya na hatimaye, akapatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya na kupata nafuu. Tarehe 31 Machi 2020 akaondoka kuelekea Songea na kufika Abasia ya Hanga tarehe 1 Aprili 2020. Alifuraia kurejea nyumbani na alikuwa amejipangia kuanza kwanza na mafungo ya binafsi, kabla ya kuendelea na majukumu mengine ambayo angepangiwa na Wakuu wa Shirika. Tarehe 2 Aprili 2020 hali yale ilibadilika na kuanza kudhohofu tena akapelekwa kwenye Hospitali ya Mtakatifu Yosefu, Peramiho, Songea. Alikuwa na joto kali sana na baada ya kupimwa akagundulika kwamba, kiwango cha sukari kilikuwa juu sana, hali iliyopelekea kuwa na shinikizo la damu. Aligundulika pia kushambuliwa na homa ya matumbo iliyopelekea hali kuwa mbaya zaidi!

Tarehe 4 Aprili 2020 majira ya asubuhi, Abate Mstaafu Alcuin Maurus Nyirenda, akaondoka hivi hivi bila kuaga! Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, sasa aamstahilishe kuyaona wazi wazi mafumbo aliyokuwa anaadhimisha na kuyashuhudia katika maisha na utume wake. Tutaendelea kumkumbuka kwa wema, upole na ucheshi wake! Aliwahi kuandika kwenye tafakari ya Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020, “The End”.

Abate Nyirenda Wosia
14 April 2020, 11:43