Zaidi ya Mapadre 20 wamekwisha kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 nchini Italia, wengi wao ni wale waliokuwa wanawahudumia wagonjwa. Zaidi ya Mapadre 20 wamekwisha kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19 nchini Italia, wengi wao ni wale waliokuwa wanawahudumia wagonjwa. 

Virusi vya Corona: Mapadre zaidi ya 20 wamekwisha kufariki dunia!

Takwimu zinaonesha kwamba, kuna Mapadre zaidi ya 20 ambao tayari wamefariki dunia kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19 nchini Italia. Na wengi wao ni kutoka Jimbo kuu la Bergamo. Hawa ni wale Mapadre ambao wamekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa waathirika wa Virusi vya Corona pamoja na familia zao. Kuna madaktari 15 waliopoteza pia maisha yao katika huduma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Askofu mkuu Francesco Beschi wa Jimbo kuu la Bergamo lililoko Kaskazini mwa Italia anasikitika kusema kwamba, Bergamo ni kati ya maeneo yaliyoathirika sana na Virusi vya Corona, COVID-19. Mapadre na watawa wameendelea kuwa karibu na ndugu, jamaa na marafiki ya wale wote walioathirika kwa ugonjwa huu, lakini hata wao wamekumbwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna Mapadre zaidi ya 20 ambao tayari wamefariki dunia kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19 nchini Italia na wengi wao ni kutoka Jimbo kuu la Bergamo. Hawa ni wale Mapadre ambao wamekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuwapatia Sakramenti. Kuna Mapadre 20 ambao wamelazwa kwenye vyumba vya wagonjwa mahututi huko Bergamo. Hadi kufikia tarehe 19 Machi 2020, madaktari waliofariki kwa ugonjwa huu nchini Italia walikuwa ni 15. Hali ni tete sana kwa sasa!

Hali inatisha sana kwa kila mtu, kumbe, watu wanapaswa kuwajibika barabara kwa kufuata itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 kwani ugonjwa huu si wa kufanyiwa mzaha hata kidogo na wala si kutaka kuwaogofya watu. Jumatatu, tarehe 16 Machi 2020 zaidi ya watu 300 walifariki dunia huko Bergamo kutokana na kushambuliwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Askofu Antonio Napolioni wa Jimbo Katoliki la Cremona, aliyekuwa amelazwa kwa muda wa siku kumi, Jumatatu, tarehe 16 Machi 2020 aliruhusiwa kurejea tena jimboni mwake. Askofu mkuu Francesco Beschi anasema, hata katika kifo, Kanisa limeendelea kuonesha mshikamano wa dhati na watoto wake katika Neno, Sakramenti na huduma ya faraja. Hadi kufikia, Alhamisi, asubuhi tarehe 19 Machi 2020, idadi ya watu waliokuwa wameambukizwa kwa virusi vya Corona, COVID-19 sehemu mbali mbali za dunia ilikuwa ni watu 198, 178. Wagonjwa waliokwisha kufariki dunia ni 7, 954.

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, katika waraka wake wa kichungaji kwa wakleri na watawa wote wanaotekeleza dhamana na utume wao nchini Italia, anapenda kuwapongeza kwa moyo wa dhati kabisa, kwa uwepo wao wa karibu kwa wagonjwa, familia na watu walioathirika kutokana na Virusi vya Corona, COVID-19. Kwa namna ya pekee, anawashukuru mapadre ambao wameendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waamini katika parokia mbali mbali bila kuwasahau watu wenye mapenzi mema wanaoendelea kuonesha imani na matumaini yao kwa Kanisa. Mapadre wamekuwa ni mashuhuda wa Uso wa Kanisa ambalo ni rafiki kwa maskini na daima liko karibu na watu wanaoteseka kwa njia ya huduma makini.

Mapadre wamekuwa ni kielelezo makini cha ushuhuda wa: heshima, upendo na mshikamano, utambulisho wa huduma yao ya kichungaji hasa wakati huu ambapo watu wengi wameshikwa na hofu ya mashambulizi ya ugonjwa wa Virusi vya Corona, COVID-19. Wameendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha afya ya umma kwa kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini, wagonjwa na wazee. Hata katika hali ya faragha sana, wamekuwa ni vyombo vya matumaini na faraja kwa wagonjwa na wale waliofiwa na wapendwa wao. Wamesaidia kuwapatia baraka, wale wote waliotangulia mbele za haki, wakiwa na matumaini ya ufufuko, maisha na uzima wa milele.

Vifo vya Mapadre
19 March 2020, 15:16