Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A. Kristo Yesu ndiye ufufuko na uzima. Mtu yeyote anaye mwamini ajapokufa, atakuwa anaishi. Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya V ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka A. Kristo Yesu ndiye ufufuko na uzima. Mtu yeyote anaye mwamini ajapokufa, atakuwa anaishi. 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili V ya Kwaresima: Ufufuko Wa Wafu!

Yesu akasema: "Mimi ndimi huo ufufuko, na uzima. Yeye aniaminiye mimi ajapokufa, atakuwa anaishi." Kwamba, Yesu ameshafungua milango ya mbingu hivi mmoja akifa harudi tena duniani bali anapita "sheol" hadi kwenye makao ya maisha na uzima wa milele yaani nyumbani kwa Mungu. Yesu hakufika kufufua maiti, bali kuwapa watu utimilifu na hatimaye, maisha ya uzima wa milele.

Na Padre Alcuin Maurus Nyirenda, OSB. – Roma.

Ndugu zangu, dominika iliyopita tuliona kuwa, wale wanaokutana na Yesu wanapata mwanga wa kuona mambo tofauti na wanavyoona wengine. Hivi wanamfuata Kristu na Injili yake kwa furaha. Lakini wanakereketwa kujihoji sana kuhusu hatima ya maisha yao yaani kifo. Wakati mwingine unajiuliza, kama hatima ya kifo ni kufukiwa kaburini, iko faida gani basi kuzaa watoto halafu unawakabidhi ardhini. Hapo unaweza hata kukufuru kusema na kumwona Mungu kuwa mkatili aliyetuumba ili tuishie kufa na kuzikwa. Kwa hiyo swali zito ni hatima ya kifo. Injili ya leo inahusu "Kufufuliwa kwa Lazaro." Mwinjili alituandika kutokana na uponyi fulani wa pekee alioishafanywa naa Yesu kabla akiwa na lengo la kujibu swali kuhusu hatima yetu baada ya kifo. Kadiri ya imani na utamaduni wa Waisraeli, watu wote waliokufa waliingia Sheol, (shaal maana yake tunaitwa.) Sote tunaitwa kuingia katika awamu ya pili ya ulimwengu. Kwa hiyo kama mmoja atafaulu kunitoa kutoka huko “Sheol” na kurudisha tena duniani, huko kulijulikana kuwa ni kufufuliwa. Yaani mmoja anarudishwa katika mazingira yaleyale aliyokuwa aliyoishi kabla.

Huko kumbe, siyo kufufuka bali ni kuhuishwa. Kwa sababu baada ya maisha ya muda fulani hapa duniani itambidi kufa tena na kurudia ulimwengu wa “Sheol” kulekule alikotoka. Kwa kufanya hivyo, kifo kitaendelea kutamba na kueneza utawala wake. Kumbe kufufuka siyo kurudi tena katika ulimwengu. Yesu ni mshindi wa kifo. Leo anaonesha wazi kwamba yabidi tuingie “Sheol”, lakini huko siko kikomo wala hatima ya maisha ya binadamu! Aidha anatupa wazo zaidi kuhusu uzima, kwamba baada ya kifo na kuingia Sheol (kaburini) hakuna kurudi tena duniani. Kwa hiyo Lazaro hakufufuliwa bali alihuishwa. Hebu tuufuatilie ukweli huo. "Mtu mmoja Lazaro alikuwa Mgonjwa." Katika familia hii hakuna baba wala mama bali kaka tu na dada wawili. Aidha familia hii ilikuwa na mahusiano ya mwandani sana na Yesu. Unaliona hilo leo pale dada hawa wanapompelekea Yesu taarifa ya ugonjwa, hawasemi kuwa Lazaro ni mgonjwa, bali: "Yule ambaye unayempenda ni mgonjwa". Halafu sehemu nyingine inasema kwamba "Yesu aliwapenda Maria Martha na Lazaro." Aidha hata kule kaburini, watu wanapomwona Yesu analia, Wayahudi walisema: "angalia jinsi alivyokuwa anampenda." 

Kwa hiyo familia hii inaakisi Jumuiya ya kikristo ambako hakuna mkubwa wala mdogo, wala baba, au mwalimu, bali wote tu ndugu (dada na kaka) wanaopendwa na Yesu kwa raha zao! Yesu anaurudisha ujumbe huu kwa wapendwa wake kwa maneno yenye utata kidogo. "homa hii si ya kifo bali kwa ajili ya utukufu wa Mungu." Kwa tamko hili tunawekwa sawa kuuelewa ujumbe wa leo juu ya ufufuo. Kwamba, kwa upande wa Yesu ugonjwa unaopelekea kifo cha kimwili siyo ugonjwa wa kifo katika maana halisi ya kifo. Kwa sababu kifo cha kimwili hakigusi uzima wa binadamu bali kinaonesha tu utukufu wa Mungu. Na utukufu wa Mungu ni pale utakapoona jinsi Mungu anavyompenda binadamu. Ndiyo maana Yesu anasema: "ugonjwa huu siyo wa kifo kwani ukipita hatua hii, yaani kifo cha kimwili utaona “sapraisi” aliyokutayarishia. Yaani jinsi gani Mungu anavyompenda binadamu, wewe mwenyewe utazimia na roho yako! Ndiyo maana baada ya kuzipata taarifa hizi Yesu hakwenda siku mbili zaidi. Kulikoni Yesu alimwacha Lazaro afe. Huo ni ujumbe muhimu sana kwa Jumuia zetu za kikristo.  Kwamba Yesu hakufika duniani kuzuia kifo cha kimwili. Kazi ya Yesu si kuvuruga mwenendo wa hulka ya kibinadamu. Kumbe hulka ya binadamu ni kufa kimwili. 

Baada ya siku hizo mbili Yesu anasema: "Twendeni Yudea, ... rafiki yetu Lazaro analala. Lakini mimi nitaenda kumwamsha." Picha ya kifo iliyokuja kutumika na Wakristo wa Kanisa la mwanzo hadi wa leo ni kwamba kufa ni kulala, wengine wakachombeza na kusema, eti kufa kunoga! Kwamba aliyekufa amelala katika Bwana. Kwa Watesalonike Paulo anasema: "hatutaki kuwaacha katika ujinga juu ya wale waliolala." Aidha neno la lugha ya Kiitalia cimitero au Kilatini coimeterion kutoka lugha ya Kigiriki coimaomai ni kulala. Tafsiri hiyo ina toa maana kidogo kuwa si kifo bali ni kama kulala wakisubiri kuamshwa. Kisha Yesu anaongeza kusema: "Ndugu yetu Lazaro amekufa." Kwamba kulala kwa mtindo ule ni kifo.  Yesu anapofika kijijini Bethania, Lazaro alishakufa tayari siku nne zilizopita. Kadiri ya utamaduni wa Wayahudi, baada kifo na mazishi bado hawakuthibitisha kifo. Hivi wafiwa walikuwa wanaenda makaburini kwa siku tatu mfululizo kuhakikisha kama kuna dalili zozote za uhai. Ila siku ya nne wanapokosa kuona dalili zozote za uhai hapo walithibitisha na kutangaza kwamba "Ndugu yetu amekufa." Pengine huu ndio ulikuwa wakati wa kuanua tanga!

Siku hizi kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, watu wanafanya tanga ndugu! Kwa hiyo siku hizo Wayahudi walikuwa bado wanaenda kwa Maria na Martha kama tufanyavyo leo ili kuwaauni wafikwa kwa maneno yanayojulika na wote: "pole; sisi tulimpenda lakini Mungu alimpenda zaidi; jikaze; maisha yanaendelea; watu wema tu ndiyo wanaoenda; marehemu tutamkumbuka daima; hakuna anayekufa bila ya mwingine kubaki moyoni mwake, nk". "Martha anaposikia kwamba Yesu anafika anatoka wakakutane hukohuko nje. Maria anabaki nyumbani." Martha anapokutana na Yesu tungetegemea angempigia magoti kama atakavyofanya dada yake baadaye. Kumbe, yeye akiwa amefura hasira akaanza kumgombeza Yesu."Bwana, ungalikuwapo hapa, ndugu yangu hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yoyote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa." Martha anakumbuka Agano la Kale wale Manabii kama akina Eliya na Eliseo ambao waliwahuisha watoto. Mtoto wa mwanamke yule wa Sarepta, binti wa familia ile ya Sunem.

Yesu anamwambia: "Ndugu yako atafufuka." Fikra za Myahudi, wafu watafululiwa ili warudi tena kuufaidi ulimwengu huu na raha zake! Na Martha akiwa na fikra za Kiyahudi juu ya ufufuko, hakuwa na wasiwasi juu ya kufufuka kwa ndugu yake kwani alimwona alivyokuwa mtu mwadilifu. Hivi anamjibu. "Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho." Yesu anamwambia Martha: "Mimi ndimi huo ufufuko, na uzima.Yeye aniaminiye mimi ajapokufa, atakuwa anaishi." Kwamba Yesu ameshafungua milango ya mbingu hivi mmoja akifa harudi tena duniani bali anapita sheol holoholo hadi kwenye makao ya maisha na uzima wa milele yaani nyumbani kwa Mungu. Hapa unaona kwamba Yesu anarudisha fikra tulizo nazo za ule ufufuko wa siku ya mwisho na kutufanya tuuone ufufuko kuwa ni sasa. Yesu hakufika kufufua maiti, bali kuwapa watu utimilifu na hatimaye, maisha ya uzima wa milele. Kama yalivyo maisha wanayofurahia mapacha tumboni mwa mama. Tumboni wanajisikia kuwa wamefika, ni paradisini kila kitu “dezo” au “maji kwa glasi”. Kwao kuyaacha maisha hayo ndiyo kifo. Pacha mmoja anapozaliwa duniani, aliyebaki anajua mwenzangu amekufa. Asijue mwenzake ameingia katika ulimwengu tofauti na mkubwa zaidi anaoweza kumwona mama yake uso kwa uso na kucheka naye.

Ndugu zangu ni imani tu inayoweza kutusaidia kuelewa hali hii ya mpito ya kuingia katika ulimwengu tukaomwona Mungu na kufurahia uso wake.  Martha akamwambia: "Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu yule ajaye ulimwengu." Hadi hapa, Yesu amefaulu kumwongoza Martha hadi aelewe maana ya maisha. Martha amepata mwanga mpya. Haoni tena kifo cha kaka yake kama ilivyokuwa kabla. Kwa hiyo anatamani hata dada yake Maria apate mang'amuzi hayohayo. "Naye Martha alikwenda zake; akamwita umbu lake Mariamu faraghani akisema, Mwalimu yupo anakuita." Kwa kipindi hicho Yesu alibaki mahali palepale alipokutana na Martha."Na Yesu alikuwa hajafika ndani ya kijiji; lakini alikuwa akalipo palepale alipomlaki Martha." Inashangaza, kulikoni Yesu hakuingia kijijini hadi kwa wafiwa walau kumpa pole Maria, au kwenda kwenye kaburi la Lazaro. Kwa maelezo ya kitaalimungu ni kwamba Yesu alitaka watu wote watoke mle kijijini, yaani waachane na kuomboleza kusiko na mashiko wala tija. Martha anampwepwea dada yake faraghani. Faragha inaonesha kuwa mambo mengine hayapaswi kupwayukiwa kwa sauti wala kuanikwa hadharani kama udaga! Yaani mang'amuzi mengine ya kiroho hayapaswi kutangazwa kwa sauti ya juu, bali yawasilishwe kiutaratibu, kwa sauti stahiki na katika sehemu tulivu. Aidha muda wa kuonana na mwanga wa Kristo hauwi mmoja kwa wote. Kuna ndugu mmoja au wachache wanaoweza kuwa na mwanga kabla, nao wawashirikishe wenzao. Na hii ndiyo raha ya maisha ya Jumuiya ya waamini, ati chema kula ndugu na jirani zako!

"Wayahudi waliokuwapo na Mariamu nyumbani wakimfariji walipomwona jinsi alivyoodoka upesi na kutoka walimfuata." Kijijini kinaamanisha fikra za zamani juu ya kifo na sasa yawabidi kutoka nje ya kijiji.  Mariamu alipofika pale, alianguka miguuni na kulia. "Yesu anapomwona Maria analia na wale Wayahudi waliofuatana naye wanalia aliugua rohoni.", Yesu anaugua rohoni kwani anaona kwamba fikra ya kifo waliyo nayo na jinsi wanavyolia ni hatari. Kwamba kama unafikiri kuwa kifo ni mwisho hapo huwezi tena kuishi kama mtu huru. Kwani itabidi huishi maisha ya kujihami na kujilinga kwa hali na mali hata kwa njia ya kudhulumu wengine bora uishi vyema katika maisha haya. Kwa hiyo mtu huwi na upendo kwa Mungu na huwezi kutenda matendo ya upendo kwa wengine. Yesu anawauliza: "Mmemweka wapi?" Hata sisi tunapofikwa na ndugu tunaweza kuulizwa "Mmemweka wapi?" Yaani amezikwa wapi ambako mnaona ndiyo hatima yake na nyumba na makao yake ya milele. Wanapojibu: "Njoo utazame" Yesu anatoka machozi dacruein machozi ya kimyakimya. Kwa vyovyote kulia machozi ni kwa kila binadamu mbele ya kifo cha mpendwa. Utofauti wake ni kilio cha kukata tamaa kama ingekuwa mwisho wa yote. Kumbe, Yesu analia chozi la kimya Wayahudi walipomwona Yesu akitokwa hivyo machozi, wakasema: "Angalieni jinsi alivyompenda."

Kutokana na umbumbumbu wao walidhani upendo upo tu katika kuendeleza maisha wakasema: "Je! huyu aliyemfumbua macho yule kipofu hakuweza kumfanya na huyu asife?" Kumbe, Yesu hakufika kurefusha maisha, bali kutujuza kwamba, Mungu ametupatia maisha ambayo hayaguswi kabisa na kifo. Yesu akiwa mbele ya kaburi anatoa amri. "Liondoeni jiwe." Kwa vyovyote jiwe lile lilitenganisha ulimwengu wa wafu na ulimwengu wa wazima. Martha anasadiki lakini bado ana wasiwasi hivi anaona haiwezekani kulitoa jiwe: "Bwana ananuka sasa; maana amekuwa maiti siku nne." Yesu anamwambia: "Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu? Utukufu wa Mungu ni ile hatima ya kweli ya upendo aliotuandalia Mungu.  Ndugu zangu, ni dhahiri kwamba, kama hatuliviringishi jiwe yaani hatufunui makaburi tutaendelea kulia tukifikiri kwamba kuna bado mfuniko kaburini unaotenganisha ulimwengu wa mfu na wazima. Baada ya kuliondoa jiwe Yesu akalia kwa sauti ya juu. "Lazaro njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa."  Kumbe Yesu ametoa maiti kutoka kaburini. "Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi na uso wake umefungwa leso."

Hapa tunaoneshwa alama zote za kifo. Na kilio cha sauti ya juu cha Yesu ni alama ya ushindi wa maisha aliyotaka kuyaleta hapa duniani. Kisha anatoa amri. "Mfungueni mkamwache aende zake."  Baada ya hapo tungetegemea kumwona sasa jinsi Lazaro anavyofurahi, anakuja kumkumbatia Yesu, dada zake na wengine na kuanza sherehe. Kumbe amri hiyo mfungueni inatuhusu sisi kwamba: "Fungueni maiti na mumwache aende." Sisi tunapenda kumfunga mfu abaki nasi kwa vile tunampenda. Kumbe inabidi kumfungua na kumwacha aende kwenye nyumba ya Baba wa milele! Huo ndio mwisho wa Sinema ya Lazaro mfu! Kwa kimombo tunasema "The END".

28 March 2020, 13:47