Tafuta

Vatican News
Kifo cha Mkristo kinafafanuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini ya maisha na uzima wa milele! Kifo cha Mkristo kinafafanuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini ya maisha na uzima wa milele! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili V ya Kwaresima: Fumbo la Kifo!

Maana ya Kikristo ya Kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ndani yake mna tumaini na chemchemi ya maisha na uzima wa milele. Kwa Mkristo siku ya kifo huanzisha, mwisho wa maisha yake ya Kisakramenti: Nangojea ufufuko wa wafu na uzima wa ulimwengu ujao! Kufa kunoga!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, domenika ya tano ya Kwaresima mwaka A wa Kanisa. Katika domenika hii kuna mambo makuu mawili ya kuzingatia. Kwanza, kadiri ya utamaduni na mapokeo ya Kanisa, kuanzia Dominika hii misalaba inafunikwa, mpaka ijumaa kuu wakati wa kuadhimisha mateso ya Kristo na sanamu zinafunikwa, mpaka wakati wa maaadhimisho ya vijilia vya pasaka. Pili, kadiri ya mpangilio wa injili za mwaka A wa kiliturjia kuanzia domenika ya 3A tulipoanza matakaso matatu ya wakatekumeni, domenika hii ya 5A ya Kwaresima linapoadhimishwa takaso la tatu na la mwisho, injili inasimulia kufufuliwa kwa Lazaro ili kutufundisha kuwa katika Ubatizo, Kristo Yesu, anatufufua kutoka mauti ya dhambi na kutupatia uzima wa Kiroho ndani mwetu na maisha mapya kama waana wa Mungu.  

Kabla ya kuingia katika tafakari ya masomo ya domenika hii, ni vyema tujikumbushe haya; Siku arobaini za kipindi cha Kwaresima, zinatuhimiza kwa kurudia tena na tena, mwaliko wa kufunga, kufanya toba, kusali, kutenda matendo mema na kuwahudumia wahitaji. Zimepita siku 33 tangu tuanze kipindi hiki na zimebaki siku 7 tuingie Juma Kuu linalofunguliwa na Jumapili ya Matawi. Ni muda mwafaka kujitafakari na kujiuliza: Je, ile dhambi ninayoipenda kuliko zote nimeiacha, tendo gani la huruma nimetenda tangu Kwaresima ianze, ni nini nilichojinyima kwa ajili ya wenye shida na nimesaidia wahitaji wangapi kwa siku hizi 33 tangu Kwaresima ianze? Katika wimbo wa mwanzo tumesali pamoja na Mzaburi tukiomba na kusema; “Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, uniokoe na mtu wa hila asiye haki. Kwa kuwa wewe Mungu uliye nguvu zangu.” Sala hii ina maana kwa yule ambaye siku hizi 33 zimemfanya awe karibu zaidi na Mungu kwa kufunga, kufanya toba, kusali, kutenda matendo ya huruma.

Katika Somo la kwanza, Nabii Ezekieli anahusianisha uhamisho wa Babeli kwa waisraeli ulikuwa kifo cha Taifa teule na kwamba taifa zima lilizikwa. Sababu ya mapendo yake, Mungu anaahidi kuwafufua Waisraeli, yaani kuwarudisha katika Nchi Takatifu. Ukombozi huo ni mfano wa ufufuko wa miili yetu siku ya mwisho. Tutambue walipelekwa uhamishoni Babeli ikiwa ni adhabu waliyopewa na Mungu kwa dhambi zao. Kutubu kwao na kumrudia Mungu, ndicho kilichomfanya Mungu amtume Ezekieli kuwapa habari hii ya matumaini ya kutolewa katika makaburi yao, kutolewa utumwani na kurudishwa tena katika nchi yao. Ndivyo inavyokuwa kwetu tunatenda dhambi, tunakuwa kama wafu ndani ya makaburi, kwani dhamiri na nafsi zetu zinakuwa chafu mfano wa uchafu ulio ndani ya kaburi. Kutubu dhambi zetu ni sawa na kufufuliwa na kuvalishwa utu mpya. Unagonja nini, toka basi katika uchafu wake, nenda kwa Bwana huko kuna kwake kuna ukombozi mwingi, maana yeye haesabu maovu yetu naye atakuoa katika uchafu wako na kukuvisha utu mpya.

Mtakatifu Paulo, Mtume, katika Somo la pili la Waraka wake kwa Warumi anatukumbusha kuwa, shauku ya dhambi hutokana na mwili. Kumbe matendo mema yanayompendeza Mungu hutokana na Roho, yaani Roho Mtakatifu tulimpokea katika Ubatizo. Basi tumfuate Roho ili tumpendeze Mungu, naye Roho atatufufua siku ya mwisho na kutufanya tuwe watu wapya. Wakati wa mwisho ni upi na unakuja lini? Hakuna anayejua siku wala saa basi tuwe tayari mda wote. Tumrudie basi Mungu mapema iwezekanavyo kila tunakuwa tumemkosea na kumwomba msamaha. Injili ilivyoandikwa na Yohane inatusimuliwa namna Lazaro alivyofufuliwa na Yesu. Katika tukio hili kuna mambo manne ya kuzingatia; Urafiki wa kweli wa Yesu na Lazaro pamoja na dada zake Martha na Maria, Imani thabiti ya Martha na Maria juu ya ufufuo na uzima wa milele, thamani ya uhai wa mwanadamu uliodhihirishwa kwa uchungu mkubwa aliokuwa nao Yesu kwa kifo cha rafiki yake hata kulia kwa huzuni kama binadamu na nguvu ya sala ya Yesu kwa Mungu Baba.

Ni wazi kifo kinatisha na kuogopesha kwani kinakatisha furaha ya maisha furaha pamoja na ndugu zetu. Kifo kinatunyang’anya uhai, tunu aaliyotujalia mwenyezi Mungu. Lakini kwa imani tunasaidiki kuwa kifo si mwisho wa maisha ila ni daraja la kuelekea uzima wa milele. Kifo na kuhuishwa au kurudishiwa uzima tena kwa Lazaro kunatuambia kuwa mtu hawezi kuishi milele isipokuwa kwa njia ya Kristo mwenyewe, kwani yeye mwenyem anasema, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuamini hatakufa kabisa hata milele. Ni hulka ya binadamu kupenda kuishi, na kuogopa kufa hata mzee mwenye zaidi ya miaka 100, bado angependa kuendelea kuishi. Hamu hii ya kutaka kuishi imepandwa na Mungu ndani mwetu kwanza wakati wa uumbaji wa Adamu na Eva na sasa siku ya kutungwa mimba kwa kila mmoja. Hii hamu haiwezi kamwe kukamilishwa kwa Maisha ya hapa duniani mpaka pale tutakapomuona Mungu aliye asili ya Maisha yetu. Lakini hata hivyo tunawajibika kuuheshimu, kuulinda na kuutunza uhai ambayo ni tunu ya pekee kabisa aliyotujalia mwenyezi Mungu.

Tunapaswa kujitunza kwa kujilisha na kujivika, kutafuta tiba unapougua, kujihami na kujilinda panapotokea hatari yoyote ile. Tunu hii ya uhai ni ya milele. Kwa dhambi ya asili yaani Adamu na Eva kukosa utii kwa Mungu tuliipoteza na ikawa ndiyo mwanzo wa kifo. Lakini kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, kifo chetu sio tena adhabu bali ni njia ya kuufikia uzima wa milele kama Yesu mwenyewe anavyosema, nalikuja ili muwe na uzima tena muwe nao tele na kabla ya kumfufua Lazaro anasema, mimi ndimi ufufuo na uzima. Lakini kuupata huo uzima wa milele, sharti ni moja, Yesu akasema, Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa. Sisi tunapenda kuishi kwa muda mrefu, lakini Mungu anapenda tuishi siyo kwa muda mrefu tu bali tuishi milele. Yeye ndiye aliyetupa uzima kwanza, halafu amemtuma mwanae Yesu Kristo kutupa uzima usio na mwisho. Kile alichoahidi kupitia nabii Ezekieli; nitatia roho yangu ndani yenu nanyi mtaishi milele, amekitimiza kwa mateso, kifo na ufufuko wa mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Badala ya kutegemea ulinzi wa kibinadamu kulinda uhai wetu, tumtegemee zaidi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.

Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa uhai kwanza na ndiye atakayetupa uzima kamili kupitia. Hii haina maana kuwa tukiugua tusitumie dawa au tusiwe na ulinzi wa aina yeyote ile, la hasha, tuna wajibu wa kujilinda, kujitunda na kujikinga nay ale yote yanayohatarisha afya yetu ya kimwili lakini tukumbuke na kujua kwamba hayo yote bila nguvu za Mungu si kitu. Basi tunapokaribia kuadhimisha Fumbo la Ukombozi wetu, tumruhusu aingie na na tumpate nafasi akae ndani mwetu kwa neno lake, na sakramenti zake, tujenge unafiki na Yesu kama wa Lazaro, Maria na Martha sio tu kwa Yesu lakini pia kati yetu sisi kwa sisi katika raha na taabu. Tuwe na Imani dhabiti kama ya Martha na Maria, na tujivunie kuwa tukiwa karibu na Yesu hakuna litakaloshindikana, Bwana ungekuwepo ndugu yetu hangalikufa…lakini najua hata sasa lolote utakalomwomba Baba atakupa. Tudhamini uhai wetu na wa wengine, tudhamini Maisha ye tuna ya wengine tuone uchungu pale tunapoona mwenzetu ananyimwa haki ya kuishi kwa namna yoyote ile na kumtetea.

Tuone uchungu kama Yesu alivyoona uchungu kwa kifo cha rafiki yake Lazaro na kumlilia. Kulia kwa Yesu kwa huzuni kubwa ni kutuonesha kuwa kifo kamwe siyo sehemu ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu, bali ni kwa sababu ya dhambi kifo kiliingia katika historia ya Maisha ya mwandamu. Kulia kwake ni kutuonyesha ushiriki wake katika huzuni ya dhambi ya mwanadamu. Kisha akasali sala aliyoanza kwa neno, Baba. Kila sala ya Yesu iliyoandikwa katika injili inaanza na Baba. Kutufundisha kuwa Mungu ni Baba yetu mwema na mwenye huruma. Kisha akamshukuru Mungu kwa kumsikiliza na anasema; kwa ajili ya mkutano huu nasema haya ili wapate kusadiki kwamba ndiwe uliyenituma. Kisha akalia kwa sauti kuu, Lazaro njoo huku nje. Lazaro akatoka nje ya kaburi. Wayahudi wengi waliyoona yale aliyoyafanya wakamwamini. Basi nasi tutumie vema muda huu mfupi uliobaki kabla ya pasaka tumlilie Mungu kwa huzuni kuu, tuone uchungu wa dhambi zetu, tushukuru Mungu kwa neema anazotujalia kisha tumuite naye atatuitikia ili siku ya Pasaka tuweze kufufuka pamoja Kristo na tutoke makaburini na kuingia katika uzima mpya.

25 March 2020, 11:20