Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya III ya Kipindi cha Kwaresima: Kristo Yesu, ni chemchemui ya maji ya uzima wa milele! Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya III ya Kipindi cha Kwaresima: Kristo Yesu, ni chemchemui ya maji ya uzima wa milele! 

Tafakari Neno la Mungu Jumapili ya Tatu ya Kwaresima: Maji ya Uzima!

Liturujia ya Jumapili ya Tatu ya Kipindi cha Kwaresima, Mama Kanisa anatoa mwaliko kwa watoto wake kumkimbilia Kristo Yesu ambaye ni chemchemi ya maisha ya uzima wa milele. Ni wakati muafaka wa kurejea tena na kufanya tafakari ya kina kuhusu Sakramenti ya Ubatizo inayozima kiu ya maisha na uzima wa milele. Wokovu ni zawadi ya bure kutoka kwa Mwenyezi Mungu!

Na Padre Paschal Ighondo - Vatican.

Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya liturujia ya Neno la Mungu, domenika ya tatu ya kwaresma mwaka A wa Kanisa. Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha kutoka linatueleza kuwa ingawa Mungu amewakomboa toka utumwani Misri kwa maajabu mengi, Waisraeli wanazidi kumnung’unikia na kumjaribu. Hata hivi Mungu anawavumilia na kuwapa maji ya kunywa ingawa hawakustahili. Nasi, tulio wakosefu, Mungu hatatuacha tukimtegemea daima. Paulo katika somo la pili la waraka wake kwa warumi anatueleza kuwa Mungu aliyeanza kutupenda sisi akatuletea hata wokovu ambao ni zawadi tupu bila stahili zetu. Zawadi kubwa ni pia Roho Mtakatifu akaaye ndani mwetu ambaye anatuwezesha tumpende Mungu na tumwite Baba. Mpangilio wa Injili kuanzia domenika hii ya 3 ya Kipindi cha Kwaresima hadi domenika ya 5 kwa mwaka A ni wa kiustadi mno. Katika domenika ya 3 ya Mwaka A wa kanisa kwa simulizi la mwanamke Msamaria aliyeenda kuchota maji kisimani tunafundishwa kuwa kwa Ubatizo Kristo anakuwa chemchemi ya Uzima wa milele.

Domenika ya 4 ya Mwaka A wa Kanisa, Injili inatupatia simulizi la kuponywa mtu aliyezaliwa kipofu ili kutufundisha kuwa kwa Ubatizo Yesu anakuwa Mwanga wa Maisha yetu na domenika ya 5 ya Mwaka A wa Kipindi cha Kwaresima Injili inasimulia kufufuliwa kwa Lazaro ili kutufundisha kuwa katika Ubatizo, Kristo anatufufua kutoka mauti ya dhambi na kutupatia uzima wa Kiroho ndani mwetu. Mpangilio huu ulilenga kuwaandaa Wakatekumeni watakao batizwa usiku wa pasaka ambao jumapili ya kwanza ya Kwaresima walichaguliwa na majina yao kuandikwa kwenye kitabu cha waliochaguliwa tayari kwa ubatizo. Katika domenika hizi tatu ya 3, 4, na 5 yalifanyika matakaso matatu ya wakatekumeni. Kumbe leo katika domenika hii ya 3 linafanyika takaso la kwanza la Wakatekumeni.

Umuhimu wa Maji ya Ubatizo unatufundisha hata sisi kuona umuhimu wa Mungu katika maisha yetu. Dhambi ni kujitenga na Mungu na huu ni ubaya wa hali ya juu mno wa kumkataa Mungu aliyetuumba, hivyo tunakosa amani kabisa ndani ya nafsi zetu mpaka pale tutakapoighairi na kuijuta na kuomba msamaha ndipo tutakapopata amani tena. Mdhambi anapoghairi ubaya wake na kutambua ufinyu wa uwezo wake, anakuwa na kiu ya Mungu, anamhitaji Mungu, kwake Mungu anakuwa chemchemi ya maji kwa ajili ya uzima wake. Ndivyo anavyosema Mzaburi katika zaburi 63; Ee Mungu wewe ni Mungu wangu, nakutafuta kwa moyo. Roho yangu inakutamani kama mtu mwenye kiu, nina kiu nawe kama nchi kavu isiyo na maji.

Maandiko Matakatifu yanamlinganisha Mungu na chemchemi ya maji ya uzima, anayekaa karibu naye anapata uhai, anapata utakaso, anapata nguvu na maisha yake yanafanikiwa. Ndio maana nabii Yeremia anasema ana heri mtu yule amtegemea Bwana, amfanyaye Bwana kuwa tumaini lake. Yeye ni kama mti ulipandwa kando ya mto ambao mizizi yake imeenea hadi kwenye maji. Mti huu hauhangaiki kamwe wakati wa uchache wa mvua na mti huu huzaa matunda mengi. Nabii anaendelea kusema; amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake na moyoni mwake amemwacha Bwana. Na ni kweli tukiangalia matukio ya wanaoangamia nyakati zetu kwa kuwategemea wanadamu wapate mafanikio kwa miujiza, si haba kusikia habari za kufa kwao.

Waisraeli baada ya kukosa maji wakamsahau Mungu na matendo makuu aliyowatendea wakamnung’unikia. Mungu kupitia kinywa cha nabii Yeremia anawalalamikia Waisraeli kwa kutokuwa na shukrani kwake; Watu wangu wametenda maovu mawili, wameniacha, mimi chemchemi ya uzima na kujichimbia visima vinavyovuja ambavyo maji yake hayakai ndani yake (Jr 2:13). Nasi tulipobatizwa tulivushwa kutoka vilindi ya bahari ya dhambi, kutoka utumwa wa shetani kama waisraeli kutoka mikono ya Farao huko Misri. Tunapoendelea kusafiri katika jangwa la ulimwengu huu, Kristo ni Musa mpya anayetuongoza katika nchi ya ahadi, yaani mbingu, anatuliza njaa yetu kwa chakula cha mbingu {Ekaristi Takatifu} na kiu yetu kwa neno la Mungu. Badala ya kunywa maji ya uzima na furaha ambayo Kristo anatupa bure, tumekengeuka na kuchagua kunywa maji yaliyojaa taka na uchafu wa kila aina ya dhambi sasa tunaugua kwa magonjwa ya mlipuko. Ili tuweze kupona tunahitaji tena maji ya uzima, nguvu ya kiroho kutoka kwa Kristo, ndiye Kristo mwenyewe kama anavyomwambia mwanamke msamaria, kama ungejua ni nani akuombaye maji, ungemuomba wewe kwanza maji ya uzima wa milele.

Injili ya leo ni "pedagojia" ya Yesu ya kutuongoza kwa mfano wa mwanamke msamaria tuweze kujimbua jinsi tulivyo ndani ya nafsi zetu na kumrudia Mungu. “Pedagojia” ya mazungumzo, majadiliano na kusikilizana yanayojengwa katika heshima, uvumilivu, ukweli na uwazi kwa kila mmoja. Sharti la Yesu kumpa mwanamke msamaria maji ni kumleta Mume wake. Mwanamke anajibu sina Mume, na Yesu anamwambia umejibu vyma huna Mume maana hata uliyenaye kwa sasa ni wa tano. Hii ni hatua ngumu ya mazungumzo. Kuambiana ukweli na kuukubali. Inahitaji ujasiri na msaada wa Roho Mtakatifu tunaoupata kwa njia ya sala na kufunga. Hakuna mtu aliye mdhambi kiasi kwamba upendo na nguvu ya Mungu visimbadilishe na kumkomboa. Kwa kutambua udhaifu, dhambi zake na kuzikiri wazi, Yesu alimwongoa yule mwanamke hatua kwa hatua; kwanza alimtambua Yesu kama myahudi, alipomwomba maji, baadaye alipomwuliza una mume naye akasema sina, akamwambia umejibu vema kwa kuwa uliye naye sasa ni watano.

Kwa maneno hayo akamtambua Yesu kuwa ni Nabii. Na hatimaye, walipozungumza juu ya hekalu na kumwabudu Mungu katika roho na kweli. Akamtambua kuwa Yesu ni masiya au Kristo. Yesu alipomwambia yeye ana maji ya uzima na yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele Yoh 4:14, yule mwanamke alisema nipe maji hayo nisione kiu tena maana kwa muda mrefu alihangaika kutuliza kiu yake katika starehe na wanaume lakini kiu yake haikutulia wala haikuisha. Tungefurahi kama injili ingetuambia nini kilitokea baadaye katika maisha ya yule mwanamke. Lakini cha maana ni kuwa Mama yule siyo tu alionja maji ya uzima bali alijua kuwa ni katika Kristo tu anaweza kupata kitulizo na aliwatangazia wengine habari hii njema.

Kipindi hiki kila mmoja wetu inafaa kujitafiti na kujiuliza kiu yangu ni ipi na wanaume hawa watano kwangu ni wepi au ni nini? Ukiwatambua, utamtambua Kristo na kumwomba akupe maji ya uzima wa milele, naye atakuponya na uovu wako wote na kukujaza Roho Mtakatifu atakayekata kiu yako yote nawe utaacha mtungi wako na kwenda mbio kwa kufuraha kuwaambia watu kuwa nimekutana na Kristo njooni nanyi mkamwone yuko katika Sakramenti za Kanisa, yuko katika Neno lake, chemchemi ya maisha ya uzima, lakini zaidi yuko kati ya jirani zako, hasa maskini na wayonge anawasubiri kuwapokea ili atakase na kuwashirikisha maisha ya uzima wa milele!

Tafakari Jumapili III ya Kwaresima

 

10 March 2020, 15:07