Tafuta

Vatican News
Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Lengo la miito mbali mbali ndani ya Kanisa ni wokovu wa watu wa Mungu! Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kwaresima: Lengo la miito mbali mbali ndani ya Kanisa ni wokovu wa watu wa Mungu!  (ANSA)

Tafakari ya Neno la Mungu: Jumapili ya Pili ya Kwaresima: Lengo la Wito ni Wokovu wa watu!

Dhamira ya wito inajionesha katika Somo la kwanza: wito wa Abrahamu, somo la pili wito wa Paulo na Timoteo na Injili kwa namna fulani Kristo Yesu anaudhihirisha wito wake. Katika kuuangalia wito, kwa namna ambavyo masomo haya yameeuonesha tunaona kuwa dhana ya wito wa Mungu inabeba kumbukumbu ya mambo yaliyopita, yaliyopo na inaelekeza katika mambo yajayo.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican

Utangulizi: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, tumeingia katika dominika ya 2 katika kipindi hiki cha Kwaresima, kipindi cha kufunga na kusali na kipindi mahsusi cha kumrudia Mungu kwa toba na matendo mema. Karibu kusikiliza masomo ya dominika hii ya 2 ya Kwaresima, kupata ufafanuzi wake na tafakari ya kutusaidia kuiishi vema Kwaresima. Somo la kwanza (Mwa. 12:1-4a) ni kutoka kitabu cha Mwanzo na linaeleza juu ya wito wa Abramu. Mungu anamtokea Abramu na anamwambia “toka katika nchi yako na jamaa zako, uende nitakapokuonesha”. Kitabu hiki cha Mwanzo kinaonesha kuwa wito wa Abramu ni kitu cha pekee sana. Mungu anapomwita Abramu, anakusudia kuanzisha uhusiano mpya na mwanadamu ambaye amemuumba. Hii ni kwa sababu wito huu unakuja kipindi ambacho mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu yamezidi kuharibika. Na hili tunaliona waziwazi katika masimulizi yenyewe yanayotangulia kuitwa kwa Abramu. Dhambi ya Adamu na Eva (Mwa. 3) inafuatiwa na dhambi ya Kaini kumuua mdogo wake Abeli (Mwa. 4:8), hiyo nayo inafuatiwa na dhambi ya Lameki (Mwa. 4:23) na kutoka dhambi ya Lameki ikafuata ile dhambi ya wana wa Mungu iliyoleteleza gharika kuu ambapo ni Nuhu na wanawe tu walisalia (Mwa. 6-8).

Lakini hata baada ya uangamizi mkubwa wa gharika, dhambi haikukoma, inafuata ile ya ujenzi wa mnara wa Babeli ambapo matokeo yake Mungu anawatawanya kabisa watu na kuwafanya wasisikilizane kwa lugha moja (Mwa. 11). Ni baada ya mfululizo huu unaoonesha kuzidi kukua kwa dhambi na kuzidi kuharibika kwa mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu ndipo Mungu anaamua kumwita Abramu. Ni kwa njia ya Abramu, Mungu anaanzisha historia ya wokovu. Anataka amkomboe mwanadamu moja kwa moja kutoka katika mnyororo huu wa dhambi na uasi. Anamwita Abramu ili kwa njia yake alianzishe taifa lake na awaingize jamaa zote za dunia katika taifa hilo ili waishi ndani ya baraka zake. Uhusiano huu Mungu anaouanzisha kwa njia ya Abramu ni uhusiano unaojengeka juu ya imani na Abramu mwenyewe ndio anakuwa wa kwanza kuionesha. Aliambiwa “toka katika nchi yako” na yeye “akatoka”. Jibu la Abramu kwa mpango wa Mungu lilikuwa kuitikia anachoagiza Mungu: kwa uzito uleule, kwa uharaka uleule na bila kusita akijikabidhi chini ya maongozi yake Mungu. Ni kwa hili, Abramu anaitwa Babu wa Imani.

Somo la pili (2Tim. 1:8b-10) ni kutoka katika waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timoteo. Timoteo alikuwa ni msaidizi wa Paulo katika kazi ya uinjilishaji. Kisha kuusimika ukristo katika mji wa Efeso, Paulo alimwekea mikono awe mchungaji mkuu - Askofu wa kanisa la Efeso. Sasa Paulo yupo Roma anatumikia kifungo chake kwa sababu ya injili, anamwandikia Timoteo waraka huu ili kumuimarisha katika kazi yake ya uchungaji. Kimsingi katika somo la leo, Paulo anamkumbusha kuwa wito alioupokea ni wito mtakatifu na una asili yake kwa Mungu mwenyewe. Tena ni wito ulio na madai yake. Na moja ya madai hayo ni kudumu kuutolea ushuhuda bila kuona haya hata katika magumu yake. Anamkumbusha kuwa Mungu mwenyewe anayo makusudi kwa wale anaowaita, asife moyo asonge mbele.

Injili (Mt. 17:1-9 Injili ya dominika hii ni kutoka kwa mwinjili Mathayo na inahusu tukio la kugeuka sura kwa Yesu.  Kadiri ya simulizi la Mathayo, Yesu aliwatwaa wanafunzi wake watatu; Petro, Yakobo na Yohane akaenda nao hata juu ya mlima mrefu faraghani. Akiwa huko akageuka sura; uso ukang’aa na mavazi yakawa meupe kama nuru. Hapa kugeuka sura hakuelezwi katika maana ya kubadilika kwa uso bali ni kubadilika kwa umbo lake lote (metamophosthe). Mwili wa Yesu ulitwaa sura nyingine na hapo uso wake ukang’aa na mavazi yakawa meupe kama nuru. Tunaona alama nyingi sana ambazo Mwinjili Mathayo anazotoa katika simulizi hili. Na ni kwa kupitia alama hizi ndipo tunaweza kupata nini maana ya tukio hili zima. Alama ya kwanza ni hiyo ya kung’aa kama jua na mavazi kuwa na meupe kama nuru. Hii ni alama ya mwanga, alama inayomuelezea Mungu mwenyewe aliye mwanga na anayeishi katika mwanga. Hii ni alama inayoonesha kuwa kugeuka sura kwa Yesu au kama tulivyoonesha kugeuga umbo ni kwamba Yesu alibadilika kutoka sura ya kibinadamu akachukua sura ya kimungu iliyo ya utukufu. 

Na tukizingatia kuwa tukio hili la Yesu kugeuka sura katika Injili ya Mathayo linafuata baada ya kuwatangazia wanafunzi wake kuwa atateswa na kuuwawa, tukio hili la Yesu kuwaonesha umungu wake lilikuwa ni la kuwaimarisha. Lilikuwa ni kuwaonesha kuwa mateso na kifo chake havitakuwa mwisho bali vitakuwa ni njia ya kuingia katika utukufu wake wa kimungu. Ipo pia alama ya Musa na Eliya. Hawa waliwakilisha Torati na Manabii. Kwa upande mmoja, Torati na Manabii ndiyo kwa pamoja ilikuwa ni Biblia ya wayahudi. Waliwakilisha ufunuo wa Mwenyezi Mungu kwa watu wake. Kwa upande mwingine Musa na Eliya waliwakilisha wajumbe wote ambao Mungu aliwatumia kuwaandaa waisraeli kumpokea Masiya. Kumbe, Musa na Eliya wanaonesha kuwa yote Mungu aliyokuwa ameyafunua na kuyaandaa kwa njia ya wajumbe wake mbalimbali, sasa yametimia kwa njia ya Yesu.

Hii ndiyo sababu Yesu hakulijibu ombi la Petro kujenga vibanda vitatu kwa sababu havina haja tena. Vibanda hivi viliwakumbusha wayahudi tukio lao la kukombolewa kutoka Misri na Yesu anachokwenda kukifanya ni ukombozi mkubwa zaidi kuliko ule wa kutoka Misri. Mwisho ni alama ya sauti ya Mungu: “huyu ni mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Msikieni yeye”. Ni uthibitisho wa Mungu mwenyewe juu ya kile alichokionesha Yesu na kile anachokwenda kukifanya na ni sauti inayoalika kumsikiliza Yesu; kumpokea kwa imani ili kuweza kuushiriki utukufu aliouonesha.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News, katika masomo tuliyoyasikiliza na kupata ufafanuzi wake mfupi, dhamira ya wito inajionesha waziwazi. Somo la kwanza lina wito wa Abrahamu, somo la pili wito wa Paulo na Timoteo na hata katika injili kwa namna fulani Yesu anaudhihirisha wito wake.  Katika kuuangalia wito, kwa namna ambavyo masomo haya yameeuonesha tunaona kuwa dhana ya wito wa Mungu inabeba kumbukumbu ya mambo yaliyopita, yaliyopo na inaelekeza katika mambo yajayo. Mambo yaliyopita yanaonesha mazingira na mahitaji ambamo Mungu anamwita mtu katika wito wowote ule anaoukusudia. Tumeona kwa Abrahamu mazingira haya yalikuwa ni kukithiri kwa dhambi. Mambo yaliyopo ni yale madai na matakwa ya wito yanayomdai yule aliyeutikia kuyatekeleza. Na yajayo daima ni wokovu; wokovu wa aliyeitwa na wokovu wa wale ambao kwa ajili yao mtu ameitwa.

Haya yote yanatuonesha kuwa wito wowote ule ambao Mungu anamwitia mtu, umebeba ndani yake Fumbo kubwa sana. Ni fumbo hili linaloalika bidii katika kuuishi wito kiaminifu na ni fumbo hili linaloalika uvumilivu na ustahimilivu bila kukata tamaa hasa katika magumu ya madai ya wito. Njia ya wito sio rahisi na haijawahi wakati wowote kuwa rahisi lakini mwisho wake umehakikishwa na Yesu mwenyewe kuwa ni kuufikia utukufu wa kimungu. Tuiishi dominika hii ya pili ya kwaresima kwa kuomba neema ya kuishi vizuri miito yetu tuliyoitiwa ili mfungo tuufanyao upate kibali mbele ya Mungu na utufae sote kuufikia wokovu.

Liturujia Jumapili ya II ya Kwaresima
06 March 2020, 17:38