Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka: Wale waliotkaswa kwa Maji na Roho Mtakatifu wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Pasaka: Wale waliotkaswa kwa Maji na Roho Mtakatifu wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa! 

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili IV ya Kwaresima: Ubatizo: Imani!

Injili ya Dominika hii inaakisi safari yetu ya siku 40 za Kwaresima, kipindi cha kwenda katika ahadi na hasa utakatifu ule tulioupokea siku ya Ubatizo wetu. Hivyo muujiza tunaousikia katika Dominika ya leo si tu muujiza kwa yule aliyezaliwa kipofu bali unatuonesha safari ya kila mmoja kutoka katika maisha ya giza na dhambi na kuanza kutembea katika maisha na mwanga wa Kristo Mfufuka!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Mwinjili Yohane katika Injili yake anatupa miujiza saba iliyofanywa na Yesu na anaitambua kama ‘’ishara’’, ndio kusema msomaji anapaswa kwenda mbali zaidi na kutokuishia katika miujiza hiyo ili kupata ujumbe kusudiwa. Na ndio katika Injili ya leo tunakutana na moja kati ya ishara alizozifanya Yesu yaani kumponya mtu aliyezaliwa kipofu. Mwanga na maji ni moja kati ya ishara zinazotumika mara nyingi katika Maandiko Matakatifu kama ishara za uwepo wa Mungu. Yesu anajitambulisha ‘’Mimi ndimi nuru ya ulimwengu’’. Injili ya leo tunaona ilikuwa katika muktadha wa sherehe ya vibanda, ni sherehe ambayo wana waisraeli wanakumbuka safari yao wakiwa jangwani wakitoka nchi ya utumwa na kuelekea nchi ile ya ahadi. Sherehe hii iliadhimishwa kwa muda wa siku saba. Vibanda wakikumbuka vibanda walivyojenga wakiwa safarini jangwani. Usiku waliwasha mioto na mianga katika kuta za Hekalu la Yerusalemu zilizoangaza mji ule mtakatifu, na wakati huo huo kuhani mkuu kwa maandamano alishuka na kuelekea katika birika la Siloamu ili kuteka maji katika chupa ya dhahabu na kisha kwenda kutumika katika altare ile ya kutolea sadaka. Hivyo mwanga na maji ya birika la Siloamu ni muhimu ili kupata ujumbe kusudiwa katika ishara hii ya uponyaji kwa yule aliyezaliwa kipofu.

Katika Kanisa la mwanzo Ibada ya Ubatizo ilijulikana pia kama Sherehe ya ‘’kunurishwa’’, ndio kufanyika au kupewa nuru na mwanga. Na ndio maana hata leo unapokwenda katika ‘’Roman Catacombs’’ samahani kwa kukosa neno la Kiswahili, ndio mahandaki, sehemu ambamo wakristo wa mwanzo walizikwa na kuandikwa majina yao ya ubatizo pamoja na ishara nyingine za Kikristo. Katika ‘’Roman Catacombs’’ kuna ushahidi wa Wakristo wa mwanzo walichora picha za muujiza huu wakiufananisha na Ubatizo. Mtakatifu Augustino pia katika kuelezea maana ya Ishara ya Muujiza huu anajaribu kuturudisha katika jina la Birika lile la Siloamu, maana yake ‘’aliyetumwa’’. Kadiri ya Mt. Augustino aliyetumwa ni Yesu Kristo mwenyewe. Hivi yule aliyezaliwa kipofu anaalikwa na Kristo kwenda kuosha uso na hasa macho yake katika birika lile la Siloamu (maana yake aliyetumwa), maana yake alibatizwa katika Kristo aliye mtumwa wa Mungu, aliyepelekwa na Mungu Baba yake na yetu pia.

Sehemu ya Injili ya Dominika hii ya leo inaakisi safari yetu ya siku 40 ya Kwaresima, kipindi cha kwenda katika ahadi na hasa utakatifu ule tulioupokea siku ya Ubatizo wetu. Hivyo muujiza tunaousikia katika Dominika ya leo si tu muujiza kwa yule aliyezaliwa kipofu bali unatuonesha safari ya kila mmoja kutoka maisha ya kale, maisha ya giza, maisha ya dhambi na kuanza kutembea katika maisha mpya, maisha ya mwanga ya kuongozwa na ile nuru itokayo au iliyotumwa ndio Yesu Kristo mwenyewe. Katika simulizi la mtu aliyezaliwa kipofu kila mmoja wetu anatambua kuwa alikuwa kipofu kabla ya kukutana na Yesu Kristo. Ni Kristo aliyetufanya kuweza kuona tena, kwa maji katika kisima kile cha Ubatizo. Visima vya Ubatizo vya Kanisa la Mwanzo vilijulikana kwa jina la ‘’photistéria’’ likimaanisha sehemu ya kunurishwa.  

Wanafunzi wa Yesu wanamuona mtu aliyezaliwa kipofu ambaye kwa kweli kwa jina ndio kusema ni kila mmoja anazaliwa katika hali hiyo ya kuwa mbali na nuru yaani Yesu Kristo mwenyewe. Lakini zaidi sana hata namna ya kufikiri ya wanafunzi wa Yesu au wayahudi wa nyakati za Yesu bado zipo hata kati yetu leo. Wanamuuliza Yesu kama huyu aliyezaliwa kipofu ni kwa madhambi ya wazazi wake au yake mwenyewe, ndio kusema ni laana kwa yule aliyezaliwa kipofu. Hiyo ni Teolojia potofu kabisa na nikiri kuwa ni kufuru kwa Mungu aliye muumba wetu na anatuumba kutokana na wema na upendo wake usiokuwa na masharti yeyote yale. Yesu leo anatuonesha kinagaubaga kuwa si yeye wala wazazi wake waliofanya dhambi. Yesu anatualika nasi leo kuachana na kuepuka mitazamo ya namna hiyo inayomkufuru Mungu na kwenda kinyume na wema na upendo wa Mungu. Leo kuna hata baadhi ya wakatoliki wanathubutu kusema kuwa leo tumepatwa na janga la Virusi vya COVID-19 kama adhabu na laana kutoka kwa Mungu, narudia naomba tuachane na mawazo ya namna hii kwani ni kufuru kubwa kwa Mungu. Ni kumuona Mungu anayetenda na kuwa na hulka kama mwanadamu, kwa kweli hapana maana Yeye daima ni Upendo kamili na habadiliki.

Katika upofu au ulemavu ule Yesu anaonesha wema na ukuu wa Mungu. Huyu anazaliwa kipofu ndio kusema Mwinjili Yohane anatuonesha kuwa si yeye wala wazazi wake kama anavyosema Yesu wanawajibika kwa upofu wake. Ila muhimu ni kutambua amezaliwa na upofu. Aliyezaliwa kipofu hajui hata maana ya mwanga na hata katika Injili hatumsikii akimuomba Yesu amponye ili aweze kuona. Ni Yesu kwa mapenzi yake anaona haja ya kumjalia tena nuru, kumjalia uponyaji, na ndio wokovu wa kila mmoja wetu. Ni matunda na matokeo ya upendo wa Mungu kwa kila mmoja wetu. Ni kutokana na upendo wake usio na mipaka anamtuma Mwanae aliye Nuru ya kweli ili nasi tupate kuona na kutembea katika nuru na mwanga. Ukombozi ni neema, ni zawadi kutoka kwa Mungu ili nasi tuliozaliwa vipofu tuweze kutembea katika nuru na mwanga. Alipo Kristo daima kuna mwanga, kuna nuru, ni mchana na kinyume chake ni giza totoro. Tunaona pia Yesu anamponya kwa namna isiyokuwa ya kawaida sana, anatumia mate yake na kutengeneza tope na kumpaka machoni. Kwa kadiri ya wayahudi katika mate kuna pumzi, kuna uhai, kuna nguvu ya mtu, ndio kusema kutoka katika pumzi ya Yesu, kutoka katika Roho ya Yesu anazaliwa mtu mpya au kiumbe kipya. Marko 7:33; 8:23 na Mwanzo 2:7

Yesu anampaka tope na kumwamuru aende akanawe katika birika la Siloamu, katika kisima kile chenye maji ya chemchemi, maji ya uzima, ndiye maji yale ya Ubatizo wetu. Hata baada ya kupokea nuru au uponyaji tunaona anakuwa mtu mpya kiasi cha kuwafanya hata wale watu waliokuwa wanamuona kila siku nje ya hekalu akiomba wanashindwa kumtambua na kubaki kujiuliza kama ndiye au la. Hata wale watu wanaokuwa karibu nasi na kutufahamu vema kila mara tunabadili maisha yetu na kuwa watu wapya wanapata shida na ugumu kututambua. Kwani tunakuwa wapya kila mara tunapokubali kuongozwa sio kwa mantiki ya ulimwengu huu bali kwa kutii na kukubali Neno lake liwe taa na nuru ya maisha yetu ya siku kwa siku. Safari ya kufika nuru kamili kama anavyotuonesha Mwinjili Yohana ni ndefu na ya kuchosha. Pale mwanzano yule aliyepokea uponyaji anamtambua Yesu kama mtu tu. Yule mtu anayeitwa Yesu alifanya tope na kunipaka machoni wakati anajaribu kuwaeleza Mafarisayo ni kwa namna gani aliponywa. Na hata walipomwoliza yupo wapi huyo mtu, kila mara tunaposoma tunaona Mafarisayo kamwe hawamtaji Yesu kwa jina. Naye anakiri kuwa hajui yu wapi ndio kusema anakiri kuwa bado hajafikia hatua ile ya kumjua Yesu katika ukamilifu wake.

Ni hatua muhimu kwa kila mmoja katika safari ya kutaka kumjua Yesu, yafaa tukiri kuwa bado hatumjui Yesu katika ukamilifu wake ili daima tubaki na hamu na shauku na ari ya kumtafuta katika maisha yetu ya siku kwa siku. Wakuu wa dini nao pia wanamuhoji huyu aliyepokea uponyaji juu ya Yesu Kristo. Nia yao si kutaka kujua ni kwa namna au jinsi gani alimponya bali walitaka kumwangamiza kwa kuwa haendani na aina ile ya mtu wa dini waliyokuwa nayo vichwani mwao. Wanajihesabia haki na kujiona kuwa wao ni watu wa dini na Mungu hivyo wanajifunga katika kuusaka mwanga wa kweli. Hata nasi tukibaki kujiona kuwa tunajua ya kutosha kuhusu Mungu basi tunaingia katika giza kama lile la wakuu wa dini. Yule aliyepokea uponyaji anakiri na kuambua udogo na uduni wake katika imani, na hivyo kuweza kupiga hatua nyingine. Hata wanapomuhoji safari hii anamtambua Yesu si tu kama mtu bali kama ‘’Nabii’’.

Mahojiano yanaendelea tena na safari hii wanafika kuwahoji wazazi wa yule aliyepokea uponyaji. Wazazi wake kwa hofu ya wakuu wa kiyahudi wanaogopa kukiri na kusema ukweli wote kwani waliogopa kutengwa. Kutengwa si tu katika Hekalu na Sinagogi bali hata katika maisha ya kijamii, hivyo kama walikuwa wafanya biashara hakuna myahudi aliyeruhusiwa kufanya biashara na aliyetengwa kwani alihesabika kama aliyekufa na mpagani. Na ndivyo safari inavyokuwa kwa kila mmoja anayekubali kupata nuru na kutembea katika nuru ya Yesu Kristo. Anawaza na kutenda kwa mantiki ile ya Kimungu na hivyo kutengwa na namna na wana wa ulimwengu huu. Kama kwa yule aliyepokea uponyaji anatengwa na wazazi wake, hivyo hivyo nasi katika kumfuasa Yesu na kuongozwa na Neno lake tunaweza kujikuta tunatengwa hata na watu waliokuwa karibu nasi na hata wanafamilia nyakati nyingine. Wakuu wa dini bado wanamwita na kumuhoji tena na hapa tunaona mmoja aliyekomaa sasa katika imani. Mara hii tunaona anajibu bila kuwa na wasi wala hofu, anakuwa mtu huru.

Kila mmoja anayekubali kuongozwa na nuru ya Yesu anakuwa mtu huru asiyeongozwa na hofu wala uoga. Anakuwa pia mjasiri, mkweli, asiyekuwa na sura mbili na daima anabaki na kiu na hamu ya kumtafuta daima Yesu Kristo, ndizo sifa tunazoziona kwa yule mtu aliyeponywa na kwa kweli ndizo sifa za kila mfuasi na rafiki wa kweli wa Yesu Kristo. Baada ya majibizano kati ya Yesu na wanafunzi wake na pia na kipofu tunaona Yesu anapotea katika simulizi. Yesu anarejea tena katika sehemu ile ya mwisho ya simulizi letu la leo. Na ndio maisha ya kila mmoja wetu katika safari yetu hapa duniani. Safari ya imani ya yule aliyezaliwa kipofu inapaswa kuwa safari ya kila mmoja wetu katika kuelekea maisha ya heri, ya kuungana na Mungu katika maisha ya uzima wa milele baada ya maisha ya hapa duniani. Nawatakia Dominika Njema na Tafakari Njema. Tuzidi kusali ili Mwenyezi atujalie kuweza kukua katika imani, matumaini na mapendo!

21 March 2020, 09:41