Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya III ya Kipindi cha Kwaresima: Yesu ni chemchemi inayozima kiu ya maisha na uzima wa milele! Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya III ya Kipindi cha Kwaresima: Yesu ni chemchemi inayozima kiu ya maisha na uzima wa milele! 

Tafakari Jumapili III ya Kwaresima: Kiu ya maisha ya uzima wa milele!

Kiu yetu haiwezi kupoozwa kwa kusaka maji ya ulimwengu huu au chakula, afya zetu si kwa utaalamu na akili zetu bali tunapotambua kuwa tunapoishi au tunapokufa, tunaishia na kufa katika Bwana. Maji ya kweli anayotupa Yesu ni kwa ajili ya uzima wa milele. Na ndio Roho wa Mungu, ndio upendo ule wa kimungu utakaozima kiu na njaa ya kila mmoja wetu. Kisima, Maji na Kiu ya kweli.

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Mwinjili Yohane daima huwa hatuelezi matukio ya Yesu kwa lengo la kutupa historia ya kilichojiri bali daima kufikisha ujumbe na mafundisho ya kitaalimungu. Na moja ya matukio hayo ndio mkutano wa Yesu na mwanamke Msamaria pale kisimani.  Simulizi hili si tu limebeba kweli za kihistoria bali zaidi sana ujumbe wa kitaalimungu kwa lugha ile ya ishara mbali mbali kama tutakavyojaribu kuziangalia katika tafakari yetu ya leo.  Kisima katika lugha ya kibiblia ilikuwa ni mahali pa kukutania watu na hasa wachungaji walifika kunywesha mifugo yao, wafanyabiashara pia walifika kisimani pamoja na bidhaa zao kwani hapo wangeweza kupata wateja, wanawake na hasa saa za asubuhi na jioni na sio mchana kama tunavyosikia leo kwa ajili ya kuteka maji, lakini haswa kisimani ilikuwa ni mahali ambapo wapenzi walikutana aidha kwa mara ya kwanza au kwa majadiliano zaidi ya urafiki wao.

Tunaweza kusoma zaidi katika Biblia sehemu mbali mbali zinazoonesha hasa makutano ya kisimani: Mwanzo 24:10-25; 26:15-25; 29:1-14; Kutoka 2:15-21.  Simulizi la leo la makutano ya kisimani tunaona wahusika wakuu ni Yesu na mwanamke msamaria.  Kisima kinachozungumziwa na Mwinjili Yohana ni kweli kipo hadi leo na kina umri wa zaidi ya miaka 3000 na bado hadi leo kinatoa maji safi na salama kwa matumizi ya viumbe hai kama ilivyokuwa enzi zile za Yesu. Ilikuwa ni kisima ambapo wasafiri hasa watokao Galilaya kuelekea Uyahudi walisimama na hapo kuweza kupata nguvu kwa mapumziko na kupooza kiu yao. Mwinjili Yohane anatuonesha hata Yesu kwa uchovu wa safari anafika mahali hapo na anapumzika na ilikuwa mchana wa saa 6. Mwinjili Yohana hataji tu muda bila kuwa na sababu ya kitaalimungu. Tunasoma Yesu anahukumiwa kifo mchana wa saa 6. Yohane 19:14,28-30 ‘’Ilikuwa yapata saa sita mchana, siku ya maandalio ya Pasaka,Naona kiu…yametimia! Kisha akainamisha kichwa, akatoa roho’’. Saa ya kiu ya Yesu ndio saa ile ya wokovu wa ulimwengu, kiu yake ni kuona sisi tulio wadhambi tunapata wokovu.

Mwanamke msamaria anashangaa kuona Yesu akimuomba maji, hakuna cha ajabu kwa mtu kuomba maji ila ikumbukwe kwa Wayahudi na Wasamaria walikuwa ni watu wasiochangamana na hata mbaya zaidi mazungumzo kati ya mwanamke na mwanaume na wakiwa peke yao isingeeleweka wala kukubalika katika jamii ile ya Yesu. Na hata ikibidi kumsemesha mwanamke mkiwa peke yenu basi mwanaume alipaswa kutumia maneno machache sana hivyo sio kufanya mazungumzo kabisa bali kama ilipaswa kuuliza kitu au jambo fulani. Mfano kama mwanaume anafika Magomeni na anapotea hajui tena njia ya kuelekea Kariakoo hakupaswa hata kuuliza: Wapi njia ielekeayo Kariakoo? Kwani tayari sentensi hiyo ina maneno mengi itoshe tu kusema: Kariakoo? Na hapo mwanamke naye aidha kwa ishara au neno moja au mawili kumuonesha mwanaume njia.

Tunaona hata wanafunzi wa Yesu wanaporejea na kumkuta Bwana na Mwalimu wao akiongea na mwanamke Msamaria walibaki na mshangao mkubwa. Yesu ndio anawaalika wanafunzi kuwa na mtazamo mwingine, kubadili vichwa vyao kama kweli wanataka kuwa wanafunzi na wafuasi wake. Ni kufikiri na kutenda kama Yesu. Labda kabla ya kuendelea sana tunajiuliza mwanamke yule msamaria alikuwa nani haswa maana Mwinjili Yohana hamtambulishi kwa jina lake, wala wapi alitokea haswa ila anamtambulisha kama mwanamke msamaria, kwa kusema ni msamaria ni sawa na kusema ni mpagani, asiyeamini katika Mungu wa kweli. Si tu anakuja kisimani peke yake kama tulivyoona mwanzoni, kuwa kisimani ilikuwa ni makutano pia ya wapenzi, na labda ndio maana anakuja sio na akina mama wengine bali akiwa peke yake. Na si anakuja peke yake hata Mwinjili anatuonesha kuwa Yesu alibaki kisimani peke yake kwa sababu kuwa wanafunzi wake walienda mjini kutafuta chakula.

Hapo tunabaki na swali la msingi kwa nini Mwinjili anakazia kutuonesha kuwa walikuwa wao wawili peke yao pale kisimani. Kama tulivyoona kuwa kisimani ilikuwa ni sehemu au mahali pakukutania wapenzi. Na katika Agano la Kale tunaona taifa la Israeli lilibaki daima kama mchumba aliyepaswa kubaki kuwa mwaminifu katika mahusiano na Mungu. Urafiki na mapenzi yao yalianza tangu wakiwa safarini jangwani wakiwa wanaelekea nchi ile ya ahadi. Lakini tunaona wakiwa safarini mara kadhaa wanapoteza uaminifu na ukaribu wao na Mungu, na hivyo kuamsha wivu kwa upande wa Mungu. Je, Mungu aliye mume au mchumba wake Israeli anafanya nini katika mazingira ya kukosa uaminifu kwa mke wake? Je, Mungu atawaacha kwa kuwatalaki? Isaya 54:6-7 na Hosea 2:16-17. Ni katika majadiliano ya Yesu na mwanamke msamaria anamuuliza yupo wapi mume wake na kumuonesha kuwa tayari ameshakuwa na waume watano na hata huyu aliye naye sasa si mume wake halali.

Yesu anamwonesha hapa kisimani kurejea na kurudi kwa mume wake wa kwanza aliye kweli mpenzi wa moyo na maisha yake, ndiye Mungu wa kweli. Ni Mungu anamwonesha Israeli kurejea na kuwa mwaminifu kwa Mungu, aliye kweli upendo kwake. Njia ile kwa wanaojua jiografia ya nchi takatifu haikuwa lazima mmoja kuipitia atokapo au aendapo kati ya Galilaya na Uyahudi kwani njia rahisi zaidi ilikuwa ni ile ya bonde la mto Yordani. Lakini Mwinjili Yohane anatuonesha ulazima kwa upande wa Yesu na wanafunzi wake kupita njia ya Samaria, ndio kusema jinsi upendo wa Mungu kwa watu wake na hasa wale wanaokuwa mbali naye. Ni jinsi Mungu anavyoshuka na kufanyika mwanadamu ili mwanadamu apate uzima wa kweli na wa milele. Mwinjili anaonesha Yesu kuchoka ndio kusema jinsi mwanadamu anavyokuwa mbali na Mungu kila mara tunapomwasi Mungu na kugeukiwa miungu mingine ya uongo na kuiabudu. Mungu anakuwa mbali hivi anapotufikia anatuonesha jinsi Mungu alivyo na kiu kuona nasi tunakuwa na kiu ya kumtafuta Yeye ili atupe maji yale ya uzima ili tukinywa tusione kiu kamwe.

Tunaona kama vile mwanamke Msamaria alivyokuja kisimani kuchota maji ya kawaida na hata wanafunzi wa Yesu nao wanaenda mjini kusaka chakula cha dunia hii. Ni jinsi gani sote mara nyingi tunaelekea na kupoteza muda kwa mambo ya dunia hii yasiyoweza kuwa chakula wala kinywaji chetu cha kweli. Njaa na kiu ya kweli ni katika kumtafuta Mungu, ni katika kukaa karibu na pamoja na Mungu, ni katika kusafiri pamoja na Mungu hata tukiwa katika nyakati ngumu kiasi gani. Siku hizi ambapo dunia nzima tunasafiri katika hofu kubwa ya maambukizi ya Virusi vya Corona (Covid-19) na tena tukiwa katika wakati wa neema ya Kipindi cha Kwaresima, tunaalikwa kujiweka karibu zaidi na Mungu. Na ndio nafasi ya kusali zaidi na ndivyo tunavyoona juhudi mbalimbali za makusudi za kutuweka karibu na Mungu. Ni tukio la kututafakarisha sio kwamba Mungu anatuadhibu na kutuangamiza wanadamu ila ni nafasi ya neema ya kutufanya nasi tuwe na kiu na njaa ya kuwa na Mungu, ya kusafiri naye siku zote za maisha yetu.

Wanawaisraeli walipokuwa njiani kula jangwani na hasa walipokosa maji walianza kulalamika na kujadiliana wao kwa wao na hasa kwa kuanza kumlaumu Mungu aliyewatoa katika nchi ile ya utumwa. Je, nasi tuwe kama Wanawaisraeli walivyokuwa kule Masa na Meriba, Je, muda na wakati huu wa mahangahiko makubwa ya Corona virusi uwe ni muda wa kumlalamikia na kumnung’unikia Mungu? Je, uwe ni muda wa kujiona Mungu ametuadhibu na kutuacha peke yetu kati ya mateso na shida kubwa? Je, tuanze kuwa na mashaka katika uaminifu na upendo wa Mungu kwetu na hivyo tuanze kujiuliza na kuhoji ikiwa Mungu yu pamoja nasi au la? Mungu anatenda muujiza kwa kuwapatia maji wa waisraeli wakati angeliweza kuwaelekeza kuchimba kisima na kupata maji, ila anawaonesha jinsi Yeye alivyo mwaminifu daima na anavyobaki kuwa upendo usio na masharti kwa kila mmoja wetu.

Masa na Meriba ni leo dunia inapotembea na kubaki katika malalamiko na manung’uniko kwa kupoteza imani kwa Mungu na ahadi zake kwetu. Jaribu hili limepamba moto tukiwa katika Kipindi cha Kwaresima, kipindi cha neema tunapotafakari mateso na kifo chake Bwana wetu Yesu Kristo ili hatimaye tuweze kushiriki furaha ile kuu ya Pasaka. Kwetu wakristo kutambua unyonge na udogo wetu ni mwaliko wa kukumbuka kuwa sisi ni watoto wa Mungu na hivyo msaada na kimbilio letu na nguvu yetu na wokovu wetu ni Mungu mwenyewe. Tu wadhaifu lakini daima katika mikono salama ya Mungu mwenyewe. Mungu kamwe hatuachi peke yetu hata tunapokuwa mbali naye kiasi gani daima ni kiu yake kuona nasi tunakuwa na kiu ya kurudi kwake kama tunavyotafakari somo la Injili ya Dominika ya leo.

Maneno ya Mtume Paulo katika Waraka wake wa pili kwa Wakorintho yawe faraja kwetu katika kipindi hiki cha majaribu makubwa karibu ulimwenguni kote. 2Wakorintho 12:9-10 ‘’ …Kwa hiyo nakubali kwa radhi udhaifu, dharau, taabu, udhalimu na mateso, kwa ajili ya Kristo; maana ninapokuwa dhaifu, ndipo ninapokuwa na nguvu’’ Baadhi ya nchi duniani letu tunaalikwa hata kukaa mbali na wengine ili kuepuka na maambukizo ya ugonjwa huo, lakini kubaki ndani na kuwa mbali na wengine na kukosa kutembeleana kama ilivyo desturi yetu iwe nafasi ya kujiweka karibu zaidi na Mungu kwa sala na kusoma Neno lake na kulitafakari ili kuweza kupata sote ujumbe wa Mungu katika majaribu haya tunayopitia, iwe fursa ya kuamsha imani yetu kwa Mungu na kutuweka zaidi na Mungu bila kumsahau jirani anayekuwa katika uhitaji wetu. Katika sala tunaunganika na wengine tukiunganishwa na Roho wa Mungu, hivyo kubaki ndani iwe ni chachu ya kuunganika na ulimwengu mzima kwa msaada wa Roho wa Mungu. Ni nafasi ya kuingia ndani mwetu na kuchunguza tena mahusiano yetu na Mungu na jirani. Kujitenga haimaanishi kutufanya tuwe wabinafsi bali tubaki wapweke ili tuweze kuunganika na ulimwengu mzima kwa msaada wa Roho wa Mungu aliye mwalimu wetu wa sala.

Kiu yetu haiwezi kupoozwa kwa kusaka maji ya ulimwengu huu au chakula cha ulimwengu huu, afya zetu si kwa utaalamu na akili zetu bali tunapotambua kuwa tunapoishi au tunapokufa, tunaishia na kufa katika Bwana. Maji ya kweli anayotupa Yesu ni kwa ajili ya uzima wa milele.  Na ndio Roho wa Mungu, ndio upendo ule wa kimungu utakaozima kiu na njaa ya kila mmoja wetu. Mwanamke yule Msamaria kama labda wengi wetu pia katika safari hii ya Kwaresima pale mwanzoni anawaza na kufikiri juu ya maji ya kawaida, lakini tunaona taratibu anaanza naye kuelewa ujumbe kusudiwa na Yesu kwake. Ni safari ya kumtambua na kumjua Mungu ambaye nasi kila mmoja hana budi kuipitia katika kipindi hiki cha Kwaresima. Mwanzoni alimtambua Yesu kama msafiri wa kawaida aliyefika kisimani ili kupooza kiu yake na kupumzika, baadaye anamtambua kama Mheshimiwa, halafu kama Nabii na baadaye Masiha na mwishoni pamoja na Wasamaria wengine wanamtambua kama Mkombozi wa ulimwengu.

Safari hii ya kumtambua Yesu ni ya kila mmoja wetu kwani mara nyingi pale mwanzoni Yesu ni mmoja anayepaswa kututimizia mahitaji yetu ya kila siku na labda hata mwelekeo wa sala zetu unaokuwa ni huo, tunaomba chakula, kinywaji na mahitaji mengine ya msingi ya kimwili ya siku kwa siku. Pamoja na kwamba ni kweli ni mahitaji ya msingi na labda ya lazima sana katika maisha yetu lakini hatupaswi kuishia hapo bali kufika hatua ile ya kumtambua kama Mkombozi na Mungu wetu. Hitimisho la Injili ya leo linapaswa kuwa la kila mmoja wetu baada ya kukutana na Yesu. Mwanamke Msamaria baada ya kumtambua Yesu katika mazungumzo naye anajawa na shauku na ari kubwa na hivyo kuacha nyuma mtungi wake na kwenda kuwashuhudia wengine kuwa amekutana na Masiha, amekutana na Mkombozi.

Ndio mwito kwetu baada ya kukutana na Yesu na kumtambua katika Neno lake na katika maisha ya masakramenti na maisha ya Kanisa hatuna budi kutoka na kuwa wamisionari kwa ushuhuda wa maisha yetu na kuwashirikisha wengine furaha ile ya kukutana na kumtambua Yesu na kula na kunywa chakula na kinywaji kile cha uzima wa milele. Nawatakia tafakari njema huku tudumu tukiungana katika sala na maombi hasa Yesu asafiri na awe Yesu katika kipindi hiki cha neema cha Kwaresma na mahangahiko ya ugonjwa wa Corona virusi (Covid-19). Ugonjwa au hatari iwayo yote haipaswi kutuletea uoga bali daima tubaki tu na hofu ya Mungu. Mkristo hapaswi kuwa na uoga kwani ishara ya kukosa imani bali tuwe tu na hofu ya Mungu ndio kiu ya kuwa na Mungu na kubaki waaminifu kwake bila kujali nyakati na misalaba yake. Daima katika imani.

13 March 2020, 13:41